Tuesday, October 24, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 47


ILIPOISHIA:
“Broo vipi unaenda?” alisema huku akisimamisha Bajaj yake jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama, nadhani kwa sababu ya kigiza kile cha alfajiri hakuwa ameniona vizuri, aliniponisemesha na mimi kumtazama usoni, niliona jinsi alivyoshtuka, akataka kuondoa Bajaj yake haraka lakini alishachelewa.
SASA ENDELEA...
Nilishika bomba la Bajaj yake na kuingia, nikakaa siti ya nyuma, akawa ni kama amepagawa maana hakujua kama akimbie na Bajaj au aiache akimbie kwa miguu.
“Simama kwa usalama wako,” niliongea kwa sauti ya mamlaka, nikamuona jinsi alivyokuwa akihangaika, kijasho chembamba. Hakuwa tayari kusimama, inaonesha alikuwa akiniogopa sana, nilichoamua kukifanya ilikuwa ni kumtumia kutimiza mahitaji yangu.
Nilivuta pumzi ndefu na kuzibana kama baba alivyonielekeza, nikaweka utulivu kidogo kisha nikamuamrisha kunipeleka Ubungo. Nilifanya hivyo kwa kuzungumza moyoni maana ndivyo nilivyoelekezwa, nikamuona akizidi kuichochea Bajaj yake.
Hata hivyo, njia aliyokuwa anapita, ilikuwa ni ileile tuliyoipita jana wake wakati tukielekea Ubungo kupanda magari ya kwenda Kibaha. Alizidi kuongeza kasi, akawa anakimbia kama mshale, mwenyewe alidhani ananikimbia lakini kumbe tayari nilishaingia ndani ya akili yake.
Huwa si kawaida ya Bajaj kukimbia spidi kubwa na kuyapita magari lakini siku hiyo iliwezekana. Baada ya dakika kadhaa za kukimbia kwa kasi kubwa kwenye lami, hatimaye tuliwasili Ubungo, nikavuta tena pumzi na kumpa amri ya kusimama kwenye kituo cha mafuta.

Kilichonishangaza hata mimi, kweli alipunguza mwendo bila mimi kusema kitu chochote, akaiacha barabara kubwa ya lami na kuingia kwenye kituo cha mafuta, nikapeleka mkono wangu kwenye ile hirizi niliyokuwa nimevaa mkononi, nikanuiza maneno kwamba sitaki kuonekana.
“Jamani msaada! Nisaidieni washkajiii,” nilishangaa yule dereva Bajaj akipaza sauti, akazima Bajaj na kushuka huku akikimbia, akaenda kujichanganya na madereva Bajaj wenzake wanaopaki Ubungo, akawa ni kama anawaelekeza kitu fulani huku akihema kwa nguvu.
Sikutaka kupoteza muda, kwa sababu nilishakuwa na uhakika kwamba hakuna mtu anayeniona baada ya kufuata maelezo yale niliyofundishwa, niliteremka kwenye Bajaj na kusimama pembeni nikitaka kuona nini kitatokea.
Vijana kama kumi hivi waliongozana naye mpaka pale kweye Bajaj kuja kujionea kuna nini kimetokea.
“Yuko wapi?”
“Alikuwa amekaa siti ya nyuma.”
“Siti gani ya nyuma?”
“Hee! Au ameshuka nini?”
“Nani ameshuka? Mbona sisi muda wote tunakuangalia tangu umefika na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada hatujaona mtu yeyot akiteremka kwenye Bajaj?” alisema kijana mwingine ambaye alikuwa amesimama jirani kabisa na pale mimi nilipokuwa nimesimama.
Mjadala mkali ukazuka, yule dereva Bajaj akikazania kwamba ni kweli kuna mtu alikuwa amembeba kwenye Bajaj yake na alikuwa akitaka kumuua, wenzake wakawa wanamshikia bango amuoneshe huyo mtu.
“Hizo bangi mnazovuta bila kula ndiyo matatizo yake haya!” alisema dereva mwingine na kusababisha wenzake wacheke, wakaanza kutawanyika huku kila mmoja akionesha kumpuuzia. Nilikuwa na uhakika kwamba hakuna mtu yeyote aliyeniona na ndiyo maana hata pale nilipokuwa nimesimama, watu walikuwa wakinipita tu bila kuonesha dalili yoyote kwamba wameniona.
Nilishangazwa sana na kilalichokifanya yule dereva Bajaj, kwa tafsiri nyepesi, kama kweli wale watu wangenikuta kwenye Bajaj ile, nini kingetokea? Bila shaka wangenidhuru wakiamini mimi ni mhalifu, nikaamua kumkomesha zaidi.
Nilisubiri aingie kwenye Bajaj yake, akaiwasha huku mara kwa mara akigeuka nyuma, na mimi nikaingia lakini nikiwa bado nimeishika ile hirizi ya mkononi, kwa hiyo nikawa sionekani. Alipotoka na kuingia barabarani tu, niliachia ile hirizi, akageuka na kushtuka kuona nimekaa palepale kwenye siti ya nyuma, akaanza kuchachawa.
Nilivuta pumzi ndefu na kuzishikilia kisha nikamuamuru kunipeleka Kibaha, nikashangaa akikata kona kali katikati ya barabara, magari mengine yakawa yanapiga honi kwa nguvu an kufunga breki, akavuka kwenye taa za kuongozea magari kwa kasi kubwa, almanusura tugongwe na magari yaliyokuwa yameruhusiwa na taa. Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa kwa jinsi Bajaj ilivyovuka kwenye taa zile, akawa anakimbia kwa kasi kubwa kuliko kawaida. Kila alipokuwa akigeuka na kuniona nimetulia kwenye ile siti, ndivyo alivyokuwa akizidi kuongeza kasi.
Ikafika mahali Bajaj ikaisha mafuta, nilichoamua ilikuwa ni kumtesa tu, akapaki Bajaj yake pembeni ya barabara, mimi nikashika ile hirizi yangu, nikawa sionekani tena, akashuka na kwenda kusimama mbali kabisa, akionesha dhahiri kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
Niliamua kushuka kwenye Bajaj yake lakini nikajiapiza kwamba bado hatujamalizana, nilitembea kwenda mbele kidogo kwenye kituo cha daladala, tayari kulishaanza kupambazuka. Nikaiachia ile hirizi yangu, nikajichanganya na abiria wengine. Muda mfupi baadaye, gari lilikuja, nikawa wa kwanza kupanda, abiria wengine nao wakapanda.
Tukiwa ndani ya gari safari ikiendelea, mjadala kuhusu ajali iliyotokea usiku, ambayo ndiyo hasa iliyonifanya nifunge safari ile bila kumwambia mtu yeyote ilianza. Abiria mmoja aliamnza kusimua kwamba usiku yeye alikuwa akisafiri kutoka Mlandizi kuelekea jijini Dar es Salaam alipokuta ajali hiyo mbaya na ya kutisha, akaendelea kueleza kwamba aliyepata ajali alikuwa jirani yake, Mlandizi.
Mpaka hapo nilishapata sehemu ya kuanzia kwa sababu nilitaka nifike eneo la ajali lakini pia niende mpaka msibani nikajionee hali halisi. Alieleza jinsi ajali yemnyewe ilivyokuwa ya kutatanisha hukuakieleza kwamba mtoto alikufa palepale huku maiti yake ikiharibika vibaya kiasi cha kutotambulika na mama yake alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Tumbi, hali yake ikiwa mbaya.
Nilizidi kupata taarifa nyingi zaidi, lakini moyoni nikawa najiuliza hiyomaiti wanayosemaimeharibika vibaya ni ipi wakati nakumbuka mimi ndiye niliyeenda kuweka mgomba pale kwenye siti aliyokuwa amekaa yulemtoto na kuweka kipande cha mgomba?
Mjadala uliendelea, kila mtu akawa anasema lake lakini kikubwa walichokuwa wakikizungumza wengi, ni kwamba eneo ilipotokea ajali hiyo limekuwa na mauzauza mengi katika siku za karibuni, kwani hakuna mlima, mteremko wala korongo lakini magari yanap[ata ajali za kustaajabisha.
“Naskia kuna mtumishi wa Mungu kutoka Nigeria anakuja wiki ijayo na atafika pale kufanya maombi,” alisema dereva, abiria wote wakawa wanaunga mkono hoja hiyo. Nilichopanga kichwani, ni kuchukua maelekezo vizuri kwa yule mtu aliyesema marehemu ni jirani yake kisha kwenda kwanza mpaka eneo la ajali na baada ya hapo, nitakwenda Tumbi kujionea hali ya mgonjwa na hiyo maiti kama nitapata nafasi. Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua kila kitu maana moyo wangu ulikuwa na hatia kugbwa, hasa kutokana na jinsi taarifa za ajali ile zilivyowaumiza mioyo abiria wengi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...