Friday, November 17, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 50


ILIPOISHIA:
Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.
SASA ENDELEA...
“Inabidi uvue nguo zote na kukimbia kuelekea upande wa Magharibi mpaka uvuke barabara ya lami kisha kimbia mpaka utakapoukuta mti mkubwa wa mbuyu, uzunguke mara saba kisha fumba macho, usifumbue mpaka nitakapokwambia,” sauti ya baba ilisikika masikioni mwangu.
Yaani nivue nguo zote na kuanza kukimbia nikiwa mtupu? Kibaya zaidi, upande huo wa Magharibi aliokuwa anausema ilikuwa ni kulekule nilikokuwa nakimbia. Kwa lugha nyepesi nilitakiwa kuanza upya kukimbia kurudi kule nilikotoka, safari hii nikiwa mtupu! Ilikuwa ni zaidi ya mtihani.
Kitu pekee nilichokuwa nakihitaji, ilikuwa ni kuokoa na balaa hilo kwani kwa jinsi wale wazee waliokuwa wakinikimbiza walivyokuwa na hasira, kama wangenitia mikononi mwao sijui nini kingetokea. Ilibidi nipige moyo konde, harakaharaka nikavua nguo zote na viatu, nikavikunja na kuvitia kwapani.

Mpaka namaliza, lile kundi lilikuwa limenikaribia sana, kitu pekee ambacho nilikuwa nacho makini, ilikuwa ni kuifunga vizuri ile hirizi yangu mkononi, nikaanza kukimbia kulifuata lile kundi huku nikiwa na hofu kubwa mno moyoni.
Cha ajabu, japokuwa nilikuwa nikikimbia kuelekea kule walikokuwa wanatokea, tena nikiwa mtupu kabisa, ilionesha dhahiri kwamba hakuna aliyekuwa akiniona kwani waliendelea kuangaza macho huku na kule huku wakiendelea kukimbia. Nikawafikia na kupishana nao katika namna ambayo nilikuwa makini kuhakikisha simgusi yeyote wala wao hawanigusi kama baba alivyonieleza.
“Hebu simameni kwanza, mbona nywele zinanisisimka hivi?” mmoja kati ya wale wazee. Nadhani yeye alihisi uwepo wangu mahali hapo, wote wakafunga breki na kusimama, wakawa wanatazama huku na kule lakini walishachelewa kwani nilizidi kutimua mbio kama kiberenge.
Nikakwepa kidogo pale kwenye msiba na kupita pembenipembeni kwa kasi kubwa, kizaazaa kikawa kuvuka barabara ya lami. Ikumbukwe kwamba kote huko nilikokuwa napita, japokuwa ilikuwani asubuhi na kulikuwa na watu, ilionesha dhahiri kwamba hakuna aliyekuwa akiniona ingawa mimi nilikuwa nawaona vizuri.
Nilipofika barabarani, kuna pikipiki ilikuwa ikitokea upande wa Morogoro, sikuiona mapema, ile nimeshaingia barabarani ndiyo nikaishtukia ikiwa inakuja kwa kasi kubwa, nikajua kama nisipokuwa makini, inaweza kunigonga na kwa kasi iliyokuw anayo, sijui nini kingetokea.
Nilichokifanya, nilijirusha juu, nikashangaa mwili umekuwa mwepesi sana, nikamruka yule dereva na bodaboda yake lakini kwa bahati mbaya, mguu mmoja nilimgonga kichwani, nikaenda kuangukia ng’ambo ya pili ya barabara na kuinuka haraka, nikataka niendelee kutimua mbio lakini ghafla nilishtushwa na kishindo kizito barabarani.
Ilibidi nijiibe na kugeuza kidogo shingo kwa sababu miongoni mwa masharti niliyoelekezwa na baba, ni mwiko kugeuka nyumaunapokuwa kwenye shughuli zinazotumia nguvu za giza. Nilimshuhudia yule dereva wa bodaboda akiwa ameanguka katikati ya barabara na kujibamiza kwa nguvu.
Nilishtuka sana, nikajua kwa vyovyote mimi ndiyo nimesababisha kwa sababu hata kama yeye hakuwa ameniona, mimi nilimuona na ndiyo maana nilimkwepa lakini kwa bahati mbaya, nikamgonga kichwani. Kilichonitisha zaidi, ni kasi aliyokuwa nayo na uzito wa kishindo chenyewe, nikajua tayari mambo yameshaharibika.
