Saturday, November 21, 2009

MY HEART IS BLEEDING! (MOYO WANGU UNAVUJA DAMU) -I (SWAHILI VERSION)

NOVEL MANUSCRIPT
(SWAHILI VERSION)
“Beyond The Seen Scene!… Beyond The Grave Yards… There Laid…
The Hearts That Bleeds, Hearts Of Desperately Broken Victims, The Weak!! Their Hearts Are Bleeding…, But Finally A Healing Balm For Every Wound Is Found, When The Darkness Takes Its Flight…”
My Heart Is Bleeding…
(moyo wangu unavuja damu)
Novel story by:
Aziz Hashim-Hash power
amenibarikihash@rocketmail.com

EPISODE I
SEHEMU YA KWANZA
Ilikuwa ni jumatatu ya kwanza ya mwezi Septemba, asubuhi tulivu yenye anga lililopendezeshwa na rangi ya bluu, jua la asubuhi likiwa ndio linachomoza na kuzidi kuipendezesha siku ya kwanza ya juma.
Umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika katika viwanja vya mahakama kuu ulitosha kumfanya yeyote asiyejua kilichokuwa kinaendelea mahali hapo kupigwa na butwaa. Ilikuwa ni idadi kubwa kabisa ya watu kuwahi kutokea tangu mahakama hiyo ilipoanza kufanya kazi rasmi miaka kadhaa iliyopita…



Kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda, ndivyo watu walivyokuwa wanazidi kuongezeka katika eneo la kuizunguka mahakama. Wote walikuwa wamekuja kwa lengo la kutaka kusikiliza mwendelezo wa kesi nzito ya mauaji iliyokuwa ikimkabili kijana mdogo kabisa, ambaye kwa haraka haraka ungeweza kumkadiria kuwa na umri usiozidi miaka ishirini.

Hiyo haikuwa kesi ya kwanza ya mauaji kutolewa hukumu mahakamani hapo, lakini kesi hii ilionekana kuwa tofauti na kesi nyingine, kwani ilionekana kuzigusa hisia za watu wengi sana.

Iliwawia vigumu askari wa kutuliza ghasia na wale wa jeshi la polisi kuweza kuwatuliza watu wote waliofurika eneo hilo kwani walikuwa ni wengi sana na walikuwa bado wanazidi kuongezeka kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda.

Ving’ora vya magari ya polisi na kelele za mbwa wa polisi vilizidi kufanya hali ya mahali hapo izidi kuzizima, huku kila mtu akiwa na hamu ya kutaka kujua nini kingeendelea. Vurugu zilizidi kupamba moto na utulivu na amani vikatoweka kabisa katika viwanja vya mahakama wakati gari lililombeba mtuhumiwa likiwa linaingia mahakamani hapo.
Watu walikuwa wakipiga kelele na kukanyagana kila mmoja akitaka japo amwone mtuhumiwa wa kesi hiyo nzito. Kila mtu alikuwa analikimbilia gari lililombeba mtuhumiwa na muda mfupi baadae gari lote likawa limezingirwa kila upande, kiasi cha kushindwa kuelekea kwenye lango kuu la mahakama .

Akina mama waliokuwepo eneo hilo walisikika wakiangua vilio kama wanaomboleza msiba mzito, huku vijana na watu wazima wakishindana nguvu na polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wakiwazuia wasimuone mtuhumiwa.

Kilichoendelea sasa ikawa ni vurugu mtindo mmoja, Polisi virungu na mabomu… raia mawe na fimbo. Polisi wa kutuliza ghasia walioneka kuanza kuzidiwa nguvu na raia hali iliyowalazimu kuanza kufyatua hovyo risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi ili kuutawanya umati mkubwa wa watu waliokuwa wamelizingira gari alimokuwemo mtuhumiwa.

Baada ya nguvu kubwa kutumika kuwadhibiti raia, hatimaye ikalazimu gari lililombeba mtuhumiwa lirudi kwenye gereza kuu mpaka hali itakapokuwa shwari. Baada ya patashika lililodumu kwa takribani masaa mawili, hatimaye hali ilitulia.

Polisi wa kutuliza ghasia walikuwa wameongezwa maradufu, wengi wakiwa ni wale wa kikosi maalum cha mbwa wakiwa wametapakaa karibu kila sehemu sehemu kuizunguka mahakama.

Baada ya hali kuwa shwari hakimu aliamuru mtuhumiwa akaletwe na kupandishwa kizimbani tayari kwa kusomewa mashtaka mazito ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili.

Safari hii ilibidi gari lililombeba mtuhumiwa liingie kwa kupitia mlango wa nyuma “Emergency exit” ili kuzuia hali kama ile iliyojitokeza awali.

Hatimaye mtuhumiwa aliingizwa mahakamani chini ya ulinzi mkali na akapandishwa kizimbani. Utaratibu wa kawaida wa kuendesha mashtaka ukaanza huku Jaji mkuu Profesa kadir Mudhihir Simba akiwa ndiye anayetakiwa kuisikiliza kesi ile na kuitolea hukumu ya mwisho.

Minong’ono ya chinichini ilikuwa ikisikika kutoka pande zote za mahakama huku watu wakiwa hawaamini kuwa ni kweli yule aliyekuwa kizimbani upande wa kushoto wa hakimu ndio mtuhumiwa aliyeifanya nchi nzima kutetemeka kwa hofu kutokana na mauaji makubwa na ya kutisha aliyokuwa ameyafanya.

Huyo ndio alikuwa mtuhumiwa aliyezigusa hisia za watu wengi kuliko kawaida kiasi cha kufanya kila mtu awe na hamu ya kutaka kumuona na kujua nini hatma yake. Kijana mdogo kabisa, mrefu wa wastani mwenye rangi ya maji ya kunde, ambaye ungemkadiria kuwa na umri usiozidi miaka ishirini.

Usoni hakuonyesha wasiwas hata kidogo na alikuwa akitabasamu japokuwa alikuwa akikabiliwa na kesi nzito sana ya mauaji ya kutisha ya idadi kubwa ya watu, akiwa amewaua wote kwa mkono wake. Alikuwa ametulia kimya akisubiri kuona nini hatma yake.

Minong’ono ilikuwa ikizidi kuongezeka, na zaidi akinamama ambao hawakuweza kujizuia kulia kwa uchungu kwani hakika hukumu ambayo ilikuwa ikisubiriwa huenda ndio ingekuwa kali zaidi kuliko zote zilizowahi kutolewa.

Kilichovuta hisia za watu wengi ni sababu ambazo zilifanya kijana huyu mdogo kufanya mauaji makubwa na ya kutisha kiasi kile. Ni sababu ambazo ilihitajika mtu makini sana kuweza kutoa hukumu. Na hii ndiyo iliyosababisha kesi hii kuahirishwa mara saba mfululizo licha ya kwamba upelelezi ulishakamilika siku nyingi na vithibitisho vyote vilikuwa vimefikishwa mahakamani.

Mahakimu wote walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho za kesi huyo huku kila mmoja akitoa sababu zake binafsi. Mwishowe ilibidi jaji mkuu aingilie kati na kuamua kuisikiliza mwenyewe kesi ile baada ya mahakimu karibu wote kuonekana wanaikwepa.

Waliokuwa wakifahamu kisa na mkasa kilichopelekea kijana yule mdogo kufanya vile, walikuwa wakimsikitikia kwani walijua hakika asingeweza kukwepa adhabu nzito iliyokuwa inamngoja. Hakuna aliyeonekana kuwasikitikia wahanga wa mauaji yale kwani wote walistahili kufa kwa waliyoyafanya.
“Mwachieni huru mwanetu!”

Alisikika mama mmoja akiongea kwa jazba iliyofuatiwa na kilio cha kwikwi. Kwa mujibu wa taratibu na sheria za mahakamani hapo, hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuongea chochote wakati kesi ikiendelea. Lakini kwa jinsi kesi hiyo ilivyozigusa hisia za watu, mama yule alijikuta ameropoka na kuungwa mkono na umati wote uliokuwemo mle ndani. Ilibidi jaji mkuu atumie busara zake kurudisha utulivu mahakamani kwani vurugu ilikuwa almanusra ianze tena bada ya wanausalama kutaka kumtia nguvuni mama yule kwa kuvunja taratibu za mahakama.

Baada ya muda mfupi hali ikarudi kuwa shwari. Zilisikika kelele za karatasi tu, za jalada la kesi zilizokuwa zinapekuliwa na jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba. Watu walikuwa wakiwatazama mtuhumiwa na hakimu kwa zamu zamu. Ungeweza kudhani ni mchezo wa kuigiza kwenye luninga au tamthilia nzuri , lakini haikuwa hivyo.

Jaji mkuu aliuvunja ukimya uliokuwepo mahakamani hapo kwa kuanza kumsomea mashtaka mtuhumiwa, na kabla hajaendelea kutoa hukumu akamuuliza mshtakiwa…

“Je! Ndugu mshtakiwa una lolote la kujitetea kabla hukumu haijatolewa?”
Swali lile lilizua upya minong’ono ambayo iliongeza shauku ya umati ule kutaka kusikia mshtakiwa atajibu nini.

“Mtukufu hakimu, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwangu mimi huu sio utetezi bali ni ushuhuda wa yale yaliyonifanya niwaue mashetani hawa.Ninachoweza kusema ni kwamba, nakiri kufanya mauaji makubwa na ya kutisha kwa mikono yangu. Mikono yangu imetapakaa damu… damu ya kisasi. Sijuti kwa yale niliyoyafanya, zaidi najiona kama shujaa kwa kuweza kulipa kulipa kisasi cha damu kufidia maisha ya ndugu zangu waliouawa mikononi mwa mashetani hawa. Nahitaji kwenda kuungana na familia yangu kuzimu tukapumzike. Nihukumu kunyongwaaa! Nataka kufa! Mungu ibariki kazi ya mikono yangu! Amen.”

Mahakama yote ililipuka kwa vilio na makelele ya watu waliokuwa wakimsikitikia kijana yule na kuanza kushinikiza aachiwe huru. Watu wote walikumbwa na taharuki na kugubikwa na wingu zito la sintofahamu. Kwa ushuhuda ule mfupi alioutoa, hata wale ambao walikuwa wakimuona kama muuaji na gaidi hatari walianza kumuonea huruma.

Kila mmoja alionekana kusononeka sana moyoni, hata polisi waliokuwa wamejaa mahakamani mle kila mmoja alionekana kuingiwa na simanzi huku wakijitahidi kuonyesha ukakamavu wao kwa kuyazuia machozi. Hakuna aliyeonekana kuwaonea huruma watu waliokuwa wameuawa mikononi mwa kijana yule, kila mmoja aliunga mkono alichokifanya hata kama ilikuwa ni kinyume na sheria za nchi lakini kwa waliyoyafanya wote walistahili kufa.

Hali ilitisha. Kelele zile na maombolezo ya watu waliokuwa wakisikiliza kesi ile vilimtisha jaji mkuu ambaye sasa utulivu ulimuisha. Ni kweli kabisa kuwa kijana yule alikuwa na hatia kubwa mbele ya sheria na vithibitisho vyote vya kumtia hatiani vilikuwepo, lakini sababu zilizomfanya kuua ndizo zilizoifanya kesi ile kuonekana kuwa ngumu sana.

Jaji mkuu alikuwa akihaha kutafuta msaada kutoka kwa wazee wa baraza kuu la mahakama ili kujua nini kifanyike. Tai aliyokuwa ameivaa ilionekana kuwa mzigo kwake, akaivua na kuiweka juu ya meza huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Koti maridadi la suti alilokuwa amelivaa lilionekana kuwa mzigo pia, akalivua na kuliweka nyuma ya kiti alichokuwa amekalia.

Baada ya vuta nikuvute iliyoendelea kwa muda mrefu, hatimaye Jaji mkuu aliamua kusoma hukumu. Watu wote wakawa kimya kutaka kusikia hukumu ya mwisho ambayo jaji mkuu Profesa Kadir Mudhihir Simba angeitoa.
Profesa Kadir Mudhihir Simba ni hakimu mwenye uzoefu wa siku nyingi katika medani ya siasa. Alikuwa na ujuzi na utaalamu wa kutosha katika kutoa hukumu za kesi ngumu, kesi zilizoonekana kushindikana au zenye utata. Watu wote walimwamini kwani mara zote hukumu alizokuwa anazitoa zilikuwa ni zenye kuzingatia sheria na haki. Uwezo wake mkubwa wa kuchambua mambo kwa kina na busara alizokuwa nazo, vilimfanya ateuliwe kuwa jaji mkuu miaka kumi na mbili iliyopita.

Pamoja na sifa hizo zote alizokuwa nazo, kesi hii ilionekana kumchanganya sana kichwa chake na kumkosesha sana raha kiasi cha kumfanya asite kutoa hukumu. Upelelezi ulishakamilika muda mrefu kwani mshtakiwa alijisalimisha mwenyewe mikononi mwa polisi akiwa na vithibitisho vyote vya namna alivyofanya mauaji hayo makubwa na ya kutisha.

Hakukuwa na sababu yoyote ambayo ingezuia hukumu kutolewa siku hiyo, Lakini bado jaji mkuu alionekana kupoteza mwelekeo. Alitamani aiahirishe kesi ile mpaka siku nyingine, lakini alihofia kupoteza heshima ambayo alijijengea kwa raia. Sasa aligundua ni kwa nini mahakimu wote saba walioteuliwa kuisikiliza kesi ile walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho.

Aligeuza shingo kumtazama mshtakiwa, kisha wazee wa mahakama na mwisho umati uliokuwa umeijaza mahakama ile. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kazi miaka mingi iliyopita, aliuhisi ugumu uliokuwa mbele yake. Japokuwa alikuwa amevaa miwani, macho yake yalionyesha dhahiri jinsi alivyokuwa akibabaika. Usingeweza kuamini kuwa huyu ndio yule jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba wa siku zote.

Ni kweli kabisa kwamba kuua, kwa kukusudia au bila kukusudia ni kosa kubwa mbele ya sheria, lakini sababu zilizomfanya kijana huyu mdogo kufanya mauaji makubwa kiasi kile ndilo swala lililoleta ugumu.

Jasho lilianza kumtoka kiasi cha kuamuru madirisha yote yafunguliwe na viyoyozi vyote vya mle mahakamani viwashwe. Baada ya kubabaika kwa muda mrefu, hatimaye alipiga moyo konde na kuanza kutoa hukumu.
“Kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi ya mwaka 1962, ibara ya kwanza ya makosa dhidi ya ubinadamu, kifungu kidogo cha kwanza,umepatikana na hatia ya kuua idadi kubwa ya watu kwa kukusudia. Baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa dhidi yako, Una..unahukum… unahu……ku……mi……w……”

Hakuna aliyeamini kilichotokea! Jaji mkuu alianza kubabaika na kushikwa na kigugumizi kikali huku jasho jingi likimtoka kama maji. Mwili wote ulikuwa umeloanishwa kwa jasho na sasa akawa anatetemeka mwili mzima. Alijitahidi kujikaza ili aendelee kusoma hukumu lakini alishindwa. Watu walikuwa wamepigwa na butwaa wakiwa wanashangaa kilichomsibu jaji yule. Alizidi kutetemeka mwili mzima na kuazna kuzitupa hovyo karatasi za jalada la hukumu na mara akadondoka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekaa mpaka chini, kisha akawa anaporomoka kwenye ngazi. Hakika hii ilikuwa kali ya kufunga mwaka.

Ungeweza kudhani kama yanayotokea mle mahakamani ni viini macho au miujiza, lakini haikuwa hivyo. Akiwa pale chini alianza kutupa mikono na miguu huku povu lililochanganyikana na damu likimtoka puani na mdomoni. Ungeweza kuhisi anataka kukata roho. Umati wote wa watu waliokuwa mle mahakani , ulipigwa na bumbuwazi kwa mshtuko mkubwa walioupata. Ilibidi makarani wa mahakama wafanye kazi ya ziada kwa kusaidiana na watu wa huduma ya kwanza.

Waliwahi kumuinua pale chini na kumkimbiza nje akiwa juu ya machela, na muda mfupi baadae gari la wagonjwa likawa linakimbia kwa mwendo wa kasi kumuwahisha Hospitali. Mtuhumiwa bado alikuwa ametulia kizimbani na yeye akiwa amepigwa na bumbuwazi kwa yale yaliyokuwa yametokea.

Watu wakaanza kukanyagana kila mmoja akitaka ashuhudie kinachoendelea nje ya mahakama. Askari waliokuwa wamejaa mle mahakamani walifanya kazi ya ziada kuhakikisha mtuhumiwa anarudishwa gerezani. Eneo lote likazingirwa na taharuki huku hali ikiwa tete na ya kuogopesha. Polisi walifanya kazi yao kikakamavu na kuhakikisha hakuna madhara makubwa yanayotokea pale mahakamani.

Muda mfupi baadae habari kutoka Hospitali kuu ya Blaziniar zilieleza kuwa hali ya afya ya jaji Mkuu Profesa Kadir Simba ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadri muda ulivyokuwa ukienda. Kwa mujibu wa Daktari mkuu Shyroze Mahiza aliyoitoa kwa vyombo vya habari, jaji mkuu alikuwa amepatwa na mshtuko wa moyo na kusababisha mishipa ya damu iliyoko kichwani kupasuka na kuvujisha damu kwenye ubongo.

Kitaalamu hali hii iliitwa “Venule Rapture due to Hypertension BP”, na husababisha mtu kupoteza fahamu kwa muda mrefu. Hayo ndiyo yaliyokuwa yamemtokea jaji Simba kwani aliendelea kuwa katika hali ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu sana.

Kila aliyemfahamu alimuonea huruma kwa yaliyompata na kila mtu akawa anajiuliza nini kimesababisha hali kama ile itokee. Kila mtu aliongea lake kwani jambo kama hilo halikuwahi kutokea hata mara moja katika historia ya nchi. Wengine waliliona kama muujiza huku wengine wakilihusisha na imani kali za kishirikina. Hali hiyo ilizua hamu na shauku ya watu kutaka kufahamu yule kijana mdogo ni nani na alikuwa ameendesha mauaji yake kwa sababu gani na katika mazingira gani. Uchunguzi wa kina ukaanza kufanywa ili kuupata uhalisia wa kesi ile.

MANY YEARS AGO-MIAKA MINGI ILIYOPITA
Khalfan Mwalukasa alikuwa ni mzaliwa wa mkoa wa Nyanda, uliopo kusini mwa nchi ya Blazinia. Alikuwa ni mtoto wa kipekee katika familia yao, na akiwa bado kijana aliamua kuondoka nyumbani kwa wazazi wake na kwenda kujaribu kutafuta maisha katika nchi jirani ya Tanzania. Hata hivyo alipofika Tanzania aligundua kuwa maisha yalikuwa magumu zaidi kuliko kwao Blazinia.

Alichokifanya aliamua kwenda kwenye visiwa vya jirani vilivyokuwa vikipakana na nchi yake, visiwa vya Banaland vilivyokuwa katika bahari ya Hindi. Visiwa hivi vilikuwa ni sehemu ya nchi yake hivyo hakukuwa na haja ya kuwa na Passport au viza ya kusafiria. Ilimgharimu kiasi kidogo tu cha pesa kupanda meli na siku chache baadae akawa tayari ndani ya visiwa vya Banaland.

Kwa kuwa kilichomtoa kwao na kukimbilia ugenini ilikuwa ni kutafuta ahueni ya maisha , hakutaka kuchagua kazi kwani hata hivyo hakuwa amejaaliwa kusoma kutokana na wazazi wake kuwa na hali duni ya kimaisha. Alijiwekea dhamira ya kufanya kazi yoyote ambayo ingepatikana ilimradi tu imuingizie kipato. Bahati nzuri alipata kazi ya kuuza genge la mbogamboga na matunda.

Moyo wa kujituma, heshima kwa wakubwa na wadogo na busara alizokuwa nazo vilimfanya aweze kuishi kwa amani japokuwa alikuwa mbali na wazazi wake. Muda mfupi baadae alifanikiwa kufungua biashara yake mwenyewe na akaanza rasmi kujitegemea. Alifanikiwa kupanga chumba kimoja mitaa ya uswahili na taratibu akaanza kutengamaa kimaisha.

Mara zote alikuwa akijikumbusha kuwa kilichompeleka pale ilikuwa ni kutafuta maisha, aliahidi kufanya kila alichoweza ili afanikiwe maishani ikiwa ni pamoja na kujiepusha na mambo ambayo alihisi yangezuia ndoto zake.

Baada ya takribani mwaka mmoja kupita, alikuwa ameshajijengea jina miongoni mwa wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda. Aliipenda kazi yake, na faida ndogo aliyokuwa akiipata alikuwa akitumia vizuri na kujiwekea akiba. Wateja wake wengi walikuwa ni wanawake lakini kwa kuwa alikuwa akifahamu alichokuwa anakifanya, hakujihusisha nao zaidi ya uteja wa kawaida.

Miongoni mwa wateja wake, alikuwepo binti mmoja aliyekuwa na asili kama ya mchanganyiko wa damu mbili tofauti. Alionekana kuwa na mchanganyiko wa kibantu na watu wa visiwa vya ushelisheli. Mchanganyiko huu ulimfanya awe na mvuto wa kimahaba kuliko wasichana wengine wa rika lake.

Miriam, tofauti na wateja wengine, alikuwa akipenda sana kupiga stori na Khalfan Mwalukasa. Hata baada ya kuhudumiwa kila alichokuwa akihitaji, bado alikuwa akifurahia kuendelea kuongea na Khalfani bila kujali kama alikuwa akichelewa nyumbani kwao.

Japokuwa alishindwa tu kueleza wazi hisia zake, Miriam alitokea kumpenda Khalfani Mwalukasa lakini alishindwa kumwambia bayana kwa hofu ya kueleweka vibaya. Akawa anaendelea kuumia mtimani siku hadi siku huku akijitahidi kumuonyeshea kwa vitendo kuwa alimhitaji awe baba wa watoto wake. Khalfani Mwalukasa alishaelewa kilichokuwa mawazoni mwa mteja wake Miriam, lakini hakutaka kuwa na papara hasa ukizingatia kilichompeleka kule ilikuwa ni kutafuta maisha na sio mapenzi.

Pamoja na kujifanya mgumu, Khalfani naye alijikuta taratibu akianza kuvutiwa na urembo wa binti Miriam aliyekuwa na haiba ya kike haswaa…mrefu kama twiga, uso wake wa duara ukiwa umepambwa na macho madogo ambayo muda wote yalikuwa kama yana usingizi, huku sura yake ikiwa imejawa na tabasamu tamu muda wote. Taratibu alijikuta uzalendo ukimshinda na mara wakajikuta tayari wamezama kwenye dimbwi la mahaba.

“Khalfani hivi kweli utanioa? Au ndio unataka kunitumia mwisho uniache niteseke?”
Miriam alikuwa akimuuliza huku sauti yake ikwa imejawa na huba.
“Ningependa uwe wangu wa maisha Miriam, lakini hali yangu nadhani we mwenyewe unaiona…itakuwa ni maajabu kwa muuza mboga kumuoa mtoto wa milionea kama wewe, haitawezekana”

Khalfani alikuwa akijitetea mbele ya Miriam, lakini baada ya mazungumzo marefu, Miriam alimtoa wasiwasi kuwa yeye hakuhitaji chochote kutoka kwake, zaidi ya kumhitaji awe baba watoto wake bila kuzingatia hali yake ya kimaisha wala kipato.

Moto wa mapenzi ukaanza kukolea kwenye mioyo ya wawili hawa na baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu, hatimaye Miriam alimpeleka “mumewe mtarajiwa” kumtanbulisha kwa wazazi wake. Miriam alikuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, Mzee Nurdin Shamsi na mkewe. Walibarikiwa kuwa na maisha mazuri ya kitajiri, utajiri ambao ulitokana na biashara aliyokuwa anaifanya mzee Nurdin Shamsi ya madini ya Ruby. Alikuwa akinunua Ruby kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisafirisha mpaka nchi za uarabuni (U.A.E). Biashara hiyo ilimuingizia pesa nyingi sana zlizomuwezesha yeye na familia yake kuwa na maisha ya juu.

Alifanikiwa kujenga nyumba nzuri ya kifahari pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi alikokuwa akiishi na familia yake. Alinunua pia eneo kubwa kuzunguka nyumba yake, alilolipendezesha kwa bustani nzuri za maua, viunga vya minazi na karafuu. Eneo zima lilikuwa likipendeza mithili ya Edeni ndogo.

Baada ya kutambulishwa kwa wazazi wa Miriam, Khalfani Mwalukasa aliendelea kuonyesha nidhamu na heshima ya hali ya juu kwa kila mtu, hali ambayo iliwavutia sana wazazi wa Miriam na kuwafanya wamkubalie kwa moyo mkunjufu kumposa binti yao.

Baada ya kutoa posa, taratibu za ndoa zilianza kuandaliwa na siku chache baadae Khalfan Mwalukasa akawa mume halali wa Miriam Shamsi. Wakayaanza maisha mapya ya ndoa. Kwa kuwa umri wa mzee Shamsi na mkewe ulikuwa umekwenda, na Miriam ndio alikuwa mtoto wao pekee, kitendo cha yeye kuolewa na kwenda kuishi kwa mumewe kiliwafanya wawe wapweke sana. Ikabidi mzee Shamsi amshawishi Khalfan Mwalukasa na mkewe wahamie katika jumba lao la kifahari ili waendelee kuishi wote pamoja. Khalfani alijadiliana na mkewe na wakakubaliana kuhamia nyumbani kwa kina Miriam (Ukweni).

Khalfani akayaanza maisha mapya ndani ya jumba la kifahari, maisha ambayo hakuwahi kuyaota. Alikuwa amebadili sana mazingira, kutoka kuwa muuza mboga na matunda akiishi uswahilini, mpaka kuwa mume wa binti tajiri akiishi ndani ya paradiso ndogo. Alimshukuru Mungu wake na kuahidi kuwa atampenda mkewe kwa moyo wake wote.

“Daima nitakuenzi mke wangu, na kamwe sitakufanya utoe machozi ya uchungu, bali utatoa machozi ya furaha”
Khalfan alikuwa akimpa maneno matamu ya huba mkewe jioni moja wakiwa wameketi kwenye moja ya bustani nzuri zilizokuwa ndani ya kasri la mzee Shamsi. Ndoa yao changa ikatawaliwa na upendo na mahaba ya dhati.

Kwa jinsi wazazi wa Miriam, Mzee Shamsi na mkewe walivyokuwa wakimpenda mkwe wao, ilibidi wamshawishi Khalfani pamoja na mkewe Miriam wahamie nyumbani kwa Mzee Shamsi. Mzee Shamsi na mkewe hawakuwa na mtoto mwingine zaidi ya binti yao Miriam, hivyo kuondoka kwake na kumfuata mumewe, kuliwafanya wabaki wapweke sana kwenye himaya yao.

Khalfan na mkewe hawakuwa na kipingamizi chochote, wakakubali kuhamia nyumbani kwa mzee Shamsi, (Ukweni). Maisha yao yakazidi kuwa mazuri siku baada ya siku, na sasa Khalfan akawa ameachana na biashara yake ya mboga mboga na matunda.

Badala yake akawa akimsaidia mzee Shamsi kwenye shughuli zake za Biashara ya madini ya Ruby. Muda mwingi akawa akitembezwa kwenye gari ndogo aina ya “Mercedes Lexus 5 New Model” ya kisasa, akimwonyesha vitega uchumi vyake na kumwelelekeza jinsi ya kuhudumia mali zote walizokuwa nazo.

Kwa kifupi mzee Shamsi alimuamini sana Khalfan, kiasi cha kumchukulia kama mwanae wa kumzaa. Hakumficha kitu chochote, alikuwa akimpa mpaka siri zake za ndani. Aliamini kuwa kwa kuwa hakubahatika kupata mtoto wa kiume, basi khalfan ndio atakuwa mrithi wa mali zake zote akishirikiana na mkewe Miriam.

Alichokuwa akimsisitiza siku zote ni kumpenda kwa dhati mkewe, mtoto wao wa pekee Miriam. Alikuwa akimuonya pia kuwa makini sana na marafiki wa kibiashara ambao atakuwa akishirikiana nao hususani kwenye bashara ya madini kwani akili za mwanadamu hubadilika sana akiona vitu vya thamani. Nasaha alizokuwa anapewa kila siku zilimjenga upya kifikra na kumpa ujasiri kuliko ilivyokuwa mwanzo. Alijiona anaweza kufanya mambo makubwa hata kama hakuwa na elimu kubwa kichwani

Ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi, Miriam akiwa anamuandalia mumewe Khalfan kifungua kinywa, huku wakitaniana utani wa mume na mke! Kila mmoja alikuwa na furaha kuwa na mwenzake. Wakawa wakitaniana na kucheza kama watoto huku Miriam akiendelea kuandaa kifumgua kinywa.

Wakati hayo yakiendelea taarifa ya habari iliyokuwa inasomwa kutoka kituo maarufu cha redio, “The Bulletin FM” iliwashtua wote kiasi cha kufanya kila mtu aache alichokuwa anakifanya na kukimbilia jirani na redio ili asikie vizuri taarifa ile.

Ilikuwa ni habari mbaya ya ajali ya kutisha ya ndege iliyotokea muda mfupi uliopita. Ajali hiyo ilihusisha ndege ya kampuni ya “TRY EMIRATES” aina ya Jet B710 Sossoliso, iliyokuwa inatoka uwanja wa kimataifa wa Blazinair International Airport (BLIA) kuelekea Muscat Oman. Habari ilizidi kuelezea kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika moja ya injini zake, hali iliyosababisha ndege hiyo kulipuka muda mfupi baada ya kuruka, kisha ikaangukia baharini.

Kilichosikitisha ni kwamba abiria wote 67 waliokuwemo kwenye ndege walikuwa wakihofiwa kupoteza maisha katika ajali ile. Habari ilihitimishwa kwa mahojiano na watu walioshuhudia ajali ile ambapo kila aliyehojiwa alikiri kuwa hakuwahi kusikia wala kushuhudia ajali mbaya kama ile.

Khalfan na mkewe walibaki wakikodoleana macho, wasijue nini cha kufanya. Kilichowashtua ni kwamba ni asubuhi ya siku hiyo masaa machache tu yaliyopita walitoka kuwasindikiza mzee Shamsi na mkewe uwanja wa ndege, wakielekea oman kupeleka biashara yao ya madini ya Ruby.

Haikuwa kawaida kwa mzee Shamsi kusafiri na mkewe, kwani mara zote yeye aliposafiri mkewe alibaki kuwa msimamizi wa mali zao, lakini baada ya binti yao kuolewa na Khalfan Mwalukasa, shughuli zote za usimamizi wa mali zilibaki kuwa chini ya uangalizi wa Khalfan kwani walimchukulia kama mtoto wao, na kwa pamoja walikubaliana kuwa yeye ndiye atakayekuwa mrithi wa mali zao, pindi mauti yatakapowafika.

