Monday, October 23, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 43


ILIPOISHIA:
Kauli yake hiyo ilitufurahisha sana mimi na Shamila, tukawa na uhakika kwamba sasa kazi itakuwa nyepesi kwa sababu tayari tutakuwa na mtu kutoka ndani kabisa, ambaye angetusaidia kutimiza lengo letu la kupambana na mtu huyo hatari.
SASA ENDELEA...
“Kwa hiyo tunaanzia wapi?” nilimuuliza Shamila, akawa ni kama anayetafakari kitu kisha akaniambia ameshapata majibu.
“Ngoja niende kwanza na huyu binti nikampe hiyo hard disk yake,” alisema Shamila.
“Utaweza kuichomoa kwenye kompyuta?”
“Mimi naweza, nasomea Information Technology niko mwaka wa pili,” alisema Firyaal ambaye alikuwa amefanana sana na Shenaiza, yaani hata bila kuuliza ungemjua tu kwamba ni ndugu yake.
“Sijamaliza kukopi data ninazozihitaji lakini.”
“Nitakusaidia pia, ninayo ‘back up’ kubwa tu nyumbani, naweza kuhamisha data zote na kukuletea,” alisema msichana huyo, nikawa namtazama usoni kwani aliyokuwa akiyasema hayakuwa yakifanana na umri wake.
Kwa kumtazama alionekana kama msichana mdogo ambaye kwa makadirio ungeweza kudhani yupo kidato cha pili au cha tatu lakini kumbe tayari alishafika kidato cha sita na sasa alikuwa chuoni.

