Tuesday, November 27, 2012

UNENE WA KUPINDUKIA (OBESITY)


Wengi huwa wanaamini unene ndiyo afya, kwamba mtu mnene ana afya njema kuliko mwembamba lakini ukweli ni kwamba unene wa kupindukia (obesity) ni tatizo ambalo kila anayependa kuishi maisha marefu anapaswa kupigana nao.
Obesity ni hali ambayo mafuta yaliyozidi mwilini (excess body fat) hujikusanya katika sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kwenye moyo, na kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mhusika ikiwemo magonjwa ya moyo, kisukari au wakati mwingine vifo vya ghafla.
UTAJUAJE KAMA UNA OBESITY?
Wengi hushindwa kuelewa kama unene walionao ni wa kawaida au la, naamini baada ya kusoma mada hii, kila mmoja atakuwa na uwezo wa kujitambua mwenyewe bila hata kwenda kwa daktari.
BODY MASS INDEX (BMI)
Hiki ni kipimo maalum ambacho kinatumika kupima uwiano wa uzito wa mwili na urefu. Hutumika duniani kote kupima na kugundua watu wenye obesity kwa kutumia kanuni maalum. Kiligunduliwa rasmi kati ya mwaka 1830 hadi 1850 na Adolphe Quetelet, mwanasayansi wa Ubelgiji.
Kanuni ya BMI= Uzito wa mwili (Kg)
                               (Urefu (Mita))2


NAMNA YA KUJIPIMA
-Jipime uzito wa mwili wako kwa kutumia mizani ya kawaida, andika uzito huo katika kilogramu. Kwa mfano kilo 75.
-Jipime urefu wako kwa kutumia (meter rule) au kipimo chochote kinachoonesha urefu kwa meta. Andika jibu lako. Mfano Meta 1.7.
-Zidisha urefu ulioupata kwa wenyewe.
Mfano 1.7 x 1.7=  2.89
-Gawanya uzito kwa jibu la urefu ukiuzidisha kwa wenyewe
Mfano: 75÷ (1.7 x 1.7)= 25.9.
KUFAFANUA MAJIBU
1.      Endapo jibu utakalopata baada ya kufanya hesabu kama hapo juu litakuwa ni chini ya 15, utakuwa na tatizo la uzito mdogo (very severe underweigth) ambalo ni tatizo kama ilivyo Obesity. Inabidi uongeze kula chakula chenye virutubisho.
2.      Ikiwa jibu lako litakuwa ni kati ya 15 hadi 16, bado uzito wako hauendani na urefu wako (severe underweight), ongeza kula chakula bora na kufanya mazoezi.
3.      Uzito wako ukiwa kati ya 16 hadi 18.5, bado upo chini ya uzito unaotakiwa (underweight), kula chakula bora na kufanya mazoezi.
4.      Jibu lako likiwa ni kati ya 18.5 hadi 25, basi huo ndiyo uzito unaotakiwa (normal health). Una afya njema na endelea kujitunza na kufuata kanuni za afya bora.
5.      Jibu lako likiwa ni 25 hadi 30, una tatizo la uzito mkubwa (Overweight). Punguza kula vyakula vyenye mafuta na jitahidi kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza mafuta yaliyozidi.
6.      Ikiwa jibu lako linazidi 30, basi ujue unasumbuliwa na Obesity.
NINI HUSABABISHA OBESITY
-Ulaji wa vyakula visivyo na uwiano mzuri wa virutubisho.
Kwa kawaida, binadamu anapaswa kula mlo kamili, wenye kiwango stahiki cha virutubisho kulingana namahitaji ya mwili. Inapotokea mtu akawa anakulakula hovyo vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta kwa wingi au virutubisho vingi kuliko vinavyohitajika na mwili, uzito wa mwili huongezeka na kusababisha tatizo hili.
-Kutofanya mazoezi
Mazoezi ya mwili (angalau mara tatu kwa wiki kwa muda usiopungua nusu saa) husaidia sana kuchoma mafuta na nishati iliyozidi mwilini. Inapotokea mtu akawa anakula lakini hafanyi mazoezi, matokeo yake huwa ni obesity.
-Mitindo ya maisha
Maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa kwenye nchi zilizoendelea, yamesababisha kuongezeka kwa obesity. Badala ya mtu kutembea kwa miguu ili kupunguza mafuta yasiyohitajika, utakuta muda mwingi anatumia gari, badala ya kupanda ngazi anatumia lifti, ofisini badala ya kusimama au kutembea, anatumia viti vya kuzunguka vyenye magurudumu. Matokeo yake, chakula unachokula kinakosa kazi na matokeo mafuta yanaanza kurundikana mwilini.
-Vinasaba (genes)
Baadhi ya watu hurithi vinasaba vya unene kutoka kwa wazazi wao na kujikuta wakinenepeana hata kama wanaishi maisha ya dhiki.
-Sababu za kitabibu
Baadhi ya dawa wanazopewa wagonjwa kutibu maradhi mbalimbali, husababisha mgonjwa kunenepeana na kuongezeka uzito hivyo kupata Obesity. Pia kuna baadhi ya mgonjwa ambayo huambatana na Obesity.