Ni masaa mawili tu yaliyopita majira ya kama saa mbili za asubuhi Khalfan na mkewe waliwasindikiza wazazi wao uwanja wa ndege na wakasubiri mpaka walipopanda ndege ya kampuni ya usafiri wa anga ya TRY EMIRATES tayari kwa safari ya Oman. Ni baada ya kuhakikisha kuwa wamepanda ndege, ndipo Khalfan na mkewe waliporudi nyumbani kuendelea na shughuli zao.

Wakiwa wanajiandaa kupata kifungua kinywa ndipo taarifa ya kusikitisha na kutia majonzi iliposikika. Hiyo ilimaanisha kuwa mzee Shamsi na mkewe walikuwa wamepoteza maisha katika ajali ile. Msiba mkubwa kiasi gani. Habari ya ajali ile iliwashtua watu wengi, ambao kwa namna moja au nyingine waliwapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao waliokuwemo kwenye ndege ile.

Kwa Khalfan Mwalukasa, licha ya ukweli kwamba aliguswa na vifo vya wakwe zake, hii ilikuwa ni kama bahati ya mtende kuota jangwani, waswahili wanasema kufa kufaana. Ni Khalfan huyu huyu aliyekimbia kwao kutokana na ugumu wa maisha, akawa akifanya biashara ya mbogamboga na matunda, ndiye sasa alitakiwa kuwa mmiliki wa hazina ya utajiri ulioachwa na mzee Shamsi. Hakuwahi kuota wala kutegemea kuwa ipo siku atakuja kumiliki hazina kubwa ya utajiri kama ile. Kweli Mungu alikuwa ametenda miujiza katika maisha yake.

********

Siku ziwaka zinakwenda, sekunde, dakika, masaa! Mara usiku, mara mchana… mawio na machweo. Kumbukumbu ya kuwapoteza wazazi mzee Shamsi na mkewe taratibu ikaanza kupotea vichwani kwa Khalfan na mkewe Miriam. Khalfan akawa anajitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kumliwaza mkewe na kumfaya asahau yote yaliyotokea. Yeye ndiyo akawa baba na kichwa cha familia.

Mwanzoni ilimuwia vigumu kuweza kusimamia mali zote zilizoachwa na mzee Shamsi lakini kila alipokuwa akikumbuka mawaidha aliyokuwa anapewa na mzee Shamsi, akawa anajipa moyo kuwa hakuna lisilowezekana. Taratibu akawa anapata uzoefu kila siku mpya ilipokuwa ikianza. Hali hiyo ilionekana kumfariji sana mkewe, ambaye sasa akawa na uhakika kuwa kila kitu kitaendelea vizuri na kushamiri japokuwa alikuwa amepoteza wazazi wake.

Khalfan akawa anajituma kwa bidii kuhakikisha kuwa hakuna kinachomshinda.
Baada ya miezi saba tangu mzee Shamsi na mkewe wapoteze maisha katika ajali mbaya ya ndege, Miriam akiwa anarudi kutoka hospitali alikuja na habari njema kwa mumewe!

“Mume wangu, nafurahi kukuambia kuwa baada ya siku si nyingi nitakuzalia mtoto!”
“Unasema kweli mke wangu? Safi sana!” Khalfan akiwa haamini, alimkumbatia mkewe kwa nguvu… na hapo ndipo naye alipoelewa mkewe alikuwa anamaanisha nini. Mkewe alikuwa mjamzito, furaha iliyoje! Maisha yakawa kama ndio yameanza upya, muda wote wakawa wakicheza kama watoto, wakishinda kutwa nzima katika bustani za maua zilizokuwepo hapo nyumbani.

Muda ukawa unazidi kwenda, huku Khalfan akiwa anampeleka mkewe Clinic mara kwa mara, kuhakikisha anajifungua salama. Miezi ikawa inakatika, hatimaye miezi tisa ikawa imetimia. Bi Miriam akajifungua salama mtoto wa kiume, mzuri kama mama yake. Furaha katika ndoa yao ikawa imeongezeka mara dufu, na ikawa inazidi kuongezeka kila uchao.

Wakampa mtoto wao jina la Khaleed . “Mume wangu yaani furaha unayonipa maishani, sikuwahi kutegemea hata siku moja! Nakupenda sana mume wangu na Mungu azidi kuibariki ndoa yetu tudumu mpaka kifo kitakapo tutenganisha” Bi Miriam alikuwa akiongea kwa hisia nzito za mahaba kwa mumewe wakiwa na kichanga chao Khaleed, wakipunga upepo wa jioni.

Baada ya miaka miwili wakapata mtoto mwingine wa kiume, tofauti na kaka yake, yeye alifanana mno na baba yake. Watoto wakawa na afya njema, furaha na walipewa malezi bora.

Khalfan sasa akawa baba wa familia, mkewe Miriam naye akawa mama kama alivyokuwa akitamani siku zote. Waliyafurahia sana maisha yao. Muda mwingi walikuwa sambamba wakisaidiana kuwapa malezi bora watoto wao na kuwafundisha maadili mema. Utajiri nao ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, shamba na bustani zao za maua zikawa zinazidi kushamiri na kuwa “Evergreen” huku mazao yakistawi sana.

Wapo watu walioyahusisha mafanikio yale na imani za kishirina wakihisi kuwa huenda Khalfan Mwalukasa alikuwa akitumia nguvu za giza ili kupata mafanikio. Wapo walioanza kummezea mate wakiona kuwa hakustahili kuwa na mafanikio makubwa kama yale. Wala maneno ya walimwengu hayakuwarudisha nyuma. Walikuwa waimwamwini Mungu wao na walijitahidi kuishi vizuri na kila mtu, wakitoa misaada mingi ya kijamii kwa watu wenye shida na wanaoishi katika mazingira magumu.

Waliwasaidia pia watoto wenye shida mbalimbali hasa wale waliokuwa wakiishi kwenye mazingira magumu bada ya kufiwa na wazazi wao ama kutokana na hali duni za wazazi wao. Walijtahidi kwa kadri ya uwezo wao wote kugawana kile walichojaaliwa na Mungu kwa wale ambao hawakuwa nacho. Kadri muda ulivyokuwa unaenda wakazidi kujijengea jina na umaarufu huku kila mwenye shida akikimbilia kwao kuomba msaada.

Walifanikiwa pia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima na wale wa mitaani, na wakaamua kukipa jina la “Shamsi Memorium Orphanage” ikiwa kama kumbukumbu ya mzee wao Shamsi na mkewe waliokuwa wameshatangulia mbele za haki.
Baada ya miaka kadhaa kupita, walikuwa na jumla ya watoto watano, wazuri wenye furaha na afya njema. Khalfan sasa akiitwa “mzee” khalfan na mkewe Bi Miriam waliyafurahia sana maisha yao na familia yao. Muda mwingi walikuwa sambamba na watoto wao wakiwafundisha maadili mema . Utajiri ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, familia yao ikiwa gumzo kila kona ya mtaaa . Wengine waliendelea kuamini na kuhusisha mafanikio yale na ushirikiana , huku wengine wakiamini kwamba mzee Khalfan alikuwa amebahatisha

Lakini ukweli ni kuwa juhudi na maarifa ndivyo vilivyofanya maisha yao yawe gumzo kila sehemu . Siku zikawa zinakwenda, lakini kama walivyosema waswahili penye riziki hapakosi chuki , na ili ufanikiwe zaidi unahitaji kuishi vizuri na kila mtu ingawa huwezi kukwepa kuwa na maadui, taratibu mzee Khalfan akaanza kuhisi kuwa na maadui wasiopenda mafanikio yake, alianza kuhisi marafiki zake anaoshirikiana nao katika shughuli zake za biashara wameanza kumfanyia hila kutokana na mafanikio anayoyapata, hakukosea kabisa . Hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Wengi wa marafiki zake waliokuwa wakija kumtembelea pale nyumbani kwake walikuwa wakiyamezea mate mafanikio yake. Wengi walimwona kama hastahili kumiliki mali nyingi na za thamani kama alizokuwa nazo, wakaanza kupanga njama kila mmoja kwa wakati wake , wote wakitaka kumiliki mali zilizokuwa chini ya uangalizi wa khalfan na mkewe Bi Miriam. Hilo halikuwapa sana hofu khalfan na mkewe kwani waliamini Mola wao atawapigania kwa haki kwa kwa hakuna lolote baya walilomfanyia , wala hawakuwa na roho mbaya kwa mtu yeyote yule. Wote waliokuja kuomba misaada ya kimaisha walipewa walichohitaji kwa moyo wa ukarimu.

Ilikuwa ni kawaida ya familia yao kwenda kubarizi ufukweni mwa bahari kila mwisho wa wiki , siku za jumamosi na jumapili wakipendelea kukaa sehemu tulivu wakipunga upepo mwanana wa baharini huku wakibadilishana mawazo na kucheza na watoto wao.

Ilikuwa ni jumapili tulivu , majira ya jioni kabla ya jua halijazama… Khalfan na mkewe walikuwa wakirudi kutoka ufukweni walikokuwa wamekwenda kubarizi pamoja na watoto wao . Bi Miriam ndiye aliyekuwa akiendesha gari huku mumewe akiwa amekaa pembeni yake na watoto wakiendelea kucheza siti ya nyuma , baada ya muda mfupi wakawa wamefika kwenye geti la kuingia kwenye himaya yao . Bi Miriam alipiga honi mfululizo na mlinzi akatoka mbio kuja kuwafungulia.

Baada ya mlinzi kufungua mlango Bi Miriam aliingiza gari mpaka sehemu ya maegesho , akashuka na kumfungulia mumewe mlango naye akashuka kisha wakawashusha watoto wao. Kwa muda wote huo mlinzi alikuwa amesimama pembeni yao akionekana kuwa na jambo alilotaka kumwambia bosi wake, mzee Khalfani. Alisubiri wamalize kushushana ndipo ampe ujumbe aliokuwa amepewa muda mfupi uliopita kabla hawajarudi .

Khalfan aligundua kuwa mlinzi hayuko katika hali ya kawaida ikabidi amsogelee palepale alipokuwa amesimama . Mlinzi alitoa ujumbe aliokuwa amepewa na kumkabidhi mzee Khalfan, ilikuwa ni bahasha ya ukubwa wa kati iliyokuwa imefungwa vizuri. Nje ya bahasha ile hakukuwa na anuani wala jina la mtu aliyetumiwa , ila yalisomeka maandishi makubwa ya wino mwekundu “SIRI”.

Kilichomshtua khalfan ni jinsi mlinzi alivyokuwa na hofu wakati akimkabidhi ujumbe ule, alijaribu kumhoji juu ya mtu aliyeileta barua ile lakini akawa anamjibu kwa kubabaika. Alieleza kuwa muda mfupi uliopita gari ndogo nyeusi na ya kifahari ikiwa na vioo “TINTED” vya rangi nyeusi iliwateremsha wanaume wawili waliovalia makoti marefu meusi na kofia kubwa zilizoficha sura zao, mmoja akaenda mpaka pale mlangoni na mwingine akawa amebakia kwenye gari.

“Bila hata salamu akanipa bahasha na kusema nikupe wewe ukirudi!” Aliendelea kueleza mlinzi. Khalfan hakutaka kuhoji zaidi, akachukua ile bahasha na kuingia nayo ndani. Muda huo mkewe alikuwa ameshatangulia ndani na watoto akawa anaendelea kuwaandalia chakula cha jioni. Akapitiliza mpaka chumbani na kwenda kuifungua bahasha ile.

Alijikuta mikono ikianza kutetemeka alipoanza kuifungua bahasha ile akakutana na maandishi ya wino mwekundu ambayo yalisomeka vizuri. Ulikuwa ni ujumbe uliojaa vitisho na maneno ya kibabe, ukimtaka eti ‘ahame hapo nyumbani kwake yeye na familia yake yote bila kuchukua kitu chochote kwa sababu yeye Khalfan hakuwa mmiliki halali wa eneo hilo. Ujumbe ule ulizidi kutishia kwamba wanampa siku saba za kuwa ameshaondoka na onyo kali likatolewa kuwa asijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote kwa kuwa kwa kufanya hivyo angehatarisha uhai wake.’

Alijikuta akicheka kwa dharau na kisha akatoka na ile bahasha mpaka sebuleni alikokuwa amekaa mkewe na watoto wake wakiangalia luninga. Mkewe alishtuka kumuona mumewe ameanza kubadilika, ingawa usoni alikuwa akicheka lakini alionekana kuchanganyikiwa sana akampa ule ujumbe ili na yeye ausome.

“Unatakiwa uhame hapo unapoishi wewe na familia yako bila kuchukua kitu chochote. Huna haki ya kumiliki eneo zuri kama hilo, wamiliki halali tupo na tulikuwa tunangoja muda ufike tukuambie.

Usijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote , polisi wala jeshini kwani kwa kufanya hivyo utahatarisha usalama wako na hizo takataka zako (mkeo na watoto) unapewa siku saba za kutekeleza amri hii na ukiipuuza utaona matokeo yake”

NB. Uhai hautafutwi ila mali zinazotafutwa
By
Wamiliki

Bi Miriam alishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kuisoma, huku akiwa amepigwa bumbuwazi asijue nini cha kufanya. Kwa muda wote huo Khaflan alikuwa akizunguka-zunguka pale sebuleni akiwa haelewi anatafuta nini . watoto walikuwa hawana habari wakawa wanaendelea kucheza na kuruka kwenye masofa ya kisasa yaliyokuwepo pale sebuleni.

Khaflan alirudia kuisoma barua ile kisha akatoka kwa kasi kumfuata mlinzi nje. Alianza kumhoji upya ni nani aliyeleta ujumbe ule na mlinzi akarudia maelezo kama aliyoyatoa mara ya kwanza. Safari hii alionekana kuhofia zaidi baada ya kumuona bosi wake amechanganyikiwa.

Hakujua mle ndani mliandikwa nini lakini kwa hal aliyokuwa nayo bosi wake ilionyesha kuna jambo baya. Mzee Khalfan alirudi ndani na kumuelekeza mkewe awape chakula watoto haraka kisha akawalaze . Alipitiliza mpaka chumbani na kujitupa kitandani kama mzigo.

Maswali mengi yalikuwa yakipishana kichwani kama umeme wa gridi ya taifa . Alijalibu kuwaza na kuwazua ni akina nani walioleta ujumbe ule, hakupata jibu. Muda mfupi baadae mkewe akawa ameshamaliza kuwapa chakula wanae na akaenda kuwalaza kwenye chumba chao. Ama kwa hakika usiku huo ulikuwa ni usiku wa mauzauza kwao. Mpaka jogooo la kwanza linawika kuashiria mapambazuko, Khalfani na mkewe walikuwa hawajapata hata tone la usingizi.

Usiku kucha walikuwa wakijadiliana wafanye nini, hakuna aliyekuwa na jibu. Mwisho wakafikia uamuzi wa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi ingawa barua ile iliwaonya vikali juu ya uamuzi huo.
“Lakini mume wangu , si ni bora tuondoke tu tuwaachie wafanye wanachotaka ? nahofia usalama wa wanangu, tuondoke tu Mungu atatusimamia huko tuendako kwani mali hutafutwa lakini uhai hautafutwi.”
Wazo hilo halikuingia akilini mwa mzee Khalfani, kwani kufanya hivyo kungemaanisha yeye ni mwanaume dhaifu asiyeweza kuilinda familia yake aliamua kutetea msimamo wake.

”Mke wangu siko tayari hata kwa mtutu wa bunduki kuruhusu watu wengine wayaharibu maisha yetu! niamini nitafanya kila niwezalo kukulinda mke wangu na wanangu na mali zangu zote! Hakuna wa kuchukua chochote kutoka mikononi mwetu, siwezi kusalimu amri kirahisi namna hii, niamini…”

Kwa jinsi alivyokuwa akiongea kwa kujiamini, mkewe akapata imani kuwa usalama wao utalindwa kwa kila namna. Kulipopambazuka tu, mzee Khalfani na mkewe wakaanza kujiandaa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Blazinia Central Police Post”.

Walichukua barua ile kama ushahidi wa maelezo yao. Mzee Khalfan aliendesha gari lao huku mkewe akiwa pembeni yake. Hakuna aliyemsemesha mwenzake! Kila mtu alikuwa kwenye lindi zito la mawazo, maneno ya barua ile yalikuwa yakijirudiarudia vichwani mwao.
*******

Kulipopambazuka tu, Khalfani na mkewe wakaanza safari ya kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kikuu cha polisi cha Blazinia “Blazinia Central police post”. Walienda na barua ile waliyoletewa kama ushahidi wao. Dakika chache baadae walikuwa wameshafika kituoni na wakashuka na kuingia ndani mpaka kaunta ambapo waliomba kukutana na mkuu wa kituo. Muda mfupi baadae wakawa ndani ya ofisi ya mkuu wa kituo, Luteni Lauden Kambi, aliyekuwa akifahamika kwa jina la utani kama “Luteni Fuvu” kutokana na ukatili wake.

Mzee Khalfan alianza kueleza kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na Luteni akawa anaandika kila kitu kwenye faili jeusi. Alipomaliza kueleza, Luteni Lauden Kambi aliwajibu kwa kifupi kuwa waende nyumbani kwao baada ya kuacha maelezo yote ya msingi ya mahali na mtaa wanakoishi, jeshi litawapa ulinzi baada ya siku hizo saba kupita. Aliwatoa hofu kuwa vile ni vitisho vya kawaida ambavyo vinahitaji ujasiri kuweza kukabiliana navyo. Aliwapa pia maelezo kuwa warudi siku ya sita hapo kituoni ili waambiwe nini cha kufanya. Baada ya kuridhika na maelezo waliyopewa, Khalfan na mkewe waliaga na kurudi nyumbani kwao wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa msaada na jeshi la polisi

Siku zikawa zinasonga mbele kwa haraka mno, mara ikafika siku ya sita…yakiwa yamesalia masaa Ishirini na nne tu kabla ya siku ya mwisho waliyoambiwa kuwa wanatakiwa wawe wameondoka katika eneo lile, siku ya Jumapili. Hawakuwa na wasiwasi tena wakiamini wako salama wa kuwa walishahakikishiwa kuwa watapewa ulinzi. Walichokifanya ni kwenda kutoa ripoti Polisi siku moja kabla, yaani Jumamosi Kama walivyokuwa wameelekezwa na mkuu wa kituo cha polisi, Luteni Lauden kambi “Fuvu”.

Wakajitayarisha kwa safari ya kwenda tena Blaziniar Central Police post wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa ulinzi. Safari hii gari lao liliendeshwa na Bi Miriam huku Khalfan akiwa ametulia siti ya pembeni. Walipofika waliomba tena kuonana na Mkuu wa kituo. Yule Askari aliyekuwa pale kaunta aliwapa taarifa kuwa Mkuu wa kituo ameanza likizo yake ya mwezi mzima kuanzia siku ya Ijumaa, yaani jana yake na kwa muda huo alikuwa ameshasafiri kurudi kwao alikoenda kuimalizia likizo yake.

Alizidi kuwaambia kuwa shughuli za ukuu wa kituo alikuwa amepewa mtu mwingine ambaye naye alikuwa safarini kikazi. Maelezo yale yalionekana kuwachanganya mno Khalfan na mkewe. Yale matumaini waliyokuwa nayo yakawa yamepotea Kama barafu inavyoyeyuka kwenye moto mkali. Walionyesha hofu na woga waziwazi vikiambatana na kupoteza matumaini Kiasi cha kumfanya yule Askari aliyewapa taarifa ile kushtuka. “Kwani kuna tatizo gani mzee! niambieni labda naweza kuwasaidia hata kama Mkuu hayupo”

Ilibidi mzee Khalfan aanze tena kueleza upya kuanzia mwanzo. Baada ya maelezo yake
yule Askari aliwaomba waongozane mpaka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Kituo, wakatafute faili ambalo maelezo yao yalihifadhiwa pamoja ile barua waliyokuwa wameileta kama uthibitisho. Dakika chache baadae wakawa tayari ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Kituo. Yule Askari akaanza kutafuta faili lenye maelezo yao.
‘’Unasema mlikuja kutoa ripoti siku gain?” Yule askari alimhoji mzee Khalfan.
‘’Jumatatu iliyopita afande…‘’

Aliendelea kutafuta maelezo yale kwenye mafaili moja baada ya jingine.
‘’Aliweka maelezo yetu kwenye faili jeusi pamoja na ile barua’’ alizidi kusisitiza Bi Miriam huku wote wakimkodolea macho yule askari aliyekuwa akiendelea kupekua faili moja baada ya jingine. Baada ya kutafuta kwa muda mrefu karibu kila mahali, yule askari aliwageukia mzee Khalfan
na mkewe na akawaambia kuwa labda wasubiri kidogo ampigie simu bosi wake hata kama yuko likizo angewaelekeza alipolihifadhi faili lile.

Wakatoka Ofisini na kurudi kaunta ambako yule askari alinyanyua mkonga wa simu na kuanza kuongea na mkuu wa Luten Lauden Kambi. ‘’Amesema msiwe na wasiwasi, rudini nyumbani ila muache ramani ya mtaa mnakoishi, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyumba eti ameshaacha maagizo na polisi watakuja kuwapa ulinzi wa kutosha kuanzia majira ya jioni.’’

Alimaliza yule Askari kuwapa maelezo aliyopewa na Mkuu wa kituo kwenye simu. Mzee Khalfan ali shusha pumzi ndefu kisha akamgeukia mkewe, wakatazamana kwa muda kisha yule askari akawapa
Karatasi kwa ajili ya kuacha maelezo ya mahali nyumba yao ilipo, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyunba. Mzee Khalfan akaanza kuandika upya. Baada ya kuhakikisha kuwa maelezo waliyoyaacha ni sahihi mzee Khalfan na mkewe wakaaga na kuondoka.

Kengere ya hatari ilishalia kichwani mwa Khalfan, akahisi kuna mchezo mchafu unaotaka kuchezwa na askari wale askari. Iweje watoe maelezo mara ya pili ilhali walishahakikishiwa usalama wao?
Hakutaka kumwambia mkewe alichokihisi kwa kuogopa kumuongeza hofu. Wakapanda garini na safari ya kurudi kwao ikaanza safari hii pia hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake… kimya kimya
mpaka nyumbani.

Masaa yakawa yanazidi kuyoyoma, saa kumi jioni… kumi moja… kumi mbili, mara saa tatu usiku… nne tano kasoro… Hakukuwa na dalili yoyote ya polisi kufika eneo hilo kama walivyoahidiwa na Luten Lauden ‘’Fuvu”. Kwa muda wote huo mzee Khalfan alikuwa nje pamoja na walinzi wake watatu na wengine wawili aliwakodi kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa eneo zima la kuzunguka nyumba yao ili kulinda usalama.

‘’Boss! hao polisi uliosema watakuja tusaidiane nao kazi mbona hawaji na muda ndio unazidi kwenda? saa tano usiku sasa!’’ Alihoji mlinzi mmoja kwa niaba ya wenzake. Mzee Khalfan hakuwa na jibu la kuwapa, zaidi swali lile lilionekana kumchanganya akili. Tangu saa moja jioni alikuwa akiwapa darasa walinzi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bunduki wanazotumia (magobore) yako katika hali ya utayari kwa kazi muda wowote. Alihakikisha pia kuwa bastola yake aliyoachiwa na marehemu mzee Shamsi imejaa risasi za kutosha.

Wote wakawa wamejiandaa vya kutosha wakitegemea muda wowote polisi wangefika kuungana nao kuwasubiri hao wanaotaka kuwadhulumu mali zao kwa nguvu. Walijiandaa kutoa upinzani wa kutosha kwa yeyote ambaye angethubutu kuleta ujeuri wa aina yoyote ile katika eneo lile. Bi Miriam naye alikuwa amewahi kuwaingiza watoto wake ndani mapema kuliko siku yoyote. Wakawahi kula chakula cha usiku kisha wote wakaenda kulala. Alihakikisha milango yote na madirisha yamefungwa ipasavyo.

Mzee Khalfan hakutaka kuingia ndani. Alitaka ashirikiane bega kwa bega na walinzi hata kama polisi hawatafika. Walinzi walimshauri aende ndani kwani walikuwa wakijiamini kuwa wanaweza kazi. Baada ya mabishano kidogo, hatimaye mzee Khalfan alikubali kurudi ndani huku bastola yake ikiwa mkononi “standby” kwa lolote. Muda ukazidi kuyoyoma…mara saa sita usiku… Saa saba na hatimaye saa nane.

Eneo zima lilikuwa kimya kabisa huku giza nene likiwa limetanda kila sehemu. Walinzi walikuwa waki zunguka huku huko kuhakikisha hakuna mtu anayesogelea eneo lile. Bunduki zao zilikuwa “standby” mikononi wakisaidiwa na mbwa mkubwa wa mzee Khalfan. Giza lilikuwa likizidi kushamiri na kufanya hali
ya eneo lile izidi kutisha. Ilishatimia saa tisa usiku huku bado kukiwa kimya kabisa.

Ghafla zilianza kusikika kelele za mbwa aliyekuwa akibweka na kukimbilia kwenye geti kubwa la kuingilia. Walinzi wakajua mambo yameanza, kwa umakini mkubwa nao wakaanza kunyata kuelekea kule mbwa alikokuwa anakimbilia. Alizidi kubweka na walinzi nao wakawa wanazidi kusogea kuelekea kule getini. Mara walishtukia kuona mbwa akipigwa risasi nyingi kichwani kisha akadondoka chini, Puuuh! Ile milio ya risasi ilitosha kuwamaliza kabisa ujasiri wote waliokuwa nao wale walinzi, kwani ilionekana dhahiri maadui zao wamekuja na bunduki nzito za kivita.

Hawakuelewa risasi zimetokea upande gani wakawa wanaangalia huku na huko. Wakiwa bado wanashangaa walishtukia kujikuta wote wamemulikwa na tochi kali kisha mvua ya risasi ikaanza kuwanyeshea. Sekunde chache baadae walinzi wote watano walikuwa chini wakitapatapa kukata roho baada ya shambulizi la ghafla risasi zilikuwa zimepenya vichwani mwao kisawasawa.

Kelele za shambulizi lile ziliwafanya wote waliokuwa ndani ya nyumba ya mzee Khalfan kushtuka. Watoto walianza kupiga mayowe hovyo ya kuomba msaada. Bi Miriam naye alikuwa hajitambui kwa hofu. Mzee Khalfan akapiga moyo konde na kunyanyua bastola yake, akaikamata kisawasawa. Akafungua mlango wa chumbani na kuanza kutoka huku akinyata kwa tahadhari kubwa. Mkewe alijaribu kumzuia asitoke lakini wapi! Akanyatia mpaka sebuleni. Akiwa katikati ya sebule, alishuhudia mlango wa nje ukivunjwa kwa jiwe kubwa kisha watu wapatao saba, wote wakiwa wamevalia makoti marefu meusi, usoni wakiwa wamevaa vitambaa vya kuficha sura zao (masks) , mikononi wakiwa na bunduki nzito za kivita kila mtu ya kwake wakiingia kwa kasi na kumzunguka pale aliposimama…

‘’Weka silaha chini! ‘’ Mmoja wa majambazi yale alimuamuru mzee Khalfan kwa sauti ya ukali mno. Akajikuta akitetemeka mwili mzima kiasi cha kuhisi haja ndogo ikimtoka bila ya ridhaa yake. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kudondosha bastola yake chini kisha kuinua mikono juu kusalimu amri. Yale majambazi yakaanza kumshambulia kama mpira wa kona. Alipigwa na kitako cha bunduki kichwani akadondoka chini kama mzigo.

Yakaanza kumshushia kipigo cha nguvu kwa zamu zamu. Alijitahidi kujitetea lakini alizidiwa nguvu. Majambazi wengine wakaingia vyumbani na kuwatoa Bi Miriam na watoto wake wote. Kipigo kikaendelea kwa wote… hata mtoto wao mdogo wa mwisho ambaye na miaka miwili tu! Ikawa ni kichapo mtindo mmoja.

Mtoto wa kwanza wa Mzee Khalfan, Khaleed, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na miaka kumi na tatu, alifanikiwa kujificha chini ya meza kabla ya majambazi hayajamuona. Aliendelea kushuhudia jinsi baba’ake, mama’ake na wadogo zake walivyokuwa wakisulubiwa. Uchungu ulimuingia mno kiasi cha kushindwa kuvumilia. Kwa haraka alitoka chini ya meza na kunyanyua chuma kilichokuwa sakafuni, kisha akakinyanyua kwa nguvu zake zote na kukirusha kwa jambazi mmoja. Kilitua sawia kichwani kiasi cha kufanya jambazi lile lidondoke chini.

Akajikuta amedakwa juu juu kama kifaranga cha kuku mbele ya mwewe. Kisha naye akaanza kusulubiwa. Sekunde chache tu baadaye naye akawa ameloa damu mwili mzima kama wenzake. Kichapo kiliendelea mpaka wote wakawa hoi taabani. Yale majambazi yakawafunga wote kwa kamba, mikononi na miguuni na kuwajaza matambara midomoni mwao. Kisha yakaanza kuwaburuza mpaka nje ambako yalianza kuwapakiza kwenye gari yaliyokuja nayo. Yalikuwa yakiwarusha kama magunia,wakati yaiwapakia kwenye Landrover. Gari likawashwa na kuanza kuondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea kusikojulikana. Eneo zima liliachwa likiwa limetapakaa damu na maiti tano za walinzi zikiwa zimelala chini. Ukimya ukatawala eneo zima, tena safari hii kukiwa kunatisha zaidi kwani hakuna aliyekuwa amesalia akiwa hai eneo lile.

Saa kumi na nusu alfajiri gari aina ya ya landrover 110 lilikuwa likiacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi kuelekea pori la gamutu . Gari lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kubwa mno, na dereva hakupunguza mwendo wakati akikata kona kuiacha barabara ya vumbi na kuingia katikati ya vichaka. Gari lilizidi kutokomea ndani kabisa ya pori kisha likasimama katikati ya pori.

“Hebu washusheni hao wanaharamu haraka!”
Sauti ilisikika ikitoa amri kwa ukali . Lilikuwa ni gari la yale majambazi yaliyowateka mzee Khalfan na familia yake. Kutokana na kipigo walichokuwa wamekipata kutoka kwa majambazi yale yenye roho mbaya kupindukia wote walikuwa wamepoteza fahamu isipokuwa Mzee Khalfan aliyekuwa akiendelea kuguna kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyahisi baada ya kula kichapo kikali.

Kwa msaada wa tochi kubwa zenye mwanga mkali, majambazi yale yalianza kuwashusha toka garini mmoja baada ya mwingine. Mzee Khalfan ndio alikuwa wa kwanza kushushwa. “Huyu mfungeni peke yake kwenye huo mti mkubwa”

Jambazi mmoja aliyeonekana kuwa ndio kiongozi wao alitoa amri kwa sauti nzito.
“Hawa wengine wafungeni watatu kwenye miti hii miwili” Kilichofuata ikawa ni utelekezaji wa amri iliyotolewa. Kamba za katani zikaanza kufungwa kwenye mashina ya miti kisha wakaanza na Mzee Khalfan, akafuatia Bi Miriam aliyeunganishwa na kufungwa na mabinti zake wadogo wawili. Alifuatia mtoto wao wa kwanza Khaleed ambaye kwa muda wote huo fahamu zilishamrudia naye akawa akishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea . Yeye alifungwa pamoja na wadogo zake wawili kwenye mti mmoja.

