Tuesday, October 24, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 45


ILIPOISHIA:
Nguo maalum aliyofunikwa upande wa kichwani, ilifanya iwe vigumu kwa mtu yeyote kumtambua, tukaendelea kusonga mbele mpaka tulipofika kwenye geti la kutokea nje ya hospitali, hapo tukakumbana na kipingamizi ambacho hakuna aliyekitegemea, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
SASA ENDELEA...
“Haroo! Mnaenda wapi usiku? Harafu hao wagonjwa mbona mumewafunika sura, wafunueni, hima,” alisema askari aliyekuwa amevalia sare maalum, mkononi akiwa ameshika bunduki. Ilibidi Shamila atumie mbinu ya ziada kumtuliza kwani tayari alishaonesha wasiwasi nao.
“Kamanda, ina maana hata mimi hunijui? Hiki hapa ni kitambulisho changu, naitwa Shamila, nawapeleka wagonjwa wangu hapo kwenye maabara za Lancet hapo nje kwenye kipimo cha MRI, si unajua humu ndani hakuna na isitoshe kesho asubuhi kutakuwa na foleni kubwa sana,” alisema Shamila kwa lafudhi laini ambayo ilimfanya yule mlinzi awe anamtazama tu usoni.
“Ooh! Nesi Shamira, kumbe ni wewe, basi wapereke ila ukitoka basi uje hapa nina mazungumzo na wewe kidogo sawa nesi,” alisema mlinzi huyo kwa lafudhi ambayo ilionesha dhahiri kwamba ni Mkurya, kwa kutambua udhaifu wake, Shamila alimbania kijicho kimoja, akawa anachekacheka mwenyewe na kwenda kufungua geti.

Nilimsifu sana Shamila kwa sababu aliutumia vizuri uzuri wa sura na umbo lake, kama asingewahi kumkabili mlinzi yule, ni dhahiri lazima angekuja kunifunua usoni na angeenda kumfunua pia Shenaiza na hapo picha ingeungua, lazima tungeishia pabaya.
Kweli alifungua geti, Shamila na Raya wakaendelea kusukuma vitanda vile vya magurudumu huku kila mmoja kijasho chembamba kikimtoka, hakuna aliyemsemesha mwenzake mpaka tulipozamia gizani, Shamila ndiye aliyevunja ukimya kwa kumuelekeza Raya mahali gari lilipokuwa.
Kwa kuwa tayari tulishafika mbali, ilibidi nijifunue usoni, kwa mbali nikawa naliona gari jeusi, Toyota Noah likiwa limepaki pembeni ya barabara, niligeuka nyuma na kutazama kule tulikotoka, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akitufuatilia.
Niliona kama Raya ananichelewesha, nilisimama kwenye kile kiti cha magurudumu na kuanza kutembea mwenyewe, jambo lililoonesha kumchukiza Shamila, hakusema kitu lakini uso wake tu ulionesha hivyo, nikajikaza kiume na kutembea mpaka lile gari lilipokuwa limepaki.
Tulipofika tu, mdogo wake Shenaiza, Firyaal alishuka na kuja kutufungulia mlango, nikawa wa kwanza kuingia. Nilitegemea nitamkuta mtu mwingine mle ndani ya gari kwani bado sikuwa naamini kwamba Firyaal anaweza kuendesha gari peke yake, kutoka nyumbani kwao, Kurasini.
Hata hivyo, hakukuwa na mtu mwingine yeyote ndani ya gari, wote tukaingia, Shamila akakaa siti ya mbele pamoja na Firyaal ambaye ndiye aliyekuwa nyuma ya usukani, safari ikaanza. Sikuamini jinsi Firyaal alivyokuwa na ‘control’ ya gari kwani alilitoa pale alipokuwa amepaki kwa spidi kubwa na kulingiza barabarani, akakanyaga mafuta na kulifanya liwe linakimbia kwa kasi kubwa.
Mbele kidogo alikata kona kali na kuzidi kukanyaga mafuta, tukaingia Barabara ya Umoja wa Mataifa ambako aliendelea kukanyaga mafuta kwa nguvu, gari likawa linakimbia kama tupo kwenye mashindano. Nadhani alikuwa na wasiwasi kwamba huenda kuna watu wanatufuatilia kwa nyuma.
Safari iliendelea, Shamila akawa anamuelekeza njia ya kupita kuelekea nyumbani kwake. Kitu ambacho sikukishtukia kuanzia mwanzo, kumbe wakati Firyaal akiendesha gari, mara kwa mara alikuwa akinitazama kupitia kioo cha juu ya dereva (driving mirror). Hata sijui kwa nini alikuwa akinitazama sana.
Safari iliendelea huku Raya akiwa kimya kabisa pembeni yangu, Shenaiza yeye akiwa amelazwa kwenye siti ya nyuma, akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea. Hatimaye tulifika salama nyumbani kwa Shamila, akashuka na kwenda kufungua geti, Firyaal akaliingiza gari kinyumenyume mpaka ndani.
Nilimvulia kofia msichana huyo, japokuwa alikuwa akionekana kama mdogo, ilionesha na ujuzi wa vitu vingi sana ndani ya kichwa chake. Baada ya kuingiza gari, nilishuka, akafuatia Raya, ndani ya gari akawa amebaki Shenaiza. Ilibidi watatu hao wasaidiane kumshusha kwani mimi nilikuwa nikihofia kujitonesha tena kidonda changu.
