Thursday, September 13, 2018

SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 66


ILIPOISHIA:
Kazi iliyokuwa imesalia, ilikuwa ni kuvunja lile godauni kuangalia ndani kulikuwa na nini? Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua kilichokuwemo mle ndani kwani kwa jinsi nilivyosikia stori za mzee huyo na mazingira ya ile ngome yake aliyokuwa akiishi, achilia mbali ulinzi wa hali ya juu, ilionesha ana mambo mengi sana maovu.
SASA ENDELEA...
Askari waliokuwa na silaha, walilizunguka godauni lote na wengine waliokuwa na vifaa maalum vya kuvunjia mageti, walisogelea geti hilo na kuseti mitambo yao, tayari kwa kazi. Kwa muda wote huo, yule mwandishi wa habari alikuwa bize kuhakikisha hakosi picha hata moja.
Alikuwa akichakarika kisawasawa, akawa anapiga picha za mnato na za video, kwa ajili ya kuwajuza wananchi juu ya kilichokuwa kinaendelea. Wakati askari hao wakijiandaa kuvunja godauni hilo, milio ya ving’ora vya magari mengi ya polisi vilisikika.
Kwa kuwa nilikuwa mwepesi, niliweza kupaa juu na kutazama upande wa kule barabarani, nikashtuka kuona magari mengi ya polisi, yakiwa naaskari wengi wenye silaha, yakija kwa kasi eneo lile. Nadhani awali Junaitha alipowapelekea taarifa juu ya oparesheni hiyo, walidhani ni tukio dogo tu lakini kilichotokea, kiliwafanya walipe tukio hilo uzito wa juu.
Binafsi hata sikuona umuhimu wa wao kufika muda huo kwa sababu tayari jeshi la mtu mmoja nilikuwa nimesafisha njia. Wale askari waliendelea na kazi yao na muda mfupi baadaye, walifanikiwa kuvunja geti hilo.
Katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, milio ya risasi ilianza kusikika upya kutokea ndani ya lile godauni, ikabidi haraka sana niingie mstari wa mbele, nilipigwa na butwaa kwa nilichokikuta mle ndani.
Ilikuwa ni himaya nyingine inayojitegemea kabisa, mlangoni upande wa ndani kulikuwa na walinzi karibu saba, kila mmoja akiwa na bunduki mkononi. Pia kulikuwa na eneo maalum la mapokezi ambapo kulikuwa na wasichana kadhaa waliovalia magauni mekundu yenye mchanganyiko wa rangi nyeupe. Kila kitu kilionekana kuwa rasmi sana kwa sababu hata wale askari walikuwa na sare kabisa.
Baada ya eneo lile la mapokezi, kulikuwa na geti jingine na ofisi ndogondogo zilizokuwa na vifaa vya kisasa kabisa. Taa zote za ndani ya godauni hilo zilikuwa na mwanga mkali kiasi kwamba ukiwa ndani humo, isingekuwa rahisi kutambua kama ni mchana au usiku.
Kwa kasi kubwa niliingia na kuanza kuwaangusha wale walinzi, mmoja baada ya mwingine, nikawa nawavunja shingo kwa kasi kubwa, hali iliyowapa nguvu wale askari ya kusonga mbele, wakafanikiwa kuingia ndani lakini wale waliokuwa wa kwanza kuingia, walionesha kupigwa na mshangao kwa sababu hawakujuani nani aliyekuwa akiwasaidia kuwaangusha maadui zao, tena bila kuwa na majeraha yoyote ya risasi.
Wakafanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi wale wasichana wote na kuwatoa nje. Wakati wakiwatoa nje, wale wengine walikuwa wakihangaika kuvunja lile geti la ndani na hatimaye, walifanikiwa.
Nilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha nakuwa wa kwanza kuona kila kilichokuwa kikitokea. Nilishtushwa sana na nilichokiona, kwani kulikuwa na ngazi zilizokuwa zikielekea upande wa chini ya ardhi, ambako kulikuwa na jengo kubwa mithili ya hospitali, likiwa na vitanda zaidi ya mia moja, kila kimoja kikiwa na mgonjwa juu yake.
Kulikuwa pia na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamevalia kama madaktari, waliokuwa wakiendelea na kazi lakini ghafla, kila mmoja aliacha baada ya kuona wakivamiwa na polisi.