Mzee Khalfan hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutokwa na machozi ya uchungu wa kuonewa kwani aliamini huo ndio mwisho wao kwani wasingeweza tena kutoka salama ndani ya pori lile. Kilichomsikitisha zaidi ni aina ya kifo kilichokuwa kinawangoja, kuwa kitoweo cha simba kabla ya mapambazuko… ilitisha.

Baada ya kumaliza kuwafunga wote, majambazi yale yalimsogelea Mzee Khalfan na kumuinua uso pale chini aliofungwa, kisha yule aliyeonekana kuwa na amri zaidi akaanza kumsemesha kwa sauti kavu na nzito iliyokwaruza.

“Pole Khalfan kwa kuwa muda si mrefu wewe pamoja na familia yao mtakuwa chakula cha simba wa Gamutu. Laiti kama ungetii amri uliyopewa, usingepatwa na balaa hili… ila ubishi wako ndio umekuponza. Kabla hujafa ningependa ujue kwamba sisi ni watekelezaji tu, hii kazi tumetumwa na wenzako mnaofany nao Biashara… The Holly Trinity wakiongozwa na swahiba wako Musa Mtaki na Pius Bagenda. Bila shaka unawafahamu vizuri kwa kuwa ni marafiki zako wapendwa. Hao ndio waliotutuma tukumalize… haa! Haa! Haa!… majambazi yale yaliangua vicheko vya dharau huku yakigongeshana vitako vya bunduki zao. Walichokifurahia ni donge nono la mamilioni ya pesa waliyoahidiwa na “The Holly Trinity” Umoja wa wafanyabiashara wakubwa watatu wakiongozwa na rafiki mpendwa wa mzee Khalfan, Musa Mtaki.

“Salamu zao kuzimu kwani hamuwezi kunusurika na mauti! msisahau kusali kabla simba hawajafika kuwatafuna…” vicheko vya kebehi vikaanza upya, kisha wakaanza kuondoka kulifuata gari lao. Muda mfupi baadaye yakawa yameshaingia ndani ya gari lao na kutoweka eneo lile kwa kasi.

Mzee Khalfan alishindwa kujizuia kutoa machozi… sasa alikuwa ameshapata picha kamili ya watu waliokuwa nyuma ya tukio lile, “The Holly Trinity”. Hawa walikuwa ni marafiki zake wa kibiashara “Business friends” wa siku nyingi aliokuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kibiashara. Kundi hilo la lilikuwa likiundwa na Pius Bagenda, Musa Mtaki na Jamal Maziku, wote wakiwa ni wafanyabiashara wa madini na vito vya thamani.

Mawazo yalianza kupishana kichwani akijaribu kuwaza na kuwazua kuwa aliwakosea nini rafiki zake hao mpaka wakafikia hatua ya kumfanyia unyama wa kiasi kile? Hakukumbuka kama alishawahi japo kuwakwaruzana na yeyote kati yao! Sasa kwa nini wafanye vile?... hakupa jibu.

Kwa muda wote huo mwanae wa kwanza Khaleed alikuwa kimya akimuangalia baba yake. Alimuonea huruma kwa jinsi alivyokuwa akisikitika. Aliyasikia pia mazungumzo ya yale majambazi na akaelewa vizuri waliohusika kuwafanyia vile kwani hata yeye alikuwa akiwafahamu vizuri sana, Mzee Mtaki ambaye licha ya kuwa alikuwa akiwatembelea mara kwa mara nyumbani kwao, pia alikuwa akisoma darasa moja na mwanae kwenye shule ya kimataifa ya St Benedict -Blaziniar wote wakiwa kidato cha kwanza. Alijikuta akiwachukia mno wote waliohusika kuwafanyia unyama ule na akajiapiza kuwa lazima aje kulipa kisasi!
“I must revenge…”

Alijikuta akifoka kwa hasira maneno yake yalimshtua baba yake aliyekuwa amezama kwenye lindi la mawazo machungu. Alishindwa kujibu kitu kwani matambara aliyojazwa mdomoni yalimpa shida ya kuzungumza. Akilini mwake alimhurumia mwanae kwani alikuwa ameshuhudiaukatili wa kutisha usiku huo, tena akiwa bado mdogo, na zaidi aliwahurumia wanae, kwani aliamini wasingeweza kutoka salama porini Gamutu. Aliamini Simba wa Gamutu wangewamaliza palepale bila ya mtu yeyote kujua . Alibaki kusali kimoyomoyo ili Mungu wao awaepushie kifo cha namna ile.
Ilikuwa imeshatimia saa kumi na moja alfajiri, giza likiwa limeanza kupungua polepole. Khaleed alikuwa akijaribu kujinasua kwa nguvu kutoka pale alipofungwa. Baba yake alikuwa akimtazama huku akimkataza kwa ishara kwani kwa kuendelea kufanya vile angezidi kujiumiza kwani kila alipojaribu kuinuka, kamba zilizopita mwili mzima zikawa zinamrudisha chini.

“Baba!... Baba!... Ona wanarudi tena”
Aliongea Khaleed akimuonyeshea baba yake upande ambao vitu kama tochi vilikuwa vikiwasogelea. Mzee Khalfan alipojigeuza kwa shida na kuangalia upande ule alioonyeshwa na mwanae Khaleed, nguvu zilimwishia kabisa akajikuta ametamka kwa sauti ya kukata tama… Mungu wangu !!

Khaleed kwa uelewa wake mdogo alidhania ni watu walioshika tochi nyingi ndio waliokuwa wakiwasogelea, lakini haikuwa hivyo! vile vilivyoonekana kama tochi yalikuwa ni macho ya Simba wa Gamutu waliokuwa wakiwasogelea. Macho ya simba yalikuwa na tabia ya kuwaka gizani kama tochi.

“shiiii…shiiii…”
Mzee Khalfan alijaribu kumzuia Khaleed asipige kelele kwani kwa kufanya hivyo ndio kuongeza hatari iliyokuwa ikiwakaribia. Sekunde chache baadae, mti aliofungwa Khaleed na wadogo zake wawili ulizingirwa na simba wapatao saba waliokuwa wakitoa ngurumo za kutisha wakionyesha meno yao makali. Khaleed hakuwahi kuwaona simba ana kwa ana zaidi ya kuwaona kwenye TV, kitendo kile cha simba wale kuunguruma kwa njaa kali waliyokuwa nayo, tena wakiwa karibu kabisa… kilimfanya Khaleed ahisi kama yuko ndotoni. Mwili wote ukafa ganzi akawa akitetemeka kupita kiasi.

Kufumba na kufumbua wale simba waliwavamia kwa kishindo kikuu na kukatakata kamba walizokuwa wamefungwa . Khaleed alijaribu kujitetea kwa kuwatisha samba lakini haikusaidia kitu. Kwa macho yake alishuhudia mdogo wake wa kwanza akiraruliwa kwa meno na makucha makali ya simba wenye njaa… akiwa bado amepigwa na butwaa , alishuhudia mdogo wake wa pili naye akiraruliwa vibaya na simba , ikabakia zamu yake…

Akili yake ilifanya kazi kwa kasi ya ajabu, akakumbuka mbinu aliyowahi kufundishwa shuleni na mwalimu wake wa somo la Biology, akajinyoosha taratibu chini na kubana pumzi kiasi cha kufanya aonekane kama amekufa. Wale Simba wakaanza kumnusa huku na huko wakijiandaa kumrarua. Akazidi kubana pumzi na kujifanya amekufa…aljitahidi mno kujibana na kweli akaweza…Simba wakahisi ni mzoga , wakamuacha palepale chini. Muda mfupi baadae alisikia wale simba wakiburuza miili ya wadogo zake na kutokomea nayo gizani. Alizidi kujibana pale chini mpaka alipohakikisha wale simba wametokomea kabisa vichakani. Eneo zima likawa limetapakaa damu. Alipoinuka na kumtazama babaake mzee Khalfan, naye alikuwa amejikausha kama amekufa huku naye akiwa amezibana pumzi zake.

Baada ya Simba kuwavamia pale chni ya miti walipokuwa wamefungwa, Khaleed anatumia mbinu kali ya kubana pumzi na kujifanya amekufa, mbinu ambayo inamuokoa kutoka kwenye shimo la mauti. Anashuhudia wadogo zake wawili wakiburuzwa na kwenda kuwa kitoweo cha simba wenye njaa. Anamgeukia baba yake ambaye naye amejikausha kama amekufa ili kukwepa kuliwa na Simba.

Alipougeukia mti aliofungwa mamaake, alimuona akiwa bado hajitambui kutokana na kipigo cha yale majambazi kilichomfanya apoteze fahamu. Wadogo zake wawili waliosalia ambao walikuwa wamefungwa pamoja na mama yao, nao walikuwa hawajitambui kwa majeraha makubwa waliyoyapata na kusababisha wapoteze damu nyingi.

Matumaini ya kunusurika yalikuwa yamefifia kabisa, kwani kwa mbali kidogo ilisikika mingurumo ya wale simba wakijichana mawindo yao. Roho ilimuuma sana Khaleed na akawa anahisi kama yuko ndani ya ndoto ya kutisha. Haikuwa ndoto…Alijikuta akishindwa kujizuia kulia kimya kimya kwa kuomboleza.

Akili yake iliacha kufanya kazi kwa muda akiwa kama mtu aliyepigwa na ‘shock’ ya umeme. Hakutaka kuamini kama yale matukio yalikuwa ni ya kweli lakini ukweli ukabaki kuwa uleule. Walikuwa wakisubiri kifo cha kuliwa na simba muda wowote.

Mara akaanza kuhisi manyunyu ya mvua yakianza kudondoka. Alipotazama angani, wingu zito la mvua lilikuwa likitanda kila mahali na kuimeza kabisa ile nuru hafifu ya alfajiri iliyokuwa imeanza kuonekana. Radi kali zikaanza kupiga na kumulika huku na kule na kufanya hali iwe ya kutisha kupita kiasi. Radi na ngurumo ziliendelea huku manyunyu yakizidi kuongezeka. Mara Khaleed akaanza kusikia tena sauti za wale simba zikisogelea pale chini ya miti walipokuwa wamefungwa.

Akawa anatetemeka akijua zamu yake imefika. Akiwa anahaha kujiokoa ndipo alipogundua kuwa zile kamba alizokuwa amefungwa kumbe zilikuwa zimekatwakatwa wakati walipovamiwa na samba kwa mara ya kwanza. Kwa haraka alinyanyuka huku miguu ikiwa inatetemeka kupita kiasi. Sauti za wale simba zilizidi kusogea jirani na sasa zikawa zinasikika mita chache tu kutoka pale walipokuwa wamefungwa. Kwa ujasiri wa ajabu, Khaleed aliinuka na akakimbilia pale alipokuwa amefungwa baba yake na kwa kasi ya ajabu akaanza kumfungua kamba alizokuwa amefungwa mwili mzima.

Radi zilizidi kuongezeka na manyunyu nayo yakawa yanaongezeka kwa kasi kuashiria mvua kubwa. Mzee Khalfan alishtuka kuona akiguswa akidhani ni wale simba wameishafika, lakini alipoinua uso alimuona mwanae Khaleed akihangaika kumfungua. Alijikuta akipata nguvu na matumaini mapya ya kunusurika na kifo kibaya kama kile.

khaleed alimtoa baba yake matambara aliyojazwa mdomoni na akawa anaendelea kumfungua kwa kasi.
‘’Kazana nwanangu! Do it hurry my son… simba wameishafika!”
Mzee Khalfan alikuwa akimhimiza mwanae kuongeza kasi ya kumfungua kwani tayari Simba walikuwa jirani kabisa.

Alipomaliza tu kumfungua, kundi kubwa la simba lilikuwa limeshafika pale chini ya miti walipokuwa. Mtu na baba yake wakabaki kutazamana wasijue cha kufanya.

‘’What can we do dad?’’
Khaleed alimuliza baba’ake kwa sauti ya kunong’ona huku akijificha nyuma yake. Ile Bunduki ilikuwa mbele yao umbali wa hatua chache, jirani kabisa na kundi la wale simba ambao walikuwa wakizidi kuwasogelea. Swali likabaki kuwa wataichukuaje ilhali simba nao ndio walikuwa wakizidi kusogea huku wakinguruma kwa sauti za kutisha.

Mzee Khalfan akiwa bado anatazamana na wale simba ana kwa ana, akili yake ikawa inafanya kazi kwa kasi ya ajabu. Wazo jipya likamjia… akakumbuka kuwa mfukoni alikuwa na kibiriti cha gesi. Akamwita Khaleed kwa ishara na kumwelekeza kitu cha kufanya. Kwa haraka Khaleed akavua shati lake na kuliwasha moto kama alivyoelekezwa, akampa babaake kisha wakaanza kusogea mbele taratibu wakiwasogelea wale simba.

Simba kuona moto ukiwasogelea, wakaanza kurudi nyuma huku wakizidi kunguruma kwa hasira . Mzee Khalfani alijikaza kiume na akawa anazidi kusogea mbele huku mwanae Khaleed akiwa anamfuata mgongoni. Walizidi kusogea mbele na wale simba wakawa wanazidi kurudi nyuma huku wakionesha meno yao makali. Walisogea mpaka walipoifikia ile bunduki iliyokuwa chini kwenye majani. Walipoifikia, Mzee Khalfani alimpa ishara Khaleed aiokote upesi wakati yeye akizidi kuushikilia moto usizimike.

Khaleed alifanya kama alivyoelekezwa. Kwa haraka aliiokota na kuishika mikononi mwake huku akitetemeka. Mvua nayo ilianza kumwagika kwa kasi na kusababisha ule moto uzimike. Wale Simba kuona moto umezimika, wakawa wanarudi kwa kasi, safari hii wakiwa wengi kuliko awali. Kwa kasi ya ajabu, Mzee Khalfan aliichukua ile bunduki kutoka mikononi mwa Khaleed na kufyatua risasi mfululizo hewani.

Hiyo ndio ikawa ponapona yao kwani milio ya risasi iliwachanganya wale simba na wakatawanyika kwa kasi na kupotelea vichakani.
Mzee Khalfan alizidi kufyatua risasi nyingi kuwafukuzia mbali wale Simba. Sekunde chache baadae eneo lote likawa kimya. Baada ya kuhakikisha kuko salama, Mzee Khalfan alimgeukia mwanae Khaleed aliyekuwa nyuma yake, wakakumbatiana kwa nguvu.

“You are a real soldier my son, grow brave-hearted! Im proud of you” (hakika mwanangu wewe ni mwanajeshi kamili, endelea kukua ukiwa na moyo shujaa kama huu! Najivunia kuwa nawe)

Mzee khalfan aliongea kwa furaha kubwa huku akizidi kumkumbatia mwanae Khaleed kwa nguvu. Japokuwa alikuwa bado na umri mdogo alikuwa shujaa mno, hali ambayo ilimshangaza hata baba yake. Mvua ilikuwa ikizidi kumwagika na kuzidi kulifanya pori la Gamutu lizidi kutisha. Baada ya kupongezana, Kwa haraka khaleed na baba yake wakaanza kupanga namna ya kuwaokoa wenzao.

Bi Miriam na wanawe walikuwa wamepoteza fahamu tangu walipotekwa na kupigwa vibaya na majambazi nyumbani kwao usiku uliopita. Baridi kali iliyokuwa ikiambatana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha alfajiri ile iliwafanya wazinduke na kurejewa na fahamu zao. Fahamu zilipomrudia Bi Miriam alianza kupiga mayowe kama aliyerukwa na akili huku akimuita mumewe.

Hakujua hapo walipo ni wapi na wamefikaje. Mzee Khalfan akawa na kazi ya ziada kumtuliza mkewe huku Khaleed naye akiwanyamazisha wadogo zake waliokuwa wakilia kwa maumivu makali wakati wakiwafungua zile kamba walizokuwa wamefungwa.

Mvua kubwa ikawa inaendelea kunyesha ikisindikizwa na ngurumo kali za radi. Ilibidi watafute sehemu ya kujificha ili wasizidi kuloana. Wakangia ndani ya pango lililokuwa chini ya mti mkubwa. Mvua ilikuwa haiingii kabisa mle ndani ya pango. Wakakumbatiana huku kila mmoja akitetemeka kwa baridi kali waliyokuwa wakiihisi. Mzee Khalfan, bunduki yake ikiwa “Standby” mkononi, alikuwa amekaa tayari tayari kuilinda familia yake endapo Simba wangerudi tena.

Wakiwa ndani ya lile Pango wakawa wakisali kumshukuru Mungu wao kwa yote. Japokuwa tayari walikuwa wameshawapoteza wenzao wawili, walimshukuru Mungu kwa kuwanusuru mpaka muda ule kwani hakuna aliyetegemea wangekuwa hai mpaka muda ule. Mvua kubwa iliendelea kunyesha mpaka kulipopambazuka kabisa. Hali ya hewa ikaanza kubadilika na kuwa shwari.

Baada ya muda, jua lilianza kuchomoza na miale yake kupenya vivuli vizito vya miti mikubwa iliyofungamana ndani ya msitu wa Gamutu. Ile mvua kubwa iliyonyesha na kuutetemesha msitu wote tangu alfajiri ikawa imekatika kabisa. Hali ya hewa ikaanza kuwa ya kupendeza huku zikisikika kelele za ndege wa kila aina waliokuwa wakiimba na kurukaruka juu ya matawi ya miti mikubwa ya pori la Gamutu wakifurahia mpambazuko ya siku mpya.

Licha ya kuwa Mzee khalfan na mkewe Bi Miriam walikuwa tayari wamewapoteza watoto wao wawili wa kike walioliwa na Simba porini Gamutu, walizidi kumshukuru sana Mungu wao kwani hakuna aliyetegemea kama wangeiona siku hiyo mpya.

Kwao ilikuwa ni kama miujiza kubaki hai mpaka asubuhi hiyo. Walikuwa wameshakata tamaa kwa yaliyowatokea usiku, lakini Mungu alitenda miujiza kwao, kitu ambacho hakuna aliyekitegemea. Pamoja na kunusurika kuliwa na simba usiku uliopita, mzee Khalfan na familia yake iliyosalia bado hawakupata jibu namna ambavyo wangeweza kutoka salama ndani ya msitu wa Gamutu.

Mzee Khalfan alipiga moyo konde na kwa ujasiri akasimama kutoka pale walipokuwa wamejificha usiku uliopita. Akamwamsha Khaleed na kumkabidhi ile bunduki aendeleze ulinzi. Alimwamsha pia mkewe Bi Miriam kisha wanae wengine, wadogo zake Khaleed. Alitaka kutoka kutafuta njia salama ya kutokea mle porini yeye na familia yake.

Alivuta taswira ya pori la Gamutu, pori ambalo alikuwa akisikia ushetani unaofanyika humo ndani kila kukicha. Hicho ndicho kilichokuwa kituo cha majambazi ambayo baada ya kufanya uhalifu hukimbilia humo kujificha mchana kutwa mpaka giza liingie. Kilikuwa pia ni kituo cha wachuna ngozi waliyoivamia Blazinia wakitokea upande wa nyanda za juu Kusini.

Pia kilikuwa kituo cha watu hatari waliokuwa wakiendesha mauaji ya Albino na kisha kuwachuna ngozi na kuwatoa baadhi ya viungo vya miili yao kwa ajili ya shughuli za kishirikina. Kama hiyo haitoshi, Gamutu pia ilikuwa ni kitovu kikuu cha biashara ya madawa ya kulevya.
Suala la mzee Khalfan na familia yake kutoka salama ndani ya Gamutu likabaki kuwa shughuli nyingine ngumu, Walitegemea muujiza mwingine utokee, wakawa wanazidi kumlilia Mungu wao kila mmoja kwa nafsi yake. Kabla hajaondoka kwenda kutafuta njia ya kutokea nje, Mzee Khalfan alitaka kuhakikisha anawaacha salama mkewe na wanae.

“Inabidi wote tujitahidi kupanda juu ya miti kwani Simba wa humu hawatabiriki, wanaweza kurudi muda wowote. Khaleed, anza kazi…
Alipomaliza tu kusema kauli ile, mara milio ya ajabu kama ile walioisikia usiku ikaanza kusikika kwa mbali. Safari hii hawakupata shida kugundua milio hiyo kuwa ni sauti za simba wenye njaa wa Gamutu. Wakaanza kuhangaika upya kupanda juu ya miti.

Haraka haraka mzee Khalfan akaanza kumsaidia mkewe kupanda juu ya mti huku Khaleed naye akijitahidi kuwapandisha wadogo zake wawili juu ya mti mkubwa. Sauti za miungurumo ya simba wenye njaa zikawa zinazidi kusogea kwa kasi kuelekea pale walipokuwa.

Hakuna aliyekuwa tayari kuona wanampoteza mwanafamilia mwingine tena, kila mmoja akawa akijitahidi kujiokoa. Khaleed kwa kwa kutumia nguvu zake zote alifanikiwa kuwapandisha wadogo zake wawili juu kabisa ya mti mkubwa.
“Jishikilieni kwa nguvu, Simba wameshafika” Khaleed alikuwa akiwahimiza wadogo zake kujishikilia vizuri wasije kudondoka.

Baba yao nae alikuwa akihangaika kumpandisha mama yao juu ya mti mkubwaq. Ilimuwia vigumu sana kumpandisha Bi Miriam juu kabisa kwani alikuwa akiteleza na kurudi chini mara kwa mara. Hatimaye nao wakawa wamepanda juu kabisa, Bi Miriam akajishikilia kwa nguvu kwenye moja ya matawi ya mti ule.

Sauti za wale simba sasa zikawa zinasikika hatua chache tu kutoka pale kwenye ile miti walipokuwepo. Katika purukushani za kujiokoa kumbe mtoto wao wa mwisho, kitinda mimba wa Bi Miriam, aitwaye Ismail alikuwa bado yuko chini. Hakuna aliyemkumbuka kwani kila mmoja alikuwa kwenye harakati za kutaka kujiokoa nafsi yake. Walikuja kushtuka baada ya kumsikia akianza kulia peke yake chini huku akimuita mama yake. Simba tayari walikuwa wameshamkaribia kabisa.

“I do it or I die…” mzee Khalfan alijikuta akijisemea mwenyewe pale juu ya mti. Aliamua kujitosa kumuokoa mwanae ama wafe pamoja naye. Ulikuwa ni uamuzi mgumu unaohitaji moyo shupavu. Akaanza kuporomoka kwa kasi ya ajabu kushuka mtini…kwenda kumuokoa mwanae Ismail. Tayari Simba walikuwa wameshafika eneo lile na kumzunguka Ismail huku wakinguruma kwa sauti za kutisha. Ilibidi atumie uanaume wake kuhakikisha anamuokoa mwanae.

Aliruka kwa nguvu mpaka chini huku mkononi akiwa ameshikilia tawi kubwa alilolivunja wakati anaruka. Kishindo alichotua nacho kiliwashtua wale simba kiasi cha nao kuanza kurudi nyuma. Akautumia vizuri muda huo kwa kukimbia mpaka pale alipokuwa mwanae. Akamuinua juu juu kwa mkono mmoja na kumuweka kifuani. Kwa kasi ya ajabu akaanza kukimbia kurudi kwenye ule mti alikomuacha mkewe.

Kuona anakimbia wale simba nao wakaanza kumfukuza huku wakizidi kutoa milio ya kutisha. Wote waliokuwa juu ya miti walifumba macho yao wakiamini huo ndio mwisho wa baba yao mzee Khalfan. Ndani ya sekunde chache mno, mzee Khalfan akawa ameshaufikia ule mti.

Akajirusha kwa nguvu na kufanikiwa kudaka tawi kwa mkono mmoja huku mkono mwingine akiwa amemkumbatia mwanae kifuani. Akajigeuza juu juu kama mwanasarakasi na kuanza kupanda juu kwa kasi, akiwaacha wale simba mita chache kutoka pale chini.

Walipofumbua macho yao hakuna aliyeamini kumuona mzee Khalfan akiwa ameshapanda juu kabisa ya mti, huku mwanae Ismail akiwa kifuani mwake. Wakajikuta wote wakitoa machozi ya furaha kumshangilia baba yao.
**********
Ndani ya Cassino la kifahari la Platinum classic, mambo yalikuwa yamechangamka huku mandhari tulivu ya mahali hapo ikipafanya paonekane kama peponi. Muziki wa taratibu ulikuwa unatumbuiza kutoka kwenye redio ya kisasa iliyounganishwa na spika kubwa zilizotawanywa kila kona ya Cassino ile.

Mzee mmoja wa makamo aliingia ndani ya cassino akiwa anasindikizwa na wapambe wenye miili mikubwa( Mabaunsa) watatu. Baada ya kuteremka kutoka kwenye gari la kifahari, alitembea kwa hatua za taratibu na kuingia ndani. Baada ya kuuliza kitu kwa msichana aliyekuwa mapokezi, aliingia mpaka ndani huku wapambe wake wakimfuata nyuma.

Waliongoza mpaka kwenye meza ya pembeni iliyokuwa nyuma kabisa, kisha wakakaa. Mhudumu aliwaletea kinywaji cha Shampeni (Champagne) ya bei mbaya. Mpambe mmoja akasimama na kuanza kummiminia bosi wake kwenye glasi, kisha akamsogezea.

Dakika chache baadae gari aina ya landrover 110 lenye maandishi makubwa ubavuni “BK85” liliwasili ndani ya Platinum Cassino na vijana wapatao saba waliokuwa wamevalia makoti marefu meusi waliteremka na kuongoza moja kwa moja hadi ndani.

Walienda mpaka kwenye ile meza aliyokaa yule kigogo na wapambe wake. Ilivyoonekana ni kama walikuwa na miadi ya kukutana pale. Baada ya salamu, wote walichukua nafasi zao na kuketi. Mmoja kati ya wale vijana walioingia akasimama na kuanza kuongea.

“Holly Trinity!...”
Wote wakajibu
“Forever!!”
“Mzee kazi yenu imeshakamilika, hivi tunavyozungumza bila shaka Khalfan na familia yake yote wameshakuwa kitoweo cha simba wenye njaa wa Gamutu. Tumekwenda kuwatupa katikati ya msitu wa Gamutu, hawawezi kusalimika kamwe!...”
“ Holy Trinity…”

Wote wakajibu tena “Forever!”, kisha akakaa.
Kilichofuatia ikawa ni vicheko mfululizo huku wakigongesheana Cheers( Chiaz). Yule mzee akasimama na kuanza kushikana mikono na wale vijana saba, huku uso wake ukiwa umechanua tabasamu la kinafiki.

“Nawaamini sana vijana wangu na na ndio maana sintoacha kuwatumia kwenye oparesheni za kundi letu. Kwa niaba ya wenzangu nataka niwakabidhi mzigo wenu.”

Aliongea yule kigogo huku akichukua Briefcase kutoka kwa mmoja wa wapambe wake. Akaiweka juu ya meza na kuifungua.
Wote walitabasamu na kugongesheana ngumi kama ishara ya ushindi.
Noti mpya mpya za dola ya kimarekani zilikuwa zimepangwa vizuri ndani ya Briefcase ile.

Baada ya wote kushudia kilichomo ndani akaifunga na kumkabidhi mmoja wa wale vijana saba, aliyeonekana kuwa ndio kiongozi wa wenzake.

Mzee Khalfan alikuwa akikatiza vichakani akitembea kwa tahadhari kubwa, akitafuta njia ya kutokea nje ya msitu wa Gamutu. Aliwaacha mkewe na wanae wakiwa bado juu ya miti wakihofia kuliwa na simba wa Gamutu. Alimuachia Khaleed jukumu la ulinzi kwani aliamini anaweza baada ya kufanya vizuri usiku.

Aliamini kwamba Mungu yuko pamoja nao na ni lazima wangepata msaada wa kuitoa familia yake salama kutoka ndani ya msitu wa kutisha wa Gamutu. Alizidi kuchanja mbuga kwa kufuata vinjia vidogo vilivyokuwemo humo msituni.

Bunduki yake ilikuwa mkononi kwa ajili ya kujihami na simba waliokuwa wamejaa ndani ya msitu huo.

Safari yake ilikuwa ngumu kutokana na umande mwingi uliosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa imetoka kunyesha alfajiri.

Alipofika mbali kidogo, sehemu yenye mwinuko alitafuta mti mkubwa na kupanda ili aone yuko upande gani wa msitu. Alipanda harakaharaka na alipofika juu alishusha pumzi ndefu kwa furaha baada ya kugundua kuwa amekaribia kabisa kufika nje ya msitu. Kwa mbali aliweza kuyaona mashamba ya mpunga na minazi na makazi ya watu.

“Oooh! Thanks my Lord.”

Alijisemea kimoyomoyo wakati akishuka mtini kwa haraka. Akiwa kwenye harakati za kushuka toka mtini, alishtukia kitu kama kamba ngumu ikimviringisha kwenye mguu wake wa kushoto. Alivyopeleka macho kwenye mguu wake, alishtuka kupita kiasi na kujikuta akiliachia tawi alilokuwa amelishikilia na kudondoka chini kama mzigo.

Nyoka mkubwa mweusi alikuwa amemgonga mguuni na kumwachia meno yenye sumu kali.
“What the hell is this? Jesus! Im finished”

Alijikuta akitamka peke yake wakati akijitazama kwenye jeraha alilong’atwa na yule nyoka. Damu nyeusi ilikuwa ikichuruzika kuashiria kuwa yule nyoka alikuwa ana sumu kali kupita kiasi.

Kitu pekee alichokumbuka kukifanya ilikuwa ni kuvuta kamba kutoka kwenye bukta yake aliyoivaa kwa ndani na kuifunga juu la lile jeraha. Alihakikisha ameikaza kwa nguvu li kuzuia sumu isizidi kusambaa mwilini. Kwa mara nyingine alijikuta matumaini ya yeye na familia yake kupona yakiyeyuka kama theluji kwenye jua kali. Alipomaliza kuifunga ile kamba akaanza kuhisi giza nene machoni likiambatana na kizungunguzungu kikali. Akajinyoosha pale chini na kulala tuli.
****

Kengere ya hatari iliyokuwa imefungwa kwenye mti mkubwa wa mwembe katikati ya kijiji, pembeni mwa nyumba ya Chifu wa kijiji au Zumbe kama wanakijiji walivyozoea kumuita iligongwa kwa nguvu na mmoja wa wajakazi wa Zumbe kuashiria kuna jambo la hatari limetokea kijijini hapo.

Wanakijiji walianza kukimbia mbio kuelekea kule kengere ilikokuwa inasikika. Hakuna aliyefahamu kumetokea nini.
“Mulamu kumetokeaga nini wajameni asubuhi yote mwee!
“Sijui mulamu, twende tukamsikilize Zumbe”
Walisikika wanaume wawili wakiulizana huku wakitimua mbio. Dakika chache baadae wanakijiji wote wakawa wamekusanyika chini ya mti wa mwembe, nyumbani kwa chifu wao. Wake kwa waume, vikongwe kwa watoto, wote walikua kimya wakisubiri kusikia kumetokea nini kijijini kwao.

Zumbe akatoka kwenye nyumba yake akiwa ameshika mkuki na sime akifuatana na walinzi wake, wote wakiwa na silaha za jadi mikononi mwao.
Baada ya salamu Zumbe alianza kuwatangazia wanakijiji kilichotokea usiku kijijini hapo.

Kundi kubwa la simba walikuwa wamevamia kijijini hapo na kusababisha madhara makubwa ambapo idadi kubwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo waliliwa. Alizidi kueleza kuwa mtoto mmoja alikuwa ameliwa baada ya kukutana na simba hao alipotoka nje usiku kujisaidia.

Taarifa ile ilimshtua kila mtu na hofu kuu ikatanda kijiji kizima. Alizidi kueleza kuwa Simba hao walikuwa wamekimbilia ndani ya msitu wa Gamutu. Amri ikatolewa kuwa wanaume wote waweke silaha zao begani kwa ajili ya kwenda kuendesha msako mkali ndani ya pori la Gamutu kuhakikisha Simba wale wanapatikana na kuuliwa.

Wanawake, watoto na wazee wakapewa amri ya kurudi vibandani mwao na kujifungia mpaka wanaume watakaporudi kutoka porini. Bila kupoteza muda kila mtu akaanza kutelkeleza amri aliyopewa. Baada ya muda mfupi wanaume walikuwa tayari kila mmoja ana silaha za jadi. Wanawake wakawa wanahangaika kuwakusanya watoto wao na kuwafungia vibandani mwao.

Wanaume wakiwa na marugu, mapanga, mikuki, sime , mishale na kila aina ya silaha za jadi wakawa wanajiandaa. Mbiu ya mgambo ikapigwa na wote wakajipanga uwanjani wakiwa tayari kuuvamia msitu wa Gamutu kuwaangamiza Simba. Baada ya gwaride fupi lililoendeshwa na Zumbe mwenyewe, safari ya kuuvamia msitu wa Gamutu ikaanza.

“Mama! mama!... mbona baba harudi au amekutana tena na Simba?” Aliuliza binti mdogo wa mzee Khalfan, huku wote wakiwa wameanza kuingiwa na hofu baada ya kuona muda unazidi kwenda bila ya baba yao kurudi kama alivyokuwa ameahidi.
‘’Mama njaa inauma…” alilalamika Ismail, kitindamimba wa Bi Miriam huku akianza kulia.
“Nyamaza mwanangu! Baba ameenda kuleta chakula anarudi sasa hivi nyamaza baby!”
wote wakawa wameshaanza kukata tamaa.

Upande wa pili jeshi la jadi lilikuwa limejigawa katika makundi mawili na kuuvamia msitu wa Gamutu. Waliwakurupusha na kufanikiwa kuwaua samba wengi… wakawa wanazidi kuingia ndani kabisa ya msitu.

Masaa yalizidi kuyoyoma huku Bi Patricia na wanae wakiwa bado juu ya miti huku kukiwa kimya kabisa. Mara walishtuka kusikia kelele vichakani, wakahisi wale Simba wanarudi tena. Walishtuka kuona watu wengi waliovalia mavazi ya asili mikononi wakiwa na silaha za jadi wakitokeza vichakani na kuizunguka ile miti waliyokuwa wamepanda.

‘’Mungu wangu tumekwisha! Wanangu tusali sala ya mwisho‘’ alitamka Bi Miriam huku akitetemeka
Mwili mzima.

‘’Nyinyi ni wanani na mnafanyaga nini juu ya mamiti huku porini peke yenyu‘’ aliuliza mmoja wale watu kwa kiswahili kibovu.

‘’Tusaidieni! Tusaidieni! tumetekwa na majambazi ‘’ aliongea Khaleed kwa sauti na akaanza kushuka mtini kwa ujasiri mkubwa. Wale watu wakawa wanatazamana usoni wakionekana kushtushwa na uwepo wa Binadamu msituni humo kwani haikuwa kawaida.

Khaleed akashuka mpaka chini, bila woga akawasogelea wale watu na kuanza kuwaeleza kilichowasibu mpaka wakawa pale. Wote waliingiwa na huruma sana, kwa haraka wachache kati yao wakapanda juu ya miti kuwateremsha Bi Miriam na wanae wawili.

Khaleed alizidi kuwaeleza kuwa baba yao aliondoka kwenda kutafuta msaada muda mrefu uliopita na hajarudi mpaka muda huo. Ikabidi lile kundi ligawanyike tena. Wengine wakawabebea Bi Miriam na wanawe wawili kuwarudisha kijijini huku kundi lingine likiongozwa na Khaleed kufuata njia ya kule alikoelekea baba yake.

‘’Shhh! Simama!... aliongea Zumbe akiwaamrisha vijana wake kusimama baada ya kuona kitu kisicho cha kawaida mbele yao. Ulikuwa ni mwili wa mwanaume ukiwa umelala chini. Ulionekana kuvimba sana na kubadilika rangi na kuwa mweusi kama mkaa. Wote wakaanza kusogea kwa tahadhali. Silaha zikiwa mikononi tayari kwa lolote.

‘’Zumbe’’ aliusogelea ule mwili huku akiuchunguza kwa makini. Macho yake yakatua mguuni alipoona jeraha kubwa likiwa linatoa damu nyeusi. Meno ya nyoka yalikuwa bado yameng’ang’ania mwilini na kufanya sumu kali isambae mwili mzima. Akasogea zaidi na kuugusa kifuani kusikiliza mapigo ya moyo kisha akainuka na kuwaeleaza kitu vijana wake kwa lugha yao ya kiasili. Vijana wenye nguvu wakauinua ule mwili na kuubeba juu juu. Wakiwa bado wanashangaa lile kundi lingine likiongozwa na mtoto Khaleed likawasili eneo lile.

Khaleed aliwatambua kuwa ni miongoni mwa wale aliokuwa nao kwani nao walivalia vilevile na walikuwa na silaha kama zilezile. Aligeuza macho pembeni na kwa haraka alimtambua yule mtu aliyebebwa kuwa ni baba yake, mzee Khalfan.

‘’Dad! Daaad! Whats happened to you ‘’( Baba! Baba! umepatwa na nini?)
Aliwakimbilia wale waliombeba na kuanza kuwaeleza kuwa huyo ni baba yake wanayemtafuta. Machozi yalianza kumtiririka baada ya kumwona jinsi alivyobadilika na kuvimba mwili mzima huku rangi ya ngozi yake ikiwa imebadilika na kuwa ya kutisha.

Hawakupoteza muda, safari ya kurudi kijijini ilianza kwa mwendo wa haraka. Khaleed akabebwa begani na mmoja wa wasaidizi wa Zumbe. Wakawa wanakatiza vichakani kwa kasi na muda mfupi baadaye wakawa wameshawasili kijijini.

Kengere ya hatari ikagongwa kwa mara ya pili na watu wote wakakusanyika tena chini ya ule mwembe. Bila kupoteza muda ‘’Zumbe” akaanza kueleza waliyokutana nayo huko porini na akumuomba Khaleed awaelezee wanakijiji yaliyowapata, huku waganga wa jadi wakihangaika kunusuru maisha ya mzee Khalfan.

Khaleed alieleza kila kitu kilichowapata tangu walipovamiwa na majambazi usiku wa jana yake wadogo zake wawili walivyoliwa na simba wa Gamutu mpaka muda huo wakiwa mikononi mwa Wanakijiji. Kila mtu aliguswa mno na yaliyowapata kiasi cha wakinamama kuanza kuangua vilio. Muda mfupi baadaye kundi lililowachukua Bi Miriam na wanae wawili nalo liliwasili na kujumuika na wenzao.

Kila kitu kilionekana kama hadithi za kutunga lakini huo ndio ulikuwa ukweli halisi. Waganga wa jadi wakawa wanafanya kazi ya ziada kuokoa maisha ya Mzee Khalfan. Baada ya muda mfupi alirudiwa na fahamu na kufumbua macho, akawa anashangaa pale alipo ni wapi na amefikaje. Khaleed alikuwa pembeni yake kumtuliza. Hakuna aliyeamini kama kweli amepona kwani kwa hali aliyokuwa nayo awali, wote walijua lazima afe.

Wote wakapelekwa kwenye kibanda cha makuti pembeni ya nyumba ya Zumbe na wakaanza kupewa huduma ya haraka kuwasafisha majeraha yao na kuwapa chakula laini pamoja na maziwa ya moto. Siku ya kwanza ikapita… Jumatatu… Jumanne… furaha ya kuwa pamoja tena baada ya misukosuko mizito ikawa ndio kitu pekee kilichosalia maishani mwao. Hawakuwa tena na nyumba ya kifahari, wala magari ya kutembelea. Khaleed alikuwa akikumbuka usemi mmoja aliofundishwa na mwalimu wake, “When everything has gone, The future still remain dark” (Bada ya kila kitu kupita, bado maisha ya siku zijazo yanabaki kuwa siri gizani).

Kila siku iliyopita ilikuwa kama inasukumwa na upepo. Maisha mapya ya kijijini ndani ya kibanda cha makuti yalimuumiza sana mzee Khalfan. Kila uchao alikuwa akiwaza na kuwazua ni nini hasa alichowakosea wenzake mpaka wafikie hatua ya kutaka kumuangamiza kikatili namna ile. Hakupata jibu…alichoweza kufanya ni kumwachia Mungu kila kitu huku akizidi kumwomba Maulana aonyeshe miujiza yake.
*****
Katika kipindi cha uhai wa mzee Shamsi, mkwe wa Khalfan, siku zote alikuwa akipenda kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu. Ilikuwa ni kawaida yake kuwapa misaada watoto yatima na wanawake wajane. Hakuacha kumuusia mkwe wake Khalfan juu ya umuhimu wa kufanya hivyo katika maisha ya hapa duniani. Khalfan naye akaanza kufuata nyayo za mzee Shamsi. Yeye pamoja na familia yake wakawa wakijumuika pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kila siku za mwisho wa wiki na siku za sikukuu wakitoa zawadi za vyakula, nguo na vinywaji.

Hata baada ya kifo cha mkwewe, mzee Khalfan bado aliendelea na ukarimu wake kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu. Kwa kumuenzi mzee Shamsi, Khalfan na mkewe Bi Miriam waliamua kutoa msaada wa kumsomesha mtoto mmoja aliyetengwa na jamii yake kwa sababu ya ulemavu wa ngozi (Albinism). Mtoto huyu alikuwa akishinda kwenye madampo akiokota mabaki ya vyakula na makopo ambayo baadae alikuwa akienda kuyauza ili apate mkate wake wa kila siku.

Mzee Khalfan alianza kujenga mazoea na urafiki na yule mtoto ambaye alikuja kujitambulisha kuwa anaitwa Girbons au Gebo kama watoto wenzie wa mitaani walivyozoea kumuita. Mwishowe walimchukua na kwenda kuishi naye nyumbani kwao wakimchukulia kama mtoto wao wa kumzaa licha ya ulemevu wake wa ngozi. Bi Miriam akawa na kazi ya ziada ya kumfundisha tabia njema na maadili mazuri kwani maisha ya kushinda kwenye madampo yalimfanya awe na tabia isiyoeleweka. Taratibu akaanza kubadilika tofauti na maisha aliyokuwa anaishi kama mtoto wa mitaani.

Kwa kipindi hicho Girbons alikuwa na umri wa miaka kumi na nne, akimzidi mtoto wa kwanza wa mzee Khalfan, Khaleed kwa miaka miwili. Baada ya kuhakikisha amekuwa na tabia njema, Wakampeleka kuanza kidato cha kwanza katika shule maarufu ya kulipia ya St Benard Blaziniar.

St Benard Blaziniar maarufu kama ‘’SBB Academy’’ ilikuwa ni shule maarufu sana nchini Blaziniar. Ilikuwa ikisifika kwa kufaulisha wanafunzi wengi katika mitihani ya kikanda na Kitaifa na kupelekea kutoa Watalaamu wengi nchini Blazinia. Pia ilikuwa ikiaminika kuwa ndio Shule pekee inayotoa elimu bora inayomfanya mwanafunzi asitegemee ajira bali kujiajili katika sekta binafsi. Elimu ya nadharia na vitendo ilikuwa ikitolewa kitalaamu na Walimu waliobobea.

Girbons akawa ameachana kabisa na maisha ya mtaani na kurudi shule. Kwake Mzee Khalfan na Bi Miriam walikuwa kama Miungu wake baada ya kufiwa na wazazi akiwa na umri mdogo kasha kutengwa na ukoo wake kwa sababu ya kuzaliwa akiwa Albino. Kwa mila za kwao waliamini kuwa mtoto akizaliwa na ulemavu wa ngozi ni kama laana kwa ukoo mzima, hivyo walienda kumtoa kafara kwa mizimu au kumfukuza kabisa ndani ya ukoo na kumtenga. Hilo ndilo lililotokea kwa Girbons.

Baada ya kukutana na familia yam zee Khalfan, maisha yake yalibdilika sana na sasa akawa anajisikia kama binadamu wa kawaida. Aliapa kuwaheshimu daima na akawahidi kusoma kwa bidii zake zote ili elimu ndiyo ije kuwa mkombozi katika maisha yake ya ukubwani. Hakuacha kuwapenda Khaleed na wadogo zake na aliwachukulia kama wadogo zake wa damu nao wakamuona kama kaka yao licha ya ulemavu wa ngozi aliokuwa nao (AIbinism)

Girbons aliendelea kung’ara shuleni na alipoingia kidato cha pili akachaguliwa kuwa kiranja wa mazingira. Ni katika kipindi hicho, Khaleed naye alikuwa amemaliza darasa la saba. Mzee Khalfan
akaamua kumpeleka naye ‘’SBB Academy ‘’akaungane na kaka yake wa hiari Girbons. Khaleed na Girbons wakawa kama ndugu wa damu wakisoma shule moja. Girbons akawa ndio msimamizi wa Khaleed kipindi ambacho Khaleed alikuwa bado hajazoea maisha ya kukaa mbali na wazazi, tena akiwa shule ya bweni.

Ilipofika kipindi cha likizo, Girbons hakutaka kurudi nyumbani kwa mzee Khalfan kwani alikuwa akifanya maandalizi ya misho ya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili. Baada ya shule kufunga kwa likizo ndefu, alimsindikiza Khaleed kisha yeye akarudi Shuleni. Alipania kusoma kwa bidii na hilo alikuwa akilitekeleza kwa vitendo. Kwake muda ulikuwa mali, na hakutaka kuona akipoteza muda bila sababu. Aliendelea kujiandaa na mtihani, akiwa na wanafunzi wenzake wachache waliobaki kipindi cha likizo kama yeye.

Jioni moja Girbons alikuwa amekaa peke yake akipunga upepo baada ya azii nyingi za siku nzima. Tofauti na siku zote, alionekana kuwa mnyonge na mwenye mawazo mengi.
‘’Kaka Girbons mbona leo hauko kawaida? Naona kama una mawazo yanayokusumbua. Kwani kuna nini? Aliuliza Nancy, mwanafunzi mwenzake waliyekuwa wakisoma kidato kimoja. Swali hilo lilimzindua
Girbons aliyekuwa amezama kwenye lindi zito la mawazo.

Ukweli ni kwamba akili ya Girbons ilikuwa ina uwezo wa kuvuta hisia za matukio hata kama yuko mbali. Kwa siku ya pili sasa alikuwa akihisi kuna matatizo yameikuta familia yao, hasa baba yake wa kufikia, mzee Khalfan. Hali hiyo ilimfanya akose amani na kuonekana mwenye mawazo muda wote.
‘’Naongea na wewe Girbons, mbona hunijibu?
Alizidi kuhoji Nancy baada ya kuona Girbons akimkodolea macho badala ya kumjibu.
‘’Ooh I’m sorry Nancy! leo sijisikii vizuri kabisa…nahisi kama homa inaninyemelea. Niache nikapumzike please!”

Aliongea Girbons na kusimama kutoka pale na kuelekea bwenini akiwaacha wanafunzi wenzake wakimshangaa kwani haikuwa kawaida yake kuonekana mnyonge kiasi kile. Akili yake iliendelea kuhisi kuna tatizo limetokea nyumbani kwao ingawa bado hakujua ni nini. Akawa anasubiri kusikia kilichotokea. Kwa jinsi familia ya mzee Khalfan ilivyokuwa ikimpenda, hakutaka jambo llote baya liwakute.

****
Simu ya mkononi ya Pius bagenda ilikuwa Inaita mfululizo. Alipoitazama namba ya mpigaji akaisogeza sikioni haraka na kuanza kuongea na upande wa pili.
“Jidaw kutoka BK85 hapa naongea! Vijana wako wa kazi.”
“Holly Trinity!”

Bagenda akajibu kwa shauku ‘’4reva ‘’
‘’Tumepokea taarifa sasa hivi kutoka kwenye vyanzo vyetu kuwa kuna mtu mmoja amesalia katika
Familia ya mzee Khalfan ‘’Marehemu ‘’

Yule mtu aliyejitambulisha kama Jidaw aliendelea kumpasha habari bosi wao, kiongozi wa pili wa kundi la wafanyabiashara hatari wa ‘HOLLY TRINITY’’

Alizidi kumueleza kuwa licha ya kazi nzito waliyofanya ya kuiteketeza familia nzima ya Khalfan Mwalukasa, bado kuna mtoto mmoja amesalia na siku ya tukio alikuwa bado yuko shuleni anakosoma kidato cha pili bweni.

‘’Umesema anaitwa nani na anasoma shule gain?” alizidi kuhoji Pius Bagenda.
“ Anasoma st Benard Blaziniar iliyoko mtaa wa Senator Avenue mkabala na kanisa Katoliki la Majengo. Jina lake anaitwa Girbons na zaidi huyu mtoto ni mlemavu wa ngozi… Albino.

Analelewa na kusomeshwa na mzee Khalfan na kuna taarifa kwamba anafahamu hata uhusiano wa ‘’HOLLY TRINITY ‘’na baba yake. Anaweza kuwa hatari kwetu iwapo atafahamu kilichotokea.’’

Aliendelea kutahadharisha Jidaw huku akiongea kwa msisitizo. ‘’Tumfanye nini kiumbe huyu!’’
Mzee Mtaki akajibu kwa amri… ‘’Nawapa masaa machache akachukuliwe haraka shuleni na kuletwa ngomeni pale Boma tukirudi tumkute! Over and out’’

‘’Sawa Bosi!”
Alijibu Jidaw na kukata simu.

*********
Girbons alikuwa akiendelea na maandalizi ya mtihani wake wa Taifa wa kidato cha pili na wenzake Shuleni St Benard Blaziniar Academy . Kwa siku ya pili sasa Girbons alikuwa hayuko katika hali ya kawaida. Ndoto alizokuwa akiota usiku zilitosha kuashiria kuwa baba yake (Khalfan) alikuwa amepatwa na jambo baya. Hisia zile zilimfanya naye aonekane kama mgonjwa. Alipoteza hamu ya kila kitu na akawa akishinda kutwa nzima akiwa amelala bwenini.

Saa tatu asubuhi… chumba alichokuwa amelala Girbons kilifunguliwa na kiranja wa bweni akaingia.
‘’Oya we vipi mwanangu? Yaani mpaka muda huu umepiga mbonji? Class huendi?”
Kabla hajajibu yule kiranja akampa taarifa Girbons kuwa anaitwa kwenye ofisi za Utawala (Adminstration Block) na Mwalimu wa Malezi.

“Kuna wageni kutoka kwenu wamekuja! Jiandae fasta twende Ofisini…” Girbons akashtuka kutoka pale kitandani na kuanza kujiandaa haraka kwenda kuwaona hao wageni wake. Alihisi ni wazazi wake, Mzee Khalfan na mkewe.

Kwa haraka akajitayarisha na wakaongozana mpaka Ofisini alikoitwa. Aliongoza mpaka kwa Patron wao. ’’Girbons, kuna wageni ambao wamejitambulisha kama wajomba zako. Wametumwa kuja kukuchukua kwani baba yako anaumwa sana na amelazwa hospital!’’

Aliongea mwalimu wa malezi kwa lugha ya upole akimuelezea Khaleed alichomuitia.
Baada ya kuelezwa hivyo na Patron, hakutaka hata kuhoji wajomba zake wako upande gain, akatimua mbio kurudi bwenini kuchukua begi lake ili awahi kumuona baba yake Khalfan.

Muda mfupi baadae akawa anarudi Ofisini begi lake likiwa mgongoni. Kichwani mwake mawazo yalikuwa yakipishana kama umeme. Akagundua maana ya zile ndoto alizokuwa akiziota mfululizo. Mwalimu wake alikuwa akimwangalia kwa huruma kwa jinsi alivyohuzunika kusikia habari mbaya kutoka kwao, kwamba baba yake anaumwa sana.

Patron akamwongoza mpaka sehemu ya mapokezi walipokuwa wajomba zake.
‘’Haya nawatakia safari njema ila Girbons awahi kurudi shule mara baba yake atakapopata nafuu’’
Patron alikuwa akiwaaga Girbons na wale watu waliojitambulisha kama Wajomba zake, akiwapa
mkono wa kwa heri.

Wakanyanyuka wote na kuanza kuondoka, mmoja akampokea Girbons begi alilobeba huku mwingine akimshikia mkono na kuelekea kwenye eneo la maegesho walikobaki gari lao. Milango ya Nissan Patrol ya kisasa ilifunguliwa kwa “remote control” na wote watatu wakaingia ndani. Taratibu gari likaanza kutoka eneo la shule na likaingia barabara ya kutokea iliyoenda kuungana na barabara kuu ya Mtaa wa Senator. Mita chache mbele wakawa wameshafika kwenye barabara kuu iendayo mjini.

Kila mtu ndani ya gari alikuwa kimya, hakuna aliyemsemesha mwenzake. Gari lilizidi kushika kasi
likiyapita magari mengine.

‘’Kwani amelazwa hospitali gani uncle?’’
Girbons alimuuliza yule waliyekaa naye siti ya nyuma.
’’Nyamaza utajua mbele!‘’
Lile jibu lilimshitua Girbons kiasi cha kuanza kuingiwa na wasiwasi na kuanza kuwatazama wale watu mmoja baada ya mwingine. Sura zao zilikuwa ngeni kabisa na hakuwahi kuziona sehemu yoyote. Kengere ya hatari ikalia kichwani mwake.

Kilomita chache mbele gari liliiacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi iliyoelekea mashambani huku likitimua vumbi. Baada ya muda wakawa wamefika ndani kabisa ya mashamba ya karafuu na minazi. Mita chache mbele gari likaegeshwa pembeni na wale watu wakashuka na “kulock” milango yote ya gari. Mmoja akatoa simu ya mkononi na kuanza kuongea na upande wa pili.

’’Tumeshampata! Tuko naye hapa.
‘’HOLLY TRINITY! ‘’
Upande wa pili ukajibu…
‘’4reva ‘’

“Tumfanye nini?”
“Mleteni ngomeni, Boma palace kama nilivyowaeleza sawa bosi’’
Upande wa pili ukakata simu.

************
Wanafunzi wa shule ya st Benard Blaziniar walikuwa wamejipanga uwanjani wakisubiri
matangazo kutoka kwa mwalimu wa zamu. Baada ya salamu fupi, Mwalimu akaanza kutoa matangazo…

‘’Jamii yote ya Wanafunzi tunatakiwa kuishi kwa amani na upendo na tunatakiwa kufanya
mambo yetu kwa ushirikiano katika shida na raha. Ukiona mwenzako kapatwa na tatizo ujue kuwa inawezekana kesho ikawa ni zamu yako. Jana asubuhi mwenzenu Girbons wa kidato cha pili ameletewa taarifa na wajomba zake kuwa baba yake anaumwa sana.

Hivyo Girbons aliongozana nao kwenda kumuona baba yake hospitali. Kwa kuwa Girbons ni mwenzenu inatakiwa mjitolee mchango wa hiyari kwenda kumuona mgonjwa, halafu wateuliwe watu kwenda kuiwakilisha shule.

Alimaliza matangazo mwalimu wa zamu kisha wanafunzi wakawa wanatawanyika. Kila mwanafunzi alionekana kuguswa na tangazo lile hasa ukizingatia jinsi ambavyo alikuwa akiishi vizuri na wenzake.

Alikuwa akiishi vizuri sana na wenzake mchango ukapitisha na kwa haraka kila mtu akachanga alichokuwa nacho. Wakateuliwa wanafunzi watatu Jacks, Rose na Jumanne pamoja na walimu wao wawili kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha shule. Kesho yake asubuhi na mapema msafara wa watu watano walioteuliwa ukaanza safari ya kuelekea nyumbani kwa mzee khalfan kwa kutumia gari la shule.

Iliwachukua takribani dakika 45 wakawa wamewasili kwenye makazi ya mzee Khalfan. Gari likawa linakatiza katikati ya mashamba ya karafuu na minazi yaliyotunzwa vizuri hali iliyoyafanya yapendeze sana, ndani ya himaya ya khalfan.
“The scenery of this fields looks beautiful!” “
Sure! Its like we are in Eden”

Jacks na Rose walikuwa wakiongea wakifurahia mandhari mazuri waliyokuwa wanayaona ndani ya himaya ya Khalfan.
Muda mfupi baadaye wakawa wameshawasili kwenye lango la mbele. Dereva akafunga breki na kupiga honi ili wenyeji wawafungulie, dereva alizidi kupiga honi lakini hakuna mtu aliyejitokeza. Ukimya ulivyozidi kutawala ikawabidi washuke garini na kuanza kutembea kwa miguu kulisogelea geti. Walikuta limeegeshwa hivyo wakaingia mpaka ndani wakiongozwa na mwalimu wao wa malezi Sir Kameta.

Walichokutananacho hawakuamini macho yao. Maiti za watu ambao walionekana kuwa ni walinzi zilikuwa zimetalala chini kiasi cha kuanza kutoa harufu mbaya. Mlango wa mbele ulikuwa umevunjwa huku kukiwa na matundu mengi ya risasi ukutani. Vioo vya madirisha vilikuwa chini baada ya kuvunjwa vunjwa. Eneo zima lilitapakaa damu ambayo sasa ilikuwa imeganda na kuanza kukauka.

“Ooh jesus! What’s the hell is this? A serial destruction around here! Lets move out quickly!”

Mwalimu Kameta aliwaamuru kutoka eneo lile haraka. Wakakimbilia mpaka lilipo gari lao. Dereva akawasha injini na kukanyaga mafuta mpaka mwisho, kwa mwendo wa kasi safari ikaanza kurudi shuleni. Hali waliyoikuta pale ilitosha kuelezea kila kitu kilichotokea. Wote walijikuta wakitetemeka kwa hofu.

“What can we do people ?”
Aliuliza mwanafunzi Jumanne… Hakuna aliyekuwa na jibu la haraka.
“Mimi napendekeza tukatoe kwanza taarifa Polisi kabla ya kufika shuleni”. Wote waliafiki wazo hilo na safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza. Muda mfupi baadae wakawa mbele ya jengo kubwa lenye maandishi yaliyosomeka vizuri… BLAZINIA CENTRAL POLICE POST” Wakateremka garini wakiongozwa na Mwalimu Kameta mpaka sehemu ya mapokezi “counter”. Baada ya salamu ambayo haikuitikiwa, Mwalimu Kameta akaanza kutoa taarifa kwa askari waliokuwa zamu.

Pamoja na kujitahidi kunyoosha maeleza, cha kushangaza hakuna askari aliyeonekana kuwajali, huku kila mtu akiendelea na shughuli zake. Sir kameta akawageukia wenzake ambao nao walibaki wamepigwa na butwaa. Wakatazamana kwa muda kama waliokuwa wakiulizana tufanye nini.

Askari mmoja akajibu kwa nyodo za kike… “tutafuatilia”
Mwalimu Kameta akadakia na kufoka kwa jazba
“mnafuatilia nini wakati hali tuliyoikuta inajieleza kila kitu? This is what we call Bureaucracy, abuse of power…hivi nyinyi polisi kazi yenu ni nini?”

“We mzee hivi huelewi? unataka kutufundisha kazi sio? Utaingia lockup sasa hivi kwa kuitania dola” Alijibu yule askari mwingine kwa ukali , akimtolea macho mwalimu Kameta na wenzake. Wakatazamana tena, kisha wakapeana ishara ya kutoka nje!
Hakuna aliyepata jibu la nini kinaendelea… “What are the duties and responsibilities of police force?” alihoji Jacks, mwanafunzi aliyeongozana na wenzake.

“Nadhani hilo swali ungewauliza mwenyewe kule ndani “ akadakia Jumanne kwa masihara, wote wakatabasamu wakiliendea gari lao huku wakiwa wamesononeka sana mioyoni mwao. Kwa hali waliyoikuta pale kituoni , ilionyesha dhahiri polisi wanafahamu kinachendelea na wanahusika kwa namna moja au nyingine .

****
Hawakuwa na jinsi , iliwabidi warudi shuleni kutoa taarifa kwa mkuu wa shule wajue nini cha kufanya . Baada ya mkuu wa shule ya St Benard Blaziniar “Mr Kihiyo” kupokea taarifa maalum ya yaliyojiri kwenye safari ya kwenda kwa mzee Khalfan, “mzazi wa mwanafunzi Girbons” kumjulia hali baada ya kusikia amelazwa hospitali…Alibaki kupigwa na mshangao. Hakuna aliyejua kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia

Wakabaki kushauriana…hakuna aliyeyejua wale watu waliokuja kumchukua Girbons ni akina nani na wamempeleka wapi. “Kwani mliwahoji vizuri wao ni akina nani?” Alikuwa akihoji mkuu wa shule, Headmaster. Kabla hata hajajibiwa akaendelea… “nina wasiwasi mkubwa na usalama wa mwanafunzi wangu Girbons! my lord ! rescue them all”

THE ALBIN POWER
Taarifa ya habari kutoka Planet Link fm, kituo maarufu cha redio nchini Blaziniar!” kila mtu alitega masikio kutaka kusikia nini kitazungumzwa , kwani haikuwa kawaida kwa taarifa ya habari kusomwa asubuhi , tena katikati ya saa…

Habari maalum kutoka chumba cha habari zilizotufikia hivi punde, tega sikio kusikia yaliyojiri…
Mtangazaji aliyekuwa Studio alikuwa akivuta usikivu wa wasikilizaji wake . Habari iliyotangazwa ilimshtua kila aliyesikia . Ilikuwa ni kupatikana kwa miili sita ya watu waliouwawa kikatili , kisha wakatundikwa juu ya miti na kukatwa viungo kadhaa na kisha kuchunwa ngozi kama ngombe ndani ya pori la kutisha la Gamutu .

“Uchunguzi wa polisi unaendelea kubaini chanzo na wahusika wa tukio hili la kinyama “. Alikaririwa kamanda mkuu wa polisi Lauden Kambi wakati akihojiwa na vyombo vya habari. Kilichowashtua watu wengi ni kwamba watu wote sita waliouwawa walikuwa na ulemavu wa ngozi, albino. Nchi nzima ilizizima kwa hofu kuu, hakuna aliyeamini kuwa hayo yanayotangazwa redioni yametokea kweli .

