HASH POWER 7113
Kugombana ni jambo ambalo halikwepeki
katika uhusiano wa kimapenzi. Upo ugomvi ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi
lakini upo ugomvi ambao huwa mkubwa na kama ukitokea na ukashindwa kujua nini
cha kufanya kuweka mambo sawa, husababisha ufa kwenye penzi lenu.
Leo tutazungumzia mambo ya muhimu ya
kufanya inapotokea wewe na mpenzi wako mmeingia katika ugomvi mkubwa,
mmetoleana maneno machafu au hata kupigana.
1.
TAFAKARI CHANZO CHA TATIZO
Kuna usemi kwamba ukitaka kulitatua
vizuri tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo cha tatizo lenyewe. Ukishindwa
kugundua chanzo cha tatizo, basi na wewe unakuwa sehemu ya tatizo.
Utashangaa kwamba wapenzi wengi
hugombana na mambo kuwa makubwa kabisa kwa sababu ya vyanzo vidogo ambavyo
walishindwa kuvigundua mapema na matokeo yake vikazaa matatizo mengine.
Mfano rahisi, chanzo kinaweza kuwa
mpenzi wako amekupigia simu lakini ukashindwa kuipokea kwa muda muafaka.
Atakapopiga kwa mara nyingine au mkikutana, usitegemee atakufurahia kwa sababu
atahisi umemdharau kwa kutopokea simu yake.
Endapo ukifanya makosa ya kushindwa
kuliona kosa lako mapema na kushindwa kuomba radhi au kutoa maelezo
yanayoeleweka kwa nini hukupokea simu, matokeo yake utamjibu vibaya, naye
atakujibu vibaya na mwisho mtaishia kupigana au kuachana kabisa mkiwa
mmeshatoka kabisa kwenye kosa la msingi.
Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi
chanzo kidogo kinavyoweza kusababisha tatizo kuwa kubwa. Ndoa nyingi au
uhusiano unaofika mwisho huwa umesababishwa na mambo madogo ambayo yalishindwa
kutafutiwa suluhu mapema.
Katika kila ugomvi unaotokea, jambo la
kwanza jipe muda wa kutafakari chanzo kilichosababisha mkagombana. Wakati
mwingine wewe ndiyo unaweza kuwa chanzo cha tatizo lakini kama ukiyajua makosa
yako mapema na kukiri kisha kuomba radhi kwa mwenzio, utakuwa kwenye nafasi
nzuri ya kurudisha mapenzi kwa haraka.
2.
MPE MUDA HASIRA ZIISHE
Kila binadamu ameumbwa akiwa na hasira
na kwa bahati mbaya ni wachache wanaoweza kuzidhibiti hasira zao. Ni rahisi mtu
kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na hasira. Baada ya kugombana, kila mmoja lazima atakuwa
na hasira na njia pekee inayoweza kuepusha matatizo zaidi, ni kujipa muda na
kumpa muda mwenzako ili hasira zipungue.
Kama mpo sebuleni na umetokea ugomvi,
ni busara kwenda chumbani au nje mpaka hasira zako zikiisha. Ni makosa
kulazimisha suluhu wakati kila mmoja akiwa na jazba kwani mtaishia pabaya
zaidi.
Endapo ukishaona hasira zako zimetulia
na mwenzako naye ametulia, unaweza kuanzisha mada juu ya kilichosababisha
mkagombana. Tumia lugha ya upole kwani endapo utakuwa ukifoka au kuzungumza kwa
sauti ya juu, matokeo yake mtarudia tena kugombana.
3.
MPE NAFASI YA KUZUNGUMZA
Huwezi kumuelewa mtu kabla hujampa
nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile alichokusudia kukisema. Endapo tatizo
limetokea na upo kwenye hatua za kusaka suluhu, mpe mwenzako nafasi ya kueleza
dukuduku lililopo ndani ya moyo wake. Usimkatishe wala kumbishia chochote,
muache aongee ulichomuudhi mpaka dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze kwa
upole na sauti tulivu.
4.
OMBA MSAMAHA
Hakuna silaha nzuri inayoweza
kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutuliza mambo kabla hayajawa mabaya kama
kuomba msamaha. Neno ‘samahani’ ni dogo lakini lina maana kubwa kwa yule mtu
anayelitoa na anayelipokea.
Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa
siyo lako, omba msamaha kwanza kisha baada ya hapo anza kumuelewesha mpenzi
wako kwa upole. Lazima mwisho na yeye atayaona makosa yake na kukuomba msamaha,
mtaweza kuepuka kuukuza ugomvi huo na kurudisha hisia za mapenzi.
5. USIWEKE KINYONGO
Endapo umeamua kuomba msamaha kwa
mpenzi wako, au yeye amekuomba msamaha, samehe kwa dhati kutoka ndani ya moyo
wako na sahau kile kilichotokea. Ni kosa kubwa kuweka kinyongo rohoni, yaani
unamwambia kwamba umemsamehe wakati moyo wako bado una hasira naye.
Ukisamehe kwa dhati, jifunze na
kusahau kwani kusamehe kunaenda sambamba na kusahau, wazungu wanasema forgive
and forget. Elewa kwamba mpenzi wako ni binadamu ambaye hajakamilika, wala si
malaika.
Lazima atakuwa akikosea mara kwa mara,
endapo utakuwa ukilimbikiza vinyongo, unafuga matatizo makubwa kwani siku
nyingine akikukosea hata jambo dogo, utakumbushia na ya jana na juzi na mwisho
ugomvi utakuwa mkubwa sana.
Tukutane next issue kwa mwendelezo wa mada hii nzuri.
No comments:
Post a Comment