The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 65


ILIPOISHIA:
Nilihisi kama kuna kitu kinanilamba hivi, nikaanza kutetemeka huku nikiendelea kujikausha nisisababishe mtikisiko wa aina yoyote, nilipozidi kuvuta utulivu, nikahisi kuna kitu cha baridi kinatingishikatingisha upande ule niliokuwa nalambwa, mapigo ya moyo yakawa yanadunda kama nimetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
SASA ENDELEA...
Nilitulia tuli huku nikiendelea kutetemeka, mara nikaanza kuhisi kile kitu kikitambaa na kunivuka mwili, kutoka upande mmoja kuelekea upande mwingine. Japokuwa kulikuwa na giza niliweza kukitambua vizuri kiumbe hicho kuwa alikuwa ni nyoka. Hata sijui ushujaa wa kutulia vile niliupata wapi maana kama nilivyowahi kusema, hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa maishani mwangu kama nyoka.
Basi yule nyoka mdogo alinitambuka na kupotelea upande wa pili wa kitanda, nikashusha pumzi ndefu kisha kwa tahadhari kubwa nikainuka pale nilipokuwa nimelala, nikasimama kwenye uchago wa kitanda na kujivuta mpaka kwenye swichi ya taa, nikaiwasha.

Japokuwa kulikuwa na baridi kali ya usiku, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, nikajitazama kwenye lile jeraha langu ubavuni, nikashtuka kugundua kwamba lilikuwa limeanza kujichimba na kutengeneza kidonda. Kumbe wakati yule nyoka akinilamba, alikuwa akitoa ganda la juu ambalo lilikuwa likiashiria kuanza kupona, nikashtuka mno huku nikiwa sielewi nini hatma yangu.
Cha ajabu ni kwamba safari hii sikuwa nasikia maumivu kabisa. Nikageuka na kutazama pale kitandani, hapakuwa na kitu zaidi ya shuka, nikalivuta na kujaribu kujikung’uta nikihofia kwamba yule nyoka anaweza kuwa bado yupo lakini hakukuwa na chochote.
Nikashuka na kuchungulia chini ya kitanda, pale palipokuwa na ule mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia. Cha ajabu, ulikuwa umefungwa vilevile, nikashusha pumzi ndefu na kurudi kitandani.
Kama ingekuwa amri yangu, siku hiyo nisingelala kabisa lakini usingizi ulikuwa ukinitesa sana. Nilichoamua, ilikuwa ni kufungua mlango na kuuegesha ili kama hali ikitokea tena, nitoke mbio mpaka nje. Sikuzima tena taa kama mwanzo, nikataka kuona nini kitatokea tena.
Nilipojiegesha kitandani tu, usingizi mzito ulinipitia, nilipokuja kuzinduka, tayari kulishakuwa kumepambazuka kabisa, harakaharaka nikashuka kitandani na kuchungulia kule chini ya kitanda.
Cha ajabu ni kwamba ule mfuko haukuwepo, niliangaza kila kona lakini sikuuona, nikahisi labda yule nyoka alitambaa nao na kujifuicha kwenye nguo zilizokuwa chini, nikapekua kila sehemu lakini sikuona dalili zozote.
“Unatafuta nini?” sauti ya baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, naye akawa ananitazama.
“Kuna kitu kimenitokea usiku sijakielewa.”
“Kitu gani?” baba aliniuliza kwa mkato, ikabidi niinue shati na kumuonesha pale ubavuni palipokuwa na kidonda, nikaanza kumueleza jinsi nilivyoshtuka na kukutana na mauzauza ya yule nyoka chumbani kwangu na jinsi alivyokuwa akinilamba pale kwenye kidonda.
Tofauti na nilivyotegemea, baba alicheka kwa dharau, akaniambia kama naipenda pepo kwa nini naogopa kufa? Sikumuelewa anamaanisha nini, ikabidi nimhoji, akanijibu kwa mafumbo na kutoka zake, akaniacha nikiwa na mawazo tele kichwani mwangu.
Baadaye nilitoka na kwenda kuoga, nikarudi na kujiandaa kisha nikatoka na kwenda kibarazani ambako baba yake Rahma alikuwa amekaa akisoma kitabu. Nilipomsalimia, aliacha kila alichokuwa anakifanya na kuitikia salamu yangu kwa uchangamfu.
Kwa jinsi alivyonipokea, nilipata nguvu ya kumuuliza kwa kina kuhusu mambo mbalimbali ambayo nilikuwa siyaelewi, akaniambia jambo ambalo lilinishtua sana. Aliniambia kwamba usiku wakati tukirejea nyumbani kutoka Bagamoyo, kuna sehemu tulipita na kusikia mwanamke akipiga kelele za kuomba msaada.
Akaniambia kwenye msitu ule ndipo mahali watu waliochagua njia kama yangu, ya kuwa na utajiri wa kichawi, wanapoenda kutolea makafara yao, akaniambia hata mimi mambo yakichanganya nitakuwa naenda kutoa kafara kwenye msitu huo. Nilishtuka sana kutokana na maneno aliyoniambia, nikawa nahisi kama nipo ndotoni.
“Ukiwa mwanachama wa kawaida, unatoa kafara za kawaida, kama ambazo tayari wewe umeshazitoa, si unakumbuka umeshatoa mara ngapi?” aliniuliza baba yake Rahma huku akigeuka huku na kule kuhakikisha hakuna anayetusikiliza.