Blaziniar ilikuwa ni nchi yanye amani kiasi, ingawa watumishi wengi wa selikali walikuwa wakiivuruga kwa makusudi kwa maslahi yao binafsi, kutokana na na uchu wa kumiliki mali. Matukio ya ujambazi yalikuwa ni kawaida, watu kuporwa mchana mchana mali zao kama magari, mabenki yalivamiwa na waporaji wenye silaha asubuhi na mapema, huku polisi mara zote wakichelewa kutoa msaada kwa raia , na hata walipofika maeneo ya matukio walikuwa na desturi ya kukamata watu wasiohusika.

Umajinuni laana kwa wenye tama ya kumiliki mali kwa njia za mikato! Pamoja na hayo yote haikuwahi kuripotiwa tukio la kutisha kama hilo , binadamu kuchinjwa kama wanyama,kukatwa viungo na kuchunwa ngozi…kisa wana ulemavu wa ngozi, ilitisha.

Baada ya muda mfupi magari ya polisi yakawa yametapakaa mitaani yakielekea porini Gamutu kulikotokea tukio lile la kutisha... redio ya Planet -link ilituma wawakilishi wake wengi kufuatilia kwa karibu yote yaliyokuwa yanatokea Gamutu. Muda si mrefu habari zikawa zimesambaa nchi nzima.
*******************
Majambazi yaliyomteka Girbons yalikwenda naye mpaka Mafichoni, yakiwa yanamalizia taratibu za kumkabidhi Girbons mikononi mwa watu hatari wa “The Holly Trinity”. Baad ya kuwasiliana na matajiri wao, yakaanza kumfunga kamba mikononi na miguuni na kumjaza matambara mdomoni. Baada ya kumfunga, jambazi moja lilimuinamia pale chini na kuanza kumsemesha kwa kejeli na vitisho…

“Wewe kiumbe zeruzeru! anza kusali sala zako za mwisho kwani uko mikononi mwa watu hatari , muda mfupi ujao utawafuata wazazi wako kuzimu…tena wewe utakuwa dili safi kwetu kwani nyie maalbino mna utajiri mkubwa viungoni mwenu ingawa wenyewe hamjui”
Aliongea Jidaw, kiongozi wa kundi la majambazi hatari wa “BK85 killers” linalodhaminiwa na matajiri wa Holly Trinity.

Hapo Girbons akapata picha kamili kuwa wale waliomfuata shuleni na kudai kuwa ni wajomba zake walikuwa ni majambazi na mpaka muda huo walishawaua wazazi wake, mzee Khalfani na familia yake yote. Alijikuta mwili wote ukifa ganzi. Akafumbua macho taratibu na kuanza kusali kimoyomoyo .

Akiwa bado anaendelea kusali kimoyomoyo alinyanyuliwa kama furushi na kuingizwa kwenye buti la gari iliyokuja kumchukua kule shuleni. Milango ikafungwa na safari ya kuelekea Boma Palace, Makao makuu ya The Holly Trinity, ikaanza kwa kasi.
“Tuko njiani bosi tunakuja naye, fungueni kabisa mageti yenu“ Jidaw alikuwa akiongea kwa simu na kiongozi wa The Holy trinity.

Gari la kisasa aina ya Nissan Patrol lilikuwa linatambaa na barabara kwa kasi ya ajabu.
“Nyoosha mguu kwenye excretor baba! Unakuwa mzee nini? Inabidi tuwahi kuchukua mamilioni yetu.“ Yale majambazi yalikuwa yanataniana huku yakicheka kwa furaha . Kwao ilikuwa pesa tu! Ubinadamu pembeni.
Muda mfupi baadae gari lao likawa limewasili “Boma Palace”, makazi ya kisasa kama ikulu , ilipo ngome ya The Holly Trinity. Walipofika mageti yote yalikuwa wazi na gari likapitiliza mpaka ndani kwa kasi ya ajabu. Lilipoingia tu, milango ikafungwa, huku walinzi wenye silaha nzito wakilizunguka huku na kule kuhakikisha usalama.

Mzee mmoja wa makamo alitoka kuwapokea wageni na baada ya salamu fupi wakawa wanakabidhiana malipo yao. Aliwakabidhi wale vijana brifkesi ndogo iliyojaa dola za kimarekani, kisha buti likafunguliwa na Girbons akatolewa akiwa amefungwa kitambaa cheusi machoni kilichomzuia kuona chochote. Akavutwa mkono na kupelekwa mbele ya yule mzee wa makamo.

Wote wakatabasamu kinafiki. Waliamini kitendo cha kumpata Albino Girbons ndani ya himaya yao ilikuwa sawa na kupata dili la mamilioni ya pesa. Wakapeana mikono na yale majambazi yakarudi kwenye gari lao yakitabasamu kwa furaha baada ya kushikishwa kilicho chao.
“Albino millions!...” wote wakajibu “For holly Trinity…”

Gari likawashwa, mageti yakafunguliwa na dereva akakanyaga mafuta mpaka mwisho…Gari likashika kasi na kuondoka kwa mkwara mzito kama kaiwada yao, wakiachia moshi mwingi na vumbi nyuma yao.
Girbons akabakia amejiinamia kama kondoo machinjioni.

“Apelekwe surgery room 7 na kazi ianze mara moja” Yule mzee wa makamo alitoa amri huku akipiga makofi akiashiria kila mmoja aendelee na kazi aliyopangiwa. Girbons akabebwa juu juu na kuingizwa ndani, walipofika ndani kabisa, akashushwa juu ya kitanda kasha akaanza kufunguliwa kamba za miguuni na mikononi na mwisho kile kitambaa cha usoni. Akajikuta yuko kwenye chumba kidogo chenye vitanda, mikasi, madawa na vifaa kama hospitali.

Yule mtu aliyemleta akatoka na kuufunga mlango kwa nje. Girbons akabakia pale juu ya kitanda akiwa haelewi kinachoendelea. Alikuja kushtuka kutoka kwenye lindi zito la mawazo baada ya kusikia mlango ukifunguliwa. Wakaingia watu wawili waliovalia mavazi kama madaktari, nyuso zao zikiwa zimefunikwa kwa vitambaa vyeupe huku wote wakiwa wamevalia miwani. Mmoja alikuwa amebeba sinia lenye vifaa kama sindano, mikasi na visu vikubwa, huku mwingine akiwa amebeba tray la dawa mkononi. Ilivyoonyesha walikuwa wakitaka kumfanyia kitu kibaya sana Girbons.
****
Alfajiri na mapema, Mzee Khalfan akawa ameshaamka na kukaa juu ya kitanda cha miti, kwenye kibanda cha makuti walimopewa hifadhi baada ya kuokolewa porini Gamutu. Alimtazama mkewe Bi Miriam aliyekuwa bado amelala fofofo, akageuza macho na kuangalia upande wa pili walipokuwa wamelala watoto wao khaleed na wadogo zake. Alijikuta akisikia uchungu moyoni kiasi cha kudondosha machozi.

Kwake matukio yote yalikuwa kama mchezo wa kuigiza. Hakuamini kuwa hatimaye yuko salama na familia yake licha ya kuwapoteza wanae wawili walioliwa na simba wa Gamutu. Bi Miriam alishtuka toka usingizini na kumkuta mumewe amejiinamia.
“Mume wangu mbona unaumia sana. Tumshukuru Mungu kwa kutunusuru na kifo kilichokuwa kinatukabili. Tumwachie Mungu kila kitu kwani yeye pekee ndiye ajuaye hatma yetu”

Bi Miriam alikuwa akimbembeleza mumewe, mzee Khalfan alimgeukia mkewe na wakawa wanatazamana usoni.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa mke mwema kama wewe unayejua kunifariji ninapoumia” mzee Khalfan alimjibu mkewe wakalala, kulipokucha kabisa Bi Miriam akawa anaongea na mumewe kuhusu mtoto wao wa kufikia Girbons, ambae waliamini bado yuko shuleni st Benard Blaziniar .

“Inabidi tumuombe Zumbe awatume watu wake shuleni kwa kina Girbons wakamuone kama yuko salama kisha warudi naye hapa kijijini aungane nasi “ mzee khalfani alitingisha kichwa kuafiki ushauri wa mkewe na akaamka na kwenda kuonana na Zumbe .

Bila kipingamizi Zumbe akaamuru vijana wawili waende shuleni kwa kina Girbons kwenda kumchukua kwa kutumia baiskeli , safari ndefu ikaanza. Wale vijana walipewa onyo la kutoongea na mtu yeyote zaidi ya mkuu wa shule, Mr Kihiyo .

Iliwachukua takribani masaa sita , wakawa tayari wameshafika kwenye geti la shule . mwalimu wa zamu aliwapokea na kuwaongoza mpaka ofisi kuu mwalimu kihiyo alikuwa ameitisha kikao cha dharura kujadili nini cha kufanya baada ya Girbons kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hali ilikutwa nyumbani kwa mzee Khalfan.


Mara simu ya mezani ikaita kutoka kwe Secretary wake akimjulisha kuwa kuna wageni wanataka kuonana naye . “waambie waingie ….”
Mr kihiyo aliongea huku akisimama kuashiria wote waliokuwa ofisini watoke kwa muda ili aongee na wageni, baada ya kuketi wale vijana wakaanza kueleza shida iliyowaleta kwa Kiswahili kibovu. Kengere ya hatari ikalia kichwani mwa Mr Kihiyo akihisi kuwa hao nao ni miongoni mwa majambazi yaliyomteka mwanafunzi wao.

Akaamuru mwalimu wote waingie ofisini. Baada ya mahojiano ya muda mrefu , wakaamini kuwa ni kweli wale vijana wametumwa na mzee Khalfani
“Mmesema mzee Khalfan yuko salama ? mbona hatuelewi nini kinachoendelea” aliongea Mr kihiyo akionyesha kuchanganyikiwa. Muafaka ukafikiwa kwamba mkuu wa shule Mr kihiyo na mwalimu wa malezi Sir kameta waongozane na wale vijana kwa kutumia gari la shule mpaka kijijini, wakahakikishe kama ni kweli.

Barabara ya kwenda, kijijini aliko mzee Khalfan ilikuwa ni mbaya sana, yenye madimbwi mengi ya maji na matope . Baiskeli za wale vijana zilikuwa zimefungwa juu ya keria ya landrover 110, Four wheels drive. Safari ilikuwa ngumu na ya kuchosha kwani gari lilikuwa likikwama kwenye matope mara kwa mara. Ziliwachukua zaidi ya masaa matatu wakawa tayari wamekaribia kijijini.

Mzee Khalfan ndio alikuwa wa kwanza kuliona gari. Moyo ulimlipuka akihisi kuwa huenda ni “The
Holly Trinity” wameamua kumfuata tena. Alihisi wale vijana waliotumwa wametekwa na ndio wameonyesha mahali alipo.Taarifa zikasambaa upesi kijijini kuwa kuna gari linakuja.

Kengere ya hatari ikagongwa,na watu wote wakaamriwa kuingia vibandani mwao ili jeshi la jadi la Zumbe lifanye kazi yake. Wanaume wenye silaha za jadi wakawa wamejipanga tayari wakisubiri amri kutoka kwa Zumbe.

Wale vijana ndani ya gari kwa kuwa nao walikuwa wakifahamu sheria za kijijini kwao,ilibidi washuke garini na kutangulia mbele huku wakipunga mikono hewani kama ishara ya amani. Kwa muda wote mzee Khalfan na familia yake walikuwa wamefichwa kwenye pango, nyuma ya nyumba ya Zumbe. Walikuwa wakisali kimoyomoyo kwa Mungu wao ili awapiganie.

kijiji chote kikawa kimya kabisa, ulisikika muungurumo wa gari tu, lililokuwa limewabeba mkuu wa shule Mr kihiyo na Sir Kameta, Walimu kutoka St Benard Blaziniar Academy. Wale vijana wakaliongoza gari mpaka sehemu ya kupaki, kisha wakawaamuru walimu Kihiyo na Kameta kushuka huku nao wakipunga
mikono hewani kama alama ya amani.

Zumbe akatoka mafichoni na kuja kuwalaki wageni kutoka mjini. Baada ya salamu wakaongozwa mpaka chini ya mwembe, nje ya nyumba ya Zumbe. Wakaketi tayari kwa mazungumzo. Baada ya mahojiano marefu na Zumbe, hatimaye walipewa nafasi ya kuonana na mzee Khalfan ana kwa ana. Akaenda kutolewa mafichoni na kuletwa pale chini ya mti. Wakalakiana kwa furaha na kuanza mazungumzo.

Walimu hawakuamini kumkuta mzee Khalfan akiwa hai, kwani watu wote walishaamini kuwa tayari yeye na familia yake ni marehemu. Wakaanza kumsimulia yote waliyoyaona nyumbani kwake na taarifa ya kupotea kwa mwanae Girbons. Kupotea kwa Girbons likawa pigo jingine kwa familia ya mzee Khalfan. Hakuna aliyeweza kuificha huzuni yake kwa yaliyotokea. Mzee Khalfan naye akaanza kuhadithia yaliyowapata yeye na familia yake mpaka muda ule wakiwa pale kijijini.

Ilikuwa ni simanzi kubwa mno… Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Mr kihiyo, Mkuu wa shule ya “SSB Academy” alijitolea kumpa hifadhi ya muda mzee Khalfan na familia yake mpaka hapo haki yao itakapopatikana. ”Tutakupigania kwa nguvu na uwezo wetu wote mpaka tuhakikishe unapata haki yako”. Waliongea walimu Kihiyo na Kameta kwa msisitizo.

Mzee Khalfan hakuwa na njia nyingine zaidi ya kukubali msaada wa hifadhi aliyopewa. Mr kihiyo aliahidi mbele ya Zumbe kuwa atawaficha nyumbani kwake kwa siri, na hakuna atakayejua mahali walipo mpaka haki yao itakapopatikana.

Wakakubaliana kuondoka pamoja na familia yake usiku wa siku hiyo mpaka nyumbani kwa Mr kihiyo, kwenye nyumba za shule ya St Benard Blaziniar Academy. Wazee wa pale kijijini
wakawaruhusu kwa moyo mkunjufu huku wakiwaombea amani na uzima kutoka kwa Miungu na mizimu yao. Wakawafanyia tambiko la kuwalinda kisha wakaanza kujiandaa kuondoka.

Saa moja jioni safari ikaanza kurudi mjini… Mzee Khalfan na familia yake wakawa na amani mpya
mioyoni mwao. Kazi iliyobaki mbele yao ikawa ni kuandaa kisasi cha damu kwa wote waliohusika.

********
Ndani ya ngome ya the Holly Trinity,Boma Palace, maandalizi ya mwisho yalikuwa yakifanyika kabla ya kijana Girbons mwenye ulemavu wa ngozi (albino) hajakatwa viungo na kuchunwa ngozi. Kila kitu kilishakamilika na sasa kazi ikawa inatarajiwa kuanza muda wowote.

Baadhi ya watu nchini Blaziniar walikuwa wameanza kuingiwa na imani za ajabu na za kishetani, wakiamini kwamba viungo na ngozi za watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino ) vinaweza kumfanya mtu kupata utajiri wa haraka na kuwa milionea kwa muda mfupi . haikufahamika imani hiyo ya kishenzi imetoka wapi, kwani kitu kama hicho hakikuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo.

Siku moja tu baada ya kuripotiwa mauaji ya kutisha ya maalbino sita waliochinjwa porini Gamutu, kuliripotiwa kupotea kwa maalbino wengine watatu , wawili kutoka familia moja na mwingine mwanafunzi aliyeenda kutekwa shuleni kwao (Girbons). Hali ya hatari ikatangazwa na jeshi likaahidi kukomesha matukio hayo haraka iwezekanavyo .

Girbons alikuwa bado juu ya kitanda, akiwangaalia kwa hofu wale watu waliongia mle chumbani alimokuwa . Hakuelewa mara moja wanataka kumfanya nini, ila vifaaa walivyokuwa navyo vilitosha kuashiria shari…walionekana kutaka kumtoa uhai wake.

Chumba hakikuwa na dirisha hata moja zaidi ya mataa makubwa yaliyofungwa kila kona ya chumba, chumba kilinuka damu kama machinjioni ingawa mandhari yake yalikuwa kama hospitali ya kisasa. Jasho lilianza kumtoka Girbons wakati wale ”madaktari” wakijiandaa kwa kuvaa ‘gloves’ mikononi na kusogeza mikasi, nyembe, sindano na visu vikali, vidogo kwa vikubwa pembeni mwa kitanda alichokuwa amefungwa juu yake.

Mapigo ya moyo yakawa yanapiga kwa kasi huku mwili ukimtetemeka, aliamini kuwa bila muujiza kutokea huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yake. Wakiwa wameshajiandaa kila kitu , wale madaktari walikumbuka kuwa wamesahau dawa ya usingizi (Dopamine Sedative Serum) ‘DSS’ maabara. Ikabidi mmoja atoke kuifuata kwa haraka , huku mwingine akiendelea kusogeza vifaa karibu na kitanda.

Girbons akaona huo ndio muda pekee wa kujiokoa. Wakati yule mmoja akiendelea kujiandaa, kwa umakini mkubwa Girbons akasogeza mkono mpaka kwenye sinia lenye vifaa, akapapasa na kushika kisu kikali chenye makali pande zote mbili, akaupandisha mkono kitandani taratibu na kukificha kile kisu.

Yule daktari akamsogelea karibu ili amfunge mikanda iliyounganishwa na kitanda, tayari kwa kazi ya kumchuna ngozi na kumkata viungo. Girbons akabana pumzi kwa nguvu tayari kwa mashambulizi…
alipomgusa tu mkono, Girbons akainuka kwa ghafla, kisu kikiwa mkononi, akamlenga shingoni na kukizamisha kisu kwa nguvu zote! mkono mmoja akawahi kumziba mdomo asipige kelele na kuwashtua wengine.

Kwa kasi ya ajabu akaruka mpaka chini na kumbana vizuri mdomo yule daktari. Akamvuta na kuuficha mwili wake chini ya kitanda, kisha akaruka hadi nyuma ya mlango, akajibana huku kisu kilicholoa damu kikiwa mkononi. Mwiliwote ulikuwa ukitetemeka, kwa mbali akaanza kusikia vishindo vya mtu akija upande wa kile chumba, akatambua kuwa lazima ni yule wa pili anarudi, akabana pumzi tena tayari kwa kazi.

Girbons hakuwahi kuwaza kuwa ipo siku atakuja kuua mtu kwa mikono yake, akabaki kushangaa ujasiri ule umetoka wapi, akiwa bado amejificha nyuma ya mlango, yule daktari wa pili akaingia. Alishtuka kuona damu zimetapakaa kitandani huku mwenzie akiwa anatapatapa chini kukata roho. Kabla hata hajajua afanye nini…Girbons akajirusha kwa nguvu zake zote, akamkandamiza chini huku amemziba mdomo . Kile kisu kiliingia kisawasawa shingoni kiasi cha damu kuvuja kama bomba lililopasuka.

Wakati familia yam zee Khalfan ikiokolewa kutoka ndani ya Gamutu, Girbons
Mzee Khalfan ndio alikuwa wa kwanza kuliona gari. Moyo ulimlipuka akihisi kuwa huenda ni “The
Holly Trinity” wameamua kumfuata tena. Alihisi wale vijana waliotumwa wametekwa na ndio wameonyesha mahali alipo.Taarifa zikasambaa upesi kijijini kuwa kuna gari linakuja.

Kengere ya hatari ikagongwa,na watu wote wakaamriwa kuingia vibandani mwao ili jeshi la jadi la Zumbe lifanye kazi yake. Wanaume wenye silaha za jadi wakawa wamejipanga tayari wakisubiri amri kutoka kwa Zumbe.

Wale vijana ndani ya gari kwa kuwa nao walikuwa wakifahamu sheria za kijijini kwao,ilibidi washuke garini na kutangulia mbele huku wakipunga mikono hewani kama ishara ya amani. Kwa muda wote mzee Khalfan na familia yake walikuwa wamefichwa kwenye pango, nyuma ya nyumba ya Zumbe. Walikuwa wakisali kimoyomoyo kwa Mungu wao ili awapiganie.

kijiji chote kikawa kimya kabisa, ulisikika muungurumo wa gari tu, lililokuwa limewabeba mkuu wa shule Mr kihiyo na Sir Kameta, Walimu kutoka St Benard Blaziniar Academy. Wale vijana wakaliongoza gari mpaka sehemu ya kupaki, kisha wakawaamuru walimu Kihiyo na Kameta kushuka huku nao wakipunga
mikono hewani kama alama ya amani.

Zumbe akatoka mafichoni na kuja kuwalaki wageni kutoka mjini. Baada ya salamu wakaongozwa mpaka chini ya mwembe, nje ya nyumba ya Zumbe. Wakaketi tayari kwa mazungumzo. Baada ya mahojiano marefu na Zumbe, hatimaye walipewa nafasi ya kuonana na mzee Khalfan ana kwa ana. Akaenda kutolewa mafichoni na kuletwa pale chini ya mti. Wakalakiana kwa furaha na kuanza mazungumzo.

Walimu hawakuamini kumkuta mzee Khalfan akiwa hai, kwani watu wote walishaamini kuwa tayari yeye na familia yake ni marehemu. Wakaanza kumsimulia yote waliyoyaona nyumbani kwake na taarifa ya kupotea kwa mwanae Girbons. Kupotea kwa Girbons likawa pigo jingine kwa familia ya mzee Khalfan. Hakuna aliyeweza kuificha huzuni yake kwa yaliyotokea. Mzee Khalfan naye akaanza kuhadithia yaliyowapata yeye na familia yake mpaka muda ule wakiwa pale kijijini.

Ilikuwa ni simanzi kubwa mno… Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Mr kihiyo, Mkuu wa shule ya “SSB Academy” alijitolea kumpa hifadhi ya muda mzee Khalfan na familia yake mpaka hapo haki yao itakapopatikana. ”Tutakupigania kwa nguvu na uwezo wetu wote mpaka tuhakikishe unapata haki yako”. Waliongea walimu Kihiyo na Kameta kwa msisitizo.

Mzee Khalfan hakuwa na njia nyingine zaidi ya kukubali msaada wa hifadhi aliyopewa. Mr kihiyo aliahidi mbele ya Zumbe kuwa atawaficha nyumbani kwake kwa siri, na hakuna atakayejua mahali walipo mpaka haki yao itakapopatikana.

Wakakubaliana kuondoka pamoja na familia yake usiku wa siku hiyo mpaka nyumbani kwa Mr kihiyo, kwenye nyumba za shule ya St Benard Blaziniar Academy. Wazee wa pale kijijini
wakawaruhusu kwa moyo mkunjufu huku wakiwaombea amani na uzima kutoka kwa Miungu na mizimu yao. Wakawafanyia tambiko la kuwalinda kasha wakaanza kujiandaa kuondoka.
saa moja jioni safari ikaanza kurudi mjini mzee Khalfan na familia yake wakawa na amani mpya
moyoni mwao.kazi iliyobaki mbele yao ni kuandaa kisasi Cha damu kwa wote waliohusika.


Ndani ya ngome ya the holly trinity” boma palace “ maandalizi ya mwosho yalikuwa yakifanyika , kabla ya kijana Girbons mwenye ulemavu wa ngozi (albino) hajakatwa viungo na kuchunwa ngozi .
Baadhi ya watu nchi blaziniar walikuwa wameanza kuingiwa na imani za kishenzi na kuamini kwamba viungo na ngozi za watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino ) vinaweza kumfanya mtu kupata utajiri wa haraka na kuwa milionea kwa muda mfupi . haikufahamika imani hiyo imetoka wapi , kwani kitu kama hicho hakikuwahi kutokea nchini humo siku za nyuma .

Siku moja tu baada ya kuripotiwa mauaji ya kutisha ya albino sita , waliochinjwa porini Gamutu kuliripitiwa kupotea kwa maalbino wengine watatu , wawili kutoka familia moja na mwingine mwanafunzi aliyeenda kutekwa shuleni kwao. Hali ya hatari ikatangazwa na jeshi likahahidi kukomesha matukio hayo haraka iwezekanavyo .

Girbons alikuwa bado juu ya kitanda , akiwangaalia kwa hofu wale watu waliongia mle chumbani alimokuwa . hakuelewa wanataka kumfanya nini, ila vifaaa walivyokuwa navyo viliashilia kumtoa uhai wake dakika chache , cumba hakikuwa na dirisha hata moja zaidi yab mataa makubwa yaliyofungwa kila kona ya chumba , chumba kilinuka damu kama machinjioni ingawa madhari yake yalikuwa kama hospitali jasho lilianza kumtoka Girbons wakati wale”madaktari “ wakijiandaa kwa kuvaa gloves mikononi na kusogeza mikasi , vyembe , sindano na visu , vikubwa pembeni mwa kitanda alichokuwa juu yake.

Mapigo ya moyo yakawa yanapiga kwa kasi huku mwili ukimtetemeka , aliamini kuwa bila muujiza kutokea huo ndio ulikuwa mwisho wake , wakiwa wameshajiandaa kila kitu , wale madaktari wakakumbuka kuwa wamesahau dawa ya usingizi Dopamine Sedative Serum “DSS” maabara ikabidi mmoja atoke kuifuata kwa haraka , huku mwingine akiendelea kusongeza vifaa ka ribu na kitanda .

Girbons akaona huo ndio mudaa pekee wa kujiokoa , wakati yule mmoja akiendelea kujiandaa , kwa umakini mkubwa Girbons akasogeza mkono mpaka kwenye sinia lenye vifaa , akapapasa na kushika kisu kikali chenye makali pande zote mbili,akapandisha mkono kitandani na kukificha kile kisu , yule daktari akmsogerea karibu ili aaamfungue mikanda iliyounganishwa na kitanda , tayari kwa kumchuna ngozi na kumkata viungo ,

Girbons akabana pumzi kwa nguvu tayari kwa mashambulizi , alipomgusa tu mkono mmoja Girbons akainuka kwa ghafla , kisu kikiwa mkononi , akamlenga sehemu ya shingo na kukizamisha kisu kwa nguvu , mkono mmjoa akawahi kumziba mdomo asipige kelele na kuwashtua wengine kwa kasi ya ajabu akaruka mka chini na kumbana vizuri mdomo yele daktari akajivuta na kuuficha ule mwili chini ya kitanda, kisha akaruka hadi nyuma ya mlango akajibana huku kisu kilicholoa damu kikiwa mkononi , kwa mbali akaanza kusikia vishindo vya mtu a kija upande wa kile chumba , akatambua kuwa yule wa pili alikuwa anarudi , akabana pumzi tena tayari kwa kazi

Huku akitetemeka kwa hofu , akanyanyuka na kwenda kuufungua mlango kwa ndani , Girbons akajikuta amewaua wale wachuna ngozi wote kwa mpigo , alishusha pumzi ndefu na kukisogerea kioo kidogo cha ukutani kilichokuwa pembeni mwa sinki la maji , akajikuta mwili mzima umeowa damu kwa haraka akafungua bomba na kuanza kunawa mikono yake iliyotapakaa damu . akili ikamjia kichwani baada ya kuona koti jeupe la daktari limetundikwa ukutani , akajsafisha mwili mzima na kujifuta damu , kisha akavua nguo alizokuwa amezivaa . akaliendea lile koti na kulivaa ,isha akainama chini na kumvua mmoja ya wale maiti kitambaa cha usoni . kofia ya kidaktari na viatu akarudi nyuma ya kioo na kujiangalia upya .

Akajikuta akitabasamu kwani sasa alionekana kama mmoja wa wale madaktari . akajifunga kitambaa cheupe usoni na kuvaa miwani kisha akafunga mlango kwa kasi . akaanza kutembea kwenye korido ya ile nyumba akatafuta sehemu ya kutokea ilimuwia vigumu kupata mlango wa kutokea nje. Kwani kulikuwa na vyuma vingi vinavyofanana . mwosho akajikuta ameonga choo cha wanaume “Gents room” akaingia na kujifunga kwa ndani . macho yakatua juu ya dirisha dogo la humo chooni kwa masaada wa mabomba akaoanda mpaka dirishani ,akatoa mkasi aliokimbia nao chumba cha mauaji na kuanza kukata nyaya za dirisha ,

dakika chaxhe baadae akawa ameshazikata katika ukubwa uliomuwezesha kupenya , akavua lile koti la kidaktari na kulitupa chini , akabaki na kitambaa cha usoni na kofia nyeupe , kwa haraka akapenya na kutoka nje , akaninginia huu ya bomba la maji machafu na kuanza kuporomoka kwa upande wanje , akawa amefanikiwa kutoka nje ya jingo , ingawa kazi ilibaki ya kuruka ukuta mrefu wa uzio ilitaka kumkatisha tama . alipogeuza macho upande wapili ,akaona ngazi ndefu ikiwa imelazwa chini na mafundi waliokuwa wanarekebisha nyaya za umeme juu ya uzio ule. Akashusha pumzi ndefu na kuisimamisha ile ngazi . kwa haraka akaanza kupanda kuelekea juu kabisa yya ukuta ule mrefu

Wkati akihangaika kupanda , mara akawaona walinzi wawili wenye bunduki wakija upande ule aliokuwepo. Hakufa moyo akaendelea kupanda lwa kasi huku wle walinzi wakizidi kusogea , kumbe walikwishamuona tangu anasimamisha ile ngazi , mmoa wao akaamuru ashuke kabla hawajamchakaza kwa risasi ,Girbons akawa ameshafka juu . hakutaka kurudi tena nyuma . akaona ni bora apigwe risasi afe kishujaa kuliko kukatwa viungo na kuchunwa ngozi . alichokifanya ni kuruka jwa nje , urefu wa ukuta haukumtisha kitu akaona bora kujioka .
Wakati anaruka akasikia milio ya risasi ikimfuata kwa nyuma . akajirusha mpaka chini , akatua juu ya mawe yaliyomjeruhi vibaya miguuni na usoni . akainuka haraka na kuanza kukimbia huku akichechemea mafunzo ya uaskari aliyoyapata shuleni yalimuongezea ujasiri .

Alipofika umbali kidogo akageuka kutazama alikotoka , aliwaona wale walinzi wakiwa juu ya ule ukuta akiangalia upande aliokimbilia , akavuta ile kofia na kitambaa alichojifunga usoni . mbio zikamuokoa akawa anachanja mbuga kuzama kwenye mashamba ya karafuu , mbele kidogo akasikia muungurumo wa gari likija upane wake akajificha pambeni alione vizuri . hakuamini macho yake alipoliona trekta la shule yao . likiwa limebeba nyasi kwa ajili ya chakula cha ngombe wa maziwa wanaofugwa shuleni hapo hakutaka yule dereva amuone , akasubiri lipite na kuanza kulikimbilia akiwa ameinama na kufanikiwa kudandia , akajichomeka ndani ya magunia ya nyasi na kutulia tuli.

