Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 54


ILIPOISHIA:
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza totoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
SASA ENDELEA...
“Poooh! Pooh!” honi kali ya treni ilisikika ikifuatiwa na msuguano mkali wa vyuma, nikaona watu wote waliokuwa mle ndani ya treni la ajabu wakirushwa upande wa mbele. Nilijishikilia kwa nguvu, treni likajisugua juu ya reli na kusababisha cheche nyingi ziruke, eneo lote likawa kama karakana ya kutengenezea vifaa vya chuma.
Treni liliposimama, nilishtukia nimeshashuka, hata sikumbuki nilipitia mlango gani, macho yangu yakatua kwenye kitu kilichosababisha treni hiyo ifunge breki za ghafla kiasi kile. Msichana mmoja, aliyekuwa na macho yanayong’ara kama paka awapo gizani, nywele ndefu zilizokosa matunzo na kucha kama mnyama wa porini alikuwa amekaa katikati ya reli huku akinguruma kama mnyama wa kutisha.
Sijui nilipata wapi ujasiri wa kumsogelea, kadiri nilivyokuwa nasogea mbele ndivyo msichana yule alivyozidi kutoa mlio wa kunguruma na kusababisha nipatwe na hofu kubwa mwilini. Lakini cha ajabu, eti muda huohuo nilikuwa nasikia sauti ya Junaitha ikiniambia napaswa kuishinda hofu yangu, nikazidi kumsogelea.

Kwa msaada wa taa moja kubwa iliyokuwa mbele ya lile treni, kufumba na kufumbua, nilishangaa yule niliyekuwa namuona kama msichana akibadilika na kuwa jibwa lenye meno na kucha ndefu, likaanza kubweka kwa nguvu huku likitokwa na mate mengi mdomoni.
Kiukweli nafsi yangu ilielemewa na hofu lakini eti cha ajabu sauti ya Junaitha ikawa inaendelea kusikika ndani ya moyo wangu ikiniambia sipaswi kuogopa chochote, nikapiga hatua moja mbele na sasa tukawa tumekaribiana sana na jibwa hilo ambalo lilikuwa likiendelea kubweka kwa hasira lakini lilipoona sishtuki, liligeuka na kuanza kutimua mbio huku likiendelea kubweka.
Nikasikia sauti ikiniambia nianze kulifukuza jibwa lile, bila hata kuuliza nikaanza kukimbia kuelekea kule lilikokimbilia, huku nyuma nikasikia lile treni likianza kunguruma tena kwa kasi, moshi mwingi ukatanda eneo lote kisha likaanza kuondoka.
Nilifunga breki za ghafla na kugeuka nyuma, nilishindwa kuelewa kama lile treni linaondoka mimi nitaondokaje kwenye mazingira yale ambayo kwanza sikuwa najua ni wapi halafu yalikuwa yakitisha sana?
“Mkimbize Jamal, utakosa vyote,” ilisikika sauti ya Junaitha, nikaachana na treni hilo na kuanza kutimua mbio, lile jibwa lilikuwa likikimbia na kufika mbali kidogo, linasimama na kugeuka kunitazama, likawa linaendelea kubweka kwa nguvu na likiniona nakuja, linaanza tena kukimbia.
Japokuwa kulikuwa na giza nene, niliweza kuyatambua mazingira hayo kuwa ilikuwa ni katikati ya msitu mkubwa wenye miti iliyofungana kwani hata nilipojaribu kutazama juu, sikuona mwezi wala nyota, kila sehemu kulikuwa na giza. Kilichosaidia niweze kuelewa jibwa lile lilikokimbilia, ilikuwa ni mwanga wa macho ya lile jibwa, ambayo sasa yalikuwa yaking’aa sana.
Niliendelea kukimbia, mara nikajikuta nimetokezea sehemu iliyokuwa na majimaji, nikawa kila nikipiga hatua nakanyaga kwenye matope, sikupunguza mwendo, niliendelea kutimua mbio, nikawa najikwaa kwenye visiki, wakati mwingine nakanyaga miiba lakini sikuchoka, mara tukatokezea kwenye sehemu ambayo hakukuwa na giza kama kule tulikotoka.
Giza lake lilikuwa ni kama katikati ya usiku wa manane na mapambazuko, kwamba kunakuwa na giza lakini siyo totoro na kwa mbali kuna mwanga unaonekana. Hali hiyo ilifanya niweze kuona vizuri mazingira yote, nikawa pia na uwezo wa kuliona vizuri jibwa lile ambalo liliendelea kutimua mbio huku likibweka kwa hasira.
