Friday, February 2, 2018

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 60



ILIPOISHIA:
Junaitha alimkokota mpaka bafuni na kufunga mlango kwa ndani, nikabaki nimesimama pale koridoni. Ghafla nikaanza kusikia sauti ya Firyaal akilia kama mtu anayekabwa na kitu, nikakurupuka mpaka kwenye kile chumba walichokuwa wamelala wote, nikafunga breki za ghafla mlangoni, nikiwa siamini kile nilichokuwa nakiona.
SASA ENDELEA...
Firyaal alikuwa amejikaba shingoni kwa kutumia mikono yake miwili, macho yakiwa yamemtoka pima, akikoroma kama mtu anayeelekea kukata roho. Sikuwahi kusikia hata mara moja kama kuna mtu amewahi kufanikiwa kuyakatisha maisha yake kwa kujikaba mwenyewe lakini kwa Firyaal ilionesha kama hilo linaweza kutokea muda wowote.
Kwa kasi ya ajabu nilisukuma mlango na kwenda kumkamata Firyaal, kwa jinsi alivyokuwa na mwili ‘teketeke’, niliamini itakuwa rahisi kwangu kumtoa ile mikono yake shingoni lakini kumbe nilikuwa najidanganya.
Nilishangaa nilipomgusa Firyaal kukuta mwili wake umekakamaa na kuwa mgumu kama mti, nikaanza kuhaha kujaribu kumnasua bila mafanikio, aliendelea kukoroma huku wenzake wakiwa wamelala fofofo.

