Wednesday, October 25, 2017

Seven Days ih Hell (Siku Saba Kuzimu)- 46


ILIPOISHIA:
“Ulisema unasomea IT, hebu chukua ile laptop pale uje hapa unisaidie kitu,” nilimtega, naye ni kama alikuwa akiisubiri nafasi hiyo, harakaharaka aliinuka pale alipokuwa amekaa, akaenda kuchukua laptop ya Shamila na kuja nayo kwenye lile kochi nililokuwa nimekaa, akaja kukaa karibu kabisa na mimi kiasi cha kunifanya niwe nalisikia joto la mwili wake, lililonakshiwa kwa manukato mazuri aliyokuwa amejipulizia.
Mara mlango wa jikoni ukafunguliwa.
SASA ENDELEA...
“Vipi?” Shamila aliuliza huku akiwa ni kama ameshtuka f’lani hivi kuniona nikiwa nimekaa jirani namna ile na Firyaal.
“Kuna kazi namuelekeza anisaidie.”
“Ooh! Tena huyo atakufaa zaidi, si amesema anajuajua mambo ya IT?”
“Ndiyo japo bado sijathibitisha,” nilisema huku nikijifanya kumkandamiza Firyaal ili kuua soo, naye ni kama alijua kilichokuwa ndani ya akili yangu, akatulia kiasi cha kufanya iwe vigumu kwa Shamila kuelewa kilichokuwa kikiendelea kati yangu na msichana huyo mdogo lakini mrembo.
Akaenda kwenye friji na kuchukua baadhi ya vifaa kisha akarudi jikoni, akaniacha nikiwa bize nikijifanya namuelekeza kitu Firyaal ambaye naye alikuwa akiitikia kwa umakini, alipoingia jikoni tukatazamana.

