Thursday, January 25, 2018

KIVURUGE WA TANDALE- 1


Saa saba na dakika zake mchana, tumbo la Ashrafu lilikuwa likiunguruma kwa kusakamwa na njaa kali, aliamua kutoka ofisini kwao ndani ya Jengo la Al- Haramain, Mtaa wa Shaurimoyo jijini Dar na kuamua kushuka kwa kuzikanyaga ngazi moja baada ya nyingine.
Kazi yake ya ufundi wa kompyuta na vifaa vya kielektroniki ilimfanya kuwa kijana maarufu sana na hii ilitokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao kwenye kazi yake kiasi cha makampuni mengi kugombea kumwajiri lakini mwenyewe akawa hataki.
Kwake aliona ni bora ajiajiri lakini kama kuna kampuni inahitaji huduma yake, inamfuata na wanafikia makubaliano kisha kazi inafanyika.
Baada ya kushuka ngazi kwa tabu hatimaye alijisogeza taratibu hadi mgahawani ambapo palijulikana kwa jina maarufu la Kwa Makofia.
Hapo alikutana na umati mkubwa hivyo kushindwa kabisa kuagiza chakula alichokuwa akihitaji hivyo aliamua kuhamia kwenye mgahawa wa jirani yake, kabla hajachukua uamuzi wa kuondoka Kwa Makofia, macho yake yalikutana na kitu kilichomfanya ashtuke kidogo.

