Tuesday, September 5, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 36


ILIPOISHIA:
“Naam baba,” niliitikia huku nikijaribu kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika kimahaba, baba akaja mbiombio na kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi hatujamaliza kwa hiyo anisubiri, alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea nje lakini tulipofika kwenye kingo za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
SASA ENDELEA...
Kishindo kikubwa kilisikika, nikamuona baba akianza kuyumbayumba kama amelewa, na mimi nikaanza kusikia kizunguzungu kikali huku damu zikianza kututoka wote, mdomoni na puani. Muda huo tulikuwa tumeshavuka kizingiti cha mlango.
Sijui nilipata wapi ujasiri kwani ni muda huo ndipo nilipogundua kwamba kuna kosa nilikuwa nimelifanya, Isri aliniambia kwamba nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, jambo ambalo nililikiuka kwa hiyo ili kurekebisha makosa, nilimvuta baba kwa nguvu, wote tukaangukia upande wa ndani wa mlango.
Kilisikika kishindo kingine kisha baba akawa ni kama amezinduka kutoka kwenye usingizi mzito.
“Nini kimetokea?” baba aliniuliza huku na yeye akiwa ni kama amepigwa na butwaa, akainua shingo na kutazama huku na kule, nikamuona akishtuka zaidi baada ya kuona damu zinamtoka mdomoni na puani pale chini.
“Hata mimi sijui,” nilimjibu huku nikisimama, na yeye akasimama kisha akawa anajifuta damu huku akitazama vizuri pale mlangoni. Aliangalia kwa sekunde kadhaa kisha akanigeukia na kunitolea macho ya ukali.
“Umeweka nini hapa?” aliniuliza kwa ukali.
“Hakuna kitu.”
“Una uhakika?” aliniuliza huku akinisogelea mwilini. Miongoni mwa sifa za baba, huwa hapendi kabisa mtu muongo, ni bora akikuuliza unyamaze kuliko kutoa majibu ya uongo. Ili kuepusha shari, nilinyamaza na kujiinamia.
“Si naongea na wewe?”
“Wakati naingia nilipakaza damu hapo kwenye mlango,” nilisema, akaonesha kushtuka mno, hakusema kitu zaidi ya kunishika mkono, akawa ananivutia ndani huku akiendelea kujifuta damu.
Tulienda mpaka kwenye kile chumba changu, tukaingia huku baba akiwa makini kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayetutazama. Wakati naingia, nilitupia macho kwenye mlango wa chumba cha Rahma, nikamuona akiwa anatuchungulia. Nilimuonesha ishara kwamba anisubiri, akatingisha kichwa kuniitikia.
“Mimi ni nani kwako?”
“Ni baba yangu.”
“Haya nataka unieleze kila kitu, umetokaje mahabusu na nini kimetokea mpaka ukapaka damu kwenye mlango,” alisema baba kwa sauti ya chini, lakini akionesha kutokuwa na hasira na mimi.
Kabla sijamjibu, niliingiza mkono mfukoni na kutoa ile dawa ya ajabu ambayo kwa kiasi kikubwa ilinisaidia sana.
“Hiyo ni mimi nilikuwekea muda ule wakati polisi wanakuchukua, naamini imekusaidia sana,” alisema baba huku akiichukua ile dawa mikononi mwangu na kuiweka kwenye mfuko wa shati. Ni hapo ndipo nilipoanza kupata picha juu ya nini kilichotokea.
“Sasa baba, unataka nikueleze nini wakati kumbe unajua kila kitu na wewe ndiye uliyenielekeza jinsi ya kutoka mahabusu?”
“Unachokisema ni sawa lakini najua kuna mambo mengi yametokea ukiachilia mbali wewe kutoka mahabusu na ndiyo maana nimekutoboa mkono wako na kukinga damu yako, mimi ni baba yako na hakuna mtu mwenye uchungu na wewe kuliko sisi wazazi wako, ni lazima ujifunze kuniamini na kuwa muwazi kwangu,” alisema.
Kiukweli sikuwahi kumsikia baba akizungumza kwa busara na mimi kiasi hicho, yaani ni kama alikuwa akizungumza na mkubwa mwenzake na hata ule ukali wake wa siku zote, hakuuonesha kabisa.
Nilishusha pumzi na kukaa vizuri, sikuona sababu ya kuendelea kumficha, nilianza kumueleza kila kitu kilichotokea, kuanzia nilipofikishwa kituoni, wale wachawi waliokuja usiku kule mahabusu na jinsi yule mwingine alivyobadilika sura na kufanana na mimi.
Nilipofikia kipengele hicho, baba alinikatisha, akaniambia kwamba dawa aliyokuwa amenipa, ina nguvu kubwa ya kufanya chochote ninachokitaka. Akaniambia kwamba yule mchawi aliyebadilika sura, alishindwa kutoka mpaka asubuhi na askari walipoingia kwa ajili ya kufanya ukaguzi.
“Nasikia wameshtuka sana kumuona, wakadhani ni wewe lakini tofauti ikawa ni kwamba sura mmefanana lakini yeye ni mzee na amekutwa hana nguo hata moja, mtaani kote ndiyo gumzo na hata vyombo vya habari vimeanza kuripoti tukio hilo la ajabu,” alisema baba.
Kauli yake ilinifanya niwe na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimeendelea, akaniambia nisiwe na wasiwasi atanieleza lakini pia akaniambia kwamba anataka kumtumia yule mchawi kama funzo kwa watu wengine wenye tabia ya kufanya uchawi wa kijinga.
Aliposema uchawi wa kijinga, sikumuelewa anamaanisha nini, nikataka kumuuliza tena lakini aliniambia niendelee kumueleza kilichotokea. Nilimueleza kila kitu na jinsi nilivyokutana na yule msichana usiku ule.
“Lakini si nilishakukataza kuwa karibu na Isri?” alisema huku akinitazama usoni, nilishtuka kumsikia baba akimtaja jina. Kwa ilivyoonesha, kumbe baba alikuwa akimfahamu vizuri msichana huyo na hata aliponikataza kuwa naye karibu, alikuwa na maana yake.
“Huyo si ndiye aliyekusababishia matatizo mpaka ukakamatwa kwa tuhuma za mauaji? Ina maana wewe hukushtuka mtu amekufia mchana gesti halafu usiku unakutana naye tena? Akili zako zinafanya kazi sawasawa kweli?” baba alinibadilikia, nikawa nataka kujitetea lakini alinikatisha na kuniambia anaelewa kila kitu kilichotokea kati yetu.
“Hebu hiyo mikono yako,” alisema, nikasita kidogo lakini baadaye nilimpa, akaishika na kuanza kuitazama upande wa mbele kisha akanitazama usoni.
“Na wewe umeshakuwa kama yeye,” alisema huku akiniachia, akaniambia nifumbue mdomo wangu. Nilifanya hivyo, akawa anayatazama meno yangu kwa makini. Bado nilikuwa na maswali mengi kuliko majibu na ilionesha kwamba baba anamfahamu vizuri sana Isri.
Kitendo cha kutazama mikono yangu kisha wakati huohuo akaanza kukagua meno yangu, kilitosha kunifanya nielewe kwamba kumbe anajua jinsi msichana huyo alivyonigeuza na kuwa kiumbe wa ajabu.
“Umewapa ushindi maadui zangu kwa sababu ya mambo yako ya kipumbavu,” alisema baba huku akiinuka, bado damu zilikuwa zikimtoka puani ingawa safari hii haikuwa kwa wingi kama ilivyokuwa mwanzo.
Alipotaka kutoka, nilimuita, akageuka na kunitazama, nikamwambia Isri ameniambia nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, akanijibu kwa kifupi kwamba anajua kisha akaondoka zake.
Harakaharaka niliinuka na kukimbilia bafuni kwani nilikuwa najisikia aibu kukutana na Rahma nikiwa na harufu mbaya kiasi kile, nikajifungia na kufungulia maji kwa wingi, nilivua nguo zangu kisha nikaanza kujimwagia maji huku nikijikagua kama hakukuwa na kitu chochote kisicho cha kawaida mwilini mwangu.
Mara nilisikia mlango wa bafu ukigongwa, nikahisi ni Rahma amenifuata, harakaharaka nikaufungua, nikakutana uso kwa uso na baba.
“Ogea hii,” alisema huku akinipa ile dawa ambayo aliwahi kunipa niogee, ambayo ukiogea mwili unatoa uchafu mweusi kama mkaa. Nilimshukuru na kufunga mlango, nikaendelea kuoga. Maji machafu, meusi tii yalianza kunitoka, safari hii nikawa sina wasiwasi maana nilikuwa naelewa kinachotokea.
Nilioga mpaka uchafu wote ukaniisha mwilini, nikachukua nguo zangu na kuzikung’uta sana kisha nikavaa na kutoka. Rahma alikuwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake, akionesha kunisubiri kwa shauku kubwa.
Hakuwa amevaa chochote zaidi ya kujifunga upande wa khanga nyepesi, akawa ananitazama usoni kwa macho yake mazuri, ambayo yalikuwa ni kama yana usingizi kwa jinsi yalivyolegea.
Nilitazama huku na kule, nilipoona hakuna mtu anayetutazama, nilimsogelea, akanikumbatia kwa mahaba kisha akanivutia ndani. Hatukukumbuka hata kufunga mlango, kwa makusudi aliuachia ule upande wa khanga, ukadondoka chini, nikawa kama fisi aliyeona mfupa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...