PENZI LILILOKUFA (DEAD LOVE)- 1

Upepo wa bahari ulikuwa ukivuma kwa nguvu na kusababisha mawimbi makubwa ya maji yawe yanapiga kwa nguvu ufukweni, yakizoa mchanga na kuupeleka bahari kisha kurudi tena.
Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, ndivyo upepo ulivyokuwa ukizidi kuongezeka huku wingu jeusi likianza kutanda angani. Watu wote waliokuwa wakiufurahia upepo wa baharini, sasa walianza kuuona kuwa kero kwani ulikuwa ukiambatana na baridi kali huku kijua cha jioni kilichokuwa kikiwaka, kikimezwa na wingu zito jeusi.


Watu waliokuwa wamekaa ufukweni, waliendelea kupungua kwa kasi na muda mfupi baadaye, ufukwe ulikuwa kimya kabisa huku ngurumo za hapa na pale zikianza kusikika kuashiria mvua kubwa iliyokuwa ikitaka kunyesha.