Mrembo matata mwenye mvuto wa kipekee, mweupe aliyepanda juu, mwenye macho kama anasikia usingizi, alikuwa amekaa kama anayesubiria huduma!
“Dah, huyu ni mtu wa kawaida au ni malaika ameshuka kupunga upepo duniani?” Ashrafu alijikuta akiropoka ingawa ni kwa sauti ndogo na ya chini kabisa na hakuna aliyemsikia hata kwa herufi moja.
“Nafanyaje jamani kuhusu huyu msichana mzuri hivi? Naanzaje kumuacha tena amekaa mwenyewe katika mazingira kama haya? Sasa sijui yuko na mwenzake na ametoka kidogo tu au yuko mwenyewe na mbona leo nimekosa kabisa ujasiri ambao nimekuwa nao kwa siku zote?” Ashrafu alijiwazia moyoni huku akiondoka eneo hilo na kujisogeza kwenye mgahawa wa jirani na hapo.
Alifika na kuagiza chakula ambapo alichagua moja ya viti vilivyokuwemo ndani na kukaa huku mawazo yake yakibaki kwa msichana aliyekutana naye pale Kwa Makofia.
Katika hali ya kushangaza, wakati anawaza juu ya mwanamke huyo, alishangaa kumuona msichana yule akiingia mgahawani hapo na kukaa kwenye moja ya viti na kisha kuagiza chakula.
Ni hapo ndipo Ashrafu alishindwa kuvumilia na kuamua kutumia ujasiri wake wa asili ambao humuwezesha kumvaa mtu yeyote kwa wakati wowote na kumwambia chochote kwa mazingira yoyote.
“Dada, samahani kidogo,” Ashrafu aliita kwa nidhamu zote na kuonesha heshima ambayo hata yeye mwenyewe aliishangaa imetoka wapi.
“Mimi…?” Msichana wa watu aliitika kwa mshangao na macho ya kuuliza kama ni yeye aliyekuwa akiitwa.
“Yeah…” Ashrafu aliitikia na kumpa ishara ya mkono msichana yule ambaye alionesha kusita...akatingisha bega lake kuonesha kukataa wito wake.
“Samahani nakuomba au ni vibaya kukuita? Kataa neno usikatae wito,” Ashrafu alichombeza.
“Samahani kaka! Samahani lakini, mimi kwa watu ambao siwafahamu siwezi hata kuwasogelea...” alisema yule msichana na kuagiza chakula.
Ashrafu alishusha pumzi chini...lile tumbo lake lililokuwa likiunguruma safari hii aliona limezidi mara mbili yake.
“Hata mimi nikuombe samahani! Naomba nikae hapo karibu na wewe!” Ashrafu alirusha karata nyingine tena huku akimtolea jicho la aibu.
Yule msichana alikubaliana na Ashrafu, ilikuwa furaha kubwa kwake kama siyo ushindi kutokana na mazungumzo ambayo alipanga kuyaendesha kwa muda ambao watakuwa wanasubiri chakula, aliamini kabisa hadi zoezi la kula linamalizika, atakuwa ameshaibuka kidedea.
“Siwezi kumkosa huyu mtoto, kwanza anaonekana laini na mwepesi kama maharage ya Mbeya,” Ashrafu aliwaza huku akimtazama usoni msichana yule.
“Samahani tena kwa usumbufu…”
“Bila samahani kaka…”
“Naitwa Ashrafu kwa kirefu, sijui wewe mrembo unaitwa nani?”
“Kwa nini unaniita mrembo jamani?” Aliuliza yule msichana huku akijiangalia kiunoni hadi miguuni.
“Si kama hivi ulivyo mzuri na mrembo au huoni?”
“Aaah, kawaida bwana na huwa sipendi kabisa mtu akiniita mrembo…”
“Okey, samahani kwa hilo.”
“Wala usijali.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Nancy, ni mwenyeji wa Morogoro eneo la Kilombero.”
Ashrafu aliendelea kumtolea macho na masikio akiwa haamini kama maneno yale yanatoka kwa yule msichana.
“Mi mwenyewe mkazi wa Morogoro!”
“Weee! Sehemu gani?” Nancy alishangaa, alionekana kubadilika sura na kuwa ya tabasamu mara baada ya kuambiwa kuwa wanatoka mkoa mmoja kumbe ulikuwa uongo wa Ashrafu ili kumnasa.
“Mi natokea Morogoro mjini kabisa eneo moja hivi linaitwa Kihonda, unapajua?”
“Ndiyo, sasa mara nyingi huwa nafikia kwa Shangazi sehemu moja inaitwa Mji Mpya nakaa siku mbili tatu ndiyo naelekea Kilombero.”
Wakati wanaendelea na mazungumzo ya kufahamiana, mhudumu alileta vyakula kulingana na maagizo ya kila mmoja wao, ambapo kwa pamoja waliamua kutumia meza moja kula.
“Hujaniambia lakini kuhusu kazi yako,” Nancy alianza kuchokoza.
“Ah, mi mzugaji tu mjini hapa, nabangaiza ilimradi siku ziende. Nakaa mtaa wa tatu kutoka hapa,” Ashrafu alidanganya kwa mara nyingine hali iliyomfanya Nancy ashtuke.
“Mh! Hongera, kama kweli unafanya kazi hizo na unaonekana mtanashati hivyo!”
“Asante sana na wewe je?”
“Mimi nafanya kazi katika kampuni ya kuuza vifaa vya solar kutoka China, pale karibu na ‘round about’ alimuelekeza Ashrafu kwa kumnyooshea mkono.
“Naishi Mikocheni, niko mwenyewe na maisha yanasonga kwa kweli,” alisema Nancy huku akimtazama Ashrafu kwa macho yaliyojaa aibu za kikekike.
Kwa ilivyoonesha, Nancy alikuwa mzungumzaji sana maana ndani ya muda mfupi tu, alishayatawala mazungumzo na mbinu kali alizozitumia Ashrafu, zilimfanya ajikute akimzoea haraka utafikiri wamefahamiana miaka kadhaa iliyopita.
Walimaliza kula. Nancy akamwambia alikuwa na safari ya kuelekea Posta kufuatilia hundi ya malipo kwenye kampuni moja waliyofanya nayo biashara.
“Okey, basi nakuomba tubadilishane mawasiliano ili tuendelee kuwa karibu zaidi,” Ashrafu alitupa ndoano kimtego kwa Nancy.
“Namba za simu tena? Hapana huwa sitoi namba za simu, utanisamehe kwa hilo,” Nancy alisema huku akiinuka, akachukua mkoba wake mdogo na kuanza kutembea kimadaha, akaenda mpaka kaunta na kulipa bili yake, akamgeukia Ashrafu ambaye bado alikuwa amekaa palepale akiendelea kuusifu uumbaji wa Maulana kwa kiumbe yule.
Alimpungia mkono kichokozi huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akatoka zake na kumuacha Ashrafu akiwa bado ameganda palepale kama barafu.
“Ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu,” alijisemea huku tabasamu hafifu likichanua kwenye uso wake, akashusha pumzi ndefu na kuinuka kuelekea kaunta kulipa.

Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...