Na Aziz Hashim
Kishindo kikubwa nyuma ya nyumba ndicho kilichomshtua babu yake Kahungo, akatoka akiwa ameshika sime kubwa. Alipogundua kuwa ni mjukuu wake, tena akiwa na msichana aliyesababisha akaasi miiko ya kichawi alifurahi sana na kumpongeza.
“Kweli umekuwa Kahungo, hata nikifa leo najua nimeacha mrithi duniani,” alisema huku akicheka kwa furaha. Yule msichana alibaki kuduwaa akiwa haelewi kilichotokea kwani alipofumba macho alikuwa nyumbani kwao lakini sekunde chache baadaye alipoambiwa afumbue, alijikuta akiwa kwenye mazingira tofauti kabisa.
Akiwa bado anashangaashangaa, alishikwa mkono na babu yake Kahungo, akampeleka chini ya mti mkubwa uliokuwa na kivuli na kumwelekeza akae.
SASA ENDELEA…
Alimtolea kigoda cha miguu mitatu kilichokuwa kimepakwa vitu kama dawa za kienyeji sehemu ya kukalia, akamwamuru akae. Hakuwa mbishi, alitii alichoambiwa. Kilichomchanganya ni kwamba Kahungo ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wake alitoweka kimazingara muda mfupi baada ya kumfikisha pale kwa babu yake.
Kila alipopepesa macho akitaraji kumuona Kahungo, aliambulia patupu, hali iliyoanza kumpa hofu. Kwa muda huo babu yake Kahungo alikuwa bize kuanza kuandaa dawa za kienyeji ambazo zilikuwa maalum kwa ajili ya kumkomboa mjukuu wake aliyekuwa hatarini kuuawa kwa nguvu za kishirikina baada ya kuvunja masharti ya kichawi.
“Unaitwa nani binti na umetokea wapi?”
“Naitwa Fauzia, nimetokea Chwaka, Unguja.”
"Unaweza kuniambia jinsi ulivyookoka kutoka kule chini ya bahari kwenye Makaburi ya Nungwi?"
"Kahungo alinisaidia kwa kiasi kikubwa, siwezi kueleza chochote zaidi ya kuwa yeye ndiye aliyeniwezesha kurudi duniani."
“Unajua kwamba wewe na yeye mnastahili adhabu ya kifo kwa kitendo mlichokifanya ufukweni?" aliongea babu yake Kahungo huku akiwa amemkazia macho yule msichana ambaye alimweleza kuwa anaitwa Fauzia.
"Kahungo ndiye aliyenishawishi, sikuweza kumkatalia kwa kuwa ndiye aliyekuwa ameyashikilia maisha yangu kwa wakati ule."
Kauli ile ya yule msichana ilimfanya babu yake Kahungo aanze kumfikiria vibaya mjukuu wake. Hakuwahi kumsikia wala kumuona hata mara moja akishughulika na wasichana, alishangaa kivipi amshawishi msichana yule, tena katika mazingira hatarishi? Hakupata jibu.
Aliendelea na maandalizi yake na baada ya kukamilisha kazi ya kuchanganya dawa za kienyeji, aliweka ndani ya kibuyu cheusi kilichokuwa kimevishwa shanga nyeupe na nyeusi shingoni na kumpelekea yule msichana pale alipokuwa amekaa.
"Kunywa hii kwa faida yako na Kahungo, vinginevyo wote mtarudishwa kwenye makaburi ya Nungwi mkaendelee kuwa misukule na vijakazi wa wachawi," alisema babu yake Kahungo. Yule msichana alikipokea kile kibuyu huku mikono yake ikitetemeka, akapeleka mdomoni na kunywa dawa iliyokuwa ndani yake kama alivyokuwa ameelekezwa.
Katika hali ambayo hakuitegemea, alipokunywa tu, alianza kuhisi maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu. Maumivu yalikuwa yakiongezeka kwa kadiri muda ulivyokuwa unaongezeka. Babu yake Kahungo aliondoka na kurejea chumbani kwake na kumuacha yule msichana akiugulia maumivu makali.
Licha ya kumlalamikia sana kuwa dawa aliyomnywesha imemdhuru, babu yake Kahungo hakujali, akaendelea na shughuli zake kama hakuna kilichokuwa kimetokea. Maumivu yale yaliambatana na hamu ya kujisaidia haja ndogo ambayo ilikuja ghafla. Kwa kuwa hakuwa mwenyeji wa eneo lile, alijaribu kwa mara nyingine kumuita Kahungo ili amuoneshe mahali palipokuwa na choo.
Licha ya kuita kwa sauti, Kahungo hakuitikia, hali iliyomfanya ainuke pale kwenye kiti cha miguu mitatu alipokuwa amekaa na kuelekea nyuma ya nyumba ya babu yake Kahungo, mahali walipotua kimiujiza muda mfupi uliopita. Wakati akizidi kutembea, alizidi kubanwa na haja ndogo, uzalendo ukamshinda, akaamua kujisaidia pembeni ya ule mbuyu, mahali ambapo aliamini hakuna mtu atakayemuona.
Aliinama na kujiweka sawa, akaanza kujisaidia haja ndogo. Cha ajabu wakati akiendelea kukidhi haja zake, kuna wakati mkono wake uligusana na haja ndogo, alipotazama almanusra aanguke kwa kihoro. Haikuwa haja ndogo kama alivyokuwa amefikiria, bali alikuwa akitokwa damu nyingi na nzito iliyokuwa na rangi nyekundu iliyochanganyikana na nyeusi. Mapigo ya moyo wake yaliongezeka kwa kasi, tumbo likawa linazidi kumuuma na akawa haamini kile kilichomtokea. Alikatisha haja yake na kusimama, akashangaa nguo yake ya ndani ikilowana damu, hali iliyomfanya aanze kulia kwa hofu kuu huku akiomba msaada.
"Hee! Mamaa! Nakufa… nakufa…" alisema kwa sauti ya juu iliyojaa woga.
"Hauwezi kufa Fauzia? Hili ni tambiko kwa dhambi mliyoifanya na Kahungo ya kukutorosha kutoka kwenye makaburi ya Nungwi na kuzini, ni lazima wote mtolewe damu kutoka kwenye miili yenu ili itumike kwenye tambiko la kuvunja nguvu za laana zinazowakabili,” Fauzia alisikia sauti ambayo hakuelewa imetokea wapi.
“Lakini mbona mimi sina kosa?” Fauzia alijibu huku akipepesa macho huku na kule kuangalia ni nani aliyekuwa anaongea naye bila mafanikio.
"Huu ni ulimwengu tofauti na uliouzoea, haki, sheria na usawa havitumiki kwenye ulimwengu wa giza bali mwenye nguvu ndiye mwenye nafasi ya kufanya chochote anachokitaka, tii maelekezo ili uwe salama."
Fauzia alizidi kulalamikia maumivu makali ya tumbo huku akizidi kutokwa na damu nyingi. Mara alianza kuhisi kizunguzungu kikali akiwa palepale chini ya mbuyu, akakaa chini na kuegamia shina la mti ule mkubwa. Kizunguzungu kilizidi kuwa kikali, giza likaanza kutanda machoni mwake na taratibu akaanza kuhisi fahamu zake zikimtoka. Hakuelewa tena kilichoendelea.
Kahungo alikuwa kwenye chumba cha giza, ndani kabisa ya nyumba ya babu yake. Aliingia kule kutii maelekezo ya babu yake baada ya kukamilisha kazi ya kumtafuta na kumpeleka pale Fauzia. Alilala juu ya kitanda cha kamba kilichokuwa katikati ya chumba kile huku akiwa amevua nguo zote kama alivyokuwa ameelekezwa na babu yake.
Chini ya kitanda kuliwekwa dawa za kienyeji pamoja na kibuyu kikubwa. Kahungo akiwa amelala pale kama alivyokuwa ameelekezwa na babu yake, alishangaa kuona anaanza kutokwa na damu nyingi puani, mdomoni na masikioni. Damu ilikuwa ikiongezeka kwa kadiri muda ulivyokuwa unaenda, kilichomshtua zaidi ni kuona inachuruzikia kwenye kibuyu kikubwa kilichokuwa chini ya kitanda.
Mwili ulimsisimka kuliko kawaida, akawa anatetemeka kwa hofu kuu.
Je, nini kitafuatia? Usikose wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment