Thursday, January 25, 2018

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia)- 62


ILIPOISHIA:
“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.
SASA ENDELEA...
“Mbona sikuelewi Togo?”
“Ni kuhusu wazazi wetu.”
“Wamefanya nini?”
“Wanajihusisha na...” kabla sijamalizia nilichotaka kukisema, jambo la ajabu lilitokea. Yule muuzaji wa lile duka, alifungua mlango na kutoka huku akikimbia, cha ajabu, hakuwa amevaa nguo hata moja.
“Vipi kwani mbonaumeshtuka?”
“Umemuona?”
“Nani? Vero? Nini cha ajabu kwani?” Rahma alinishangaa sana, na mimi nikawa namshangaa. Yaani mtu atoke dukani akiwa mtupu, halafu aanze kukimbia mitaani, siyo jambo la kushangaza hilo?”

“Itakuwa labda kuna anaenda kuomba chenji, tuendelee na mazungumzo yetu,” Rahma alizidi kunishangaza. Sikuelewa kwamba alikichukuliaje kitendo kile kiasi cha kutokipa uzito hata kidogo, hata baadhi ya wateja waliokuwa wamekaa upande wa pili, nao wakipata vinywaji, hawakuonesha kushtuka kabisa.
“Ndiyo atoke bila nguo?”
“Togo, umeanza kuchanganyikiwa nini?”
“Rahma, ina maana huoni kama hajavaa nguo yule? Kwa hiyo kumbe ndiyo maana alikuwa anajificha dukani?”
“Nani hajavaa nguo? Una matatizo gani Togo? Usije kunitia aibu hapa, hebu maliza twende,” alisema Rahma huku akimalizia soda yake. Nadhani alihisi huenda nikatokewa na maruweruwe kama yale yaliyokuwa yakinitokea.
“Basi Rahma, tuendelee na mazungumzo yetu,” nilijaribu kumsihi lakini alishaonesha kama ameingiwa na hofu ndani ya moyo wake, hakutaka kukaa tena eneo lile, ikabidi nimalizie soda yangu na kusimama.
Sikuwa nimemlipa yule muuzaji, lakini Rahma aliniambia kwamba nisijali yeye atampa hata baadaye. Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyonipuuza ila sikutaka kumuonesha.
Kwa jinsi alivyonichukulia, hata kama ningemweleza kile kilichofanya nikakutana naye pale, huenda pia angenipuuza kwa hiyo nilichokifanya, niliamua kunyamaza na dukuduku langu moyoni.
“Hujamalizia ulichotaka kuniambia,” alisema Rahma wakati tukitembea kurudi ndani, nikamwambia asiwe na wasiwasi nitamueleza siku nyingine.
“Kwani siku hizi umeshapata mwanamke mwingine anayekuzuzua?”
“Hapana Rahma, na ndiyo maana nilitaka kuzungumza na wewe, lakini basi tuyaache.”
“Sikuelewi Togo na kama unaona ulichokifanya kwangu ni sawa, wala mimi sina cha kusema ila kumbuka chozi langu haliwezi kwenda bure,” alisema Rahma, nikajaribu kumbembeleza lakini ilikuwa sawa na kazi bure.
Mpaka tunaingia ndani, Rahma alikuwa akiendelea kulalamika tu, akaniambia anashukuru kwa yote niliyomfanyia na kumuumiza moyo wake. Nilishindwa cha kusema, ikabidi ninyamaze tu, bado wale madereva bodaboda na Bajaj pale nje hawakuwa wamerejea.
Tuliingia ndani lakini Rahma hakutaka kabisa kujishughulisha na mimi, alienda moja kwa moja sebuleni, mimi nikaenda chumbani huku nikiwa nimekosa kabisa furaha. Nilijilaza kitandani, nikaanza kutafakari tukio la yule muuzaji wa lile duka.
Nilichokihisi kwa harakaharaka, huenda alikuwa akitumia nguvu za kishirikina kwenye biashara yake maana nimewahi kusikia kwamba kuna wafanyabiashara ambao ukiingia kwenye duka lake au sehemu anayofanyia biashara, hata kama umevaa nguo, anakuona kila kitu lakini wapo wengine ambao inakuwa kinyume chake, kwamba muuzaji anakaa kwenye biashara akiwa hana nguo hata moja ingawakwa macho ya kawaida anaonekana amevaa nguo.
Lengo la kufanya hivyo inakuwa ni kuvutia wateja na kiukweli hata kwenye lile duka la pale nje, lilikuwa kubwa lenye kila kitu unachokihitaji na kiukweli alikuwa akifanya sana biashara kwa sababu kwa muda mfupi tu tuliokaa pale, wateja walikuwa hawakauki.
“Ulitaka kumwambia nini Rahma,” sauti ya baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Alikuwa amesimama pembeni ya kitanda changu, hata sikukumbuka ameingia saa ngapi, nilichoshtuka ni kumuona akiwa ndani.
“Mimi?” niliongea kwa kubabaika huku nikiinuka pale kitandani.
“Kwani nazungumza na nani?” baba aliniuliza akionesha kuwa na jazba, nikawa nababaika. Kwa jinsi ilivyoonesha, alikuwa anajua kwamba nilitaka kumweleza Rahma ukweli, jambo ambalo walinionya sana kwamba sitakiwi kutoa siri za jamii yetu kwa mtu yeyote asiyehusika.
“Tulikuwa tunapiga stori za kawaida tu.”
“Stori za kawaida ndiyo muende dukani?” baba alinihoji huku akinitazama kwa macho ya ukali, sikuwa na cha kujibu na kwa jinsi baba alivyo, nilitegemea kabisa kwamba pale lazima angenizibua makofi, nikawa nimekaa ‘attention’.
“Kuna maagizo yako kutoka kwa Mkuu, usiku itabidi tukupeleke sehemu, umeyaanza mwenyewe lazima uyamalize,” baba alisema huku akigeuka na kuanza kuondoka, nikabaki na mshangao mkubwa, nikiwa sijui alichokimaanisha. Akiwa anamalizikia kutoka, aligeuka na kunitazama kwa macho makali.
“Ole wako ufumbue domo lako!” Nilishusha pumzi ndefu, mambo yalianza kuwa mengi na kunielemea kwa sababu kabla moja halijaisha, lingine lilikuwa likiibuka. Kwa jinsi nilivyozungumza na baba yake Rahma, nilitambua kwamba hizo salamu kutoka kwa Mkuu lazima zitakuwa zinahusu masharti ya uamuzi nilioufanya.
Niliona kama muda unaenda taratibu sana, sikutoka chumbani, hata chakula nililetewa kulekule na Rahma ingawa safari hii alionesha kuwa na chuki za waziwazi kwangu maana hakutaka hata kunisemesha wala kunitazama usoni.
Hatimaye jioni iliwadia, baba na baba yake Rahma, wakiwa tayari wameshajiandaa, walinifuata chumbani na kuniambia muda wa safari umewadia, wakanitaka nijiandae, baba Rahma akanipa koti kubwa jeusi.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Jiandae bwana, maswali mengi ya nini?” alisema baba kama kawaida yake, nikajiandaa na muda mfupi baadaye, safari ilianza. Kwa jinsi nilivyokuwa nimevaa, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kunitambua, lile koti lilinibadilisha kabisa. Tulitoka na kuelekea moja kwa moja kwenye stendi ya mabasi ya Makumbusho, tukapanda kwenye ‘coaster’ moja ambayo mbele ilikuwa imeandikwa kwamba inaenda Bagamoyo. Sikuwa nimewahi kufika Bagamoyo zaidi ya kusoma tu darasani kuhusu mji huo wa kihistoria.
Basi tulienda mpaka tulipofika sehemu moja iitwayo Mlingotini, tukateremka kwenye gari na kuvuka barabara, tukaanza kutembea kwa miguu. Tulienda umbali mrefu sana maana mpaka inafika saa tano za usiku, bado tulikuwa tukitembea.
Hatimaye tuliwasili kwenye eneo lililokuwa na nyumba kama tatu hivi, moja ikiwa imeezekwa kwa bati na zile nyingine kwa makuti, baba akabisha hodi ambapo sauti ya mwanamke ilisikika ikitukaribisha.
Muda mfupi baadaye, mwanamke mmoja mzee alitoka, ilionesha alikuwa akifahamiana vizuri na baba na baba yake Rahma kwani aliwakaribisha kwa uchangamfu, tukaingia ndani na kukaa kwenye jamvi lililokuwa pale sebuleni.
“Ndiyo huyu?” aliuliza yule mwanamke, baba akamjibu kwamba ndiyo mimi, sikuelewa kwamba ndiyo mimi nimefanyaje na kwa nini ameniuliza, ikabidi niwe mpole.
“Mchumba hujambo? Ukifanikiwa na mimi nataka uninunulie gari,” alisema yule mwanamke huku akitabasamu, mapengo yake yakaonekana. Sikuelewa kwa nini amesema vile, nikazidi kuwa gizani. Alinishika mkono na kuwapa ishara akina baba kwamba wamsubiri, tukatoka nje na kwenda kwenye kibanda cha makuti.
Wakati tunatoka, nilimsikia baba akimwambia baba Rahma kwamba kuwana mtoto kama mimi ni hasara, wakacheka. Sikuelewa kwa nini baba amesema vile lakini sikujisikia vibaya maana mimi na baba kukwaruzana ni jambo la kawaida kabisa, ingawa mimi ndiyo nilikuwa mwanaye kipenzi.
“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...