Wednesday, January 24, 2018

Double Life! (Maisha Mara Mbili)- 1


MVUA kubwa inanyesha na kila mtu anakimbilia sehemu ya kujisitiri ili asilowane lakini mimi sijali, naendelea kutembea taratibu kama hakuna chochote kinachoendelea. Mvua inazidi kumwagika kwa nguvu, radi zinapiga na upepo mkali unafanya hali iwe tete, wenye biashara ambazo zipo barabarani, wanakimbizana kuokoa mali zao zisiharibiwe na mvua hiyo, wengine wanafunga kabisa milango ya maduka yao.
Miamvuli haifui dafu kwenye mvua hii kutokana na upepo mkali, muda mfupi baadaye, mitaa yote inakuwa kimya kabisa, watu wamejibanza pembeni, wengine wakiwa wamejikunyata kutokana na baridi iliyoambatana na mvua hii.
Kwangu hali ni tofauti, kama nilivyosema, sijali chochote, naendelea kutembea taratibu kandokando ya barabara, maji machafu yanachuruzika kutoka kwenye nywele zangu nyingi na chafu mpaka kwenye nguo zangu zilizofubaa kwa uchafu.
Nina muda mrefu sijagusa maji kuusafisha mwili wangu, hali iliyonifanya niwe nanuka kama beberu, naisikia vizuri harufu mbaya inayotoka kwenye mwili wangu lakini sijali, naendelea kutembeatembea, hata sijui naelekea wapi lakini najikuta tu siwezi kukaa sehemu moja na kutulia. 
Miguuni sijavaa viatu na mgongoni nimebeba begi chafu nililoliokota kwenye jalala na kulijaza chupa tupu za maji pamoja na uchafu mwingine. Nimevaa suruali iliyochoka na kiunoni nimejifunga kwa kamba ya katani, huo ndiyo mkanda wangu, sina habari na mtu.