“Huyo siyo mbwa, ni binadamu, mganga wa baba yake Shenaiza, anajua siri nyingi sana kumhusu na ndiye atakayetusaidia kuiona nafsi ya Shenaiza ilikofungiwa, jitahidi uishike ile kamba yake ya shingoni, usijali hata kama litakurarua,” sauti ya Junaitha ilisikika tena ingawa sikuwa na uwezo wa kumuona. Kauli hiyo ilinitisha sana, nikaanza kuamini kwamba kumbe zile stori nilizokuwa nazisikia tangu kitambo, kwamba kuna binadamu wanaoweza kubadilika na kuwa mbwa, zilikuwa za kweli.
Nilipiga moyo konde, nikaongeza mwendo na hatimaye nikawa nimelikaribia kabisa lile jibwa ambalo sasa lilipoona naelekea kulizidi mbio, liligeuka kwa hasira na kutaka kunirukia, likiwa limetoa makucha yake. Nilifanya kama nilivyoagizwa na ile sauti, mkono mmoja nikautumia kuibana miguu yake ya mbele iliyokuwa na nguvu kubwa, likadondoka chini kama mzigo.
Kwa bahati mbaya sikuweza kuidhibiti miguu ya nyuma, likaitumia kunirarua mapajani mwangu ambapo kama isingekuwa uzito wa ile nguo niliyokuwa nimevaa, huenda lingenijeruhi zaidi ya vile.
Japokuwa nilisikia maumivu makali, sikujali, nikalishika shingoni ambapo lilikuwa limefungwa kwa kamba iliyokuwa na mafundofundo kadhaa.
“Unaniuaaaa, nisamehe unaniuaaa,” nilishangaa mno kuona jibwa lile likibadilika na kuwa mtu ambaye alianza kupiga kelele akiniomba msamaha. Bado nilijihisi kama nipo ndotoni, nikawa nimekodoa macho nikiwa ni kama siamini.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilishangaa Junaitha naye akidondoka kutoka kusikojulikana kama mzigo, harakaharaka akainuka na kujikung’uta, akasogea pale nilipokuwa nimelikaba lile jibwa ambalo sasa lilibadilika na kuwa mwanamke, tena mzee tofauti na msichana ambaye nilimuona pale treni liliposimama ghafla.
“Nilikwambia nitakupata tu ukabisha, sasa yako wapi?” nilimsikia Junaitha akisema wakati akinisaidia kumfunga mwanamke yule ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akifurukuta. Nilishangaa kugundua kwamba kumbe Junaitha alikuwa akifahamiana na yule mtu wa maajabu.
Nikawa najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, Junaitha alipomaliza kumfunga mikono kwa kutumia kamba za miti, alihamia miguuni. Akamfunga na kumgeuza, akamburuza na kumkalisha akiwa ameegamia kisiki cha mti.
“Unaona ulivyomuumiza? Haya nataka umtibu sasa hivi, vinginevyo nitakufunza adabu,” alisema Junaitha kwa hasira huku akimshika nywele na kumtingisha, kwa msaada wa mwanga hafifu nikawa namshangaa yule mwanamke jinsi alivyoumbwa usoni.
Alikuwa na masikio makubwa, pua nene ya duara na meno yaliyochongoka pembeni. Ama kwa hakika alikuwa akitisha. Baada ya Junaitha kumwambia vile, huku akitetemeka alitoa ishara kwamba nifunue lile eneo alilokuwa amenijeruhi, akatoa ulimi wake na kunipa ishara kwamba nisogeze majeraha yangu anilambe, jambo ambalo nilisita.
“Sogea tu hawezi kukufanya chochote, si unaona nimeshamvua kamba yake ya shingoni,” alisema Junaitha huku akinionesha kamba iliyokuwa na mafundo kadhaa aliyokuwa ameishika mkononi. Nikasogeza mapaja yangu ambapo alitoa ulimi wake mrefu na kuanza kunilamba damu zilizokuwa zinachuruzika.
Ulimi wake ulikuwa mgumu na unaokwangua kama wa mnyama mkali, nikashangaa maumivu niliyokuwa nikiyasikia yakiyeyuka ghafla, Junaitha akanihakikishia kwamba nitapona baada ya muda mfupi, nikawa bado nimepigwa na butwaa.
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu.
Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment