SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 66


ILIPOISHIA:
Kazi iliyokuwa imesalia, ilikuwa ni kuvunja lile godauni kuangalia ndani kulikuwa na nini? Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua kilichokuwemo mle ndani kwani kwa jinsi nilivyosikia stori za mzee huyo na mazingira ya ile ngome yake aliyokuwa akiishi, achilia mbali ulinzi wa hali ya juu, ilionesha ana mambo mengi sana maovu.
SASA ENDELEA...
Askari waliokuwa na silaha, walilizunguka godauni lote na wengine waliokuwa na vifaa maalum vya kuvunjia mageti, walisogelea geti hilo na kuseti mitambo yao, tayari kwa kazi. Kwa muda wote huo, yule mwandishi wa habari alikuwa bize kuhakikisha hakosi picha hata moja.
Alikuwa akichakarika kisawasawa, akawa anapiga picha za mnato na za video, kwa ajili ya kuwajuza wananchi juu ya kilichokuwa kinaendelea. Wakati askari hao wakijiandaa kuvunja godauni hilo, milio ya ving’ora vya magari mengi ya polisi vilisikika.
Kwa kuwa nilikuwa mwepesi, niliweza kupaa juu na kutazama upande wa kule barabarani, nikashtuka kuona magari mengi ya polisi, yakiwa naaskari wengi wenye silaha, yakija kwa kasi eneo lile. Nadhani awali Junaitha alipowapelekea taarifa juu ya oparesheni hiyo, walidhani ni tukio dogo tu lakini kilichotokea, kiliwafanya walipe tukio hilo uzito wa juu.
Binafsi hata sikuona umuhimu wa wao kufika muda huo kwa sababu tayari jeshi la mtu mmoja nilikuwa nimesafisha njia. Wale askari waliendelea na kazi yao na muda mfupi baadaye, walifanikiwa kuvunja geti hilo.

KIVURUGE WA TANDALE- 10


ILIPOISHIA
“Unanikaribishaje hivyo?” alisema huku akitanua mikono yake kama anayesema ‘njoo unikumbatie’. Basi na mimi nilifanya kama alivyotaka, nikaenda na kumkumbatia kwa nguvu, muda mfupi baadaye midomo yetu ilikuwa imegusana, hata sijui nini kilitokea, nilishtukia tu tayari tukiwa kwenye uwanja wa fundi seremala, mara mlango ukagongwa kwa nguvu.
“Ngo! Ngo! Ngooo!”
SASA ENDELEA...
“Nani tena huyo jamanii,” alisema Madam Bella huku akionesha kukasirishwa sana na kitendo cha mtu huyo kugonga. Niliamka, nikajifunga taulo na kusogea mlangoni, nikafungua kidogo na kuchungulia nje.
“Hivi unajua kwamba ni zamu yako kununua umeme?”
“Ooh! Kumbe zamu yangu imeshafika? Ok, naomba basi nikupe pesa umuagize hata mtoto akanunue.”
“Mtoto gani? Hakuna mtu hapa nyumbani, kama unavyojua wakienda shuleni nabaki peke yangu, hebui nenda kanunue kwa sababu utakatika sasa hivi, tafadhali tusije tukagombana bure,” mama mwenye nyumba alisema huku akiwa ameshika kiuno.
Haikuwa kawaida yake kuzungumza na mimi kwa namna hii, siku zote tulikuwa tukihheshimiana na kama kuna jambo lolote, alikuwa akiniambia kwa ustaarabu lakini siku hiyo alikuwa amebadilika.
Nilibamiza mlango na kurudi ndani, huku nikiwa nimepanda na jazba. Kwa alichokisema, maana yake alikuwa anataka niache kila nilichokuwa nakifanya eti nikanunue umeme, ambao kwanza hata haukuwa umekatika.
Kama hiyo haitoshi, asubuhi hiyo wakati naondoka aliniona sana lakini hakuniambia chochote kwa hiyo kama nisingerudi ingekuwaje? Niliona kama ameamua kunifanyia visa kwa makusudi ili kuniharibia mambo yangu.
“Vipi tena baba’angu,” alisema Madam Bella huku akinishika mkono kwa upole na kunirudisha uwanjani, nikamweleza kilichotokea.
“Usijali, kwani shilingi ngapi?”

SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 65


ILIPOISHIA:
“Dont worry Jamal, each and everything is going to be okay!” (Usiwe na wasiwasi Jamal, kila kitu kitakuwa sawa) alisema Firyaal na kunisogelea, akanikumbatia na kunibusu mdomoni huku kila mtu akishuhudia. Sikujali, nilikuwa nampenda sana Firyaal na sikuwa tayari kuona jambo lolote baya linamtokea, hasa kabla ya mimi na yeye kukutana na kumaliza kile tulichokuwa tayari tumekianza.
SASA ENDELEA...

“Inabidi ubaki usaidiane na hawa askari, bado kuna kazi kubwa mbele yetu. Nakukumbusha tu kwamba huonekani na mtu yeyote kwa hiyo utakuwa na nafasi ya kuyafanya hata yale ambayo watu wa kawaida hawayawezi, ni lazima Loris akamatwe, umepigwa risasi na Firyaal naye amepigwa risasi, haiwezekani iwe ni kwa ajili ya kazi bure,” alisema Junaitha, sauti ambayo ilipenya vilivyo masikioni mwangu, akawa ni kama amezidi kuniongezea hasira.

Wale askari walipoingia, wengine ilibidi wabaki nje, wakatawanyika kule ndani kwa tahadhari kubwa na muda mfupi baaddaye, mvua nyingine ya risasi ikaanza kumwagika.
Nilishindwa kuelewa ni kwa sababu gani nyumba hiyo ilikuwa ikilindwa kiasi hicho, nikasikia sauti ya Junaitha masikioni mwangu akinielekeza kusonga mbele haraka mpaka pale walipokuwepo walinzi wengine waliokuwa wakifyatua risasi kwa kasi.

SEVEN DAYS IN HELL (SIKU SABA KUZIMU)- 64


ILIPOISHIA:
“Tulia jamal, mbona una haraka, nimesema leo ndiyo leo na watu wote watatujua sisi ni akina nani. Shenaiza na Firyaal, naomba mkaze mioyo yenu maana kinachoenda kutokea kwa baba yenu siyo kizuri lakini lazima tufanye hivi,” alisema Junaitha, akawasha gari, tukaondoka huku ile difenda ikitufuata kwa nyuma.
SASA ENDELEA...
Msafara uliendelea na safari mpaka tulipofika Kurasini, tukakata kushoto na kuiacha barabara ya lami, nikaikumbuka vizuri njia hiyo kwani ndiyo tuliyopita siku ile tulipoenda nyumbani kwa akina Shenaiza.
Tulipoingia kwenye barabara hiyo, ile difenda iliyokuwa nyuma, ilituwashia taa, nikamuona Junaitha akipunguza mwendo na kupaki pembeni, ile difenda nayo ikapunguza mwendo na kusimama. Yule askari aliyekuwa na nyotanyota begani akamsogelea Junaitha.
“Kumbe mlikuwa mnamaanisha huyu mzee Loris?”
“Ndiyo, kwani maelezo yote si yanajitosheleza afande?”
“Ni hatari sana kwa kweli, hata sidhani kama itawezekana.”
“Kwani mheshimiwa, wananchi wanapoletamalalamiko kwenu, tena mazito kama haya, wakiwa na ushahidi wa kila kitu, ni nani anayeweza kuwasaidia kama siyo jeshi la polisi?”
“Wewe ni nani unayeuliza maswali ya namna hiyo? Isitoshe sizungumzi na wewe, naongea na huyu mama aliyeleta taarifa.”

KIVURUGE WA TANDALE- 9


ILIPOISHIA:
Madam Bella hakusema lolote zaidi ya kusimama, akawa anatutazama huku akionesha kushtuka sana kutokana na hali aliyotukuta maana Salma alikuwa amepeleka mkono wake shingoni kwangu kwa lengo la kunikagua ile aliyosema mwenyewe lipstiki, kwa hiyo mazingira yalionesha ni kama tulikuwa tumekumbatiana.
SASA ENDELEA...
“Yaani badala ya kufanya kazi iliyowaleta mna kazi ya kukumbatiana kwenye korido! Hivi mna akili kweli nyie?”
“Hapana Madam, nilikuwa namsaidia kumfuta madoa ya lipstiki kwenye shati lake, hebu angalia mwenyewe,” alisema Salma kwa namna ya kujihami sana.
“Lipstiki? Sasa lipstiki kwenye shati lake wewe inakuhusu nini?”
“Nisamehe Madam!”
“Ile cheki niliyokupa umeshaipeleka uhasibu?”
“Hapana bosi, ndiyo nilikuwa na...”
“Salma! Kuwa makini, kama kilichokuleta ni kazi, fanya kazi. Na wewe Ashrafu, unatakiwa kuheshimu kazi ninayokupa, yaani mimi nakutuma kitu halafu badala ya kwenda kufanya nilichokwambia unaanza kufanya mambo yako mengine.”
“Nisamehe bosi,” nilisema huku nikijitahidi kuvaa uso ambao hautamfanya Salma ashtukie chochote. Kweli hilo lilifanikiwa, Madam Bella alitoa amri ya kila mmoja kuendelea na kazi zake, harakaharaka Salma akapita mbiombio na kuelekea uhasibu na mimi nikaondoka haraka kuelekea ofisini kwangu.

KIVURUGE WA TANDALE- 8


ILIPOISHIA:
“Kumbe unajua kuimba vizuri hivyo, itabidi nikupeleke studio,” nilimchombeza, akacheka sana, tayari tulishafika maana konda alipaza sauti akisema hapo ndiyo mwisho wa gari, abiria wengine wakawa wanateremka lakini mimi nikajikuta nikipata uzito na kubaki nimekaa, naye hakuonesha kuwa na haraka sana, akawa amekaa akiwa ni kama anayenisubiri niinuke ili na yeye ainuke.
Ndani ya muda mfupi tu tayari tulishakuwa tumezoeana f’lani hivi, akili fulani ndani ya kichwa changu ikawa inaniambia ‘jaribu kutupia mistari’.
SASA ENDELEA...
“Twende basi tushuke jamani,” alisema huku akinigusa begani, nikamgeukia nakumtazama, safari hii tukiwa tumesogeleana sana maana alishaanza kuinuka.
“Mbona unaniangalia hivyo mpaka mwenzako najisikia aibu,” alisema huku akijichekesha, nikaona huo ndiyo muda mzuri wa kutekeleza kile ambacho akili yangu ilikuwa ikinituma sana.
“Wewe ni mzuri sana, hivi mumeo huwa anakusifia kila siku kabla hujatoka nyumbani?” nilimwambia, akacheka kwa nguvu na kwa kuwa abiria wote walikuwa bize kuteremka kwenye gari, hakuna aliyemjali sana, nikasimama, na yeye akasimama kwani tayari abiria walikuwa wamepungua sana ndani ya gari.
“Umejuaje kama nina mume?” aliniambia huku akinitazama kwa macho ya bashasha.
“Mwanamke mrembo kama wewe utakosaje mume?” nilizidi kumchombeza, akazidi kufurahi. Miongoni mwa udhaifu mkubwa wa wanawake, huwa wanapenda sana kusifiwa na wajanja kama sisi tunaojua namna ya kuzifikisha hizo sifa zenyewe kwa staili ya kuchombeza, huwa inakuwa rahisi sana kuwanasa.

KIVURUGE WA TANDALE- 7ILIPOISHIA:
“Mungu wangu, nitasema nini nyumbani,” alisema huku akikurupuka na kuanza kutafuta nguo zake, nikaona analeta masihara, ataondokaje muda huo wakati hata kipindi cha pili kilikuwa bado?
SASA ENDELEA... 