“Chizi huyooo! Mwendawazimu huyooo!” kwa mbali nasikia kelele za watu waliojibanza mvua kwenye viambaza vya nyumba na maduka yaliyopo jirani na barabarani, nadhani wananishangaa kwa jinsi ninavyoendelea na ‘hamsini’ zangu bila kujali mvua hiyo kubwa lakini siwajali. 
Nimeshaitwa sana kila aina ya majina mabaya, nimeshanyanyasika sana, kama si ukakamavu wangu pengine ningeshafanyiwa vitendo vingi vya kikatili, kila mtu akiamini kwamba mimi ni kichaa!
Mwonekano wangu unatosha kutoa majibu kwamba kweli mimi ni kichaa, matendo yangu pia yanaonesha wazi kwamba nimechanganyikiwa, sipo sawa na kila mmoja ananishangaa lakini mwenyewe najua wazi kilichosababisha nikawa hivi! Naona bora kila mtu anione kama nimechanganyikiwa, sioni tatizo lolote na mwenyewe nimeridhika na hali halisi.
Waingereza wanao msemo mmoja kwamba ‘better this way’ wakimaanisha bora hali hii! Kwangu mimi naona better this way, acha watu wote wanione kama nimechanganyikiwa, acha wanicheke na kunidhihaki, acha waniite majina yoyote mabaya ingawa sipo tayari kuona mtu akiokota jiwe na kunipiga au akinifukuza kama mbwa, hapo huwa sina uvumilivu.
Yawezekana ukashangaa kwamba kwa nini nimeamua kuishi aina hii ya maisha, nikiwa sina sehemu yoyote ya kulala, kinachopatikana mbele yangu ndicho ninachokula, mwili wangu umedhoofika, sitaki kuchanganyikana na mtu yeyote, nataka nikae peke yangu tu, yaani niishi dunia ya peke yangu.
Nimepitia mambo makubwa sana maishani mwangu mpaka mwenyewe ikafika mahali nikaamini kweli mimi ni kichaa niliyechanganyikiwa na akili zangu zinafanya kazi tofauti na binadamu wengine. Ndiyo! Kila anayenijua, kila aliyewahi kupata nafasi ya kukaa na mimi jirani anaamini kwamba mimi ni kichaa lakini mwenyewe najua kabisa kwamba sijachanganyikiwa, sina tatizo la kiakili lakini kuna jambo halipo sawa kwenye maisha yangu, tofauti kabisa na binadamu wengine. Lilianza kama masihara lakini sasa limefikia mahali ambapo linaonekana kunizidi uwezo! 
Linaonekana kuwa kubwa kuliko mimi, kubwa kuliko akili za kibinadamu, hakuna daktari yeyote, mchungaji, shehe wala mganga wa kienyeji anayeweza kutoa majibu ya nini hasa kinachoendelea kwenye maisha yangu! Wote wameshindwa na kwa kukosa kwao majibu, wameishia kutoa majibu kwamba nimechanganyikiwa, jambo ambalo mwenyewe nalipinga mno.
Nalala mitaani, wakati mwingine kwenye mazingira ya hatari sana, si kwa sababu kwetu tuna shida sana, la hasha! Nakula vyakula vichafu si kwa sababu wazazi wangu hawawezi kunihudumia! Wanaoijua historia ya familia yetu huwa hawapati majibu kwa sababu ukweli ni kwamba natokea kwenye moja ya familia zenye uwezo mkubwa sana kifedha. Nitalifafanua hili baadaye.
Napata shida kwa sababu mimi mwenyewe nimeamua kuutafuta ukweli wa maisha yangu, kwa hiyari yangu nimeamua kujitenganisha na huu ulimwengu wa kawaida kwa sababu najiona kuwa ‘si-fit’ kuishi na binadamu wengine, najihisi kwamba pengine nipo hapa duniani kimakosa lakini nilitakiwa nikaishi sehemu nyingine tofauti kabisa.
Binadamu wa kawaida wanashindwa kuelewa kile ninachokisema, wanashindwa kufikiri kama ninavyofikiri, wanashindwa kusadiki kila ninachowaambia, wanaishia kuniona kuwa mwendawazimu kwa hiyo kama nilivyosema awali, nimeamua kuutafuta ukweli mwenyewe.
Kichwa changu kinaniambia kwamba nipo karibu sana kuujua ukweli, ipo siku nitajua ni nini hasa kinachoendelea kwenye kichwa changu, na pengine kupitia mimi dunia itapata majibu ya maswali ambayo hayakuwahi kuwepo.
Mvua imepungua sasa na bado nazidi kutembea, kama nilivyosema, sielewi naelekea wapi lakini sitaki kukaa sehemu moja, sitaki kutulia kwa sababu akili yangu inapopata muda wa kutulia tu, ndipo hapo inapoanza kuchemka na kunisababishia hali ambayo hata sijui niielezee vipi.
Kuanzia kulipopambazuka, nimetembea umbali mrefu kwa sababu nakumbuka nililala jirani na machinjio ya Vingunguti lakini saa kumi na mbili jioni tayari nipo Mtongani, Kunduchi na bado naendelea kutembea tu! Kwa wenyeji wa Dar es Salaam watakuwa wanaelewa kuna umbali gani kati ya sehemu hizo mbili lakini kwa kifupi ni umbali usiopungua kilometa kama kumi na tano hivi.
Sijapanda gari wala kutumia usafiri wa aina yoyote, natembea tu mwenyewe kwa miguu, wala sina haraka kwa sababu hata sijui nakwenda wapi kufanya nini.
Jua linapoanza kuzama, najikuta tayari nimefika ufukweni mwa bahari, kwa makadirio yangu nadhani nipo kwenye Ufukwe wa Bahari ya Hindi, Kunduchi jijini Dar kwa sababu nakumbuka nilipofika Mtongani Kona, nilikata kona upande wa kulia na kuifuata barabara ya lami inayoelekea kwenye Hoteli ya Kunduchi Wet & Wild lakini nilipofika kwenye lango kuu la kuingilia kwenye hoteli hiyo, nilipinda kushoto na kuendelea kutembea.
Kama ilivyokuwa tangu alfajiri nilipoamka, kila aliyekuwa akiniona alikuwa akiamini mimi ni mwendawazimu, wengine walikuwa wakinikwepa kabisa wakihofia huenda naweza kuwadhuru endapo nikiwakaribia, watoto wasio na adabu walikuwa wakiniimbia nyimbo za kuudhi lakini kwa sababu nilishajiapiza kutomdhuru mtu yeyote bila sababu, nimekuwa na kawaida ya kuwaacha wafurahi wenyewe.
Najihisi mwili umechoka sana, naona njia nzuri ni kujilaza chini, juu ya mchanga wa bahari na hapo ndipo ninapogundua kwamba kumbe miguu yangu imevimba sana, nadhani ni kwa sababu ya kutembea umbali mrefu bila kupumzika. 
Haya yamekuwa maisha yangu kwa takribani miezi saba sasa, leo nikilala upande mmoja wa Jiji la Dar es Salaam, basi kesho nitalala sehemu nyingine tofauti kabisa. Kwa jinsi mwonekano wangu ulivyo, ni vigumu sana kwa watu waliokuwa wakinifahamu, kunitambua kwa urahisi, nimebadilika na mwenyewe nafurahia sana hali hii kwa sababu sasa hakuna anayeweza kunisumbua ingawa najua ndugu zangu wananitafuta sana.
Nikiwa nimejilaza kwenye mchanga, miguu yangu ikiendelea ‘kupwita’ na kunisababishia maumivu makali, naanza kujihisi kama usingizi mzito ukininyemelea! Ndiyo, lazima nichoke, nani anaweza kushinda kutwa nzima akipuyanga, jua na mvua vikiwa ni sehemu ya maisha yake?
“Hivi nitaendelea kuwa hivi mpaka lini? Kwa nini majibu hayapatikani haraka? Nifanye nini niupate ukweli?” najiuliza lakini kabla hata sijapata majibu, kichwa changu kinazidi kuzongwa na usingizi mzito, sioni sababu ya kuendelea kuumiza kichwa changu, nauacha mwili na akili vipumzike ingawa sina uhakika kama nitalipata pumziko ninalolihitaji.
Muda unayoyoma, licha ya macho yangu kuwa mazito kwa usingizi lakini silali, nazidi kuusikia mwili wangu ukizidi kuniuma kila sehemu, upepo wa bahari nao unazidi kupiga na kunifanya nijisikie ahueni kidogo, huku mwanga hafifu wa jua la Magharibi ukizidi kumezwa na kigiza cha jioni kilichoanza kutanda.
Kwa mbali naanza kusikia vishindo, si vishindo vya binadamu, la hasha! Nahisi ni vya mnyama mwenye miguu minne, natamani niinuke kutazama ni mnyama gani kwani inaonesha kama anakimbia lakini mwili unakuwa mzito.
Naamua kuendelea kujilaza, vishindo vinazidi kusogea na sasa vinasikika mita chache tu kutoka pale nilipojilaza, naamua kuushinda usingizi na kuyafumbua macho yangu, napigwa na butwaa na ninachokiona mbele ya macho yangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...