ILIPOISHIA:
Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika
suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa
nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu
waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba
ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo
yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana
uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.
SASA ENDELEA...
“Inabidi uvue nguo zote na kukimbia
kuelekea upande wa Magharibi mpaka uvuke barabara ya lami kisha kimbia mpaka
utakapoukuta mti mkubwa wa mbuyu, uzunguke mara saba kisha fumba macho,
usifumbue mpaka nitakapokwambia,” sauti ya baba ilisikika masikioni mwangu.
Yaani nivue nguo zote na kuanza kukimbia
nikiwa mtupu? Kibaya zaidi, upande huo wa Magharibi aliokuwa anausema ilikuwa
ni kulekule nilikokuwa nakimbia. Kwa lugha nyepesi nilitakiwa kuanza upya
kukimbia kurudi kule nilikotoka, safari hii nikiwa mtupu! Ilikuwa ni zaidi ya
mtihani.
Kitu pekee nilichokuwa nakihitaji,
ilikuwa ni kuokoa na balaa hilo kwani kwa jinsi wale wazee waliokuwa
wakinikimbiza walivyokuwa na hasira, kama wangenitia mikononi mwao sijui nini
kingetokea. Ilibidi nipige moyo konde, harakaharaka nikavua nguo zote na viatu,
nikavikunja na kuvitia kwapani.