Saturday, February 18, 2012

BOTI YAZAMA ZIWA VICTORIA, ZAIDI YA WATU 40 WAHOFIWA KUFA

HASH POWER 7113// Acreditation FikraPevu, Sitta Tumma
 WATU wanaokadiriwa kuwa 35 wanahofiwa kufa maji katika eneo la Kahunda Maisome, Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, baada ya boti ya abiri waliyokuwa wakisafiria kuzama maji ndani ya Ziwa Victoria.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 10 jioni, ambapo inasadikiwa boti hiyo ilikuwa ikitoka Maisome kwenda Kahunda, na kwamba ilipofika katikati ya Ziwa, ilipigwa na dhoruba kali, hali iliyosababisha maji kuingia kisha kuzama boti hiyo ya mtu binafsi.
Taarifa zilizotufikia kutoka wilayani Sengerema zinadai kwamba, boti hiyo iliyokuwa imesheheni abiria, ilikumbwa na dhoruba hiyo kali, kisha kupoteza mwelekeo na baadaye kuzama ndani ya maji katika Ziwa Victoria.

Ajali hii ni ya pili kutokea ndani ya mwezi huu, ambapo hivi karibuni boti mbili ya wavuvi na abiria ziligongana ndani ya Ziwa Victoria, katika eneo la Musoma Vijijini Mkoani Mara, ambapo watu kadhaa walinusurika kufa maji kutokana na ajali hiyo mbaya.
Duru nyingine za habari kutoka wilayani Segerema zinaeleza kwamba, watu wanaohofiwa kufa maji wanaweza kufikia 40, na wapo baadhi ya watu waliokolewa, lakini taarifa nyingine zinadai abiria wengine wengi wamezama ndani ya boti hiyo ambayo mmiliki wake alitajwa kwa jina moja la Mhindi.
“Boti imezama Kahunda jioni hii. Mmiliki wake wa boti anaitwa Mhindi…wamekufa watu wengi sana!. Kwa taarifa kamili watafute watendaji wa kijiji cha Maisome na Kahunda”, alisema diwani wa Kata ya Nyampulukano, Hamis Tabasam.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ambazo kwa baadaye zilithibitishwa na Jeshi la Polisi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, zimedai kwamba, idadi ya watu waliozama bado haijajulikana, ingawa kulikuwa na harakati maalumu za kutafuta boti ya uokozi na mafuta kwa ajili ya kwenda kuokoa katika ajali hiyo mbaya.
Mkuu wa Polisi wilayani Sengerema, Prudensiana Protasi (OCD), alimwambia mwandishi wa habari hizi jioni hii ya leo kwamba, jeshi hilo na vyombo vya usalama vinafanya harakati za kwenda kuokoa watu katika ajali hiyo aliyoiita ni mbaya sana.
“Ni kweli taarifa za kuzama kwa boti nimezipata sasa hivi. Naomba niache kwanza maana nashughulikia kutafuta boti na mafuta ili twende kuokoa watu huko. Jamani mwandishi niache, maana siwezi kukaa kuzungumzia taarifa hii wakati huko watu wanaumia.
“Nakuomba nitafute baadaye, ila sasa hivi nahangaikia kutafuta boti, wala sijui ni wangapi walioumia. Ndiyo tunataka kuelekea huko kwenye tukio la ajali”, alisema OCD Protasi kwa njia ya simu yake ya kiganjani.
Alipoulizwa kuhusiana na ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Welle Ndikilo (RC), alisema: “Sina taarifa kuhusu ajali hiyo. Yaani ndiyo napata taarifa hizi kutoka kwako, ngoja nimtafute OCD maana mimi nipo ziarani Geita na nipo hapa mgodi wa dhahabu wa GGM. Na nitatoka hapa baada ya saa mbili”.
Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi alipomtafuta kwa njia ya simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia taarifa za kuzama majini kwa boti na watu, Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Ellinas Palagyo (DC), na yeye majibu yake yalifanana na ya Mkuu wa mkoa, Ndikilo, kwani alisema hana taarifa kabisa juu ya tukio hilo la kuzama watu ndani ya Ziwa Victoria katikaeneo lake la utawala.
“Ndugu yangu sina kabisa taarifa kama hizi. Unasema boti imezama Kahunda Maisome?. Mmmh, mbona sijapewa taarifa?. Hebu ngoja nicheki ya OCD wangu haraka ili nipate usahihi wa mambo”, alisema Mkuu wa wilaya hiyo ya Sengerema, Palagyo.
Habari hii imeandikwa na  – Mwanza

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...