Tuesday, October 24, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 44


ILIPOISHIA:
Ilibidi Raya abaki palepale hospitalini mpaka usiku ili iwe rahisi kufanya kazi yetu, muda ukazidi kuyoyoma na hatimaye giza likaingia, ule muda tuliokuwa tukiusubiri kwa hamu ukawa umewadia.
SASA ENDELEA...
“Tunakusikiliza wewe Shamila!”
“Yaah! Inabidi mnisikilize kwa makini vinginevyo hakuna kitakachofanikiwa.”
“Tunaanzia wapi?” nilimuuliza Shamila huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio.
“Tulia Jamal, mbona una haraka namna hiyo,” alisema Shamila, nikashusha pumzi ndefu na kutulia, hakuna muda ambao nilikuwa nahitaji msaada wake kama huo na kubwa zaidi, sikuwa mimi tu ambaye nilikuwa nahitaji msaada wake, bali Shenaiza pia.
Shamila aliingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo, muda mfupi baadaye alitoka akiwa na gauni jingine, akampa Raya na kumuelekeza kuingia kule ndani kwenda kubadilisha nguo. Kweli akatii alichoambiwa, muda mfupi baadaye akatoka akiwa ndani ya mavazi ya kinesi, usingeweza kumtambua kwamba hakuwa nesi.
“Sasa wewe kazi yako itakuwa ni kutoka na mgonjwa mpaka nje, unaona hili faili lake, inatakiwa ulishike na kufuata maelekezo ya nitakachokuwa nakwambia. Ukikosea tu basi hakuna kitakachowezekana,” alisema Shamila wakati akimpa maelekezo Raya, akatingisha kichwa kwa utiifu kuonesha kwamba alikuwa ameelewa alichokuwa ameambiwa.
“Inabidi pia njia ambayo itatumika kukutoa wewe itumike pia kwa Shenaiza, tena kwa wakati mmoja kwa hiyo tutaongozana wote, sijui kama mnanielewa,” alisema Shamila huku akiwa amevaa uso wa ‘usiriaz’, wote tukaitikia kuonesha kwamba tulikuwa tumemuelewa.
“Mimi nitaenda kumchukua Shenaiza wakati huo nyie mtakuwa mkinisubiri hapo chini, tutatoka pamoja mpaka pale getini, mimi nitaongea na walinzi, wakituruhusu kutoka tu, Firyaal yupo nje anatusubiri na gari la familia yao kwa hiyo hakutakuwa na muda wa kupoteza, tumeelewana?” alisema Shamila ambaye aligeuka na kuwa mwalimu wa kutuelekeza, sisi kazi yetu ikawa ni kuitikia tu.
“Nifuate,” alimwambia Raya huku akinitaka na mimi nivae vizuri nguo maalum za wagonjwa.
“Kamanda, huyu mgonjwa inatakiwa akafanyiwe kipimo cha MRI kesho sasa kwa sababu mashine ya hapa hospitalini ni mbovu na kesho kutakuwa na foleni kubwa, tumeomba akafanyiwe kipimo hicho usiku huu pale kwenye maabara za Lancert zilizopo nje ya hospitali,” Shamila alimwambia mlinzi aliyekuwa nje ya wodi ile kwa sauti ya juu, japokuwa mimi nilikuwa ndani niliweza kusikia kila kitu, nikatabasamu na kutikisa kichwa kwani ama kwa hakika mbinu ya Shamila ilikuwa kali mno.
Muda mfupi baadaye, nilisikia mlango ukifunguliwa, Shamila akatangulia kuingia, nyuma yake akafuatia Raya aliyekuwa akisukuma kiti cha magurudumu (wheel chair) huku akionesha dhahiri jinsi alivyokuwa na hofu kubwa moyoni mwake.
“Inatakiwa uchangamke, ukiwa unatetemeka hivyo watatushtukia, muone kwanza,” Shamila alimshushua Raya kwa sauti ya chini, nikanyamaza kimya kama sijasikia chochote. Wakasogeza ile wheel chair mpaka pale pembeni ya kitanda changu, Shamila akaniambia anajua ninao uwezo wa kutembea mwenyewe lakini ni lazima nikubali kusukumwa kwenye kiti cha magurudumu ili isiwe rahisi kwa mtu yeyote kutushtukia.
Basi nikashuka kitandani na kukaa kwenye kitanda cha magurudumu, Shamila akamuelekeza Raya namna ya kukisukuma na akarudia kumsisitiza kwamba anatakiwa kuchangamka. Ilibidi vitu vyangu vingine vyote niviache mlemle wodini, tukatoka mpaka kwenye korido, nikamuona yule mlinzi akisimama na kutusaidia kubonyeza kitufe kwenye lifti.