Mbele kidogo akaanza kusiikia vingora vya magari yakija mbele yao . yule dereva wa trekta akasimamisha pembeni kuwapisha wababe . alipochungulia akaona ni yale magari yaliyokuwa mle ndani ya ngome , na bila shaka walikuwa wakimtafuta yeye. Akazidi kujibanza . walipopita dereva akawasha gari na kuendelea na safari ya kupeleka chakula cha ngombe shuleni st benedict blaziniar

Saaa saba na nusu usiku , gari la shule aina ya landrover 110 liliwasili nyumbani kwa mwalimu kihiyo likiwa limewabeba khalfani na familia yake . watu wote walishaamini kuwe mzee khalfani na familia yake walikuwa wamekufa kwa kuvamiwa na majambazi nyumbani kwao ingawa taarifa hizo hakuna aliyekuwa tayari kuzitoa , ukabaki kuwa uvumi au tetesi za mtaa.

Taa zote za nyumba ya mwalimu kihiyo zikazimwa kukawa giza totoro la usiku , ,zee khalfani na familia yake wakasaidiwa kushuka ndani ya gari na kuongozwa na mwenyeji wao. Mr Kihiyo wakaaapelekwa mpaka vyumbani vya ndani ile , self contained . usalama ukahakikishwa kwa kiwango kizuri kiasi cha kufanya watu wengine wasielewe kinachoendelea , mke wa mwalimu kihiyo . mama asna akapewa jukumu la kuwalea watoto na kuhakikisha wanapata mahitaji yote muhimu , huku Bi mariam akisaidiana na mama asna kumpa huduma ya jiani mzee Khalfani ambaye alionekana kuelemewa na “stress” au huzuni kali mitaalamu , kiasi cha kumfanya aanze kuhisi anaumwa .

Manyunyu ya mvua iliyokuwa inarashia usiku wa manane ndiyo vilivyomshtua Girbons kutoka kwenye usingizi wa kifo . akajinyanyua kutoka pale alipokuwa amelala ndani ya magunia ya nyasi za ngombe , akatafuta upenyo na kutazama angani . ilikuwa tayari ni usiku . akazidi kunyanyuka na hatimaye akatoka mwili mzima . alikuwa juu ya tela la trekta la shule , alilodandia mchana wakati aliponusulika kutolewa uhai akiponea chupuchupu . akahisi usalama ndani ya nafsi baada ya kugundua lile trekta limeegeshwa ndani ya fensi ya shule , karibu na mazizi ya ngombe wa maziwa wanaofugwa pale shuleni . kwake ule ulikuwa ni kama muujiza kwani matukio yaliyomtokea ndani ya masaa machache yasiyozidi 24 usingeweza kuamini kuwa amerudi salama .

Tangu alipokuja kuchukuliwa asubuhi ya siku hiyo na waliojifanya ni wajomba zake wakimletea taarifa ya kulazwa hospitali kwa baba yake mzee khalfani , kumbe ni majambazi hatari yaliyomteka na kwenda kumuua za ili akatwe viungo na kuchunwa ngozi … Alivyonusurika dakika za mwisho na kufanikiwa kukikwepa kifo kwa kuua na kuruka ukuta , alivyoumia wakati akiruka ukuta mrefu na kutua juu yam awe, mpaka mwisho alipofanikiwa kudandia trekta la shule alimojificha mpaka muda huo, alikuwa bado haamini

nyie maalbino mna utajiri mkubwa viungoni mwenu ingawa wenyewe hamjijui alijikuta akishtuka baada ya kuyakumbuka maneno aliyokuwa anaambiwa kwa kejeli , alipokuwa ametekwa , asubuhi ya siku hiyo hiyo ! alijitazama mwili kwa masikitiko , uchungu ukamwingia na kuanza kulia …

Eeeh mungu wa islaeli, kwanini niumbwe mimi nikiwa hivi? why me albino ? Oooh Jesus, save me from this trespass in you I lay heart.. alishindwa kujizuia kutamka maneno yaliyomzidisha uchungu moyoni mwake, alijitazama tena ngozi yake iliyokosa rangi kama binadamu , hakudhani kuwa hiyo ndiyo sababu pakee ya yeye kuteseka chini ya jua .

Alivyofahamu yeye ni kuwa ngozi ya binadamu inapokosa pigiment iitwayo melanin inayofanya kazi ya kuweka rangi halisi kenywe nywele , macho kucha , na ngozi ni upungufu huu ndio husababisha mtoto kuzaliwa zeruzeru na hali hiyo hujitokeza mara chache , kwa mtu mmoja mmoja “individual . character” hivyo ndivyo mwalimu wake wa malezi sir Maketa anayefundisha somo la Biolojia alivyowafundisha darasani . alishangaa imani hizo za kishetani zimetoka wapi , kiasi cha binadamu kuwindana kama wanyma . eti kisa UTAJIRI – WEALTH, the deadly wealth



Girbons alizinduliwa kutoka kwenye dimbwi zito la mawazo na manyunyu ya mvua ambayo sasa yalikuwa yakizidi kuongezeka. Akajisogeza pembeni ya banda la ngombe na kujiinamia chini ya nguzo. Alianza kuhisi maumivu makali kwenye goti lake na mkono wa kushoto , akakumbuka jinsi alivyoruka ukuta mrefu na kutua juu ya mawe. Japokuwa alikuwa ameumia , alimshukuru Mungu wake kwa kumnusuru na janga lile lililokuwa mbele yake.

Akaona mahali pekee anapoweza kuwa salama ni nyumbani kwa mwalimu wake mpendwa, Sir Kameta. Akaamua kwenda kuomba hifadhi ili kuyanusuru maisha yake kwani sasa alianza kuishi kwa hofu kubwa kama myama wa kuwindwa(Beast). Alitia huruma sana…hakutaka kuonekana kwa mtu mwingine yoyote akihofia usalama wake. Akawa anatembea kwa kunyata kutoka pale kwenye banda la ngombe kuelekea kwenye dirisha la chumba anacholala mwalimu wake. Kwa mbali akawa anamsikia mwalimu na mkewe wakiwa kwenye maongezi ya chini chini(Pillow Talks)

Alivyojaribu Kutega sikio zaidi , akagundua kuwa wanazungumzia tukio lililotokea hapo shuleni na nyumbani kwa mzee Khalfan. Walikuwa wakimzungumzia yeye pamoja na familia yake. Walionekana kuwaonea huruma sana na zaidi wakawa wanamsikitikia yeye. Akaamini kuwa kweli walikuwa wakimpenda na akaanza kujihisi amani moyoni mwake.

Hakupenda kuendelea kusikiliza mazungumzo yao zaidi kwani yalikuwa yakimkumbusha machungu yaliyomo moyoni mwake. Akaona bora awagongee mlango hata kama ilikuwa ni tayari usiku wa manane. Wazo jingine likaja, akaona ni bora agonge dirishani. Taratibu akagonga dirisha na mara pazia likafunguliwa , macho yake yakagongana ana kwa ana na mwalimu wake Sir kameta.

Mwalimu akahisi kuwa labda yuko ndotoni , kwani alishaamini Girbons tayari ni marehemu .
Kwa haraka akamwamsha mkewe na wakaenda kumfungulia mlango . Ilikuwa kama muujiza kwao.
“Girbons ni wewe! Oooh thanks be unto our God for saving your life” Aliongea mwalimu Kameta na kukumbatia Gibons kwa nguvu.

Alichompendea zaidi mwalimu wake ni kwamba pamoja na ulemavu wake wa ngozi aliokuwa nao, bado alimpenda kama mwanae wa kumzaa. Hata alipokuwa na tatizo lolote hapo shuleni, Sir Kameta ndie aliyekuwa kimbilio lake .

Waliendelea kukumbatiana kwa nguvu huku Girbons machozi yakimtoka . Hakuweza kukizuia kilio cha kwikwi kilichotokana na uchungu wa yaliyomkuta. Mwalimu akawa na kazi ya ziada ya kumbembeleza na kumfariji. Akamchukua mpaka ndani ambako alipokelewa vizuri na mkewe na kwa pamoja wakaanza kumpa huduma ya haraka, walianza kwa kumvalisha masweta na kumfunika nguo nzito kwani alikuwa akitetemeka mwili mzima kutokana na baridi baada ya kuwa ameloana kwa mvua mwili mzima tena akiwa kifua wazi.

Baada ya muda mfupi akawa ameanza kurudi katika hali yake ya kawaida ingawa bado alikuwa na maumivu makali kwenye mguu na mkono alivyoumia katika harakati zake za kutoroka ngomeni. Akaandaliwa chakula haraka huku akitayarishiwa sehemu ya kulala.

Kutokana na ujuzi wa saikolojia aliokuwa nao malimu kameta alitambua haraka kuwa Girbons amekumbana na mambo mazito sana yaliyoonekana kumuathiri sana kisaikolojia, walichoamua ilikuwa ni kumpa sehemu ya kulala ili apumzishe akili mpaka asubuhi ndio waanze kuumuliza kilichomsibu.

Alichowasisitiza Girbons ni kuficha siri ya uwepo wake mahali hapo kwani alikuwa akisakwa kwa udi na uvumba. Hakutaka mtu yoyote ajue zaidi ya mwalimu Kameta na mkewe .
***********
Alfajiri na mapema, mapambuzuko yakiwa yanalikimbiza giza la usiku huku miale ya jua ikianza kuchomoza na kulipendezesha anga. Wanafunzi wa shule ya st Benard Blaziniar walikuwa wakijiandaa kwa siku mpya ya masomo. Kengere ya asubuhi iligongwa na kiranja wa zamu kuwaashiria wanafunzi waanze kujiandaa kuianza siku mpya ya masomo.

Taratibu wanafunzi wakawa wanatoka mabwenini wakielekea mabafuni kujiandaa kuianza siku mpya. Hakuna aliyefahamu kinachoendelea shuleni hapo. Baada ya mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi Girbons kutekwa na kupelekwa kusikojulikama, wote walishaamini Girbons ametekwa na maharamia wanaofanya biashara ya kishetani ya viungo vya albino kwa malengo ya kujipatia utajiri wa haraka haraka .

Hakuna aliyefahamu uwepo wa Girbons wala familia ya mzee Khalfan katika mazingira ya St Benard Blaziniar academy. Ilibaki kuwa siri ili kulinda usalama wao. Hata Girbons mwenyewe hakujua kuwa familia yao ipo hapo shuleni mafichoni nyumbani kwa mkuu wa shule. Kila kitu kikawa kinaendelea kwa usiri mkubwa mno kati ya mkuu wa shule Mr Kihiyo na mwalimu mlezi Sir Kameta.

Asubuhi na mapema kabla Girbons hajaamka, mwalimu wake alitoka kwenda kwa mkuu wa shule kumpa taarifa ya kupatikana kwa Girbons.
“Can’t belive this! Unasema Girbons yuko salama?”
Aliuliza kwa mshangao mwalimu Kihiyo. Kwake haikuwa rahisi kuamini…aliona kama muujiza.
Mwalimu kameta alizidi kumweleza kuwa yuko salama ingawa ameumia goti na mkono wa kushoto. Alizidi kumhakikishia kuwa yuko salama na kwa muda ule alikuwa nyumbani kwake akiwa bado amelala.

“Siwezi kuamini mpaka nikamwone kwa macho yangu, nahisi ni kama muujiza “
Yalikuwa ni mazungumzo ya mwalimu Kihiyo na Kameta. Hakuna aliyeamini kuwa ni kweli Girbons na familia ya Khalfan walikuwa salama ndani ya eneo la shule ya kimataifa ya St Benard Blaziniar Academy.

Mipango ya siri ikapangwa kuongeza ulinzi maradufu katika eneo la shule, hakuna mwanafunzi wala mwalimu mwingine yeyote aliyefahamu kinachoendelea , zaidi ya walimu wawili Mr Kihiyo na Sir Kameta.
********
Mr Mtaki, kiongozi wa kundi la wafanya biashara haramu, alipopata taarifa za kutoroka kwa ‘kitoweo’ wao Girbons, alimanusra afe kwa presha ya moyo. Alistaajabu jinsi alivyoweza kutoroka na kusababisha madhara makubwa ndani ya ngome. Haikuwahi kutokea mtu akaingizwa kisha kufanikiwa kutoka salama ndani ya ngome hiyo.

Hasira , hofu , chuki na ukatili vikamjaa mwili mzima. Alijua kuwa siri zote za mambo yanayoendelea ndani ya ngome zitatolewa na Girbons na kuwafanya watu wafahamu siri za utajiri haramu waliokuwa wanaumiliki yeye pamoja na wenzake wa “The Holy Trinity”... huo ndio ungemaanisha mwisho wake na wenzake na kundi lao haramu, kabla hawajaanza kuipata laana ya wafu , na majonzi ya walioonewa hapa hapa duniani na kesho ahera… . Hakuwa tayari kuona hilo likitokea.

Bila kupoteza muda akanyanyua mkonga wa simu ya kisasa iliyokuwa mezani kwake , muda mfupi baadaye tayari akawa ‘on line’ na majambazi ya BK85 Killers.

“Mnafanya nini sasa..
Mmelipwa millions of dollars kwa kazi feki! Damn it! hivi ninavyoongea nawataka wote hapa Boma Palace! Emergence alert! Over.”
Mtaki alikuwa akiongea kwa kufoka akionekana amechanganyikiwa mno kutokana na kutoroka katika mazingira ya kutatanisha kulikofanywa na kijana Girbons. Muda mfupi baadae kila mmoja akaonekana kuwa “busy” kupita kiasi ndani ya Boma Palace, yaliko makao makuu ya kundi hatari la matajiri, simu zikawa zinaingia na kutoka kila sekunde iliyopotea.

“We are waiting for you right now” alisikika Mataki akiongea na upande wa pili wa simu huku akiwa na jazba kupita kawaida. Hali ya mambo kwenye mitaa ya kuzunguka Boma Palace mpaka katikati ya jiji ilikuwa si shwari .honi za magari na breki vilisikika huku na kule wapiti njia wakinusuru kugongwa . wakati msafara mrefu usio na mpangilio ukishika kasi kuelekea Boma palace pembezoni mwa jiji karibu na ufukwe wa bahari ya Indi . mipango mikubwa ya himaya ya The holy trinity ikafunguliwa na msururu wa magari yaendayo kwa kasi ukawa umeshawasili . eneo zima likajazwa na pilika pilika za nguvu .

Muda mfupi baadae , ukumbi wa mikutano ulioko chumba cha chini kwenye himaya ya Boma palace ulikuwa umejaa . meza kuu walikaa watu wawili amatajiri wa the holy trinity musa Mtaki na pius Baganda na upande wa kulia walikaa majambazi wa BK&5 Killers huku upande wa kushoto wakiwa wamekaa wanaume kumi waliovalia suti nyeusi , kiongozi wao akiwa na “crown nyekundu “ kwa jinsi Mtaki alivyokuwa akiongea kwa jazba kila mmoja akaingiwa na tahamaki

“ mbwa nyie ! manalipwa mamilion ya pesa kwa kazi zisizoeleweka . mbwa mwenzenu zeruzeu ametoroka na kufanya maaangamizi ndani ya ngome hii na kuna taarifa wazazi wake na familia yake wako salama wamejificha pambezoni mwa pori la gamutu !, kila mmoja alishtushwa na taarifa hiyo iliyokuwa inatorewa na Mr Mtaki , bosi wa The holy trinity . hakuna aliyehamini kuwa ni kweli Girbons ametoroka kwenye ngome ya boma palace . wote wakabaki kutazamana . hawakuelewa kinachoendelea kwani waliamini mzee khalfani na familia yake walishaliwa na simba huko gamutu na Girbons alishachunwa ngozi .

Kiongozi wa majambazi wa BK &5Killers akaomba dakika moja kuongea na vijana wake juu ya kilichotokea . wakatoka nje huku wakiacha miguno mingi ndani ya chumba cha siri cha mikutano . walipotoka . Mr Mtaki akaendelea kwa ku toa tahadhari juu ya hatari iliyopo ikiwa halfan na familia yake na zeruzeru Girbons wakatoa siri ya walichofanyiwa . kila mmoja akawa anakuna kichwa kuonyesha kuguswa na mkasa huo wa kimiujiza .

Kwa vijana wa BK&5 Killers hiyo ilikuwa ni fedheha kubwa , kwani walionekana wameshindwa kazi kitu ambacho kiliwashushia heshima waliyojijongea. Waliporudi ukumbini kiongozi wao jidaw akasimama na kwa niaba ya enzake akasimama na kutoa maelezo . wakapewa masaa48 ya kukamilisha kazi . huku kikosi kingine cha majasusi wa black python kikiongozwa kusaidiana nao kukamilisha kazi mapema iwezekanavyo kabla ya mambo yahajaharibika , hakuna aliyetaka kupoteza muda, wote wakainuka na kila mmoja akatawanyika kinyake .BK&5Killers walitoka vichwa chini huku wakiapa kufanya “ kweli kulinda hadhi yao.

Mipango ilikuwa ikfanywa kuongeza usalama kwenye eneo zima la st benard blaziniar shule ya kimataifa iliyopo pembezoni mwa jiji . kikundi cha ulinzi binafsi kikaombwa kuja kihakikisha usalama , the spoiler security guard.

Usiku wapili tangu mzee khalfani na familia yake waingie ndani ya nyumba ya mwali kihiyo mkuu wa shule ya St benard Blaziniar , masaa machache tangu wakutanishwe na Girbons aliyekuwa amefichwa kwenye nyumba ya mwalimu kameta walikuwa kwenye chumba cha ndani kabisa wakifurahia kukutana kwao kwa mara nyingine . chakula kikaandaliwa kama shukrani kwa mungu kwa kuwanusuru .

Baada ya chakula ilibidi waanze kusimuliana kilichowatokea kila mmoja . ilikuwa ni hadhithi yenye kutia simanzi mtimani .Girbons muda wote alikuwa akitokwa na machozi kiasi cha kufanya uso wake uwe mwekundu zaidi . aliamini kuwa yeye ndio chanzo cha matatizo yote yalimkumba baba yake na familia nzima . aliomboleza zaidi misiba ya dada zake waliouliwa na simba wa gamutu wote wakaitikia “aamen!?


Khaleed na Girbons walikuwa salama kwa mara nyingine baada ya kupitia misukosuko ya kutisha. Walimshukuru sana Mungu wao kwa kuwanusuru na mauti yaliyowakosa kosa. Walimshukuru zaidi mzee Nyanda kwa moyo wa huruma aliokuwa nao, kwani bila yeye huenda wangepoteza maisha wakiwa eneo la tukio. Walimchukulia kama babu yao na yeye aliwaona kama wajukuu zake. Baada ya kuwa wamemueleza kwa kifupi yaliyowatokea, naye aliwasimulia historia fupi ya maisha yake. Wakazoeana haraka na wakawa kama ndugu wa familia moja.

Mzee Nyanda aliendelea kuwapa tiba za mitishamba, mpaka wakapona majeraha yao na kubakia na makovu ambayo nayo yalikuwa yakifutika taratibu. Siku zikawa zinaenda, Khaleed na Girbons wakiwa mafichoni. Haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kugundua kuwa bado wako hai. Pamoja na kuwa salama, kumbukumbu za matukio yale yaliyowapata zilikuwa zikijirudia mara kwa mara hasa kwa Khaleed, ambaye mara kwa mara alikuwa akishtuka usingizini na kuwataja wazazi wake.

Iliwawia vigumu sana kusahau yale yaliyowapata, na mzee Nyanda akawa na kazi ya ziada ya kuwasahaulisha kwa kuwasimulia hadithi kila jioni kabla ya kwenda kulala. Alijitahidi kuwajenga kisaikolojia na taratibu wakaanza kusahau baadhi ya matukio yaliowatokea maishani mwao.

Jioni moja wakiwa wameshakula chakula cha usiku, walikaa kwenye kiambaza cha nyumba pamoja na babu yao na kama kawaida akawa anawasimulia hadithi, wakiwa wameuzunguka moto. Baada ya kumaliza kuwasimulia, Khaleed alimuuliza swali mzee Nyanda, swali ambalo lilimfanya abadilike usoni ghafla.

Alimuuliza kwa nini anaishi peke yake kule mashambani, kwani tangu wafike pale kwake hawakuwahi kumuona mtu mwingine yeyote. Girbons nae alimuunga mkono mwenzake kwani ni kweli tangu wafike pale kwa mzee Nyanda, hawakuwahi kumuona mtu yeyote, si mke wala watoto wa Mzee Nyanda.

Swali lile liliuchoma sana moyo wa Mzee Nyanda kwani hakika walikuwa wamemkumbusha machungu ya siku nyingi ambayo alikuwa ameshayasahau. Hakujibu kitu zaidi ya kuonekana ni kama anayevuta kumbukumbu za jambo fulani, wakashtukia kumuona akianza kutoa machozi. Walijikuta wakijilaumu kwa kumuuliza swali lile. Ilivyoonesha kulikuwa na siri kubwa nyuma ya maisha yake.

Baada ya kimya kirefu, mzee Nyanda alishusha pumzi ndefu na kuanza kuwahadithia sababu zilizomfanya aishi maisha ya upweke namna ile…

“Miaka mingi nyuma, kabla hata hamjazaliwa , enzi hizo nikiwa bado kijana! Niliamua kutafuta mwenzi wa maisha yangu, ili aje kuwa mke wangu. Mungu alinisaidia na kweli nikampata.
Tukajaaliwa kuzaa watoto wawili wa kike ambao tuliwapenda sana. Kwa kipindi hicho nilikuwa nikifanya biashara ya madini, nikinunua kutoka kwa wachimbaji wadogo na kwenda kuyauza kwenye makampuni makubwa. Mungu alizidi kunibariki na biashara yangu ikawa inakua siku baada ya siku na baadae mimi na familia yangu tukahamia mjini kwenye nyumba mpya niliyoinunua…”

Wakati anaendelea kuwasimulia Khaleed na Girbons walitazamana baada ya kusikia Historia ile ikifanana na ya marehenu baba yao. Walitazamana kwa muda na wakawa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kilichotokea, kisha mzee Nyanda akaendelea…
“Penye riziki hapakosi chuki, wale watu niliokuwa naenda kuwauzia madini walianza kunionea wivu na wakaanza kupanga mipango ya kunidhulumu mtaji wangu wote. Chuki, wivu na tamaa dhidi yangu viliwaingia na wakawa wanapanga kunipoteza ili kile kidogo nilichokuwa nakimiliki wakichukue wao…”

Mzee Nyanda alishindwa kuendelea na akawa anafuta machozi yaliyokuwa yanauloanisha uso wake. Khaleed na Girbons walikuwa wametulia wakimsikiliza huku nao wakijisikia uchungu mioyoni mwao. Akaendelea na simulizi yake yenye kutia simanzi… Aliwasimulia namna ambavyo alijikuta akidhulumiwa mtaji wote, kisha nyumba yake aliyoinunua.

“Hawakuishia hapo kwani lengo lao lilikuwa ni kutuua wote ili kupoteza ushahidi. Baada ya kunipora kila kitu, waliiteka familia yangu pamoja na mimi mwenyewe na kwa macho yangu nilishuhudia mke wangu kipenzi akiuawa kikatili, ambapo wanangu wote wawili nao waliuliwa kikatili baada ya kulazimishwa kushika nyaya zenye umeme, ambazo ziliwakausha kama kuni. Haya yote yalitokea mbele ya macho yangu”, Mzee Nyanda akaendelea kusimulia…

“Mpaka leo watu wote wanaamini kuwa nilishakufa siku nyingi zilizopita, ila kwa kudra za mwenyezi Mungu niliponea katika tundu la sindano, katika mazingira ambayo mpaka leo naamini kuwa ni kudra za mwenyezi Mungu. Baada ya kunusurika niliamua kutorokea mbali na mji kuwakimbia mashetani wale, ndio nikaja huku porini, ambako taratibu nilianza shughuli za kilimo, mpaka leo hii mnenikuta nikiwa bado niko hai.”

Alimaliza kusimulia kwa ufupi Mzee Nyanda. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu kubwa iliyomfanya yeye kuishi maisha ya kipweke namna ile, kwani baada ya mkewe na wanae kuuliwa kikatili, aliapa kutooa tena maishani mwake.
Ilikuwa ni Historia iliyoshabihiana kwa kiasi kikubwa na yale yaliyowatokea katika familia yao. Kilichofuatia ikawa ni maombolezo, kila mmoja akiomboleza kivyake. Mioyo yao ilikuwa ikivuja damu…
*******
Baada ya mwezi mmoja kupita, hali za Khaleed na Girbons zilikuwa ni za kuridhisha. Majeraha yote yalikuwa yameshapona na kuacha makovu makubwa miilini mwao. Dawa za mitishamba walizokuwa wanapewa na mzee Nyanda ‘Babu’ ziliwaponyesha kwa haraka na wakawa wamerejea katika hali zao za kawaida. Pamoja na yote, bado walikuwa wakifikiria sana juu ya hatma ya mama yao na wadogo zao wawili waliosalia, Ismail na Rahma.

Waliamini kuwa tayari nao ni marehemu, na kama walikua bado wako hai, basi kwa vyovyote walikuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa sana. Walipanga mpango wa kutaka kufahamu kama kweli bado wako hai au wameshatangulia mbele ya haki. Walimwambia Babu yao juu ya mpango wao huo, lakini mzee Nyanda aliwakatalia kwani alitambua hatari iliyokuwa mbele yao.

Aliwatahadharisha kutothubutu kufuatilia kitu wasichoweza kupambana nacho, lakini wakawa wabishi wakizidi kung’ang’ania kuwa lazima wafahamu hatma ya mama yao na wadogo zao, hata kama walishakuwa marehemu walitaka kuupata ukweli. Licha ya kuendelea kuwaambia juu ya hatari wanayoweza kukutana nayo, bado waliendelea kung’ang’ania msimamo wao.

Mzee Nyanda alishangazwa na jinsi walivyokuwa wakijiamini, kwani kama angekuwa yeye asingethubutu kuyarudia matatizo baada ya kuponea chupuchupu. Walimhakikishia kuwa wangerudi salama, na hata kama ingetokea wakatekwa tena, basi walikuwa tayari kufa kiume.
“Faith can move mountains, if you got strong faith with what you want to do, just go ahead! Im with you in all your undertakings…(Imani ina uwezo wa kuhamisha hata milima, kama mna imani thabiti juu ya mnachotaka kukifanya, basi endeleeni! Niko pamoja nanyi katika kila jambo mtakalolifanya…)

Mzee Nyanda aliwaruhusu huku akiwatia moyo na kuwatahadharisha kuwa wawe makini ili wasije wakaingia tena matatizoni. Walipanga kuondoka jioni ya siku iliyofuatia ili wafike mjini usiku kukwepa kuonekana na watu. Lengo lao ilikuwa ni kwenda kupata uhakika wa mahali walipo ndugu zao kama walikuwa bado wako hai. Maandalizi ya safari ya hatari yakaanza kufanywa.

Jioni ya siku ya pili ikawadia…mzee Nyanda akawa anawaelekeza njia ya mkato ya kupita ili wafike mjini haraka bila ya kuonekana na watu. Wakaagana huku kila mmoja akiwa na huzuni ya kutengana na babu yao. Akawa anawaombea mafanikio ili warejee salama. Safari ikaanza.

**********

Ndani ya ngome ya Boma Palace, yalipo makao makuu ya kundi hatari la wafanyabiashara wa The Holly Trinity, Bi Miriam na wanae wadogo, Ismail na Rahma walikuwa wamefungiwa ndani ya chumba kidogo cha mateso kilichokuwa kimejengwa chini ya ardhi. Chumba kilikuwa kichafu sana, kikiwa hakina hewa ya kutosha huku sakafu yote ikiwa imemwagiwa chumvi nyingi ya mawe ambayo ilikuwa ikiwatafuna miguu yao vibaya. Baridi pia ilikuwa ikiwashambulia na kuwafanya wakondeane na kubaki mifupa mitupu.

Mwezi mzima walikuwa hawajaliona jua, huku wakilishwa pumba zilizosongwa kama ugali. Walitia huruma sana. Bi Miriam alikuwa akiomboleza usiku na mchana.
Hakuna aliyewaonea huruma, wakawa wanapewa mateso makali kila siku. Miili yao ikafa ganzi na wakawa wanasubiri kifo kiwachukue. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kitinda mimba wa Bi Miriam, kwani alikuwa bado mdogo sana ingawa naye alikuwa akipewa mateso kama mtu mzima. Alikuwa akipoteza fahamu mara kwa mara.

Wote watatu walikuwa na vidonda miilini mwao na wakawa kama maiti zinazotembea (Walking corpse). Baada ya kuhakikisha wamewatesa vya kutosha, kiongozi wa Holly Trinity aliamuru wachomwe sindano ya sumu, mmoja baada ya mwingine…mpaka wote wafe. Alianza kuchomwa Ismail na sumu ile ilikuwa ikifanya kazi ndani ya masaa 72 (Siku tatu).Siku ya tatu tangu achomwe, Ismail alipoteza maisha katika kifo cha kusikitisha mikononi mwa mama yake. Mwili wake ukatolewa na kwenda kutupwa baharini kama baba yake.
*******

Safari haikuiwa fupi kama khaleed na Girbons walivyodhania, kwani walitembea usiku kucha kwa msaada wa tochi waliytopewa na babu yao, mzee Nyanda. Mpaka kunaanza kupambazuka, walikuwabado hawajafika mjini. Wakazidi kuchanja mbuga kwa kutumia njia za mkato walizoelekezwa, mpaka jua lilipokuwa linaanza kuchomoza walikuwa bado wako msituni wakikatiza vichaka na mashamba ya karafuu kuelekea mjini.

Baada ya kuwa kumeshapambazuka, wakaona ni bora watafute sehemu ya kujificha mpaka jioni ifike, kwani hawakutaka kuonekana na mtu yeyote wakihofia usalama wao. Wakatafuta mti mkubwa wenye matawi yaliyofungamana, wakapanda juu na kujificha kwenye matawi.
Jua lilishachomoza na kukawa kumepambazuka kabisa.

Kwa mbali kidogo waliweza kuyaona makazi ya watu, wakagundua kuwa wako jirani kabisa na mjini. Wakashusah pumzi ndefu kutokana na uchovu wa safari.
Girbons alikuwa akipafahamu vizuri mahali ngome ya Holly Trinity ilipokuwa, kwani ni hapo ndipo aliponusurika kuchunwa ngozi na kukatwa viungo.

Alijuikuta mwili mzima ukimsisimka alipokumbuka mambo ambayo alikutana nayo nayo ndani ya ngome ile. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, walikubaliana kuwa giza litakapoingia, Khleed aende peke yake mpaka kwenye ile ngome, na kwa kuwa alikuwa haifahamu vizuri, Girbons alimuelekeza kila kitu na namna ya kufika pale bila kushtukiwa na mtu yeyote.

Kwa kuwa Girbons alikuwa na matatizo ya ulemavu wa ngozi, na watu walikuwa wameshaingiwa na pepo mbaya vichwani mwao, pepo wa kuamini9 kuwa viungo vya maalbino vilikua na uwezo wa kumfanya mtu atajirike haraka, ilibidi Girbons awer makini sana kutoonkana na mtu yeyote kwani akili za binadamu haziaminiki na huwezi kujua yupi mwema na yupi ni adui.

Alikumbuka kuwa Mzee Nyanda alikuwa amewasisitiza sana kuhusu kutoruhusu Girbons kuonekana kwa watu kwani Albino walikuwa wamegeuzwa kama wanyama wa porini waliokuwa wakiwindwa kutokana na imani potofu zilizokuwa zinaenea kwa kasi nchini Blaziniar.