“Mungu wangui, hawezi kupona yule,” nilisikia sauti za mmoja kati ya waombolezaji waliokuwa pale kwenye msiba kwa sababu tukio hilo lilikuwa limetokea mita chache tu pembeni, hasa ukizingatia nilishaeleza kwamba nyumba yenye msiba ilikuwa karibu na barabarani.
Waombolezaji wengi walikimbilia eneo la tukio kujaribu kutoa msaada lakini wengi walisikika wakisema kwa jinsi alivyokula mzinga hawezi kupona. Nilitamani kwenda kushuhudia kilichotokea lakini kwa sababu na mimi nilikuwa na majanga yangu, niliendelea kukimbia. Nilikimbia sana, miba mikali ikinichoma miguuni lakini sikujali.
Mbele kabisa nikauona mbuyu mkubwa kama baba alivyonielekeza, nikaendelea kukimbia mpaka nilipoufikia, nikaanza kukimbia kuuzunguka kutokea upande wa kushoto kuelekea kulia. Nilipofikisha raundi ya saba, nilisikia kizunguzungu kikali, nikadondoka chini kisha nikaona kama giza nene likitanda kwenye upeo wa macho yangu, sikuelewa tena kilichoendelea.
“Wewe Togo, hebu amka,” sauti ya chini ya baba iliyoambatana na teke zito ubavuni ndiyo iliyonizindua kwenye usingizi wa kifo, nikafumbua macho na kushtuka nikiwa nyuma ya nyuma ya akina Rahma, tena nikiwa uchi wa mnyama.
“Vaa nguo haraka, unajifanya mjuaji sana wewe, siku nyingine sikusaidii, pumbavu,” alisema baba huku akiniongezea teke lingine la ubavuni lililosababisha nijisikie maumivu makali.
Niliijizoazoa huku nikijiziba sehemu za mbele kwa mikono yangu, nikaokota nguo zangu zilizokuwa pembeni na kuanza kuvaa huku nikijiuliza nimefikaje nyumbani bila kupata majibu.
“Sijui kwa nini nimeenda kukuandikisha mtu mjinga kama wewe,” alisema baba kwa hasira huku akinishika masikio yangu mawili na kuyavuta kwa nguvu, akiwa ni kama anataka kuninyanyua juu, akanisindikizia na kofi zito lililosababisha nishindwe kujizua, machozi yakawa yananitoka.
Zilikuwa zimepita siku nyingi sana bila baba kunipiga lakini naona siku hiyo nilikuwa nimemuudhi sana, nikawa nahisi kama masikio yangu yananyofoka kwa jinsi alivyoyavuta kwa nguvu, na ule upande alionizabua kofi nao nikawa nahisi kama unawaka moto.
“Chumbani moja kwa moja na ole wako utoke,” alisema baba kwa hasira, nikatembea harakaharaka huku machozi yakinitoka, uso wangu nikiwa nimeuinamisha. Ile naingia tu mlangoni niligongana na Rahma lakini kwa kuwa nilikuwa nalia na akili ilikuwa na mawenge, sikukumbuka hata kumsalimu, nikatembea harakaharaka huku nikichechemea kwani miguu ilikuwa na miba ya kutosha na sikuwa nimepata hata muda wa kuitoa.
Niliingia chumbani na kujilaza kitandani nikiwa bado najiuliza nimefikaje eneo hilo, nikalia kwanza kupunguza hasira zangu kisha nikaanza kutafakari kwa kina mlolongo wa kila kitu kilichotokea. Yaani ndani ya saa chache tu kulikuwa kumetokea matukio mengi mno ya kutisha, ya kuhuzunisha, ya kushangaza na kuchanganya kichwa.
Bado moyo wangu ulikuwa na huzuni kubwa kutokana na hali niliyoiona kule msibani, na japokuwa malengo yangu ya kwenda Hospitali ya Tumbi kuona hiyo maiti ya yule mtoto hayakuwa yamekamilika, bado nilikuwana shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea. Lakini ni hapo pia nilipokumbuka ile ajali nyingine ya bodaboda niliyoisababisha na pia nikakumbuka kisanga cha dereva wa Bajaj aliyekuwa akipaki jirani na hapo kwa akina Rahma na jinsi nilivyomkomesha asubuhi hiyo. Sikujua kama amesharudi au la na sikujua siku atakaponiona tena atasema nini.
Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo, nilisikia mlango ukifunguliwa, Rahma akaingiza kichwa na kuchungulia ndani, macho yangu na yake yakagongana.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...