Tuesday, January 6, 2015

JIMBO LA KILOSA; MAPIGANO, HUDUMA MBOVU ZA KIJAMII NI TATIZO SUGU


Na Hashim Aziz
Kilosa ni moja kati ya wilaya zinazounda Mkoa wa Morogoro ikiwa na jumla ya wakazi 26,060 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002. Pia ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na mwanasiasa mkongwe, Mustapha Mkulo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mkullo (kulia)
Wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari mpaka kwenye jimbo hilo ambapo mwandishi wetu alifanikiwa kuzungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali yakiwemo Mtendeni, Mkwateni, Magomeni, Kibaoni, Manzese A, Manzese B, Uhindini, Mazinyungu na maeneo mengine mengi ambapo alizungumza na wananchi walioeleza matatizo yao.
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara hiyo, Uwazi lilibaini matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo, kubwa ikiwa ni mapigano ya mara kwa mara kati ya jamii za wakulima na wafugaji wanaogombea ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, kama ilivyobainika pia katika Jimbo la Mvomero ambalo pia lilitembelewa hivi karibuni.
Mkullo
Wakulima wanalalamika kwamba wafugaji wa Kimasai,
wamekuwa wakiingiza mifugo yao kwenye mashamba yao, jambo linalosababisha hasara kubwa na kurudishwa nyuma kimaendeleo.
KERO ZA WAKULIMA
“Kero yetu kubwa sisi wakulima wa Kilosa ni wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba yetu na kuharibu mazao yetu hasa wakati wa kukaribia msimu wa mavuno. Tunaiomba serikali kutuondolea kero hii ya miaka mingi.
“Unakuta Wamasai wanamkabidhi mtoto mdogo wa miaka tisa au kumi kundi la ng’ombe zaidi ya 100. Sasa unafikiri mtoto kama huyu atakuwa anajua thamani ya mazao ya wakulima? Matokeo yake wanaingiza ng’ombe mashambani na kula mazao,” alisema Mzee Joseph Jonas, mkazi wa Kibaoni anayejishughulisha na kilimo.
MATATIZO YA WAFUGAJI
Wafugaji nao walikuwa na malalamiko yao wakidai kuonewa na wakulima na kupokonywa maeneo yao ya kulishia mifugo.
“Sisi wafugaji tunaoneka kama siyo raia wa nchi hii, kila tunapoingia kwenye pori tunafukuzwa na kuambiwa tunaingiza mifugo yetu kwenye hifadhi, tukitafuta sehemu nyingine tunaambiwa tunaingiza ng’ombe kwenye mashamba ya watu, sasa tukalishie wapi mifugo yetu?
“Tunamuomba mbunge atusaidie kwani wakulima wametukuta kwenye eneo hili, sisi tupo hapa miaka mingi iliyopita sasa wanataka tuende wapi?” alisema Seliodi Ole Maleyo, mfugaji wa Kimasai.
HUDUMA ZA KIJAMII
Mbali na tatizo hilo, wananchi walieleza matatizo mengine yanayowasumbua kuwa ni uhaba wa maji safi na salama ya kunywa, uhaba wa madarasa na vifaa vya kujifunzia, ukosefu wa madawa katika hospitali na miundombinu mibovu, upungufu walimu na maabara kwenye shule za sekondari na za msingi na kubwa zaidi, ukosefu wa huduma bora za kuwasaidia wanawake wajawazito kujifungua salama.
“Kero yetu kubwa sisi wanawake kwenye jimbo hili ni huduma duni kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Kilosa. Kwa mfano mimi kama unavyoniona na mtoto wangu huyu mchanga, siku zangu za kujifungua zilipokaribia, ilibidi nisafiri na tumbo langu hadi Morogoro Mjini kwenda kujifungua.
“Huduma za uzazi katika hospitali yetu ni za mashaka na usipokuwa makini unaweza kufa hivyo tunamuomba mbunge wetu  atusaidie sisi wanawake,” alisema Rozina Seganje, mkazi wa Magomeni.
UKOSEFU WA AJIRA
 Naye Kijana Athuman ldd Mkazi wa Uhindini alisema: ”Kero yetu sisi vijana ni ukosefu wa ajira. Tunajua ajira hakuna serikali hakuna lakini tunapotaka kujiajiri, tunakwamishwa na miundombinu mibovu ya huku.
“Tangu awamu Rais Mkapa, tuliambiwa kuwa kutajengwa barabra ya lami kutoka Dumila kupita kwenye jimbo letu kueleka Mikumi hadi lringa lakini ni miaka kumi sasa imepita hakuna kinachoendelea.
“Barabara ikikamilika, tutafanya biashara na kujiajiri kwani kwa taarifa tulizonazo, mabasi na malori yatakuwa yanapita hapa. Tunataka mbunge atuambie barabara hiyo itakamilika lini au mpaka tufe?”
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia kero hizo za wanananchi mwandishi wetu alipiga hodi nyumbani kwa Mbunge Mkulo, Uhindini ambapo mlinzi wa nyumba hiyo alisema bosi wake yupo safarini kikazi. Mwandishi wetu hakuchoka, akaamua kumwendea hewani ambapo alipopatikana, alikuwa na haya ya kueleza:
“Ni kweli kero hizo nazifahamu na kwamba naendelea kuzitafutia ufumbuzi ingawa baadhi ziko nje ya uwezo wangu. Kwa sasa nipo Dodoma bungeni lakini kama upo kwenye jimbo langu, baadhi ya kero kama hizo za hospitali na barabara nenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) atakupa maelezo zaidi,” alisema Mkullo kwa kifupi kisha akakata simu.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...