Kumbe lile eneo lote ambali kwa juu lilikuwana nyumba na bustani nzuri, chini lilikuwa na handaki hilo kubwa, ambalo hata sikujua niliite hospitali au maabara. Upande wa kaskazini, kulikuwa na maandishi makubwa meusi yaliyokuwa yakisomeka ‘Black Heart’.
Ni hapo ndipo nilipopata picha halisi ya kile kilichokuwa kikiitwa Black Heart. Yale maelezo niliyoyapata kwamba shirika hilo ambalo kwa nje lilikuwa likijitangaza kwamba linasaidia maskini na watu wasiojiweza, kwenda kuwalipia gharama za masomo na matibabu nje ya nchi, kilikuwa kitu kingine tofauti kabisa.
Japokuwa nilishaambiwa kwamba lilikuwa likihusika na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na viungo vya binadamu, nilikuwa siamini mpaka siku hiyo ambapo kwa macho yangu, nilishuhudia kila kitu. Katika kila kitanda, kulikuwa na mtu aliyelala ambapo wote walionesha kutokuwa na fahamu.
Walikuwepo wengine ambao tayari walikuwa wameshafanyiwa upasuaji wa kutolewa viungo mbalimbali vya miili yao, ambavyo vilihifadhiwa kitaalamu kwenye majokofu makubwa yaliyokuwa mwisho kabisa mwa jengo hilo refu.
Niliwaona askari waliokuwa wameshasambaa kila kona, wakipatwa na kigugumizi cha nini cha kufanya. Amri iliyotoka, ilikuwa ni kuwakamata madaktari wote na kuwatoa nje, huku mipango ya namna ya kuwanusuru wale watu ambao wote walikuwa kwenye usingizi wa kifo, wengine wakiwa wamefungwa mashine za kuwasaidia kupumua, ilianza kufanyika.
Lilikuwa ni tukio la kusisimua mno, nilimuona hata yule mwandishi wa habari tuliyeongozana naye, Richard Bukos akitetemeka kwa hofu. Jengo lote lilikuwa likinukia umauti.
“Inatakiwa usimamie hatua kwa hatua, usikubali mtu yeyote akatibua hii oparesheni, kuwa makini na hao wanaoingia sasa hivi,” alisema Junaitha, sauti ambayo ilisikika vizuri kwenye masikio yangu.
“Vipi huko hospitalini? Sitaki kufa tena wala sikati Firyaal apatwe na tatizo lolote,” nilimwambiaJunaitha ambaye alinitoa wasiwasi, akaniambia nifanye kazi yangu na yeye nimuachie afanye kazi yangu. Kumbuka kwamba kwa kipindi chote hiki, mimi kwa maana ya mwili wangu unaoonekana, na Firyaal, tulikuwa tumepelekwa Hospitali ya Muhimbili baada ya kupigwa risasi kwenye yale mashambulizi.
Nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kufika mwenyewe na kuona jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea lakini sikuweza kwa sababu nilikuwa na jambo muhimu sana la kulisimamia kwa wakati huo. Kweli wale madaktari wote walitolewa chini ya ulinzi mkali na kwenda kuunganishwa na wale wenzao waliokamatwa awali.
Mle ndani kukabaki wale wagonjwa tu waliokuwa wamelala, wakiwa hawaelewi chochote kilichokuwa kinaendelea. Ilibidi na mimi nitoke nje kuangalia kilichokuwa kinaendelea, askariwalikuwa wameongezeka zaidi ya mara nne ya wale waliokuwepo awali, tena kila mmoja akiwa na silaha.
Miongoni mwao, nilimuona askari mwingine ambaye alikuwa na nyota nyingi kuliko yule wa kwanza tuliyekuja naye, nikahisi lazima atakuwa na cheo kikubwa zaidi ya yule wa mwanzo, nikawa makini kumfuatilia kila alichokuwa anakifanya.
Nilimsikia akitoa amri ya yule kamanda tuliyefika naye awali aende naye wakazungumze pembeni. Kwa kuwa sikuwa naonekana, na mimi nilisogea pembeni, nikamuona akimpigia saluti na kunifanya niamini kweli kwamba alikuwa na cheo cha juu zaidi yake.
“Nani aliyetoa amri ya kuja kuvamia hapa wakati uongozi wa juu haujui?” nilimsikia akimuuliza, nikapigwa na butwa mno kwani sikutegemea kama anaweza kumuuliza swali kama lile.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

2 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...