Harakaharaka aliwasha simu yale ya bei mbaya ambayo kwa muda wote huo alikuwa ameizima. Nikamuona anavyohangaika, nadhani alikuwa akitafutwa sana kwenye simu.
“Sijui nitamwambia nini baba, sijawahi kukaa nje mpaka usiku mnene kiasi hiki.”
“Kwani wewe bado unaishi na wazazi wako?” 

“Ndiyo! Naishi na wazazi, sasa wewe ulikuwa unafikiri naishi na nani?”
“Sasa si unaweza tu kumwambia upo kwenye bethidei ya rafiki yako?”
“Hilo siyo tatizo, ilitakiwa nitoe taarifa mapema, sasa unafikiri saa saba hii naanzaje kuwaeleza kitu kama hicho? Umeniponza Ashrafu, umenisababishia matatizo,” alisema huku akianza kulia. Ilibidi niamke pale kitandani na kumfuata pale alipokuwa amesimama, nikawa najaribu kumtuliza.


“Wewe umeshakuwa mkubwa sasa, hutakiwi kuwahofia wazazi wako kwa kiasi hicho, kwani wao hawajui kwamba wewe umeshakuwa mkubwa?”
“Stop it!” alisema kwa ukali akimaanisha hataki niendelee kuzungumzia suala hilo. Kwa jinsi alivyonibadilikia, sikuwa na namna zaidi ya kumruhusu tu aondoke lakini nilifanya hivyo kwa shingo upande. 

Licha ya kazi kubwa iliyofanyika, huwezi kuamini kwamba bado mtandao ulikuwa ukisoma 4G, nikawa najitahidi kujizuia mwenyewe kwa mbinu zangu. Alivaa harakaharaka na muda mfupi baadaye, alikuwa ameshamaliza kila kitu, akanigeukia na kushtushwa na hali niliyokuwa nayo. 

“Una matatizo gani?”
“Sina tatizo lolote.”
“Mbona hivyo sasa?”
“Aah! Kawaida tu, kwani kuna tatizo?” nilisema huku na mimi nikijisikia aibu. 

KIVURUGE WA TANDALE- 6ILIPOISHIA:
“Tumeshafika bro!” alisema yule dereva wa Ubber, kauli yake ndiyo iliyotuzindua kutoka kwenye dimbwi la huba, kucheki pembeni, kweli tayari tulikuwa Tandale kwa Mtogole.
SASA ENDELEA...
Tuliteremka kwenye Uber, kwa jinsi Nancy alivyokuwa mzuri, kitendo cha kuteremka tu pale kituoni, niliwaona wahuni kibao wakiacha kila walichokuwa wakikifanya na kuanza kutukodolea macho.
Waliokuwa wakicheza kamari waliacha, waliokuwa wakicheza singeli waliacha na hata waliokuwa wakipiga stori, wote walibaki wanatukodolea macho.
Shida moja ya kwetu ndiyo hiyo, yaani vijana wana njaa kiasi kwamba kila kitu kizuri kinachopita, wao wanaanza kuhesabu kama dili! Nilijua pale wanatupigia mahesabu ya kuja kutukaba na kuchukua viwalo vya kijanja alivyokuwa amepiga Nancy, simu yake, pochi pamoja na simu yangu.
Kwa kuwa nimeshaishi sana Tandale na najua namna ya kwenda sawa na wahuni, niliamua kuchukua tahadhari mapema kwa sababu kama tungekabwa na mrembo kama Nancy, ningekuwa nimejishushia mno hadhi.

