Monday, September 3, 2018

KIVURUGE WA TANDALE- 8


ILIPOISHIA:
“Kumbe unajua kuimba vizuri hivyo, itabidi nikupeleke studio,” nilimchombeza, akacheka sana, tayari tulishafika maana konda alipaza sauti akisema hapo ndiyo mwisho wa gari, abiria wengine wakawa wanateremka lakini mimi nikajikuta nikipata uzito na kubaki nimekaa, naye hakuonesha kuwa na haraka sana, akawa amekaa akiwa ni kama anayenisubiri niinuke ili na yeye ainuke.
Ndani ya muda mfupi tu tayari tulishakuwa tumezoeana f’lani hivi, akili fulani ndani ya kichwa changu ikawa inaniambia ‘jaribu kutupia mistari’.
SASA ENDELEA...
“Twende basi tushuke jamani,” alisema huku akinigusa begani, nikamgeukia nakumtazama, safari hii tukiwa tumesogeleana sana maana alishaanza kuinuka.
“Mbona unaniangalia hivyo mpaka mwenzako najisikia aibu,” alisema huku akijichekesha, nikaona huo ndiyo muda mzuri wa kutekeleza kile ambacho akili yangu ilikuwa ikinituma sana.
“Wewe ni mzuri sana, hivi mumeo huwa anakusifia kila siku kabla hujatoka nyumbani?” nilimwambia, akacheka kwa nguvu na kwa kuwa abiria wote walikuwa bize kuteremka kwenye gari, hakuna aliyemjali sana, nikasimama, na yeye akasimama kwani tayari abiria walikuwa wamepungua sana ndani ya gari.
“Umejuaje kama nina mume?” aliniambia huku akinitazama kwa macho ya bashasha.
“Mwanamke mrembo kama wewe utakosaje mume?” nilizidi kumchombeza, akazidi kufurahi. Miongoni mwa udhaifu mkubwa wa wanawake, huwa wanapenda sana kusifiwa na wajanja kama sisi tunaojua namna ya kuzifikisha hizo sifa zenyewe kwa staili ya kuchombeza, huwa inakuwa rahisi sana kuwanasa.

Hata mwanamke aweje, ukishaanza kumsifia tu, lazima atafurahi, hicho ndicho kilichotokea kwa mwanamke huyu ambaye kama nilivyoeleza, sikuwahi kumuona sehemu yoyote na asubuhi hiyo ndiyo kwanza tulikuwa tumekutana.
Niliposimama, nilitumia ujanja wa kiume wa kumpisha yeye ndiyo atangulie mbele, lengo langu lilikuwa ni kutaka kumtazama vizuri, hasa kwenye ‘plate numbe’ ambao kiukweli umekuwa ugonjwa sugu unaonisumbua.
Nilijikuta nikijishika mdomo kwa mshangao, kwa kuwa muda wote alikuwa amekaa wala sikuweza kumuona yupoje akisimama lakini kumbe alikuwa na umbo ambalo hakuna mwanaume yeyote aliyekamilika anayeweza kupishana naye halafu asigeuke!
Alikuwa amejaaliwa haswaa, nikazidi kuchanganyikiwa na ile nadhiri niliyokuwa nimejiwekea, ya kukaa mbali na mali za watu ikayeyuka kama bonge la mafuta kwenye kikaango.
“Dah! Shemeji atakuwa anafaidi kinoma, kumbe ndiyo umeumbika kiasi hicho,” nilimchombeza wakati akimalizia kushuka ngazi ya mwisho ya gari, alipokanyaga chini, ule mtikisiko ukasababisha ‘msambwanda’ nao utingishike kwa namna iliyoyapa raha ya kipekee macho yangu.
Alicheka na kunigeukia, akanipiga kakibao kepesi begani, tukawa tunatazama huku aibu za kikekike zikiwa zimemjaa usoni.
“Wewe umeniuliza mimi jina, mbona wewe hujaniambia unaitwa nani?”
“Hujaniuliza! Kwani unataka kunijua?” aliniuliza huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Nilichokigundua ni kwamba alikuwa anapenda sana kucheka na kufurahi na katika kipengele hicho, Mungu alikuwa amenipa kipaji cha aina yake maana usingeweza kukaa na mimi halafu usitabasamu au kucheka.
Basi aliniambia kwamba anaitwa Ruqaiya au mama Abdul, akaniambia kwamba anasimamia maduka mawili ya simu ya mumewe yaliyopo mtaa wa Aggrey Kariakoo na kwamba muda huo ndiyo alikuwa akienda kazini.
Sikupoteza muda, nilimwambia mimi ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta lakini pia nilikuwa na ujuzi wa ‘kuzi-program’ simu, hasa hizi za kisasa zinapotoka kiwandani, akafurahi sana na kuniambia kwamba eti kukutana kwetu ulikuwa ni mpango wa Mungu.
“Naomba namba yako basi bosi!” nilimwambia, akawa mjanja katika hilo, akaniambia kwamba mimi nimtajie ya kwangu halafu yeye atanipigia.
Mbinu hii huwa inatumiwa sana na wanawake wajanja ambapo badala ya kukukatalia kukupa namba, anakwambia wewe ndiyo umpe halafu anazuga kama anaiandika kwenye simu, ukimpa mgongo tu anaifuta na huwezi kumpata tena, hasa katika mazingira kama yale niliyokutana nayo.
Nilimtajia namba yangu, akaiandika kwenye simu yake kisha akaniaga juu kwa juu huku akionesha kuwa na furaha sana, nilishindwa nifanye nini, nikawa namsindikiza kwa macho akitembea kwa maringo.
Alipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yangu, harakaharaka na mimi niliendelea na hamsini zangu, nikakata mitaa na muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimewasili kazini, nikapanda ngazi mpaka juu, wa kwanza kukutana naye alikuwa ni Salma.
Ofisi yetu jinsi ilivyo, unapoingia lazima upitie kwamba mapokezi kusaini kitabu cha mahudhurio kwa hiyo hakukuwa na namna ambayo ningeweza kumkwepa Salma. Aliponiona tu, alinitazama huku tabasamu pana likichanua kwenye uso wake, jambo ambalo siyo kawaida yake.
Kama nilivyoeleza awali, Salma alikuwa na sifa moja kubwa ya kununa muda mwingi na kutoa majibu ya hovyo kwa mtu yeyote hata pale unapomuuliza mambo muhimu ya kikazi.
“Mambo!” nilimsabahi huku na mimi nikijitahidi kuvaa tabasamu la uongo usoni. Hakunijibu zaidi ya kuendelea kujichekeshachekesha mwenyewe pale kwenye kiti cha kuzunguka alichokuwa amekalia.
Nilipomaliza kusaini, wakati nataka kwenda ofisini kwangu kuendelea na majukumu yangu, aliniita kwa jina langu halisi, nikamgeukia maana tayri nilishampa kisogo.
“Kwa hiyo unadhani ukipokea simu zangu nitanenepa sana au?” alisema huku akitoa bahasha kubwa aliyokuwa ameiweka chini ya meza yake. Nikiwa bado sijui nimjibu nini, alinikabidhi na kuniambia kwamba eti hiyo ni zawadi yangu, nikatabasamu na kumshukuru huku nikiwa na shauku ya kutaka kujua ndani yake kuna nini.
“Na ole wako usiwe unapokea tena simu zangu,” alisema huku akionesha dhahiri jinsi alivyokuwa na furaha ndani ya moyo wake.
Niliingia ofisini na kitu cha kwanza ilikuwa ni kufungua bahasha hiyo, nikajikuta natabasamu mwenyewe kwa furaha, alikuwa ameninunulia zawadi ya ‘boksa’ za kiume nzuri, ambazo eti alikuwa amezipulizia pafyumu yake anayojipulizia kila siku.
Nilichukua simu yangu na kumtumia meseji ya kumshukuru, hakujibu kwa wakati, ikabidi nianze kazi kwa sababu nilikuwa na majukumu mengi siku hiyo. Kuna kompyuta kadhaa za ofisi zilikuwa na matatizo na ilikuwa ni lazima nizitengeneze asubuhi hiyo ili kazi ziendelee.
Mara simu yangu ya mkononi ilianza kuita, kutazama namba ya mpigaji, nilishtuka kidogo baada ya kugundua kwamba ni bosi ndiyo alikuwa akinipigia, harakaharaka nikapokea.
“Shikamoo bosi,” nilimsalimia kwa adabu.
“Si nishakwambia hizo shikamoo zako sizitaki, una udogo gani wa kunipa shikamoo, unataka kunizeesha bure! Njoo ofisini kwangu haraka,” alisema Madam Bella kisha akakata simu. Harakaharaka nikaacha kila nilichokuwa nakifanya na kutoka kuelekea ofisini kwake.
Nilipoingia ofisini kwake, Madam Bella aliinuka kutoka pale alipokuwa amekaa na kuja mwilini, akanikumbatia kwa hisia huku akinibusubusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.
“Ndiyo nini ulichonifanya jana? Yaani nimekuja kuzinduka saa moja jioni, najikuta nimebaki peke yangu ofisini,” alisema huku akiachia tabasamu pana, akanibusu tena mdomoni, safari hii kwa hisia kali zaidi.
“Leo sitaki ufanye kazi yoyote, kajiandae kuna mahali nataka twende tukapumzike,” alisema huku akinitazama kwa macho yaliyokuwa yamebeba hisia nzito za kimapenzi, nikajua kazi ninayo maana ukweli ni kwamba sikuwa nimepumzika hata kidogo tangu jana yake.
Nilimkubalia, nikatoka kwa lengo la kurudi ofisini kwangu kuweka vitu sawa kwa sababu tayari ilishaonekana hakuna kazi itakayofanyika tena, ile natoka kumbe Salma alikuwa amenifuata ofisini kwangu na kunikosa, tukakutana kwenye korido.
“Zawadi yangu hujaipenda?”
‘Kwa nini unasema hivyo Salma jamani, nimeipenda na nimekutumia meseji kukushukuru.”
“Muongo, halafu hata kama hujaipenda, ndiyo uiache juu ya meza jamani, yaani unataka nani aione? Sawa nashukuru sana Ashrafu, ahsante sana,”alisema huku akianza kulengwalengwa na machozi, ghafla macho yake yakatua kwenye shingo yangu.
“Mh! Hii lipstiki imetoka wapi? Halafu mbona kama unanukia pafyumu ya...” kabla hata hajamalizia alichotaka kukisema, wote tulishtuka baada ya kusikia mlango wa bosi ukifunguliwa, macho yake yakatua moja kwa moja kwangu mimi na Salma aliyekuwa akiendelea kunikagua pale kwenye korido.
Madam Bella hakusema lolote zaidi ya kusimama, akawa anatutazama huku akionesha kushtuka sana kutokana na hali aliyotukuta maana Salma alikuwa amepeleka mkono wake shingoni kwangu kwa lengo la kunikagua ile aliyosema mwenyewe lipstiki, kwa hiyo mazingira yalionesha ni kama tulikuwa tumekumbatiana.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Risasi Jumamosi.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...