“Mara mbili!” Nilimjibu. Kiukweli mpaka wakati huo tayari nilikuwa nimesababisha matukio yaliyoondoa nafsi za watu wasio na hatia wawili, la kwanza lilikuwa ni lile la ajali iliyoyakatisha maisha ya yule mtoto wa Mlandizi na ya pili ikiwa ni ile ya bodaboda aliyepata ajali mbaya baada ya kugongana na mimi, mita chache kutoka pale kwenye msiba wa yule mtoto.
Jaribio lingine la kumtoa kafara Sadoki, rafiki yangu kipenzi wa Chunya lilikuwa limegonga mwamba huku ikibakia kidogo nidhalilike kutokana na nguvu ya upako aliyokuwa nayo Sadoki na mama yake.
“Sasa ka njia uliyochagua, utatakiwa kuwa unatoa sadaka za damu mara nyingi kadiri iwezekanavyo, ndiyo maana kuanzia mwanzo nilikwambia kwamba utajiri huo ni mgumu sana, bora ubaki maskini,” alisema baba yake Rahma.
Japokuwa kweli niliogopa kwa kiasi fulani, lakini tamaa ya utajiri ilishawaka ndani ya moyo wangu kiasi kwamba sikuwa nataka kusikia jambo lingine lolote la kunirudisha nyuma. Nilimkatisha kijanja na kumuuliza kuhusu kile kilichotokea usiku kuhusu yule nyoka.
Alinifafanulia kwamba ni kawaida ya mtu yeyote anayemiliki au anayetaka kumiliki utajiri kwa nguvu za giza, kufuga mnyama huyo na kuongeza kwamba chakula chake kikubwa, ukiachana na vyakula vya kawaida ambavyo nyoka hupewa, ni lazima kila siku awe anakunywa damu yangu.
“Mungu wangu!” nilishtuka sana na kujikuta nimelitaja jina la Mungu. Kwa maneno hayo ya baba yake Rahma, ni kwamba kile kilichotokea usiku haukuwa muujiza na kwamba ni jambo ambalo litakuwa linatokea kila siku kwa kipindi chote cha maisha yangu, nilijikuta nikichoka.
“Kadiri utakavyokuwa unamtunza vizuri na kumpa mahitaji yake yote, ndivyo atakavyokuwa anaongezeka ukubwa na kadiri atakavyokuwa anaongezeka ndivyo utajiri wako utakavyokuwa unaongezeka kwa hiyo ukiwa mvumilivu, unaweza kufika mbali,” alisema baba yake Rahma, nikawa na shauku kubwa  ya kuendelea kumuuliza, hasa kuhusu nyoka huyo lakini mazungumzo yetu yalikatishwa na Rahma.
“Kaka Togo za asubuhi? Naomba unisindikize dukani mara moja,” alisema Rahma kwa heshima, baba yake akanipa ishara kwamba niende, nikainuka na kutoka naye.
Tofauti na siku zote, pale nje palikuwa peupe kabisa, wale madereva Bajaj na bodaboda hawakuwepo, Rahma akaniambia eti walikuwa wameamua kuhamisha kituo chao na kukipeleka sehemu nyinginekwa sababu pale hakuna abiria.
Nilijikuta nikicheka tu maana ukweli haukuwa hivyo, moyoni nilibaki nikijiuliza, ina maana nimekuwa na nguvu kiasi cha kuwatisha watu kiasi kile?
“Mlikuwa mnazungumza nini na baba? Maana naona mnaelewana sana, sijawahi kumuona baba yangu akiwa karibu na mtu kama ilivyo kwako, siku hizi hata mimi hanipendi kama anavyokupenda wewe,” Rahma alisema wakati tukitembea taratibu kuelekea dukani.
Sikumjibu kitu chochote cha maana zaidi ya kuleta masihara kwa sababu jana yake nilipotaka kumweleza ukweli aliniona kama nimechanganyikiwa.
“Mbona mimi nakuuliza maswali ya msingi wewe unanijibu kimasihara?” Rahma alinihoji, ikabidi niache kuchekacheka na kuvaa ‘usiriasi’, nikamwambia hata mimi mwenyewe sielewi.
“Tunaenda wapi kwani?”
“Nataka twende pale tulipokaa jana, nahitaji kuzungumza na wewe,” aliniambia, moyo wangu ulisita kwani niliamini naweza kukutana na hali kama ya jana Rahma akaendelea kuniona mwendawazimu. Hata hivyo nilishindwa kumkatalia, tukaelekea mpaka pale dukani.
Cha ajabu, tulipofika tu, yule dada tuliyemkuta jana yake, aliponiona tu alikurupuka kwa kasi na kukimbia huku akiacha mlango wazi. Hakuwa amevaa nguo na nadhani hiyo ndiyo sababu iliyomfanya akimbie, Rahma akawa anashangaa akiwa haelewi kinachoendelea.
“Mbona unavuja damu nyingi hapo, umepatwa na nini?” alisema Rahma, nilipojitazama pale ubavuni, nilishtuka sana baada ya kuona damu nyingi nzito zikiwa zimenitoka bila mimi mwenyewe kujua chochote na kulowanisha kabisa shati langu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment