SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 2ILIBIDI nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda nikiamini pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yeyote ili aniwahishe kabla ile ‘ambulance’ haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja, nilijiona kuwa mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti na kawaida.
Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini, nilipiga hatua mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
SASA ENDELEA…
“OYA mambo vipi mkubwa!” nilimsalimu dereva wa bodaboda aliyekuwa pembeni yangu kwa bashasha kubwa lakini hakuniitikia, akawa anaendelea kuifutafuta bodaboda yake.
Nilirudia kumsalimu lakini bado hakunijibu chochote na wala hakuonyesha kama ananisikia. Nilimgusa begani lakini bado ilikuwa ni kazi bure, aliendelea kufutafuta bodaboda yake, nikabaki nimepigwa na butwaa.


Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye nikamsalimia kwa bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa akipiga stori na wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
“Kwani imekuwaje? Mbona sielewi kinachoendelea?” nilijisemea huku nikianza kutetemeka kwa hofu kubwa, mwisho niliamua kufanya jambo moja, nilipaza sauti kwa nguvu nikiita ‘bodabodaaa!’ niliamini yeyote ambaye atakuwa wa kwanza kuniona basi nitamchukua huyohuyo lakini wapi! Kila mmoja aliendelea na mambo yake.