Wakiwa juu ya mti, waliendelea kusubiri jioni ifike ndipo waendelee na safari yao. Kwa kuwa walikuwa wametembea usiku kucha, walijihisi uchovu sana na kwa kutmia mbinu za Kiskauti wakatengeneza kitanda cha kamba juu ya ule mti kisha wakajipumzisha. Usingizi mzito ukawapitia wote wawili.
****
BiMiriam na mwanae wa pekee aliyesalia walikuwa wakiendelea kupata mateso makali ndani ya chumba cha mateso. Baada ya ismail kuchomwa sindano ya sumu ambayo ilimtoa uhai baada ya siku tatu, majambazi bila ya kuwa na hata chembe ya huruma yalimchoma tena sindano ya sumu mtoto aliyekuwa amesalia.

Hiyo ilimaanisha kuwa baada ya siku tatu, naye angafariki dunia. Yalipanga kuwa Bi Miriam awe wa mwisho kufa baada ya kushuhudia watoto wake wote wakipukutika kama kuku wenye kideri. Hii ilitokana na hasira kali waliyokuwa nayo kutokana na ugumu walioupata wakati wa kuiteketeza familia yam zee Khalfan.

Ilikuwa ni oparesheni ngumu sana kwao kwani mpaka mwisho walikuwa wamewapoteza wenzao wengi, hali iliyozidi kuwa tia hasira.Waliamini Bi Miriam ndio angekuwa mtu wa mwisho kufa kwani walishaamini kuwa Khaleed na Girbons na walikuwa wamekufa pamoja na wenzao kwenye ile ajali mbaya ya gari.
Siku tatu baada ya mtoto wa mwisho kuchomwa sindano ya sumu, alikata pumzi mikononi mwa mama yake ndani ya chumba cha mateso kilichopo ndani ya ngome ya Holly Trinity. Bi Miriam alikuwa bado akijihisi yuko ndotoni kwani hakujua amemkosea nini Mungu wake mpaka kustahili yale yote yaliyokuwa yanamtokea. Yale majambazi yalikuja kuutoa mwili wa yule mtot na kama kawaida yakaenda kuutupa baharini.

Ikawa imefika zamu ya Bi Miriam kufa. Alichomwa sindano ya sumu kama wanae na taratibu ikaanza kusambaa ndani ya mwili wake na kuikoleza safari yake ya kuzimu. Alijua lazima atakufa baada ya masaa sabini na mbili (Siku tatu)


Ndani ya ngome ya Boma Palace, yalipo makao makuu ya kundi hatari la wafanyabiashara wa The Holly Trinity, Bi Miriam na wanae wadogo, Ismail na Rahma walikuwa wamefungiwa ndani ya chumba kidogo cha mateso kilichokuwa kimejengwa chini ya ardhi. Chumba kilikuwa kichafu sana, kikiwa hakina hewa ya kutosha huku sakafu yote ikiwa imemwagiwa chumvi nyingi ya mawe ambayo ilikuwa ikiwatafuna miguu yao vibaya. Baridi pia ilikuwa ikiwashambulia na kuwafanya wakondeane na kubaki mifupa mitupu.

Mwezi mzima walikuwa hawajaliona jua, huku wakilishwa pumba zilizosongwa kama ugali. Walitia huruma sana. Bi Miriam alikuwa akiomboleza usiku na mchana.
Hakuna aliyewaonea huruma, wakawa wanapewa mateso makali kila siku. Miili yao ikafa ganzi na wakawa wanasubiri kifo kiwachukue. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kitinda mimba wa Bi Miriam, kwani alikuwa bado mdogo sana ingawa naye alikuwa akipewa mateso kama mtu mzima. Alikuwa akipoteza fahamu mara kwa mara.

Wote watatu walikuwa na vidonda miilini mwao na wakawa kama maiti zinazotembea (Walking corpse). Baada ya kuhakikisha wamewatesa vya kutosha, kiongozi wa Holly Trinity aliamuru wachomwe sindano ya sumu, mmoja baada ya mwingine…mpaka wote wafe. Alianza kuchomwa Ismail na sumu ile ilikuwa ikifanya kazi ndani ya masaa 72 (Siku tatu).Siku ya tatu tangu achomwe, Ismail alipoteza maisha katika kifo cha kusikitisha mikononi mwa mama yake. Mwili wake ukatolewa na kwenda kutupwa baharini kama baba yake.
*******
Safari haikuwa fupi kama khaleed na Girbons walivyodhania, kwani walitembea usiku kucha kwa msaada wa ramani waliyopewa na babu yao mzee Nyanda. Mpaka alfajiri kunaanza kupambazuka, walikuwa bado wako porini.

Walizidi kuchanja mbuga kwa kutumia njia za mkato walizoelekezwa, mpaka jua lilipochomoza. Kwa kuhofia kuonekana na maadui zao walikuwa wakitembea vichakani kwa kujificha na wakawa wanaendelea kusonga mbele kuelekea mjini.

Baada ya kuwa kumeshapambazuka kabisa, wakaona ni bora watafute sehemu ya kujificha mpaka jioni nyingine ifike, kwani hawakutaka kuonekana na mtu yeyote wakihofia usalama wao.

Wakatafuta mti mkubwa wenye matawi yaliyofungamana, wakapanda juu na kujificha kwenye matawi. Jua lilishachomoza na kukawa kumepambazuka kabisa.

Kwa mbali kidogo waliweza kuyaona makazi ya watu, wakagundua kuwa wako jirani kabisa na mjini. Wakashusha pumzi ndefu kutokana na uchovu wa safari wakimshukuru Mungu wao kwa kuwalinda na safari ile ngumu ya usiku kucha.

Girbons alikuwa akipafahamu vizuri mahali ngome ya Holly Trinity ilipokuwa, kwani ni hapo ndipo aliponusurika kuchunwa ngozi na kukatwa viungo siku chache zilizopita kabla ya kufanikiwa kutoroka na kuponea chupuchupu.

Alijikuta mwili mzima ukimsisimka alipokumbuka mambo ambayo alikutana nayo nayo ndani ya ngome ile. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, walikubaliana kuwa giza litakapoingia, Khaleed aende peke yake mpaka kwenye ile ngome, na kwa kuwa alikuwa haifahamu vizuri, Girbons alimuelekeza kila kitu na namna ya kufika pale bila kushtukiwa na mtu yeyote.

Kwa kuwa Girbons alikuwa na matatizo ya ulemavu wa ngozi, na watu walikuwa wameshaingiwa na pepo mbaya vichwani mwao, pepo wa kuamini kuwa viungo vya Albino vilikuwa na uwezo wa kumfanya mtu atajirike haraka, ilibidi Girbons awe makini sana asionekane na mtu yeyote kwani akili za binadamu zilikuwa haziaminiki na huwezi kujua yupi mwema na yupi ni adui.

Walikumbuka kuwa Mzee Nyanda alikuwa amewasisitiza sana kuhusu kutoruhusu Girbons kuonekana kwa watu kwani Albino walikuwa wamegeuzwa kama wanyama wa porini waliokuwa wakiwindwa kutokana na imani potofu zilizokuwa zinaenea kwa kasi nchini Blaziniar.

Wakiwa juu ya mti, waliendelea kusubiri jioni ifike ndipo waendelee na safari yao. Kwa kuwa walikuwa wametembea usiku kucha, walijihisi uchovu sana na kwa kutumia mbinu za Kiskauti wakatengeneza kitanda cha kamba juu ya ule mti kisha wakajipumzisha. Usingizi mzito ukawapitia wote wawili.
***********
Bi Miriam na mwanae wa pekee aliyesalia walikuwa wakiendelea kupata mateso makali ndani ya chumba cha mateso. Baada ya Ismail kuchomwa sindano ya sumu ambayo ilimtoa uhai baada ya siku tatu, yale majambazi bila ya kuwa na hata chembe ya huruma yalimchoma tena sindano ya sumu mtoto aliyekuwa amesalia, Rahma.

Hiyo ilimaanisha kuwa baada ya siku tatu, naye angafariki dunia. Yalipanga kuwa Bi Miriam awe wa mwisho kufa baada ya kushuhudia watoto wake wote wakipukutika kama kuku wenye kideri. Hii ilitokana na hasira kali waliyokuwa nayo kutokana na ugumu walioupata wakati wa kuiteketeza familia ya mzee Khalfan.

Ilikuwa ni oparesheni ngumu sana kwao kwani mpaka mwisho walikuwa wamewapoteza wenzao wengi, hali iliyozidi kuwa tia hasira.Waliamini Bi Miriam ndio angekuwa mtu wa mwisho kufa kwani walishaamini kuwa Khaleed na Girbons na walikuwa wamekufa pamoja na wenzao kwenye ile ajali mbaya ya gari.

Siku tatu baada ya mtoto wa mwisho Rahma, kuchomwa sindano ya sumu, alikata pumzi mikononi mwa mama yake ndani ya chumba cha mateso kilichopo ndani ya ngome ya Holly Trinity. Bi Miriam alikuwa bado akijihisi yuko ndotoni kwani hakujua amemkosea nini Mungu wake mpaka kustahili yale yote yaliyokuwa yanamtokea. Yale majambazi yalikuja kuutoa mwili wa yule mtoto na kama kawaida yakaenda kuutupa baharini.

Ikawa imefika zamu ya Bi Miriam kufa. …Next to death! Alichomwa sindano ya sumu kama wanae na taratibu ikaanza kusambaa ndani ya mwili wake na kuikoleza safari yake ya kuzimu. Alijua lazima atakufa baada ya masaa sabini na mbili (Siku tatu) kama ilivyokuwa kwa wanae. Alijikuta akikata tama, na akawa anangoja kifo. Kilichomuumiza zaidi nikwamba alikuwa anakufa bila kujua wapi walipo wanae wawili waliosalia.

Hakujua nini kiliwatokea tangu walipotoroka usiku ule nyumbani kwa mwalimu Kihiyo. Alitamani kujua kama bado wako hai au la, lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa, alihisi kuwa tayarinao ni marehemu.
“Tutaonana Akhera!...” Aliongea Bi Miriam na kujilaza chini sakafuni, akisubiri muda wake ufike. Sumu ile ilikuwa ikiendelea kusambaa mwilini taratibu na kadri masaa yalivyokuwa yanakwenda akawa anakikaribia kifo.
*******
Baada ya kushtuka kutoka kwenye usingizi mzito, Khaleed na Girbons waliendelea kusubiri masaa yaende na hatimaye jioni ifike ili Khaleed aende kupata uhakika wa mahali walipo ndugu zake waliosalia, mama yake na wadogo zake wawili.

Njaa ilikuwa kali sana pale juu ya mti kwani hawakuwa na kitu chochote cha kula wala kunywa Masaa yalizidi kuyoyoma na hatimaye giza likaanza kuingia.
Walipohakikisha kuwa tayari giza limetanda kila mahali, Khaleed na Girbons waliagana na kama walivyokuwa wamekubaliana, Girbons akabakii juu ya mti kwa ajili ya usalama wake.

Wakaagana na kutakiana kila la Kheri, Khaleed akashuka chini na kuanza safari ya kuelekea kwenye ngome ya The Holly Trinity kama alaivyokuwa ameelekezwa na Girbons.
“Take care brother, all the Best!”( Kuwamakini kaka, kila la heri) Aliongea Girbons akimpungia mkono Khaleed.

Khaleed alipita njia za mkato na baada ya muda akawa amefika mbele ya ngome ya wafanyabiashara hatari wa Holly Trinity. Alijificha pembeni, umbali wa kama mita mia moja hivi, kwenye kichaka kilichokuwa pembeni ya ngome ile. Alikaa mahali ambapo aliweza kuona kila kitu kilichokuwa kinaendelea pale ngomeni.

Masaa yalikuwa yakikatika kwa kasi, dakika ,sekunde zikipotea kama upepo…Yakawa yamesalia masaa mawili tu, kabla ile sindano ya sumu aliyochomwa Bi Miriam haijammaliza. Alikuwa akisali kimoyomoyo akimuomba Mungu aipokee roho yake na kuipumzisha mahali pema peponi.

Mwili ulianza kumtetemeka, macho yakawa yanazingirwa na giza nene kiasi cha kupoteza kabisa nuru na kichwa nacho kikawa kinamgonga kwa nguvu. Ile sumu ilikuwa imekolea kisawasawa mwilini mwake.

“Death is my right! May God grant me eternal life”( Kifo ni haki yangu, Mungu nijalie uzima wa milele).

Wakati Bi Miriam akisubiri kukata roho, alishtukia mlango wa kile chumba cha mateso ukifunguliwa na wakaingia wanaume wawili wakiwa wamevalia makoti marefu na vitambaa vyeusi usonivilivyoziba nyuso zao. Tauyari ilishakuwa saa saa saba za usiku.

“Wee mwanamke nyanyuka! Stand up… hatutaki ufie humu ndani tupate kazi ya kuubeba mzoga wako na kwenda kuutupa. Twende ukafie nje, sio humu ndani, safari yako ya kuzimu imewadia…”
Aliongea mmoja wa wale wanaume ambao hata bila kuuliza alijiua ni miongoni mwa yale majambazi.
Walimnyanyua Bi Miriam juu juu na wakawa wanamburuza kumpeleka nje.

Bi Miriam hakuogopa tena kufa kwani moyo wake ulikuwa umeshakufa ganzi. Alijua lazima atakufa, tene usiku huo huo kabla ya jua halijachomoza.
Wakamburuza mpaka kwenye lango kuu la kutokea nje. Wakafungua mlango na kumtoa nje. Wakawa wanamburuza kuelekea kwenye vichaka vilivyokuwa pembeni kidogo ya ngome ile.
Khaleed alikuwa bado amejificha pale kwenye kichaka akitazama kila kilichokuwa kinaendelea.

Mara alishtuka kuona lango kuu La geti likifunguliwa na wanaume wawili waliovalia makoti marefu meusi na vitambaa vya kuficha sura zao wakawa wanatoka huku wakimburuza mwanamke ambaye Khaleed alimtambua Mara moja kuwa ni mamayake.

Alijikuta mapigo ya moyo yakianza kwenda kwa kasi ya ajabu.
“My God! She is my beloved Mum…”
Alikuwa ni mama yake, Bi Miriam!

Muda mfupi tangu Khaleed aondoke na kumuacha Girbons juu ya mti, Alibanwa na haja hivyo kulazimika kushuka chini. Aliamini hakuna ambaye angemuona kwani giza lilikuwa limetanda kila mahali. Alishuka taratibu mpaka chini na kuelekea kwenye kichaka kilichokuwa pembeni ya ule mti. Akiwa kwenye kile kichaka, alishtushwa kuona watu watatu wakiwa na tochi kubwa mikononi mwao, wakija usawa wa ule mti aliokuwepo. Walianza kumulika juu ya mti, wakimulika zaidi katika lile tawi walilokuwa wamejificha Girbons na Khaleed mchana kutwa tangu walipowasili asubuhi iliyopita.

Wale watu waliendelea kumulika juu huku wakiulizana maswali ambayo Girbons akiwa pale kwenye kichaka aliweza kuyasikia vizuri.
“Una uhakika ni huu mti kweli?”
“Ni huu huu, nina uhakika kabisa kwani niliwaona mwenyewe kwa macho yangu. Walikuwa wawili na huyo mmoja ndio zeruzeru”

Alikuwa akiongea mmoja wa wale watu kwa msisitizo mkubwa. Girbons alielewa moja kwa moja kuwa aliyekuwa akitafutwa ni yeye. Alijikuta akitetemeka mwili mzima na kukumbwa na hofu ya ajabu. Akiwa bado palepale kichakani alipojificha, wazo pekee lililomjia kichwani mwake ilikuwa ni kutimua mbio kwa kadri ya uwezo wake wote ili kuinusuru nafsi yake. Wale watu walikuwa wakizidi kuulizana maswali kwa sauti ya chini pale chini ya mti.

“Hata kama watakuwa wameshuka basi hawajafika mbali, tukiwawahi tutawakuta tu! Tusiachie mamilioni ya yule zeruzeru yatupotee kirahisi namna hii. Tukipata hata kiganja kimoja kinatosha sana na tutakuwa tumeuaga umaskini!”
Wale watu wenye roho za kishetani walikuwa wakizidi kujadiliana na sasa Girbons aligundua kuwa kumbe walikuwa na shida na viungo vya mwili wake.

“Why me Albino! Oooh My God, save me” (Kwa nini niumbwe nikiwa Albino? Eeh Mungu niokoe) Aliongea Girbons na kwa kasi ya ajabu akaanza kutimua mbio kuondoka pale alipokuwa amejificha. Hakufika mbali akashtukia anamulikwa na tochi kubwa, kisha wale watu wakaanza kumfukuza. Sekunde chache baadae walikuwa wameshamkamata na wakamrudisha pale chini ya mti huku wakimtishia kuwa akipiga kelele basi ule ndio ungekuwa mwisho wake.

Watu watatu waliokuwa wamevalia kofia maalum (Mask ) zilizoziba sura zao walikuwa wamemzunguka huku kila mmoja akiwa na kisu kikubwa mkononi. Girbons alijikuta akiishiwa na nguvu, akajua huo ndio mwisho wake. Alipiga yowe kubwa lakini wakamuwahi na kumziba mdomo asizidi kupiga kelele.

Walimlaza chini na mmoja akamkandamiza mgongoni kwa nguvu. Yule mwingine alimkamata mkono kwa nguvu na kuuweka vizuri. Akainua kisu kikubwa alichokuwa amekishika na kukishusha kwa nguvu kwenye mkono wa Girbons.
Kufumba na kufumbua, kiganja cha mkono kilikuwa kimetenganishwa kabisa na mkono.

Girbons alishuhudia yule mtu akikiokota kile kipande cha mkono wake na kukiweka kwenye mfuko mweusi wa plastiki wakiacha damu nyingi zikimwagika kutoka kwenye jeraha kubwa mkononi.

Yale maumivu aliyoyahisi yaliamsha nguvu za ziada za Girbons. Aliwarusha wale watu waliokuwa bado wamemkandamiza chini wakijiandaa kumkata mkono mwingine. Kwa nguvu za ajabu aliinuka na kutimua mbio kali akiwaacha wale watu wakipongezana kwa kufanikisha japo kidogo zoezi lao. Mkono wake ulikuwa umebakia kipisi ukivuja damu nyingi kuliko kawaida. Hakujali maumivu aliyokuwa akiyahisi, akazidi kutimua mbio akiwa hajui anakoelekea.
********
Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha ikiambatana na radi zilizokuwa zinapiga kwa nguvu, hali iliyowafanya watu waote wajifungie majumbani mwao. Mitaro ya kando ya barabara ilikuwa ikifurika maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi. Usafi wote uliozoeleka katika mitaa iliyopangwa vizuri, ulitoweka na barabara zote zikawa zimejaa takataka zilizosombwa na maji ya mvua.

Mitaro yote ya maji ilikuwa ikienda kumwaga maji baharini, kwenye bahari ya Hindi. Upande wa pili wa mji, kulikokuwa na bandari kubwa iliyotmika kama kitovu cha mawasiliano kati ya nchi ya Blaziniar na majirani zake, ikiwemo nchi ya Tanzania, shughuli za kupakia na kupakua mizigo zilikuwa zikiendelea kama kawaida.

Meli kadhaa zlikuwa zikiendelea kupakia mazao ya biashara na chakula kama karafuu, nazi, ndizi na mchele kupeleka nchi jirani. Blazinia ilikuwa ikitegemewa na majirani zake kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula yaliyokuwa yakisafirishwa kwa meli na kwenda kuuzwa nchi jirani.

Meli kubwa iliyokuwa na maandishi makubwa ubavuni yaliyosomeka MV PAINA ilikuwa ikijiandaa kung’oa nanga kuelekea nchini Tanzania, ikiwa na shehena kubwa ya mizigo. Manahodha na mafundi walikuwa kwenye vyumba vya chini vya meli (Main Deck) wakikagua injini na mitambo mingine kwa mara ya mwisho kabla hawajairuhusu meli ianze safari.

Nahodha mkuu, Weston Maseleka ndio alikuwa akiwaongoza mafundi wengine na kuwaelekeza sehemu za kuzifanyia uchunguzi. Yeye aliingia kwenye chumba cha ndani kabisa nilichokuwa na injini kubwa. Akiwa anaendelea na kazi yake, kwa msaada wa mwanga wa tochi kubwa aliyokuwa ameishika, aliona kitu ambacho kilimshtua mno. Ilikuwa ni michirizi mikubwa ya damu ambayo ilikuwa imetapakaa chini. Hakufahamu mara moja damu ile imetoka wapi na imekuwaje, akajikuta akipatwa na hofu. Kwa tahadhari kubwa akaanza kuifuata kuelekea kule ilikokuwa inatokea. Kwa kadri alivyokuwa anzidi kusogea, michirizi ilizidi kuongezeka, akazidi kuifuata kwa msaada wa tochi kubwa aliyokuwa ameishika.

Gkafla aliona kitu ambacho kilimshtua mno moyo wake, akajikuta aktetemeka mwili mzima. Ulikuwa ni mwili wa kijana mdogo wa kiume mwenye ulemavu wa ngozi. Alikuwa amelala chini huku mkono mmoja ukionekana kuvuja damu nyingi. Alizidi kumsogelea akiwa amemmulika na tochi kubwa pale chini alipolala. Hakuonekana kutingishika wala kugeuka, aliendelea kubaki vilevile. Aliinama na kumgusa mapigo ya moyo.
“Ooh My God! Whats this?”
*******
Khaleed alikuwa amekaa juu ya mchanga wa baharini akiwa analia kwa uchungu baada ya kuamini hatamuona tena ndugu yake wa pekee aliyekuwa amesalia duniani, girbons. Japokuwa mvua kubwa ilikuwa inanyesha, hakuonekana kujali kuloana. Akawa amekaa chini huku mvua kubwa ikiendelea kumnyeshea. Alijikuta akiichukia nchi yake kuliko kitu chochote. Akili yake ilikua ikiwaza jambo moja tu, kutoroka na kwenda nchi jirani kwani alishakosa uhakika wa usalama wake ndani ya nchi aliyozaliwa. Hakuwa na ndugu tena, alishawapoteza mama na baba, kaka na dada na mwisho alikuwa amesalia peke yake.

Mvua iliendelea kunyesha kwa muda mrefu na hatimaye ikaanza kupungua. Japokuwa alikuwa akiwaza kutorokea nchi ya jirani, hakujua angewezaje kuondoka kwani hakuwa na pesa hata kidogo. Aliendelea kukaa pale chini mchangani akizitazama meli zilizokuwa zikiingia na kutoka bandarini. Wazo pekee aliloliona linafaa kwa wakati ule ilikuwa ni kuzamia meli ya mizigo. Mvua ilipungua kabisa na sasa hali ya hewa ikaanza kuwa ya kawaida.

Khaleed aliinuka kutoka pale alipokuwa amekaa na taratibu akaanza kutembea kuelekea bandarini. Alipanga kutumia mbinu zake zote, ilimradi ahakikishe anandoka siku ileile. Alitembea taratibu ufukweni huku mawazo yakipishana kichwani mwake. Roho ya kisasi ilikuwa ikiwaka ndani yake mithili ya moto wa Jehanum. Aliamini hakustahili kuishi maisha kama yale, maisha ya upweke,maisha ya uyatima kwa sababu tu ya tamaa za watu wachache.
“I must revenge! Damn ‘em to hell! (Lazima nilipe kisasi, wote wakatupwe kuzimu)
Alikuwa akijisemea Khaleed huku akijifuta machozi. Macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa mekundu sana baada ya kulia kwa muda mrefu. Aliendelea kutembea taratibu akielekea bandarini huku kichwani akiendelea kupanga mbinu za namna atakavyofanikisha zoezi la kuzamia meli.
*****

Baada ya kuwasili mjini Tanga nchini Tanzania, Khaleed anajichanganya pamoja na watoto wanaoshinda bandarini wakifanya kazi ya kubeba mizigo na kuambulia ujira mdogo. Kwa kuwa alikuwa akiijua vizuri lugha ya Kiswahili, hakupata taabu kuchanganyikana na watoto wa mitaani. Ndani ya siku mbili tu akawa tayari ameshaanza kuyazoea mazingira ya mji mkongwe wa Tanga. Alikuwa akibeba mizigo kama wenzie na ujira mdogo alioupata ulimfanya awe na uhakika wa kula, wakati usiku alikuwa akijichanganya na wenzake na kulala kwenye meli mbovu zilizokuwa pale bandarini. Akawa ameyaanza maisha mapya ugenini, akiapa kuwa lazima atarudi kwao kwa lengo moja tu, kulipa kisasi kwa wote waliohusika kuisambaratisha familia yao.

Siku zikawa zinasonga mbele na akawa anazidi kuwa mwenyeji wa mazingira mapya. Pesa aliyokuwa anaipata kutokana na kazi yake ya kubeba mizigo aliweza kuitumia vizuri kwa uangalifu na akiba ndogo iliyokuwa inasalia, alikuwa akiihifadhi ili apate mtaji wa kufanya biashara ndogo ndogo. Baada ya siku chache, aliamua kuachana na kazi ya kubeba mizigo kwani alishapata akiba iliyomuwezesha kuanzisha biashara ndogo ya kuuza pipi barabarani. Aliendelea kuhangaika na maisha, na baada ya kuzunguka siku nzima akiuza pipi zake barabarani na kwenye stendi za daladala, usiku alikuwa akirejea kwenye meli mbovu na kulala na watoto wa mitaani.

Alijitahidi kufanya biashara kwa umakini mkubwa na taratibu mtaji wake ukawa unakua. Aliacha kuuza pipi na sasa akafanikiwa kupata meza ya kuuzia machungwa karibu na kituo kikuu cha mabasi. Baada ya miezi miwili kupita alishakuwa mwenyeji kabisa wa mji wa Tanga na usingeweza kumdhania kuwa ni mhamiaji. Alifanikiwa kupata chumba cha kujisitiri kwenye banda la uani la mama mmoja na pesa kidogo alizokuwa anazipata kwenye biashara yake akawa analipia kodi ya pango pamoja na kujikimu mahitaji madogo madogo kama chakula na mengineyo. Hakutaka mtu yeyote afahamu historia halisi ya maisha yake, hiyo ikabaki kuwa siri ndani ya moyo wake.

Heshima, upole, ukarimu na nidhamu ya hali ya juu aliyokuwa nayo vilimfanya apate wateja wengi kwenye biashara yake ya machungwa. Taratibu akaanza kuwa na jina. Mbali na kufanya biashara yake, Khaleed alikuwa na kipaji cha kuimba muziki ambao kwa Tanzania walikuwa wakiuita wa kizazi kipya. Kila siku jioni baada ya kumaliza biashara yake, alikuwa akiimba mashairi aliyoyatunga akiwa palepale kwenye biashara yake na watu wengi walionekana kuvutiwa na kipaji chake.

“Jamani huyu kaka anaimba vizuri! Mi nampenda”
Alisikika binti mmoja akiwaambia wenzake wakati wakitoka shule jioni moja. Khaleed alizidi kujijengea umaarufu mkubwa na akafanikiwa kupata marafiki wengi. Pamoja na kubadili kabisa mazingira ya kuishi, bado jinamizi la vifo vya ndugu zake lilikuwa likimwandama mara kwa mara. Alikuwa akijiwa na kumbukumbu mbaya za mambo aliyoyashuhudia akiwa na umri mdogo tu. Kumbukumbu ya vifo vya wazazi wake, wadogo zake na tukio la kaka yake mwenye ulemavu wa ngozi kufanyiwa ukatili wa kutisha vilikuwa vikimfanya alie sana usiku akiwa peke yake.

Roho ya kisasi ilikuwa ikiongezeka siku baada ya siku na kadri alivyokuwa akizidi kukumbuka, hamu ya kisasi nayo ikawa inazidi kuongezeka. Hakupenda kujihusisha na mambo ya ujana kama wenzake aliokuwa anafanya nao biashara ambao pesa kidogo walizokuwa wakizipata kama faida walikuwa wakizimalizia kwenye pombe na kustarehe na wanawake. Kwake ilikuwa tofauti na siku zote alikuwa akifahamu kuwa kuna jukumu zito mbele yake lililokuwa linamngoja, jukumu la kulipa kisasi cha damu.

Pamoja na kujitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuwaepuka mabinti kabla hajafikia umri wa kuoa kama alivyokuwa akiaswa na marehemu baba yake enzi za uhai wake, alijikuta katika wakati mgumu mbele ya mabinti wa kitanga ambao kila siku walikuwa wakienda kujaa kwenye meza yake anayofanyia biashara wengi wakionekana kuvutiwa naye kimapenzi. Kihaiba, mchanganyiko safi kati ya baba yake na mama yake aliyekuwa na asili ya visiwa vya Shelisheli ulimfanya Khaleed kuwa na haiba yenye mvuto. Ukiongeza na kipaji chake cha kuimba, alijikuta akiwa katika wakati mgumu zaidi wa kukwepa kujitumbukiza katika janga la ngono katika umri mdogo kwani miongoni mwa mambo aliyokuwa akitahadharishwa sana na wazazi wake ni hilo.

Baada ya kupata pesa ya kutosha, Khaleed alipata wazo jipya akilini mwake, la kwenda kujaribu bahati yake kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, huko Mererani mkoani Arusha, kaskazini mwa nchi ya Tanzania. Aliamini kuwa akifika huko maisha yanaweza kumnyookea kwani wengi wa vijana waliokuwa wakizamia machimboni, walikuwa wakirudi na utajiri. Akaanza kuandaa safari ya kuelekea Mererani kwa msaada wa pesa za akiba alizokuwa anajiwekea. Hakutaka kupoteza muda tena pale mjini Tanga, akafungasha kila kilichokuwa chake , akaaga kwa mwenye nyumba wake kisha akaenda stend ya mabasi ya Arusha alikokata tiketi tayari kwa safari.

Baada ya safari ndefu, hatimaye alikuwa ndani ya jiji la Arusha na hakutaka kupoteza muda jijini Arusha, alitafuta usafiri wa kumfikisha machimboni Mererani. Alifika salama na akajichanganya na vijana wengine waliokuwa wamezamia machimboni kutafuta maisha. Akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumia kwa ajili ya chakula na muda wa kulala alikuwa akilala kwenye makambi wanayolala wachimbaji wadogowadogo. Kwa kuwa alishapitia maisha ya mtaani akiwa mjini Tanga, haikumuwia vigumu sana kuyazoea mazingira.

Pesa ya akiba aliyokuwa nayo ilianza kupukutika kwa kasi kwani bado hakujua nini cha kufanya awapo machimboni pale, hali iliyomfanya awe anatumia pesa bila kuingiza chochote. Alianza kuchakarika kutafuta kazi ya kufanya kabla hajaishiwa kabisa pesa. Akafanikiwa kupata kibarua cha kutoa mchanga wenye madini kutoka kwenye mgodi uliokuwa unamilikiwa na kampuni moja ya kigeni. Aliungana na vijana wengine wengi waliokuwa wakifahamika kwa jina la utani la “Nyoka” kwani walilazimika kutambaa kama nyoka wanapokuwa chini kabisa ya mgodi kutafuta mchanga wenye madini.