Hakuwa na mawazo kabisa kwamba ndiyo tunamtoka kiaina. Nikiri wazi kwamba hilo halikuwa zoezi langu la kwanza kutoroka hospitalini kwa sababu tayari nilishamtorosha Shenaiza lakini hali haikuwa tete kama ilivyokuwa muda huo, na kikubwa kilichokuwa kikinipa hofu kubwa ndani ya moyo wangu ni kujua aina ya watu niliokuwa nadili nao; baba yake Shenaiza na watu wake.
“Inawezekana kabisa kuna watu wamepandikizwa hapa hospitalini na baba yake Shenaiza kufuatilia nyendo zako na binti yake, kwa hiyo unatakiwa kujiinamia muda wote ili mtu yeyote asikuone usoni, mtanisubiri nikamchukue Shenaiza,” alisema Shamila wakati tukiwa ndani ya lifti tukishuka chini, tukamuitikia.
Tulishuka mpaka chini, akatuelekeza kufuata korido mpaka mbele ambapo alisema tumsubiri, Raya akawa ananisukuma taratibu, yeye akaelekea kwenye wodi ya wagonjwa wa akili alikokuwa amelazwa Shenaiza.
“Im scared Jamal, I cant take it!” (Naogopa Jamal, siwezi!)
“You need to do this my love, do it for me!” (Unatakiwa kufanya mpenzi wangu, fanya kwa ajili yangu) Raya alinisemesha kwa Kimombo si unajua tena yeye alikuwa akitoka familia bora? Nikawa naendelea kumpa maneno ya kumtia nguvu, tukawa tunaendelea kutembea taratibu kwenye korido huku Raya pia akiwa na faili langu.
“Hivi akitokea mlinzi hapa na kutuuliza tunaenda wapi usiku huu tutajibu nini?”
“Tunaenda kufanyiwa kipimo cha MRI pale nje kwenye maabara za Lancert kwa sababu mashine za humu ndani zimeharibika,” nilijibu kwa kujiamini, nikaona hofu ikipungua ndani ya moyo wake.
“Maelezo haya inabidi wewe nesi ndiyo uyatoe, sio mimi mgonjwa,” nilisema kwa msisitizo, Raya akawa ananiitikia lakini jambo ambalo bado hakuweza kulidhibiti, ni hofu iliyokuwa ndani ya moyo wake.
Tulifika mpaka pale Shenaiza alipotuambia kwamba tumsubiri, tukasimama na kuanza kuangalia uelekeo wa wodi ya wagonjwa wa akili alikokuwa ameelekea. Hata hivyo, hakutokea haraka kama tulivyodhani, muda ukaanza kuyoyoma mara dakika tano zikakatika, kimya! Tano nyingine zikakatika bila Shamila kurudi, tukaanza kuingiwa na hofu.
Pale tulipokuwa tumesimama, wauguzi na ndugu za wagonjwa mbalimbali walikuwa wakitupita lakini hakuna aliyekuwa na habari na sisi kwani walijua tupo kwenye taratibu za kawaida za tiba.
“Tunavyozidi kusimama hapa ndivyo tunavyozidi kujiweka kwenye hatari zaidi, wanaweza kutushtukia.”
“Sasa tufanyeje?” nilimuuliza Raya lakini kama bahati, kwa mbali tuliona mlango wa wodi ya wagonjwa wa akili ukifunguliwa, Shamila akatoka akiwa anasukuma kitanda cha magurudumu kama kile nilichokuwa nimekalia, wote tukashusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu kwani tulishaanza kuchanganyikiwa.
Kwa mbali akatuonesha ishara kwamba tuendelee kusonga mbele, naye akawa anakuja huku akikisukuma kile kitanda ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba aliyekuwa amekaa pale alikuwa ni Shenaiza.
Akazidi kutukaribia na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa ametufikia, tukawa tunatembea bila yeyote kati yetu kumsemesha mwenzake. Kwa watu ambao hawakuwa wakielewa kinachoendelea, wangedhani kwamba ni manesi walikuwa wakiwapeleka wagonjwa wao kupata matibabu ya kawaida.
Kwa mbinu ile ilikuwa vigumu sana kwa mtu yeyote kutushtukia, tukazidi kusonga mbele huku nikijitahidi kuibia macho pembeni na kumtazama Shenaiza ambaye alikuwa amekaa kwenye kiti cha magurudumu akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea.
Nguo maalum aliyofunikwa upande wa kichwani, ilifanya iwe vigumu kwa mtu yeyote kumtambua, tukaendelea kusonga mbele mpaka tulipofika kwenye geti la kutokea nje ya hospitali, hapo tukakumbana na kipingamizi ambacho hakuna aliyekitegemea, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...