Monday, September 3, 2018

KIVURUGE WA TANDALE- 9


ILIPOISHIA:
Madam Bella hakusema lolote zaidi ya kusimama, akawa anatutazama huku akionesha kushtuka sana kutokana na hali aliyotukuta maana Salma alikuwa amepeleka mkono wake shingoni kwangu kwa lengo la kunikagua ile aliyosema mwenyewe lipstiki, kwa hiyo mazingira yalionesha ni kama tulikuwa tumekumbatiana.
SASA ENDELEA...
“Yaani badala ya kufanya kazi iliyowaleta mna kazi ya kukumbatiana kwenye korido! Hivi mna akili kweli nyie?”
“Hapana Madam, nilikuwa namsaidia kumfuta madoa ya lipstiki kwenye shati lake, hebu angalia mwenyewe,” alisema Salma kwa namna ya kujihami sana.
“Lipstiki? Sasa lipstiki kwenye shati lake wewe inakuhusu nini?”
“Nisamehe Madam!”
“Ile cheki niliyokupa umeshaipeleka uhasibu?”
“Hapana bosi, ndiyo nilikuwa na...”
“Salma! Kuwa makini, kama kilichokuleta ni kazi, fanya kazi. Na wewe Ashrafu, unatakiwa kuheshimu kazi ninayokupa, yaani mimi nakutuma kitu halafu badala ya kwenda kufanya nilichokwambia unaanza kufanya mambo yako mengine.”
“Nisamehe bosi,” nilisema huku nikijitahidi kuvaa uso ambao hautamfanya Salma ashtukie chochote. Kweli hilo lilifanikiwa, Madam Bella alitoa amri ya kila mmoja kuendelea na kazi zake, harakaharaka Salma akapita mbiombio na kuelekea uhasibu na mimi nikaondoka haraka kuelekea ofisini kwangu.