Ilibidi nitoke na kumkimbilia Junaitha ambaye muda mfupi baadaye naye alikuja na kushuhudia kile kilichokuwa kikiendelea.
“Umemfanya nini?”
“Sijui chochote, mi nimemkuta tu anajikaba,” nilisema, akamsogelea kwa hatua za harakaharaka na katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa kumuona akimzibua kibao cha nguvu upande wa kushoto, akahamia upande wa kulia, akamzibua kwa nguvu zaidi!
“Utamuumiza?”
“Hapa ndiyo namsaidia, nyamaza?” Junaitha alinifokea, akamuongeza kibao kingine cha upande wa kushoto, nikafumba macho kwani sikutaka kuona jinsi msichana huyo mrembo alivyokuwa akiadhibiwa.
“Eeeh! Hapa ni wapi? Jamal, Jamal,” sauti ya Firyaal iliyokuwa inatoka kwa kukoroma, ndiyo iliyonifanya nifumbue macho, nikashangaa kumuona akiwa amefumbua macho, akijishangaa yeye mwenyewe na kutushangaa sote mle ndani.
“Firyaal,” nilisema huku nikisimama, na yeye akajikongoja na kusimama, tukawa tunataka kwenda kukumbatiana lakini Junaitha alitukataza, akasema Firyaal amevamiwa na pepo wachafu kwa hiyo lazima asafishwe kwanza ndiyo tutakaporuhusiwa kugusana naye.
Maelezo yale yalinishtua sana, nikakumbuka kauli ya Junaitha kwamba lazima kuna mmoja wetu atapoteza maisha kama kafara, nikawa nasali moyoni kwamba asiwe Firyaal kwa sababu nilimuona kama mrembo sana, tena binti mbichi ambaye alikuwa tayari kunipa zawadi ya kuwa mwanaume wake wa kwanza, kama ilivyokuwa kwa Raya.
“Nakuomba msaidie,” nilimwambia Junaitha, akanitazama tu usoni bila kunijibu chochote. Tukiwa tunatazamana, mara tulishtuka kumuona Shenaiza akiingia ndani ya kile chumba akiwa amejifunga taulo tu, naye akapigwa na butwaa kumuona mdogo wake, Firyaal naye akashtuka mno kumuona dada yake akiwa amesimama, wote tukawa tunashangaana, ukimya ukapita kati yetu.
“Naombeni mnisikilize kwa makini, tumefikia hatua nzuri sana lakini kama tusipokuwa makini, tutasababisha matatizo makubwa zaidi, Jamal shughulika na Shenaiza, mimi ngoja nikamalizane na Firyaal, angalizo! Hamtakiwi kugusana kwa sasa,” alisema Junaitha, nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
“Bado sielewi Jamal, mdogo wangu amefikaje huku halafu mbona kama hayupo sawa?”
“Shenaiza, tulikotoka ni mbali sana kuliko tunakoelekea, amini kila kitu kitakuwa sawa kabisa, twende,” nilisema kwa sauti iliyojaa matumaini makubwa ingawa ukweli hata mimi nilikuwa sijui mwisho wa sarakasi zote zile ungekuwa nini.
Kama alivyosema Junaitha, sikutakiwa kumgusa Shenaiza ingawa mwenyewe alionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka tukumbatiane, tukaongozana mpaka chumbani kwake. Kwa kuwa siku zote hizo hakuwa na fahamu, hata chumba chake kilikuwa kizito mno, tulipoingia tu mwenyewe ndiyo alikuwa wa kwanza kuligundua hilo.
“Mbona humu ndani hewa nzito sana?” alisema, sikumjibu chochote zaidi ya kumsaidia kufungua madirisha na kuwasha feni, yeye akakaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni ya kitanda, akiendelea kunitazama kama anayetamani kuzungumza jambo na mimi.
“Unajua bado najihisi kama nipo kwenye ndoto, kumbukumbu zangu zinarudi taratibu sana kichwani.”
“Usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa sawa.”
“Wewe si ulikuwa unaumwa hoi hospitalini?” aliniuliza, nikatingisha kichwa huku nikifungua vifungo vya shati langu, nikamuonesha jeraha akubwa lililokuwa kifuani ambalo sasa lilikuwa limepona na kubakiza ganda la juu kubanduka ili lipone kabisa na kuacha kovu, akapigwa na butwaa.
“Mh! Kwa hiyo nilipoteza fahamu kwa muda mrefu kiasi hicho mpaka umepona?”
“Ni stori ndefu Shenaiza, hebu tuliza kwanza kichwa chako, nimeshakwambia kila kitu kitakuwa sawa.
“Sasa ulitokaje hospitalini na mimi nilitokaje? Yule daktari aliyekuwa akinichoma sindano za kwenye mishipa alikuwa akichanganya na nini mbona zilikuwa zikiuma sana halafu nikawa nalala sana baada ya kuchomwa?”
“Jamani Shenaiza, si nimekwambia nitakueleza kila kitu? Kuwa mpole,” nilimwambia. Kwa kuwa shuka lililokuwa limetandikwa pale kitandani lilikuwa limechafuka, ilibidi nifungue kabati na kuchukua jingine safi, nikabadilisha na kumwambia apumzike kitandani.
Kweli alifanya hivyo lakini akataka na mimi nilale naye pale kitandani, jambo ambalo sikukubaliana naye, nikamwambia ni lazima tufuate masharti kwa sababu tulikuwa kwenye kipindi kigumu. Kweli alijilaza pale kitandani kihasarahasara, mimi nikakaa pale alipokuwa amekaa yeye.
Bado alikuwa na maswali mengi lakini niliendelea kumkatisha na kumtaka apumzike. Kutokana na jinsi alivyokuwa amechoka, hazikupita dakika tatu, akapitiwa na usingizi mzito.
Muda mfupi baadaye, Junaitha alirejea akiwa na Firyaal ambaye sasa alionesha kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
“Kwa nini umemruhusu huyo alale tena wakati hajala chochote? Hebu muamshe, anaweza kupitiliza tena akatupa kazi ya ziada,” alisema Junaitha na hakusubiri mimi nifanye kazi hiyo, alimsogelea mwenyewe pale kitandani na kuanza kumtingisha.
Shenaiza akakurupuka usingizini na kukaa kitako, macho yake yakatua kwa mdogo wake, safari hii Junaitha aliwaruhusu wakumbatiane, wakafanya hivyo na kila mmoja wao akaanza kuangua kilio kwa sauti ya juu mithili ya watu waliopokea taarifa za msiba.
Cha ajabu, walipokumbatiana na kuanza kulia tu, mvua kubwa ilianza kunyesha ghafla, akina Raya na Shamila waliokuwa usingizini nao wakazinduka na kuja mbiombio kwenye kile chumba tulichokuwemo, yule mwanamke wa ajabu aliyekuwa amefungiwa naye akaanza kunguruma kwa sauti kubwa.
Kila kitu kilibadilika kwa kasi kubwa mno, mvua kubwa ikaendelea kumwagika, huku wingu kubwa jeusi likitanda kila kona na kuimeza kabisa nuru iliyokuwepo, ungeweza kudhani tayari ni usiku.
“Kuna kitu kinataka kutokea siyo kizuri, hebu nifuateni haraka,” alisema Junaitha, wote tukakurupuka na kusimama, tukatoka na kuanza kumfuata Junaitha, tukiwa hatuelewi tunaenda wapi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...