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 6


ILIPOISHIA:
Nilitafuta sehemu nzuri, upande wa nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na kuanza kupanga namna ya kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima kwa gharama yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na kiumbe, mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu na kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.
SASA ENDELEA...
Nikiwa bado palepale mafichoni, usingizi ukikizonga kichwa changu kutokana na ukweli kwamba sikuwa nimelala hata kidogo usiku kucha, nilisikia muungurumo wa pikipiki zaidi ya moja kutokea upande wa nyuma wa shamba kubwa.
Nilijiweka sawa, ‘chuma’ changu nikakikamata vizuri mkononi kwa ajili ya chochote kwani japokuwa nilikuwa sehemu ambayo naujua isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuniona, nilikuwa nafahamu vizuri jinsi Mute anavyoendesha shughuli zake. Alikuwa na intelijensia ya hali ya juu pengine kuliko hata vyombo vingi vya usalama.
Nikiri kwamba japokuwa ni kweli nilikuwa na matatizo makubwa na Mute, lakini ni yeye ndiye aliyenifundisha kila kitu nilichokuwa nakifanya. Nikiwa kwake, ndiko nilikojifunza kutumia bunduki, mbinu za mapigano ya mwilini au kwa kitaalamu ‘martial arts’, kutumia silaha nyingine mbalimbali na sehemu muhimu unazotakiwa kuwa nazo makini unapotaka kupigana na mtu, iwe ni silaha au kwa mikono.
Unajua tofauti kubwa kati ya raia wa kawaida na askari aliyepitia mafunzo, ni kwamba raia wa kawaida unaweza kuwa unajua kwamba ukimpiga ngumi usoni adui yako, utampasua na kumtoa damu au kumng’oa meno lakini hutaweza kuzuia asiendelee kupambana na wewe lakini askari anajua kabisa akikupiga sehemu gani, unaweza kudondoka na kupoteza fahamu papo hapo, au pengine kufa kabisa.

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 5


ILIPOISHIA:
Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.
SASA ENDELEA...
Yaani nisalimu amri kirahisi namna hiyo? Nijivalishe mwenyewe kitanzi kwenye shingo yangu? Lilikuwa ni jambo lisilowezekana kwa hiyo ilikuwa ni lazima nifanye kitu, tena haraka iwezekanavyo.
Pale nilipokuwa nimesimama, karibu na ukuta, kulikuwa na mtaro, ile inayochimbwa kandokando ya barabara. Kwa sababu maeneo mengi ya Masaki na Mikocheni yana kama asili ya majimaji, mitaro mingi iliyochimbwa ni mirefu na ina maji.
Kwa kasi ya kimbunga, nilijirusha kwenye mtaro, nikasikia risasi kadhaa zikipita mita chache kutoka pale nilipo, nikaangukia ndani ya mtaro. Kwa jinsi nilivyochukua uamuzi huo kwa kasi kubwa, nadhani hata polisi wenyewe hawakutegemea.
Katika medani za kivita, adui anapokuwa sehemu ambayo yupo chini kuliko wewe, kama kwenye shimo au handaki na ana silaha ya moto, huwa ni hatari sana kwa wewe uliyesimama juu ya ardhi kwa sababu yeye anaweza kukupiga risasi lakini wewe huwezi.

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 4


ILIPOISHIA:
“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti, mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone mwisho wangu. Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako)’, nikajua nimepatikana.
SASA ENDELEA...
Miongoni mwa vitu ambavyo Mungu amenijaalia, ni kutokuwa na hofu au woga ndani ya moyo wangu na pengine hiyo ndiyo sifa iliyokuwa inawafanya watu wote wanaonijua wawe wananiogopa au kuniheshimu, yaani kama huniheshimu basi uniogope kwani sikuwa na hata chembe ya woga.
Licha ya yule mtu kunigusisha bomba ambalo bila hata kuuliza nilijua lazima litakuwa ni mtutu wa bunduki, kwa jinsi ninavyowajua walinzi wengi wa Kibongo, huwa hawafanyi kazi kwa weledi.
Unaweza ukashangaa kwa nini nasema hivyo, lakini nikiri tu kwamba nimepitia mambo mengi sana hapa duniani, mengine makubwa na ya kutisha mno ambayo hata nikikusimulia, unaweza usiamini kwa haraka utakachokisikia.
Na miongoni mwa matukio mengi niliyoyafanya, yalikuwa yakiwahusu zaidi walinzi kwa hiyo nilikuwa najua jinsi walivyo wazembe.