“Nitashukuru sana ukinisaidia dada’angu,” nilisema kwa sauti ya kiungwana, Firyaal akanitazama usoni, na mimi nikamtazama, macho yetu yakagongana, harakaharaka akakwepesha macho yake huku aibu za kikekike zikiwa zimemtawala.
“Basi usitoke kwenda sehemu yoyote, mimi ngoja niende naye nyumbani,” alisema Shamila, akanisogelea pale kitandani na kunibusu kisha harakaharaka akamshika mkono Firyaal na kuanza kutoka naye nje.
Walipofika mlangoni, nilimuona Firyaal akigeuka na kunitazama, na mimi nikamtazama, macho yetu yakagongana kwa mara nyingine. Tofauti na mwanzo, safari hii hakukwepesha macho yake, tukaendelea kutazamana mpaka walipotoka nje. Sikuelewa sababu iliyofanya awe ananitazama vile kwa sababu kimsingi hiyo haikuwa mara ya kwanza mimi na yeye kuonana.
Ilikuwa ni mara ya pili. Hata hivyo sikutilia sana maanani, nikampotezea.
Nikashusha pumzi ndefu na kutulia kitandani, mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu. Ni kweli nilikuwa bado sijapona vizuri lakini ilikuwa ni lazima niondoke hospitalini hapo kabla mambo hayajaharibika. Kutokana na sifa nilizokuwa nazisikia, nilijikuta nikimuogopa mno baba yake Shenaiza kama malaika mtoa roho.
Niliendelea kutulia pale kitandani, japokuwa Shamila aliniambia nisitoke, nilipata wazo la kwenda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Shenaiza kwenda kuangalia anaendeleaje. Hata hivyo, nilipomkumbuka yule mtu aliyekuwa akinitazama sana kwa makini mle ndani ya wodi ya vichaa, nilijikuta nikipatwa na hofu moyoni, nikaghairi.
Kwa hesabu zangu za harakaharaka ukichanganya na maelezo niliyoyapata kutoka kwa Shamila, nilikuwa nimekaa hospitalini hapo kwa wiki mbili mfululizo, huku kati ya hizo, siku saba nikiwa nimepoteza kabisa fahamu.
Nilijaribu kuvuta kumbukumbu ya mambo yote yaliyotokea ndani ya kipindi hicho nilichokuwa hospitalini hapo, ungeweza kudhani kama nimekaa hospitalini kwa kipindi cha mwaka mzima. Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa mno kiasi cha kufanya hata akili yangu isipate muda wa kupumzika.
Kitu ambacho kilinipa faraja kubwa ndani ya moyo wangu, ni kuona jinsi wafanyakazi wenzangu pamoja na bosi wetu walivyokuwa wakinijali. Japokuwa nilikuwa chini ya uangalizi maalum ambapo watu hawakuwa wakiruhusiwa kuja mara kwa mara kunitazama, Raya alinihakikishia kwamba katika zile siku nilizokuwa nimepoteza fahamu karibu kila siku watu kutoka kazini walikuwa wakija kunitazama.
Baada ya kama dakika arobaini tangu Shamila na yule mdogo wake Shenaiza waondoke, Raya alikuja tena. Kiukweli japokuwa nilikuwa nikimuendea kinyume, Raya alikuwa akijitahidi sana kuwa karibu na mimi.
Muda wote yeye alikuwa akinifikiria mimi tu kiasi cha kumfanya kazini asiwe anaenda wala nyumbani kwao asiwe anatulia, muda wote ilikuwa ni kiguu na njia, kuja hospitali na kurudi kwao.
“Vipi unaendeleaje mume wangu,” alisema Raya kwa sauti ya chini, akionesha kuwa na mawazo lukuki ndani ya kichwa chake.
“Naendelea vizuri mke wangu, vipi mbona nakuona kama mudi yako iko chini sana, nini kinakusumbua,” nilimwambia Raya kwa upole, akajisogeza na kupitisha mkono wake mmoja shingoni kwangu, akanibusu kwenye paji langu la uso na kuanza kuniambia kwamba tangu nilipomweleza ukweli wa kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia, alikosa raha kabisa.
“Nahisi kama nitakupoteza mpenzi wangu na mimi siwezi kuishi bila wewe, hata sijui itakuwaje,” alisema kwa huzuni, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kumtuliza. Nikamwambia asiwe na wasiwasi, hakuna jambo lolote baya litakalotokea nakuhakikishia,” nilimwambia.
Kidogo kujiamini kwangu kulimfanya naye aanze kuona kwamba kumbe halikuwa tatizo kubwa mbele yetu, nikamueleza pia juu ya mipango ya kutoroka tuliyokuwa tumeipanga kwa ajili ya kumkimbia baba yake Shenaiza. Nilimuona naye akiniunga mkono, nadhani hata yeye hakuwa na imani kabisa juu ya usalama wangu hospitalini hapo.
Tulizungumza mambo mengi, Raya akawa ananisisitiza kwamba yeye amejitoa kwa asilimia mia moja kunisaidia, isije ikatokea kwamba nikamgeuka na kumuona hana maana tena. Kauli yake iliugusa sana moyo wangu kwa sababu ni kweli Raya alikuwa amejitoa kwa kila kitu lakini kwa bahati mbaya sana shetani alionekana kunizidi nguvu.
Nikawa namhakikishia kwamba asiwe na wasiwasi lakini ukweli, sikuwa namaanisha kile nilichokuwa nakisema. Akaniambia kwamba atashirikiana na Shamila kuhakikisha wananitorosha hospitalini hapo usiku bila mtu yeyote kujua, swali likawa nikishatoroshwa nitaenda kukaa wapi?
Raya alisema anataka nikakae nyumbani kwao kwa sababu pale kuna usalama zaidi, nikamwambia ni rahisi wabaya zangu kujua kwamba niko pale kwa sababu kuna baadhi ya watu walikuwa wakijua kuhusu uhusiano wetu wa kimapenzi. Nikatumia nafasi hiyo kumpigia chapuo Shamila, nikamwambia Raya kwamba amesema yupo tayari kunificha nyumbani kwake.
Nilimuona Raya akishtushwa kidogo na nilichokisema lakini nikamtoa wasiwasi na kumwambia kwamba mimi na yeye tutakuwa pamoja kwa hiyo asiwe na wasiwasi wowote. Akakubali kwa shingo upande, nadhani bado alikuwa na wivu juu ya ukaribu wangu na Shamila.
Muda ulizidi kuyoyoma, baadaye Shamila alirudi akiwa peke yake, akaniambia kwamba kila kitu kimeenda kama tulivyokubaliana, akaniambia kwamba Firyaal alikuwa mtundu sana kwenye mambo ya kompyuta na kwamba tayari alishanikopia data zote na kuziacha pale nyumbani kwake kama tulivyokubaliana, tukaanza kupanga mipango ya namna ya kutoroka usiku huku Raya naye akiwepo.
Jambo ambalo kuanzia mwanzo Raya hakuwa akilijua, ni kwamba katika mpango wetu huo ilikuwa ni lazima pia tumtoroshe na Shenaiza, akashtuka kusikia hivyo.
Bado nikaendelea kumsisitiza kwamba ilikuwa ni lazima tuondoke na Shenaiza kwa sababu bila yeye mimi nisingeingia kwenye mtego huo na kuanzia mwanzo alikuwa akinisisitiza kwamba mimi ndiye mtu pekee ninayeweza kumsaidia.
“Usiwe na wasiwasi, hawa wote wataenda kukaa nyumbani kwangu, mimi nina nyumba kubwa, hata na wewe ukitaka tukae pamoja tusaidiane kuwahudumia wagonjwa haina shida,” alisema Shamila, nikamuona Raya akishusha pumzi ndefu na kunitazama, akatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na mimi.
Ilibidi Raya abaki palepale hospitalini mpaka usiku ili iwe rahisi kufanya kazi yetu, muda ukazidi kuyoyoma na hatimaye giza likaingia, ule muda tuliokuwa tukiusubiri kwa hamu ukawa umewadia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

2 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...