MADHARA YA OBESITY
Madhara ya Obesity yameenda mbali zaidi na yanagusa mwili, akili na jamii kwa jumla.
Madhara ya kiafya yanajumuisha:
-Magonjwa ya moyo
Kurundikana kwa mafuta ndani ya mwili hususan ndani ya mishipa inayopitisha damu, husababisha kupungua kwa ujazo wa mishipa hiyo hivyo kuzuia damu kuzunguka mwilini kwa urahisi. Hii husababisha msukumo wa damu kubadilikabadilika, jambo ambalo husababisha shinikizo la damu (blood pressure) na shambulio la moyo (heart attack).
-Maumivu ya mgongo, kiuno na viungo
Mwili unapoongezeka uzito kuliko uwezo wake, husababisha maumivu ya viungo mbalimbali ambavyo huelemewa na uzito wa mwili. Watu wenye Obesity husumbuliwa na maumivu ya mgongo, kiuno na viungo vya miguu hususan magoti na vifundo (ankles).
-Kisukari
Mtu anayekula bila mpangilio, bila shaka atakuwa na tabia ya kupenda vitu vyenye sukari kwa wingi, mafuta na kemikali nyingine ambazo huwa na madhara kwa mwili. Si hivyo tu, mtu mwenye obesity, mwili wake hushindwa kuzalisha kichocheo cha Insulin ambacho hurekebisha kiwango cha sukari mwilini na kujikuta akiishia kupata ugonjwa wa kisukari.
-Kiharusi (Stroke)
Pia watu wenye obesity, wapo kwenye hatari kubwa ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.
 Magonjwa mengine wanayoweza kuyapata watu wenye obesity ni saratani, angina (kifua kubana), matatizo katika mmeng’enyo wa chakula na Osteoarthritis.
Madhara ya kiakili:
Mtu mwenye obesity, huwa katika hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa kama kupoteza kumbukumbu, kusumbuliwa na msongo wa mawazo mara kwa mara, kushindwa kujiamini na kushindwa kudhibiti hasira au mshtuko na kujikuta wakizimia au kupoteza fahamu wanaposhtuliwa au kupokea taarifa mbaya kama misiba, ajali na kadhalika.
Madhara ya kijamii:
Watu wenye obesity, wanaelezwa kuwa wavivu katika masuala ya uzalishaji kutokana na kuelemewa na uzito wa miili yao. Wataalam wamebaini kuwa watu wenye obesity, huchoka haraka hata wakifanya kazi ndogo na hivyo kupunguza kasi ya shughuli za uzalishaji.
Pia watu wenye obesity hukumbwa na unanyapaa kutoka wa jamii. Wengi huzomewa wanapotembea mitaani, kuchekwa au kushangawa sana, jambo ambalo huwaumiza na kuwafanya wajione kama jamii haiwakubali.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...