Sikukaa sana, niliweka kila kitu changu vizuri, nikatoka mpaka pale mapokezi, nikamdanganya Salma kwamba kuna kazi bosi amenituma nje ya ofisi kwa hiyo natoka, akanijibu kwa kutingisha tu kichwa akionesha kutokuwa na furaha.
Nadhani kitendo cha kufokewa na bosi mbele yangu kilimkasirisha sana, akawa hataki hata kunitazama. Aliitikia kwa kutingisha kichwa, nikateremka kwenye ngazi harakaharaka kwa lengo la kumfanya mtu yeyote asijue kwamba natoka na bosi.
Nilipofika chini nilimuuliza kama nimsubiri pale chini au la, akanijibu kwa meseji kwamba nipande Bajaj tutakutana Mnazi Mmoja.
Kwa kuwa mfukoni nilikuwa na vihela kidogo, sikutaka kupoteza muda, nilikalia Bajaj na muda mfupi baadaye tayari nilikuwa Mnazi Mmoja, nikakaa kituoni kumsubiri bosi huku muda wote nikigeuka huku na kule kuangalia kama hakuna mtu yeyote aliyekuwa ananijua.
“Pipii! Pipiii,” honi iliyopigwa taratibu pembeni yangu ndiyo iliyonishtua kutoka kwenye mawazo ya hofu niliyokuwa nayo. Sijui kwa nini sikuwa nataka watu wajue kwamba natoka na Madam Bella, nilipogeuka nilikutana uso kwa uso na bosi akiwa kwenye gari lake la kifahari, Toyota Lexus, akashusha kioo na kunipa ishara kwamba na mimi niingie.
Niliingia na kukaa siti ya nyuma lakini akaniambia natakiwa kukaa naye mbele. Sikuwana namna, nilishuka na kufungua mlango wa mbele, nikaingia na kuufunga harakaharaka. Kwa bahati nzuri gari lake lilikuwa na vioo vya giza (tinted), nikawa na uhakika kwamba hakuna tena mtu ambaye angetuona.
Aliondoa gari taratibu, akawa anageuka na kunitazama akionesha kuwa na dukuduku ndani ya moyo wake, na mimi nikajikausha maana nilishajua kwamba kitendo cha kunikuta na Salma pale koridoni hakukifurahia kabisa.
“Unatoka na Salma si ndiyo?”
“Aah! Hapana bosi, umewahi kuniona au kuhisi chochote zaidi ya leo?”
“Kwa nini mlikuwa mmekumbatiana?”
“Hatukuwa tumekumbatiana, alikuwa ananishangaa kwa nini nina lipstiki kwenye nguo ndiyo na wewe ukatokea, si unaona alama za lipstiki yako hizi,” nilisema huku nikijitahidi kumgeuzia kibao, ionekane yeye ndiye aliyekosea kunibusu wakati anajua amepaka lipstiki inayoacha alama.
“Hebu tuone,” alisema huku akinigeukia, safari hii ule ‘usiriasi’ ukiwa umepungua, kweli kulikuwa na alama ya lipstiki kwenye shati langu, basi akacheka sana na kuendelea kuendesha gari, muziki laini ukawa unapiga ndani ya gari sambamba na kipupwe cha nguvu, nikawa najihisi kama nipo kwenye dunia nyingine.
“Kwani nyumbani kwako unaishi na nani?”
“Naishi peke yangu bosi.”
“Unajua nataka kupumzika maana jana nilichoka sana lakini sitaki kwenda hotelini, unajua watu tunaoheshimika kama sisi, ukionekana tu hotelini, hasa na mtu wa jinsia nyingine tofauti ni rahisi watu kukuhisi vibaya,” alisema bosi lakini moyoni nikawa sijauafiki kabisa uamuzi wake.
Hadhi ya bosi ilikuwa si ya kwenda naye Tandale hata kidogo, kama nilivyosema kuanzia mwanzo, japokuwa alikuwa mwanamke wa makamo, alikuwa na uzuri fulani hivi wa aina yake ambao huwezi kuuona kwa urahisi kwa wanawake wanaotokea familia za kawaida.
Nilijaribu kutoa visingizio vingi lakini bado alishikilia msimamo wake, akawa ananiambia kwamba nisimchukulie ‘kiivyo’ kwa sababu kabla ya kupata mafanikio aliyokuwa nayo, amewahi kuishi kwa msoto wa nguvu.
“Cha msingi tupate sehemu salama ya kupaki gari, mengine hayo wala usijali! Au hujafua mashuka nini?” alinitania, tukacheka kwa nguvu. Aliniambia kwamba anataka kabla hatujafika kwangu, tupitie kwanza sokoni kununua mahitaji yote muhimu kwa sababu anataka eti akanipikie chakula ambacho sijawahi kula sehemu yoyote.
Sikuwa na namna, nilikubali kila alichokuwa akikisema, tukapitia Manzese ambapo tulinunua mazagazaga kibao, tukaenda moja kwa moja mpaka Mtogole, nikamuelekeza sehemu nzuri ya kupaki gari ambapo hakuna kibaka anayeweza kuiba ‘saiti mira’ wala ‘pawa windo’.
Mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza kuteremka kwenye gari, nikashuka na vifurushi vya mazagazaga kibao, basi bosi naye alipoteremka, watu karibu wote eneo hilo waliacha kila walichokuwa wakikifanya na kumtolea macho.
Kwa jinsi mwonekano wake ulivyokuwa, alikuwa kiumbe adimu kwenye mazingira kama hayo, basi tukakatiza vichochoro huku kila mtu akiendelea kutushangaa kwa sababu bado ilikuwa ni asubuhi na hatimaye tukawasili nyumbani.
Kwa bahati mbaya, wakati tunafika, mke wa mwenye nyumba ambaye tumezoea kumuita mama Ababuu, alikuwa akifua nguo zake uani, tena kiti chake akiwa amekiweka karibu kabisa na mlango wangu.
Siku zote nilikuwa namheshimu sana mama Ababuu na sikuwahi kumuonesha tabia zozote mbaya, nikaona kitendo cha mimi kuingia na Madam Bella ‘magetoni’, kingemfanya anione kama mtu wa ajabu sana kwa sababu kulikuwa na tofauti kubwa ya kimwonekano na kimwili kati yangu na Madam Bella.
Nilijikaza kiume, nikamsalimu na kufungua mlango huku Madam Bella akishangaa mazingira ya pale, nikamkaribisha ndani ambapo kama ilivyokuwa kwa Nancy, alipoingia tu, alinisifu kwamba chumba changu ni kizuri sana, basi nikamshukuru na kumkaribisha sana.
“Unanikaribishaje hivyo?” alisema huku akitanua mikono yake kama anayesema ‘njoo unikumbatie’. Basi na mimi nilifanya kama alivyotaka, nikaenda na kumkumbatia kwa nguvu, muda mfupi baadaye midomo yetu ilikuwa imegusana, hata sijui nini kilitokea, nilishtukia tu tayari tukiwa kwenye uwanja wa fundi seremala, mara mlango ukagongwa kwa nguvu.
“Ngo! Ngo! Ngooo!”

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...