Tuesday, September 26, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 45


ILIPOISHIA:
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
SASA ENDELEA...
“Nikikamatwa je?”
“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,” alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba, nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.
Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.
Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka. Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.

Nikaingiza mikono na kumvuta mtoto huyo aliyekuwa amebanwa pale kwenye siti, kwa kuwa nilikuwa na nguvu za kutosha, nilifanikiwa kumtoa, nikamlaza barabarani kisha nikachukua kile kipande cha mgomba na kukirudishia palepale nilipomtoa yule mtoto, kama baba alivyonielekeza.
Nilipomaliza, nilisimama, mapigo ya moyo wangu yakizidi kunienda mbio kuliko kawaida, nikageuka kutazama pale nilipokuwa nimemlaza yule mtoto. Cha ajabu, niliwaona watu wengine kama wanne hivi, nao wakiwa wanamtazama yule mtoto kama wanaoshauriana kama wamchukue au la.
Nilipowatazama vizuri watu hao, hasa maeneo ya usoni, niligundua kwamba hawakuwa binadamu wa kawaida, nikaona wanataka kunizidi ujanja. Kwa hasira nilipiga kishindo kwa nguvu kwenye lami, wote wakashtuka huku wakinitazama kwa woga, wakaanza kurudi kinyumenyume.
Ishara ya kupiga kishindo chini, alinifundisha baba tukiwa bado kule Chunya lakini aliponiambia kipindi hicho, alisema kwamba eti waganga ndiyo huitumia kuwashtua wachawi ambao mara nyingi wanapofanya mambo yao, huwa wanaamini hakuna anayewaona kwa hiyo ukipiga mguu wa kushoto chini, huwafanya waelewe kwamba kumbe umewaona.
Walipokuwa wanarudi nyuma, na mimi nilipata nafasi ya kumnyanyua yule mtoto aliyekuwa akitapatapa kama anayeelekea kukata roho, damu nyingi zikimtoka mdomoni na puani. Cha ajabu, licha ya kwamba sehemu aliyokuwa amekaa ilikuwa imebondeka vibaya, hakuwa na jeraha lolote zaidi ya kuvuja damu kwa wingi.
Hata sijui ujasiri niliupata wapi, nilimbeba begani, kiumri alikuwa na kati ya miaka sita au saba, mtoto wa kike mzuri, akiwa amevalia sare za shule kuonesha kwamba alikuwa ametoka shuleni.
“Pole kwa ajali, tunaomba tukusaidie kumbeba,” alisema mmoja kati ya wale watu, kwa sauti iliyokuwa ikisikika kama mwangwi, nikamkata jicho la ukali bila kumjibu chochote kisha nikazamia kule vichakani, nikawa nakimbia kuelekea pale nilipowaacha baba na baba yake Rahma.
“Safi sana,” alisema baba na kuungwa mkono na baba yake Rahma, wakawa wananipigia makofi kunipongeza.
“Mlaze hapo kwenye hayo majani ya mgomba kisha rudi tena eneo la tukio katoe ile mizizi yote ya mtunguja uliyoifunga, si unakumbuka mahali ulipoifunga? Ukiiacha magari mengine yataendelea kupata ajali hovyo,” alisema baba huku akinipa kisu, harakaharaka nikarudi mpaka eneo la tukio ambapo nilikuta watu wameongezeka lakini nilipowatazama vizuri, niligundua kwamba wote walikuwa ni wa jamii moja.
Walichokuwa wanakifanya kilinishangaza sana, wengine walikuwa wakilamba damu pale kwenye lami bila hofu hata kidogo huku wengine wakiwa bize kutaka kumtoa yule mwanamke aliyekuwa akiendesha gari hilo ambaye ilionesha amejeruhiwa vibaya.
Nilipofika, nilifanya kama nilivyofanya awali, nikapiga mguu chini kwa nguvu, wote wakatawanyika kisha nikaanza kukata zile dawa nilizokuwa nimezifunga pande zote mbili za barabara. Nilivuka barabara, nikakata ya kwanza, nikarudi pale katikati, nikaiokota ile nyingine ambayo ilikuwa imelowa damu kwani pale ndipo gari lilipopatia ajali kabla ya kubinuka na kwenda kugota kando ya barabara.
Niliokota ile nyingine iliyokuwa upande ule ilipotokea ajali, nikaenda kumalizia na ile ya mwisho iliyokuwa upande ule waliokuwepo baba na baba yake Rahma, cha ajabu, nilipomalizia kukata ile ya mwisho tu, wale watu waiokuwa wamejaa eneo lile, walianza kutokomea mmoja baada ya mwingine, wengine nikawa nawasikia wakiachia misonyo mikali. Sikuwajali kwa sababu hata mimi nilitaka kuwahi kuondoka eneo hilo kwani ningeweza kukamatwa ikawa balaa.