Wakamshusha na kumuingiza mpaka ndani, wakampeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha wageni, mimi nikakaa pale sebuleni huku nikiangaza macho huku na kule. Nilitaka kujiaminisha kwamba hapo ndani palikuwa salama kama nilivyopaacha.
Muda mfupi baadaye, walitoka chumbani, wakaja mpaka pale sebuleni.
“Kumbe wewe ni dereva mzuri?” nilimuuliza Firyaal, akacheka kwa aibu na kujiinamia chini, wote tukatulia.
“Sasa hapa ndiyo patakuwa ‘safe house’ yetu, mipango yote itapangwa kutokea hapa lakini cha msingi ni kuhakikisha hakuna anayejua kama mpo hapa na njia pekee itakayofanya iwezekane ni kila mmoja kuwa makini. Hata ukibanwa vipi kamwe usije kusema chochote Firyaal, umenielewa,” alisema Shamila, msichana yule akaitikia kwa kutingisha kichwa kisha akanitazama, macho yetu yakagongana kisha haraka akayakwepesha.
Bado sikuwa nimeelewa sababu ya msichana huyo kuwa ananitazama mara kwa mara, hata hivyo sikuwa na haraka, nilijiambia mwenyewe moyoni kwamba ‘nitajua tu’. Shamila alimuonesha ishara Raya kwamba amfuate, wakaelekea jikoni nadhani kwa lengo la kwenda kuandaa chakula maana jioni sikuwa nimekula chochote, pale sebuleni tukabaki na Firyaal.
“Nambie!” nilivunja ukimya, Firyaal akainua uso wake na kunitazama huku aibu za kikekike zikiwa zimemjaa, akaishia kuchekacheka tu.
“Kwani wewe unaishi na nani?” aliniuliza swali ambalo hata sikuelewa kwa sababu gani ameniuliza. Nilikuwa na uhakika kwamba alikuwa anajua naishi peke yangu kwa sababu hata siku ya kwanza kumsaidia dada yake, nilimpeleka nyumbani kwangu kabla ya baadaye kuja kuvamiwa na kuponea kwenye tundu la sindano.
“Naishi mwenyewe, vipi kwani.”
“Nilitaka kujua tu,” alisema kwa lafudhi laini huku akijitahidi sauti yake iwe ya chini. Nadhani hakutaka mtu yeyote ajue kwamba nazungumza naye.
“Wewe ni mchumba’ake dada Shenaiza?” aliniuliza swali lingine ambalo lilinifanya nicheke.
“Hapana, niliamua tu kumsaidia.”
“Kwani we mchumba wako ni nani?” aliniuliza swali lingine, kabla sijamjibu niligeuka huku na kule, nilipohakikisha Raya na Shamila walikuwa jikoni, nilimgeukia na kumuuliza swali juu ya swali.
“Mbona unaniuliza maswali mengi kama polisi?”
“Hamna, nilitaka tu kujua, samahani kama nimekuudhi.”
“Hujaniudhi chochote, kwani we mchumba wako anaitwa nani?”
“Mi sina wala sijawahi kuwa naye.”
“Unataka kusema we humjui mwanaume?” nilimuuliza kwa pupa, akatingisha kichwa kuashiria kwamba ni kweli hakuwa akimjua mwanaume, moyo ukanilipuka paah! Nikageuka na kutazama tena kule jikoni, nikamgeukia Firyaal.
“Kwa nini ulikuwa unaniuliza kuhusu mchumba wangu?”
“Nilitaka kujua tu.”
“Kwa sasa sina, nipo mwenyewe kama unavyoniona,” nilimdanganya, nikamuona tabasamu pana likichanua kwenye uso wake, akaanza kung’atang’ata kucha huku akinitazama kwa macho ya wizi, taratibu nikajikuta nikianza kufikiria mambo tofauti kuhusu Firyaal.
“Ina maana ananipenda? Lakini mbona kama mdogo?” nilijiuliza huku nikiendelea kumkodolea macho Firyaal ambaye naye alishaanza kunifanyia vituko.
Akawa ni kama anataka kukaa vizuri, sketi yake ikafunuka upande mmoja na kunifanya niyaone mapaja yake yaliyokuwa yamejaa vizuri, yenye rangi ya weupe wa kung’aa, mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio.
Ni kama alijua kwamba namtazama, akazidi kunifanyia vituko, akawa na kazi ya kubadilisha mikao, jambo lililomfanya ‘Jamal’ wangu aanze kuchachamaa, nikameza funda la mate kama fisi aliyeona mfupa. Kwa muda nilisahau kabisa kwamba nipo kwenye matatizo makubwa.
“Humu ndani kuna joto,” alisema Firyaal na kufungua kifungo cha blauzi aliyokuwa amevaa, maembe ‘bolibo’ mawili yaliyojaa vizuri yakawa yanaonekana na kunifanya nizidi kuwa kwenye wakati mgumu.
“Ulisema unasomea IT, hebu chukua ile laptop pale uje hapa unisaidie kitu,” nilimtega, naye ni kama alikuwa akiisubiri nafasi hiyo, harakaharaka aliinuka pale alipokuwa amekaa, akaenda kuchukua laptop ya Shamila na kuja nayo kwenye lile kochi nililokuwa nimekaa, akaja kukaa karibu kabisa na mimi kiasi cha kunifanya niwe nalisikia joto la mwili wake, lililonakshiwa kwa manukato mazuri aliyokuwa amejipulizia.
Mara mlango wa jikoni ukafunguliwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...