“Hapa siyo sehemu sahihi, watatushtukia sasa hivi,” nilimnong’oneza, harakaharaka akanikubalia kwa kutingisha kichwa. Nikamwambia anisaidie kutafuta majina ya watu wote ambao walikuwa ‘wamesaidiwa’ na Shirika la Black Heart lililokuwa likiongozwa na baba yake kwenye zile data tulizoziiba kwenye ile ‘hard disk’ aliyonipa.
Akahama pale alipokuwa amenifuata na kurudi kwenye kiti chake, akajiinamia kwenye laptop na kuanza kufanya ile kazi niliyomuagiza. Shamila alitoka tena jikoni na alipoona kweli Firyaal amejiinamia na kompyuta, wala hakuhisi jambo lolote baya, akawa ananitazama kwa macho fulani hivi ambayo nilimuelewa alichokuwa anamaanisha.
Firyaal aliendelea na kazi, Shamila na Raya nao waliendelea na kazi, mimi nikawa nimekaa zangu pale kwenye kochi nikiwa naendelea kuwaza hili na lile. Nikiri wazi kwamba kabla ya matatizo hayo hayajaanza kunikumba, sikuwa napenda kukaa karibu na wasichana kabisa, yaani kama ungekuja kwangu, kama usingenikuta natazama ‘movie’ basi ungenikuta nacheza gemu za ‘Playstation’.
Tangu nilipoanza kukutana kimwili na Raya, akili zilikuwa ni kama zimezibuka, nikawa najilaumu kwa kuchelewa kuvumbua ‘hazina’ iliyojificha kwa kipindi chote hicho. Kabla sijaendelea, naomba niliweke wazi hili kwa manufaa ya wengine. Wanaume wengi huwa wanaharibikiwa maishani kwa sababu ya kuruka vipengele fulani katika hatua za ukuaji.
Unakuta mtu ule muda ambao alitakiwa afanye mambo ya ‘kitoto’ yeye anakuwa bize na masomo au kazi. Akishaingia kwenye ndoa ndiyo anazibuka na kuanza kuona kama alikuwa anachelewa, matokeo yake ndiyo unakuta mwanaume ana mke mzuri lakini kila siku anasaliti ndoa yake kwa sababu kuna hatua ya ukuaji aliiruka.
Muda mfupi baadaye, chakula kilikuwa tayari, Raya na Shamila wakaandaa chakula, Raya akiwa hajui kabisa kwamba aliyekuwa akishirikiana naye kwa kila kitu alikuwa ni ‘mke mwenzie’, Firyaal naye akijifanya anawaheshimu sana dada zake hao kumbe na yeye alikuwa akijilengesha kwangu.
Baada ya kumaliza kuandaa, tulianza kula huku Shamila akitusisitiza kwamba tusiwe na wasiwasi kuhusu Shenaiza, akatuambia kwamba atamshughulikia na baada ya muda mfupi atarejewa na fahamu zake. Sote tulikuwa kimya kabisa, mtu pekee aliyekuwa akizungumza alikuwa ni Shamila.
Baada ya kumaliza kula, tulikaa pamoja sebuleni hapo na kuanza kupanga namna ya kukabiliana na baba yake Shenaiza. Nilimuuliza Firyaal amefikia wapi kwenye kazi niliyompa, akaniambia ameshapata majina ya watu wote waliosaidiwa na shirika hilo pamoja na anuani zao za makazi pamoja na ndugu zao waliokuwa hapa nchini.
“Basi naomba uunganishe na yale majina ambayo nilishayapata kuanzia mwanzo,” nilisema, Firyaal naye akaitikia kwa adabu kabisa, watu wote wakazidi kutuamini kwamba kweli tulikuwa kikazi zaidi.
Bado ule mchezo wake wa kunitazama kwa kuibia hakuwa ameuacha lakini kwa kuwa sasa Raya na Shamila walikuwa pale sebuleni, nilijifanya sijui chochote kinachoendelea kwa sababu nilihofia wanaweza kutufuma tukitazamana halafu wakatufikiria vibaya.
Tuliendelea kupanga mipango yetu na mwisho tukakubaliana kwamba kwa kuwa ushahidi wote tayari tulikuwa nao, twende tukatoe taarifa polisi ili watusaidie kupambana na genge hatari la baba yake Shenaiza.
Kilichonipa moyo kwamba kila kitu kitafanikiwa, ni jinsi Firyaal alivyoonesha kuchukizwa na vitendo vya baba yake, akatuhakikishia kwamba japokuwa anajua baba yake anaweza hata kufungwa, yupo tayari kwa chochote mpaka tufanikiwe.
Wazo hilo lilipitishwa, tukakubaliana kwamba usiku ule Shamila anatakiwa kurudi kule hospitalini ili kuhakikisha hakuna anayeshtukia kama mimi na Shenaiza tumetoroshwa hospitalini, na asubuhi na mapema ya siku inayofuatia, mimi nitaongozana na Raya mpaka kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya kwenda kutoa taarifa.
Kwa kuwa muda ulikuwa umeshaenda, Shamila alimwambia Firyaal amrudishe mpaka hospitalini kwa kutumia gari lake kisha arudi nyumbani kwao, Kurasini ili asije akashtukiwa lakini msichana huyo alikataa katakata, akasema alishamuaga mama yake kwamba anakwenda kwenye ‘birthday’ ya rafiki yake na kwamba hatarudi mpaka asubuhi na aliruhusiwa.
“Twende nikupeleke wewe kazini mi nitakuja kulala hapahapa na dadaa’ngu Shenaiza,” alisema, Shamila na Raya wakamkubalia bila kujua kwamba kuna kitu alichokuwa anakifuata.
Raya naye alipoulizwa kama atarudi nyumbani kwao, naye alisema atakaa na mimi mpaka asubuhi ya kesho yake. Shamila alikubali ingawa nilimuona kama wivu unamsumbua sana, akainuka na kwenda kuanza kuandaa mazingira ya sisi sote kulala.
Mimi aliniandalia kwenye chumba cha peke yangu, Firyaal akamwambia atalala na dada yake kwenye chumba cha wageni na Raya atalala kwenye chumba chake, wote tukamkubalia kwani kwa wakati huyo yeye ndiye aliyekuwa bosi wetu.
Alienda kuoga na kuanza kujiandaa kisha akatuaga na kututaka tuwe makini, hasa mimi, akatoka na Firyaal kuelekea hospitali huku akiniachia maagizo kwamba Firyaal akirudi, nikamsaidie kufungua geti aingize gari kisha baada ya hapo, nifunge milango yote na kuzima taa zote za ndani na nje, nikamkubalia.
Walipotoka, ndani nilibaki na Raya tu ambaye ilionesha alikuwa na hamu kubwa ya mimi na yeye kubaki wawili tu. Alipohakikisha wameshaingia ndani ya gari na kuondoka, harakaharaka alinifuata na bila kuzungumza chochote, alianza fujo zake akitaka nikamalizane naye fasta kabla Firyaal hajarejea.
Hata hivyo, kwa kuwa tayari nilikuwa na ratiba nyingine kichwani, nilimdanganya kwamba siku hiyo nilikuwa nimechoka sana na jeraha langu lilikuwa likima kwa sababu ya purukushani za kutwa nzima, nikamuomba kama hatajali, tukapumzike kwanza mpaka baadaye.
Nilimuona akikubali kwa shingo upande, akaenda kuoga na kuniacha niko pale sebuleni najifanya niko bize na laptop. Baada ya kumaliza kuoga alinifuata tena, nikaendelea kumsisitizia kwamba hali yangu haikuwa nzuri, akaniomba basi tukalale kitanda kimoja ambapo pia nilimkatalia na kumwambia nitamfuata usiku sana wakati Firyaal ameshalala ili tusije kuonesha picha mbaya.
“Basi naacha mlango wazi,” alisema, nikatingisha kichwa kuonesha kumkubalia, akaondoka kwa shingo upande na kwenda kulala. Kutokana na uchovu aliokuwa nao wa pilikapilika za kutwa nzima, hakuchukua raundi, akapitiwa na usingizi mzito.
Nusu saa baadaye, alikuwa akikoroma, hata niliponyata na kwenda kumchungulia, alionesha ameshalala fofofo, moyoni nikawa nachekelea. Harakaharaka nilienda kwenda chumba nilichopangiwa kulala, nikaingia bafuni na kujimwagia maji kupunguza uchovu kisha nikatoka na kwenda kukaa sebuleni nikimsubiri Firyaal kwa shauku kubwa, nikiwa nimejifunga taulo tu! Shetani wa mahaba alikuwa amenizidi nguvu.
Dakika kadhaa baadaye, nikasikia honi ya gari, harakaharaka nikatoka na kwenda kufungua geti, alikuwa ni Firyaal, aliponiona nimejifunga taulo tu, alijifanya kushtuka kisha nikamuona akitabasamu, akaingiza gari na kulipaki, nikafunga mageti kama Shamila alivyoniagiza, tukaingia ndani na kwenda mpaka sebuleni.
“Dada Raya yuko wapi?” aliuliza Firyaal kwa sauti ya chini, nikamwambia ameshalala na sasa anakoroma, nikamuona akishusha pumzi ndefu na kunitazama usoni, tukawa tunatazamana.
“Nataka nikalale na dada Shenaiza,” alisema kwa sauti ya kudeka huku akinisogelea na kujilaza kifuani kwangu, nikapitisha mkono wangu na kumshika kiunoni, nikamuona akiruka kama aliyepigwa na shoti ya umeme.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...