Kazi ile ilikuwa ngumu sana na ya hatari, lakini kwa kuwa hakuwa na jinsi nyingine ya kufanya, aliona ni bora aendelee kuvumilia mpaka atakapofanikiwa. Siku ya kwanza kuingia mgodini, alihisi kama anaingia kuzimu kwani njia ya kuingilia chini uliko mchanga wenye madini ya Tanzanite, ilikuwa ni ndogo sana na walilazimika kutambaa kama nyoka huku kukiwa hakuna hewa ya kutosha wala mwanga na walilazimika kufanya kazi kwa muda wa masaa mengi. Ni siku hiyo hiyo ya kwanza kuingia mgodini, alishuhudia jinsi vijana wenzake walivyokuwa wakipoteza maisha wakiwa mgodi kutokana na kuangukiwa na vifusi vikubwa vya udongo na wengine kwa kukosa hewa.

“Chalii ‘angu huku chini bila kupata imani ya kazi bado hujaweza kufanya kazi, kunatisha mno! Ukiwa na roho nyepesi utakimbia mwenyewe, ukilemaa imekula kwako”
Aliongea kijana mmoja ambaye baadae alikuja kuwa rafiki yake, kwa lafudhi ambayo Khaleed hakuitambua kuwa ni ya kabila gani. Alikuwa akimwelekeza namna ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu kama yale na akamsisitiza kuwa asiogope kukutana na maiti kila baada ya hatua chache kwani hiyo ni hali ya kawaida pale mgodini. Khaleed alijikuta akiingiwa na woga kuliko kawaida kwai aliamini akikimbilia Tanzania angekuwa na amani, sasa hali aliyokuwa akiiona kule chini ilimfanya asijue nini cha kufanya.

Muda wa kazi uliisha na wakaamriwa kutoka kuwapisha watu wa zamu nyingine waingie. Ujira waliopewa kwa kazi ile ulikuwa mdogo sana usifanana na ugumu wa kazi waliyoifanya. Khaleed alijilaumu kwa nini alifikia uamuzi wa kwenda Mererani bila ya kufahamu vizuri kilichokuwa kule. Aliona ni bora angeendelea kuuza machungwa mjini Tanga kuliko kuenda kuhatarisha maisha yake namna ile. Lakini kwa kuwa alikuwa ameshayavulia maji nguo, hakuwa na jinsi zaidi ya kuyaoga. Aliona bora aendelee kujikaza mpaka kieleweke.
Wiki ya kwanza ndani ya machimbo ya Mererani, Khaleed anashuhudia mambo ambayo yanamuogopesha kupita kawaida. Anajuta zaidi kwa kuamua kwenda Mererani kwani kila siku anashuhudia jinsi vijana wenzake wanavyopoteza maisha huku kukiwa hakuna mtu anayemjali mwenzake.

Wanatumikishwa kwa masaa mengi ndani ya mazingira yanayotisha mno, wakilazimika kukaa ndani ya mashimo kwa masaa zaidi ya kumi na mbili kila siku. Anakutana na kijana mmoja wa kimasai anayegeuka na kuwa rafiki yake mkubwa, akimuelekeza namna ya kuishi napo Mererani.

Siku moja wakiwa ndni ya mgodi, zamu ya usiku, kunatokea ajali mbaya sana. Ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili za jioni, Khaleed na wenzake wakiwa wamepangwa zamu ya usiku. Kama kawaida kila mmoja alikuwa na zana zote za kufanyia kazi, tochi kubwa iliyofungwa kichwani huku mkononi kilammoja akiwa na sululu na koleo.

Baada ya watu waliokuwa zamu ya mchana kutoka wote mgodini, watu wa zamu ya usiku walianza kuingia, Khaleed akiwa miongoni mwao. Wakati wanaingia, kulikuwa na dalili ya mawingu mazito kuashiria kuwa muda mfupi baadae mvua kubwa ingenyesha.

“Chalii angu unaona hili wingu! Mvua itanyesha kinyama leo, huko chini inabidi kuwa makini maana mvua ikinyesha hali huwa inakuwa mbaya.”
Rafiki yake Khaleed mwenye asili ya kimasai, aliyeitwa Ololosokwan alikuwa akimtahadharisha baada ya kuona dalili zote za mvua kubwa kunyesha. Walianza kuingia mgodini kwa kupitia njia mbili tofauti.

Ilibidi Khaleed aongozane na rafiki yake Ololosokwan kwa sababu za kiusalama zaidi. Waliendelea kushuka kuelekea chini kabisa ya mgodi (Mantle). Wakati wakizidi kuteremka, walianza kusikia hali isiyokuwa ya kawaida. Hewa ilipungua sana na wakawa wanahangaika kupumua. Mara walishtukia kuona maji mengi yakiporomoka kutoka juu kuwafuata kule chini.

“Si nilikuambia chalii ‘angu! Kazi imeanza. Nishike mgongoni na usiniachie”
Khaleed alitii alichoambiwa na akamshikilia Ololosokwan kweye vazi lake la kimasai. Maji yakawa yanazidi kuporomoka kwa kasi huku wenzao waliokuwa nao kwenye msafara mmoja wakianza kupiga kelele za kuomba msaada.

Muda mfupi baadae mgodi ulikuwa unatiririka maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi kubwa, na kwa macho yake, Khaleed alishuhudia wenzake wakisombwa na maji kuelekezwa chini kabisa. Yule rafiki yake wa kimasai alikuwa akihangaika kutoboa ukuta wa mgodi kwa kutumia sululu yake. Aliendelea kuchimba kwa nguvu huku Khaleed akiwa amemshikilia kwa nguvu mgongoni kuzuia asije kusombwa na maji.

Baada ya kuhangaika kwa muda, hatimaye walifanikiwa kutoboa ukuta wa udongo na kuibukia kwenye njia ya pili iliyokuwa kavu. Ololosokwan alimvuta Khaleed kwa nguvu na wakawa wako eneo salama. Waliendelea kusikia vilio vya wenzao wakilia kwa sauti kubwa kuomba msaada lakini hakuna aliyewasikia. Bila kupoteza muda, walianza kupanda juu kutafuta njia ya kutokea. Walizidi kusikia maji yakipororomoka na kuwasomba wenzao wengi, wakazidi kuongeza kasi ya kupanda juu.

Ile njia waliyokuwa wameingia Kheleed na yule rafiki yake wa kimasai ilikuwa haitumiki kwa muda mrefu kutokana na ubovu uliokuwa umetokea kwenye mlango wa kuingilia. Pamoja na ubovu ule, haikuwa na maji kama zilivyokuwa njia nyingine. Walizidi kutambaa wakipanda juu kuelekea nje. Wakiwa wanakaribia kufika nje, Khaleed aliona kitu kilichomfanya aishiwe nguvu.

Alikuwa ni nyoka mkubwa sana akitambaa kuwafuata kule walikokuwa. Alimvuta miguu Ololosokwan na kumuonyesha yule nyoka na kwa haraka Ololosokwan alitoa sime kiunoni mwake na kumuwahi kabla hajaleta madhara. Alirusha sime yake na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili. Khaleed hakuamini alichokiona. Ololosokwan aliokota sime, akaifuta damu na kuiweka tena kiunoni na safari ya kupanda juu ikaendelea.

Wakati wanaendelea kupanda, Ololosokwan alimwambia Khaleed kuwa kwenye hiyo njia wanayopita, alikuwa ameficha jiwe kubwa la Tanzanite siku nyingi zilizopita, lakini alikuwa akishindwa kulitoa nje kwa kuhofia kukamatwa nalo, kwani walinzi wangeweza kumuua. Akamwambia kuwa kwa kuwa yeye bado hafahamiki vizuri na kumetokea ajali ile ya mgodi kujaa maji, watumie nafasi hiyo kulitoa mpaka nje na kama wangefanikiwa basi wangekuwa wameuaga umaskini.

Khaleed alisita kidogo kukubali lakini alipofikiria kuwa kilichompeleka Mererani ni kutafuta pesa, ilibidi akubali. Walienda mpaka pale alipomuelekeza kuwa alilificha jiwe lile, ambalo kwa haraka lilikuwa na uzito ulio karibia gramu 900 (karibu kilo moja). Kaleed hakuwahi kuyaona madini ya Tanzanite kwa macho, akajikuta mwili mzima ukitetemeka kwa hofu kwani hakuamini kuwa masaa machache yajayo angekuwa ameuaga umaskini kabisa.

Wazo pekee lililokuwa akilini mwake ilikuwa ni namna ambavyo angerudi upya kwao kulipa kisasi. Alilificha ndani ya kaptura yake ya Jeans aliyokuwa ameivaa kwa ndani na akahakikisha haliwezi kudondoka. Waliendelea na safari ya kutoka nje na baada ya muda wakawa wamefika sehemu ya kutokea nje. Walipochungulia nje, waliona vikosi vya uokoaji vikijitahidi kuzuia maji yasizidi kuingia mgodini huku wengine wakiitoa miili ya watu ambao walikuwa wameshapoteza maisha kutokana na maji yale. Miili ya vijana wengi ilikuwa imelazwa ardhini na kufunikwa kwa mashuka meupe na bado miili mingine ilikuwa ikizidi kutolewa. Ilikuwa ni ajali mbaya kuliko zote zilizowahi kutokea kwenye machimbo yale.

Khaleed na Ololosokwan walikubaliana kuwa watumie mbinu ya kujifanya mmoja anamuokoa mwenzake ili wasije kushtukiwa na kupekuliwa kwani walitokea kwenye mgodi ambao ulikuwa umepigwa marufuku kwa mtu yeyote kuutumia. Wakakubaliana kuwa Khaleed ajifanye amepoteza fahamu na masai Ololosokwan ambebe mpaka kule waliko waokoaji kisha atajifanya amerudiwa na fahamu ndipo waondoke eneo lile. Khaleed alikubali na akalihamisha lile jiwe la Tanzanite na kulifunga vizuri kwenye sehemu zake za siri.

Khaleed alifanya kama walivyokubaliana, na yule masai akambeba kama mtu aliyepoteza fahamu. “Saidia mimi yeyoo!”. Aliongea kwa sauti Ololosokwan na waokoaji wakamkimbilia na kumpokea Khaleed aliyekuwa amembeba mikononi. Akaenda kulazwa kwenye sehemu waliyolazwa maiti wengine. Alijikuta mwili mzima ukimsisimka kwani alilazwa katikati ya maiti za vijana wenzake waliokuwa nao kule ndani ya mgodi. Ololosokwan akawawahi na kuwaambia kuwa ndugu yake alikuwa bado hajafa na anaomba aendelee kumpatia huduma ya kwanza.

Walimkubalia bila kujua kuwa walikuwa wamepanga mbinu kali ya kutorosha mali yenye thamani kubwa. Ololosokwan alimbeba tena Khaleed na akamsogeza pembeni ambako hakukuwa na watu wengi. “Sasa chalii ‘angu hapa tunaelekea kulamba dume, tukifanikiwa mi n’tanunua ng’ombe wengi sana na kurudi nao kwetu Kibororony. We utajua cha kufanya mwenyewe.” Ololosokwan alikuwa akimnong’oneza khaleed sikioni kwa lafudhi ya kimasai wakati akijifanya kama anamsaidia kupumua.

Wakati wakiendelea kutafuta mbinu ya namna ya kutoka, kuna walinzi ambao walikuwa wamewashtukia na wakawa wanawafuatilia kwa karibu. Walihisi lazima kuna mzigo waliouficha kwani walikuwa wakimfahamu vizuri yule Masai kwani mara kwa mara alikuwa akijaribu kutoroka na mzigo lakini alikuwa akishindwa kutokana na kubanwa na walinzi.

Khaleed aliinuka na kujifanya amepata nafuu na wakawa wanatembea huku Masai akiwa amemshikilia begani.

Walielekea kwenye kichaka kilichokuwa karibu na mgodi na walipofika nyuma ya kichaka, mahali ambapo waliamini hakuna anayewaona, walianza kutimua mbio kali kuzidi kutokomea porini. Mi si nilikuambia, yule Masai mjanja sana. Hebu waone wanavyokimbia! Lazima watakuwa wametoka na mzigo. Njoo tuwawahi inaweza kuwa ni bahati yetu leo. Tukikuta wana mzigo wa maana, bora kuwapiga risasi halafu sisi tutambae na mzigo.

Walinzi watatu wa mgodi walikuwa wakijadiliana baada ya kuwaona Masai na Khaleed wakitimua mbio kuzamia vichakani. Wakaweka silaha zao mikononi na kwa kasi ya ajabu wakaanza kukimbia kuelekea kule Khaleed na Masai walikokimbilia.
*****

Khaleed na rafiki yake wa kimasai, Ololosokwan walifanikiwa kutoroka na jiwe kubwa la madini ya Tanzanite kutoka kwenye mgodi wa Mererani baada ya ajali mbaya kutokea katika mgodi huo kufuatia ya maji kujaa kwenye mashimo yaliyokuwa na watu ndani yake.

Wakati wanatoroka walinzi watatu waliwashtukia na wakawa wanawafuatilia kwa makini. Baada ya kuwaona wakitimua mbio kuzama vichakani, wale walinzi nao waliweka silaha zao tayari na kuanza kuwakimbiza. Khaleed na rafiki yake mmasai hawakujua kama wanafuatiliwa kwa nyuma, wakawa wanakimbia wakiamini hakuna aliyewaona. Mbele kidogo, masai anachezwa na machale na anamwambia Khaleed anahisi kuna hatari iliyokuwa inawakaribia. Ilibidi apande juu ya mwamba mkubwa wa mawe na kutazama kule walikokuwa wametokea.

Hakuamini macho yake alipowaona walinzi watatu wenye silaha wakija kwa kasi kule walikokuwa. Alishuka haraka kutoka kwenye ule mwamba na kumwambia Khaleed alichokiona.
Kwa kasi ya ajabu walitimua mbio wakibadili uelekeo ili kuwachanganya wale walinzi. Baada ya kukimbia kwa muda, wakatafuta pango lililokuwa chini ya miamba mikubwa ya mawe, wakaingia ndani na kujificha. Khaleed alikuwa akihema kwa kasi kufuatia uchovu mkubwa aliokuwa nao kutokana na ile ajali ya kule mgodini.

Giza lilianza kuingia wakiwa bado ndani ya lile pango. Waliona ni bora waendelee kujificha mpaka kutakapokuwa shwari ndio waendelee na safari yao ya kutoroka na mzigo wa Tanzanite. Walipanga kwenda mpaka Arusha ambako ndiko kulikokuwa na soko la uhakika.

Walipohakikisha kumetulia kabisa, walitoka na kuendelea na safari yao wakikatiza maporini kuitafuta barabara kuu ya kuelekea Arusha. Baada ya kitambo kirefu wakawa wametokea barabarani. Kila mmoja alikuwa na matumaini ya kufika mjini salama na wakawa wanawaza watakavyogawana mamilioni ya pesa baada ya kuuza madini yale.

Khaleed alishaanza kupanga mipango ya namna atakavyorudi kwao kuanza kulipa kisasi. Kilometa chache mbele waliona mwanga wa taa za gari likija kutokea mbele yao. Kwa haraka walikimbilia kwenye vichaka vilivyokuwa pembezoni mwa barabara na kujificha kwani hawakutaka kuonekana na mtu yeyote.

Katika hali ya kushangaza, walishtukia kuona lile gari likipunguza mwendo na kusimama jirani kabisa na pale walipokuwa wamejificha. Wakawaona askari zaidi ya sita wakiwa na silaha wakishuka na kuanza kuelekea upande ule waliokuwa wamejificha. Walipowatazama vizuri waliwatambua kuwa ni wale walinzi watatu ambao walikuwa wakiwafuatilia tangu kule mgodini wakiwa na askari polisi.

Walijikuta wakitetemeka kwa hofu na kwa haraka wakaanza kukimbia upya kuzama porini. Japokuwa ilikuwa ni usiku na giza likiwa limwtanda kila mahali, walitimua mbhio kwa kadri ya uwezo wao wote wakikwepa kuonekana.
Wale askari walianza kumulika huku na kule vichakani na kwa mbali wakawaona Khaleed na Ololosokwan wakitimua mbio.

“Wale kule! Lazima watakuwa na mzigo mkubwa sana, si unaona wanavyojihami. Lazima tuwatie nguvuni” Aliongea mlinzi mmoja akiwaonyesha wenzake. Wakaanza kuwafukuza huku wakiwamulika na tochi kubwa.
Khaleed na masai walizidi kutimua mbio kwa uwezo wao wote lakini wakajikuta wakimulikwa na tochi kubwa.

“Simameni wenyewe kwa usalama wenu kabla hatujawafyatulia risasi”
Askari mmoja alitoa amri akiwataka Khaleed na masai wasimame lakini hawakutii, wakawa wanazidi kuchanja mbuga. Mbele kidogo wakajikuta wamefika juu ya mwamba mkubwa wa mawe ambao mbele yake kulikuwa na korongo kubwa lenye maji kwa upande wa chini. Walijikuta wakisita kusonga mbele kwani hawakuwa na uwezo wa kuruka korongo lile hasa ukizingatia kuwa ilikuwa ni usiku sana.

“Tujisalimishe tu chalii ‘angu, imekula kwetu leo! Hatuna tena ujanja”
Aliongea Masai akimwambia Khaleed kuwa ni bora wasalimu tu amri. Wazo hilo halikumuingia Khaleed akilini kwani kama angekubali kutiwa mikononi mwa askari wale, tena akiwa ugenini hiyo ingemaanisha kuwa hataweza kamwe kutimiza kazi nzito ya kulipa kisasi.

Alipokumbuka mikasa aliyokwisha kuipitia maishani mwake, aliona ni bora kufa kuliko kukubali kukamatwa kikondoo. Wakiwa bado wanajadiliana nini cha kufanya, wale walinzi na askari polisi walikuwa wameshafika na wakawa wanawamulika kwa tochi zao kubwa. Mmoja alifyatua risasi hewani kisha akatoa amri kali ya kuwataka wainue mikono juu kusalimu amri.

Khaleed aligeuka na kulitazama tena lile korongo, urefu wake ulitisha. Rohoya ujasiri wa ajabu ikamuingia na akajikuta akiamini kuwa anaweza kiokoa nafsi yake kwa kuruka lile korongo. Aligeuka mzima mzima akawa anajianza kuruka. Yule rafiki yake mmasai alimkataza kwani alijua hatari ambayo angekumbana nayo kwa kuruka korongo refu namna ile. Khaleed hakutaka kumsikiliza tena... akahesabu moja... mbili... tatu! Akajirusha kama mwanasarakasi na kuanza kuporomoka kuelekea chini. Ololosokwan alipiga kelele kubwa kumzuia lakini alikuwa amechelewa.

Hakuamini amepata wapiujasiri wa namna ile kwani licha ya yeye Ololosokwan kuwa mzawa wa maeneo Yale hakuwahi kumuona au kusikia mtu akiruka kwenye korongo refu namna ile. Alibaki amejishika kichwani akiwa haamini alichokiona. Sekunde chache baadae wale askari na walinzi walikuwa wameshamzunguka Ololosokwan. Nao hawakuamini kuwa ni kweli mhalifu wao amejitosa na kuruka kwenye korongo lile.

“Huyo aliyeruka hakuna hata haja ya kumfuatilia, hili ndio jeneza na kaburi lake kwani hawezi kusalimika” Wale askari walikuwa wakielezana wakati wakimfunga pingu Ololosokwan. Walimulika chini ya lile korongo lakini hawakuona kitu. Wakambeba Ololosokwan juu juu na kuanza kurudi naye kule barabarani walikoliacha gari lao.

Walimfunga Masai nyuma ya gari wakaanza kurudi mgodini huku wakimtolea maneno ya vitisho kuwa hatimaye mwisho wake ulikuwa umefika baada ya kuwasumbua kwa muda mrefu na asingeweza kukwepa adhabu kali ambayo angepewa na wamiliki wa mgodi baada ya kufanya hujuma kubwa.

*****
Baada ya kujirusha kwenye korongo lile, alikuwa akimuomba Mungu wake kimoyomoyo amnusuru kwani hakuna baya lolote alilokuwa amelifanya. Alizidi kumuomba Mungu wake afanye muujiza wowote ili asalimike. Aliamini hawezi kudhurika kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.

Alipokuwa akiendelea kuruka, alijikuta akinasa juu ya tawi la mti kabla hajafika chini. Kwa haraka na kwa kutumia nguvu zake zote, alijishikilia kwenye lile tawi na akawa anabembea. Alipoinua macho na kutazama juu na chini, aligundua kuwa yuko katikati ya korongo, chini mbali na juu mbali.

Aliendelea kuning’inia kwenye lile tawi la mti akiwa hajui angewezaje kutoka pale. Alijishikilia kwa mkono mmoja, na mkono mwingine akaupeleka kwenye ikulu yake alikoficha lile jiwe la Tanzanite. Alijikuta akitabasamu mwenyewe baada ya kuona kuwa liko salama. Kwa kuwa ilikuwa tayari ni usiku sana, aliona bora aendelee kujishikilia palepale mpaka kutakapopambazuka ndio atafute namna ya kujiokoa.

Alijishikilia kwa nguvu zake zote na akawa anaomba kupambazuke haraka. Moyoni aliendelea kumuomba Mungu wake atende miujiza ili hatimaye afanikiwe kurudi salama nyumbani kwao kwa ajili ya kazi moja tu, kulipa kisasi cha damu ya ndugu zake iliyomwagika bila ya hatia.

Masaa yalizidi kuyoyoma na taratibu kukaanza kupambazuka. Khaleed alikuwa bado amenin’gia kwenye tawi la mti katikati ya korongo refu. Alianza kuhisi mikono yake ikikosa nguvu na kuanza kutetemeka. Alizidi kujikaza kiume kwani kama angejiachia na kuporomoka mpaka chini, hakika huo ndio ungekuwa mwisho wake.

Kulizidi kupambazuka na kijua cha alfajiri kikaanza kuchomoza kuashiria mwanzo wa siku mpya. Sasa Khaleed aliweza kuona vizuri mahali aliokuwa. Ilikuwa ni katikati kabisa ya korongo. Alijishangaa ujasiri wa kuruka korongo refu namna ile aliupata wapi. Alipotazama kule chini tena, alijikuta mwili wote ukimsisimka kwani kama isingetokea muujiza wa kunasa juu ya lile tawi basi ule ndio ungekuwa mwisho wake.

Alianza kutafuta mbinu za kujikwamua kutoka pale alipokuwa amening’inia. Alianza kujivuta kwenye matawi ya ule mti akawa anapanda kuelekea juu. Alihangaika kwa muda mrefu sana lakini Mungu wake alimpigania kwani mwisho wa siku alifanikiwa kufika juu kabisa ya lile korongo. Alijitupa juu ya udongo akiwa haamini kama ni kweli amesalimika. Aligeuka na kutazama tena kule alikotaka kudondokea. Alijikuta akishusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu wake kwa kumnusuru na kifo kama kile.

Aliendelea kulala pale chini kwani mikono yake ilikuwa imekufa ganzi kutokana na kuninginia juu ya mti kwa siku nzima. Akiwa amelala pale chini, aliskia vishindo vya mtu akija kwa kasi. Hakutaka hata kugeuka na kumtazama. Yule mtu akamsogelea jirani na kwa sauti ya ajabu akamuuliza…
“Wewe ni nani na unafanya nini hapa!”

Khaleed alishtushwa na ile sauti, akageuka na kumtazama. Alijikuta akipiga kelele
“Mungu wangu!”

Khaleed akiwa amelala pale chini yule mtu alimuuliza tena, safari hii kwa sauti ya ukali.
“Nakuuliza wewe ni nani na unafanya nini hapa?” Kwa tabu Khaleed alijigeuza na kumtazama yule mtu aliyekuwa akimsemesha. Alikuwa ni mwanaume mwenye mwili mkubwa huku usoni akiwa na ndevu nyingi mithili ya gaidi la kiarabu.

Khaleed alijikuta akitetemeka mno kutokana na hofu. Hakuwahi kumuona mtu kama yule maishani mwake. Akashindwa kuelewa nini cha kufanya. Lile jitu lilimuamuru kusimama juu na kwa haraka Khaleed alitii amri ile. Akainuka huku mikono yake akiwa ameiinua juu.

Yule mtu hakuonyesha masihara hata kidogo, akamsogelea jirani kabisa na pale alipokuwa amesimama na kuanza kumhoji maswali. Ilibidi Khaleed aanze kujitetea na kumueleza yule mtu kuwa alikuwa amepatwa na matatizo makubwa. Hakusita kuongea uongo ilimradi tu aachiwe huru.

Baada ya kuongea uongo mwingi, yule mtu wa ajabu alimuelewa na akaahidi kumsaidia usafiri wa kufika mpaka Arusha mjini. Alimchukua Khaleed na kwenda naye yalipo makazi yake, chini kabisa ya bonde ambalo Khaleed alinusurika kupoteza maisha usiku uliopita.

Ilikuwa ni ndani ya kijumba ambacho kilikuwa kama pango na usingeweza kugundua kwa haraka kuwa kuna mtu anaishi ndani yake. Baada ya kufika, yule mtu alianza kumueleza Khaleed kuwa yeye ni jambazi na hufanya kazi ya kuteka magari yanayosafirisha madini kutoka machimboni Mererani.

Khaleed alishindwa kuelewa yule mtu amemuamini vipi mpaka amfichulie siri nzito kama zile. Alizidi kumueleza jinsi ambavyo hufanya kazi yake na akawa anamuonyesha baadhi ya vifaa ambavyo huvitumia kwa ajili ya kazi yake.

Khaleed hakuamini macho yake wakati akionyeshwa bunduki nyingi za kisasa zilizokuwa zimepangwa ndani ya sanduku kubwa la chuma. Alionyeshwa pia mabomu ya kurusha kwa mkono na silaha nyingine nyingi ambazo zilimfanya Khaleed awe anatetemeka kwa hofu.
Baada ya kumueleza kwa kirefu, alianza kumshawishi Khaleed aungane naye kwenye kazi ile na akamhakikishia kuwa hakuna hatari yoyote kwani silaha ambazo wangekuwa wanazitumia zilikuwa ni za kisasa na hata Polisi walikuwa wakiziogopa.

Khaleed alibaki kuduwaa akiwa hajui akubali au akatae kuungana na yule mtu kwenye kazi hatari ya ujambazi. Kwa kuwa alikuwa na shida, ilibidi ajifanye kukubali ili asije akadhuriwa na yule mtu. Alimkubalia kila kitu na akamdanganya kuwa alikuwa tayari kuungana naye kwani hata yeye alikuwa akitafuta pesa. Yule mtu alifurahia mno kupata kijana wa kusaidiana naye kazi.

Khaleed mawazoni mwake alikuwa akiwaza namna ambavyo angemtoroka yule mtu. Akiwa kwao alizoea kusikia nchi ya Tanzania ikisifiwa kuwa na amani na utulivu wa hali ya juu. Alishangaa kwanini vitendo hatari kama vile vya ujambazi vilikuwa vikifanyika kwenye nchi inayosifika dunia nzima kwa amani na utulivu.

Khaleed aliendelea kukaa na yule mtu kwa muda mrefu akimdadisi mambo mengi. Ndani ya masaa machache waliyokaa pamoja walizoeana kama watu waliofahamiana miaka mingi nyuma. Jioni ilipoingia, walitoka kule mafichoni na wakaenda mpaka barabarani wakitumia njia za mkato.

Katika muda wote huo, Khaleed alikuwa makini sana kuhakikisha lille jiwe la Tanzanite liko salama ndani ya bukta yake. Baada ya kufika barabarani, walisimamisha gari lillilowapeleka mpaka Arusha mjini. Waliingia majira ya saa tano za usiku na wakafikia kwenye hoteli moja iliyokuwa uchochoroni. Yule mtu alimwambia Khaleed kuwa watakaa hapo mpaka saa nane za usiku ambapo wangetoka na kwenda kufanya tukio moja la ujambazi huko Kijenge Juu.

Khaleed hakuwa tayari kuungana na yule mtu kufanya ujambazi, akili yake ikaanza kucheza kwa haraka akitafuta njia ya kumtoroka. Alimkabidhi kabisa Bastola na akawa anamuelekeza namna ya kuitumia. Hakutaka kuonyesha dalili zozote ambazo zingemfanya amshitukie kuwa anataka kumtoroka.

Ilipotimu saa saba za usiku, likiwa limebakia saa moja kabla hawajaenda Kijenge kufanya Uhalifu wa kutumia silaha, Khaleed alipata upenyo na akafanikiwa kutoroka na bastola aliyopewa. Alikimbia mpaka alipohakikisha amefika mbali kabisa, akatafuta sehemu ya kujificha na kulala mpaka asubuhi.

Kulipopambazuka tu, aliamka haraka na akahakikisha kuwa jiwe lake liko mahali pake. Alianza kutafuta sehemu ambako kuna wanunuzi wa madini ya Tanzanite na baada ya muda akawa ameshaoneshwa. Alisubiri mpaka maduka yote yalipofunguliwa, akaingia kwenye mojawapo ya maduka yanayonunua madini.

Hakuamini macho yake pale alipokuwa akikabidhiwa kitita chake cha pesa. Zilikuwa ni takribani Shilingi za Kitanzania milioni kumi na moja, ambazo alizibadilisha palepale na kupewa dola za kimarekani. Alishangaa sana kwani hakudhania kuwa jiwe dogo kama lile lingeweza kufikia kiwango kikubwa cha pesa kama kile. Bila hata kuaga alitoka na kuanza kutafuta njia ya kuondoka haraka jijini Arusha.

Kwa kuwa alikuwa na pesa za kutosha, aliona ni bora asafiri mpaka kisiwani Zanzibar ambako alipanga kwenda kuweka ngome yake wakati anafikiria na kupanga mipango ya kurudi nchini kwao Blazinia, kwa ajili ya kazi moja tu! Kulipa kisasi kwa wote waliohusika kuiangamiza família yao bila ya hatia.

Baada ya siku mbili, tayari alikuwa ametua kisiwani Zanzibar, akatafuta hoteli moja yenye hadhi ya juu iliyokuwa ufukweni mwa bahari ya Hindi. Akaweka kambi na kuanza kupanga oparesheni maalum, oparesheni aliyoipa jina la Blood Revenge( Kisasi cha damu).

***MWISHO****

JIANDAE KUSOMA SEHEMU YA PILI
Coming soon…The Blood Revenge( Kisasi cha damu)
amenibarikihash@rocketmail.com
newera7113.blogspot.com
+255 (0) 768540912
STAY BLESSED YOU ALL!

1 comment:

  1. Duuu mkuu iko poa sana,,sema kuna baadh ya vpengele havijaelezwa vzur,,sijui ulvruka?,,,mfano pale mzee Alfa ilpokua anatunzwa ndan ya shule ilfkaje mpaka kuuawa?hukuekeza hapo ila ukalukia kpengele kngne kabsa mkewe akiwa ndan ya himaya ya trinity,,,,but nmeipenda,,mafundsho kbao,,nasubr paty 2

    ReplyDelete

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...