Bado hakukuwa na gari wala chombo chochote cha usafiri kilichopita eneo hilo, nikatokomea vichakani na kurudi pale nilipokuwa nimewaacha akina baba, mwili wangu ukiwa umelowa damu. Waliendelea kunipongeza, baba akaniambia natakiwa kumalizia kazi yangu.
“Kivipi baba?” nilimuuliza huku nikihema kwani niliamini kazi nzito nimeshaimaliza.
“Inabidi tuelekee kilingeni ukamkabidhi Mkuu alichokuagiza, tukifika itabidi umtenganishe kichwa na kiwiliwili kwa kutumia hicho kisu nilichokupa, hakikisha hizo dawa unazitunza vizuri,” alisema baba na kunifanya nishtuke kupita kawaida.
“Nimchinje?” nilihoji macho yakiwa yamenitoka pima.
“Sasa kazi kubwa umeshaifanya unaogopa nini?” alisema baba huku akiinuka, baba Rahma naye akainuka na wote tukasogea mpaka pale yule mtoto alipokuwa amelazwa juu ya majani ya migomba, akionesha kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai.
Baba alinipa ishara kwamba tuiname pale yule mtoto alipokuwa amelala, mkono mmoja akamshika yule mtoto, mwingine akampa baba yake Rahma ambaye naye mmoja alimshika yule mtoto na mwingine akanipa mimi, na mimi nikafanya hivyohivyo.
“Usifumbue macho mpaka tutakapokwambia, dawa zako zote si unazo maana ndiyo tunaondoka hivyo,” alisema baba, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubali, akahesabu mpaka tatu, sote tukafumba macho.
Baba na baba yake Rahma walianza kuongea maneno fulani nisiyoyaelewa kwa kurudiarudia, wakawa ni kama wanaimba mapambio ya kutisha, mara upepo mkali ukaanza kuvuma kwa nguvu, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia nikitingishwa begani.
“Tumeshafika, mbona unazubaa,” alisema baba, kufumbua macho, nikashtuka nipo eneo lingine tofauti kabisa, nikageuka huku na kule, kumbukumbu zangu zikanijia kwamba hapo ndiyo pale ambapo usiku uliopita tulikuwa tumekusanyika. Nilitazama huku na kule, hata sura za watu karibu wote zilikuwa zilezile, nikamuona mkuu amekaa katikati kabisa, huku akiwa anajitafuna mapengo kama wanavyofanya watu waliozeeka sana.
Japokuwa huko kote tulikotoka nilikuwa nimevaa nguo zangu, nilishangaa kujikuta eti nimevaa kaniki kama ilivyokuwa jana yake, kila kitu kilikuwa ni zaidi ya maajabu.
“Mpeleke mpaka pale kwenye kile kichanja ulichokuwa umelazwa jana kisha sikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu,” baba aliniambia kwa sauti ya chini, yeye na baba Rahma wakaenda kukaa kule pembeni walikokuwa wamekaa wale watu wengine na kutengeneza duara.
Nilimbeba yule mtoto ambaye kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kuyoyoma ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakizidi kufifia huku akianza kulegea, nadhani ni kwa sababu ya kupoteza damu nyingi. Watu wote walikua kimya kabisa, nikambeba mpaka pale nilipokuwa nimelazwa jana yake, kwenye kitanda kilichotengenezwa kwa miti.
Mkuu alisimama na kusogea pale kwenye kile kitanda, akanionesha kwa ishara kwamba nimgeuzie kichwa upande wa Magharibi, nikafanya hivyo kisha akasogea na kumgusa kifuani, nadhani alitaka kuhakikisha kama bado hajakata roho.
Nilimuona akitingisha kichwa kisha akainua mikono juu, watu wote wakapiga makofi kwa wingi, sikuelewa lakini nadhani ilikuwa ni kama sehemu ya kunipongeza. Watu wote walipotulia, bila kusema chochote, alinionesha ishara kwamba niendelee, nikakumbuka maneno ya baba kwamba akinipa ishara, maana yake anataka nimchinje mtoto huyo.
Tangu nizaliwe, sikuwahi kuchinja hata kuku tu, achilia mbali ndege tuliokuwa tukiwawinda kule kijijini kwetu lakini sasa eti nilikuwa natakiwa nimchinje binadamu, mtoto asiye na hatia yoyote ili nifaulu mtihani na kuwa mwanachama kamili, nilijikuta nikitetemeka kuliko kawaida.
Nilikichomoa kisu pale kiunoni nilipokiweka, mikono ikawa inatetemeka kuliko kawaida, nikawa namtazama mtoto yule usoni, nilijikuta nikiingiwa na huruma isiyo ya kawaida.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

1 comment:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...