Tuesday, September 26, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 41


ILIPOISHIA:
“Habari za saizi nesi,” Raya alimsalimia Shamila kwa unyenyekevu, jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla. Shamila naye akajibu kwa uchangamfu, nikabaki njia panda. Sikujua walizungumza nini muda ule mpaka wakamaliza tofauti zao. Raya akaja mpaka pale kitandani na kunibusu mdomoni, Shamila akageuka na kulishuhudia tukio hilo.
SASA ENDELEA...
Alipogundua kwamba namtazama, harakaharaka Shamila alijifanya kama hakuwa ameona chochote.
“Leo nimekupikia chakula kizuuri, naamini utakipenda,” alisema Raya huku akianza kuniandalia chakula. Nikawa nimetulia pale kitandani huku akilini mwangu mawazo mengi yakipita. Nilikuwa nimeingia kwenye mtego hatari sana ambao sasa ilikuwa ni lazime nifanye kila kinachowezekana kujikomboa.
Njia pekee ambayo ingenisaidia, ilikuwa ni kuhakikisha baba yake Shenaiza na kundi lake lote wanafikishwa mbele ya sheria na mamia ya watu ambao maisha yao yalikuwa hatarini, wanaokolewa kutoka kwenye shimo la mauti.

Ni jambo hilo pekee ndiyo lingenifanya niwe na amani kwa sababu bila kumdhibiti baba yake Shenaiza, maana yake ni kwamba angeendelea kunisaka kwa lengo la kuniua, akiamini tayari kuna siri zake nyingi nazijua, lakini pia maana yake ni kwamba baada ya kunimaliza mimi, angefuatia Shenaiza na baada ya hapo, angeendelea na kazi yake haramu ya kuteketeza maisha ya watu bila huruma.
“Mbona unaonekana kama una mawazo mengi, nini kinakusumbua?” swali la Raya ndilo lililonizindua kutoka kwenye dimbwi la mawazo. Akaacha kuandaa chakula na kunisogelea, akaniinamia pale kitandani na kunibusu kwenye paji la uso, akawa ananiuliza kwa upole kinachonisumbua.
Mpaka muda huo, Raya hakuwa akielewa chochote kilichokuwa kinaendelea, zaidi ya kufahamu tu kwamba nilikuwa hospitalini nimelazwa baada ya kuvamiwa na majambazi ambao almanusra wayakatishe maisha yangu. Hakuwa anajua ‘connection’ iliyokuwepo kati ya matukio yaliyokuwa yananitokea hata kidogo.
“Kuna jambo linanisumbua sana kichwa changu.”
“Jambo gani mpenzi wangu, si unajua sipendi kukuona ukikosa raha?”
“Najua mpenzi wangu, mambo yamenifika shingoni,” nilimwambia Raya, akazidi kunidadisi ambapo nilimwambia aniandalie kwanza chakula mengine tutaongea baadaye.
Kwa jinsi hali ilivyokuwa, sikuona sababu ya kuendelea kumficha Raya, nilitaka nimueleze ili naye akae akiwa anaelewa kuhusu kipindi kigumu nilichokuwa napitia ili kama kuna msaada wowote anaweza kunisaidia afanye hivyo.
Baada ya kumaliza kuandaa chakula, alinisogezea na kuanza kunibembeleza nile. Kwa jinsi alivyokuwa amepika chakula vizuri, nilikula chote mpaka nikamaliza, jambo ambalo lilimfurahisha sana.
“Enhee, haya niambie sasa,” alisema baada ya kumaliza kutoa vyombo, kama nilivyokuwa nimedhamiria kutoka ndani ya moyo wangu, nilianza kumueleza ukweli wa kila kitu. Jambo pekee ambalo sikumueleza, kama ilivyokuwa kwa Shamila, ni kile kilichonitokea baada ya kupoteza fahamu. Nilihisi naweza kumjaza woga moyoni akaanza kunitazama kwa macho yasiyo ya kawaida.
Nilimficha pia suala la mimi na Shamila kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, nikamwambia kwamba alitokea kuguswa na kilichonipata na kuamua kunisaidia kwa sababu hata yeye kuna ndugu yake amewahi kusafirishwa na shirika hilo na mpaka muda huo hawakuwa na mawasiliano naye. Niliamua kutumia uongo huo ili asishtuke mapema kwamba mimi na Shamila tulikuwa na uhusiano wa kimapenzi
Kiukweli Raya alishtuka sana nilipomueleza kilichokuwa kinaendelea, akawa hataki kuamini, akawa anahisi labda nimeamua kumtungia stori za kumtisha. Nilimhakikishia kwamba kila kitu nilichomwambia ni kweli na kama anataka kuthibitisha, ipo siku atajionea mwenyewe.
Nilimuona Raya akishusha pumzi ndefu, akainua shingo yake akiwa anatazama huku na kule kisha akanigeukia: “Kwa hiyo wewe ulikuwa umeamuaje?”
“Ni lazima nipambane nao.”
“Jamal, umechanganyikiwa nini? Unawezaje kupambana na watu hatari kama hao?”
“Ni lazima nifanye hivyo Raya, sipo tayari kufa kama kifaranga cha kuku mbele ya mwewe, ni lazima nipambane.”
‘Sidhani kama hilo ni jambo sahihi kwa sasa, isitoshe bado hata afya yako haijawa poa, kwa nini tusitafute sehemu nje ya Dar tukaenda kujificha huko na kuanzisha maisha yetu bila mtu yeyote kujua? Mimi nipo tayari hata sasa hivi na naamini nikiwaambia wazazi wangu watakuwa tayari kutusaidia,” alisema Raya, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama.
“Ni lazima nipambane Raya, siwezi kuwakimbia. Najua ni kazi ngumu lakini mwisho wa siku ni bora nife nikiwa napambana,” niliendelea kushikilia msimamo, raya akawa hana cha kuniambia tena.
Bado alikuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu ndani ya kichwa chake, akawa ananiuliza kila alipokuwa anakumbuka. Aliniuliza kama watu hao ndiyo walioenda kuvunja nyumba yangu siku ile usiku, nikamjibu kwamba kwa ushahidi huo, inaonesha moja kwa moja kwamba ni wao.
Maswaliyalikuwa mengi mpaka ikabidi nimkatishe, nikamwambia anatakiwa kupeleka vyombo nyumbani ili na yeye apate muda wa kupumzika, nikamuona akisimama kwa shingo upande na kukusanya vitu vyake.
“Nimeongea na daktari, anasema naweza kuruhusiwa ndani ya siku hizi mbili kwa sababu naendelea vizuri.”
“Ooh! Itakuwa vizuri sana, sasa umepanga ukitoka ukaishi wapi?”
“Itakuwa ni siri yangu lakini kwa sasa sitakiwi kukaa pale kwangu kwa sababu najua watakuwa wananiwinda usiku na mchana.”
“Natamani sana tukaishi nyumbani kwetu, wazazi wangu wanakaribia kurudi lakini usijali ile nyumba ni kubwa, wanaweza kukupa hata vyumba vya uani, ukakaa hapo chini ya uangalizi wangu mpaka mambo yatakapotulia.”   
“Ahsante sana mpenzi wangu, hivi kazini unaenda kweli wewe?”
“Kazini siendi, nimeomba ruhusa kwamba nakuuguza wewe, kwanza ukiwa kama mfanyakazi mwenzangu na pia ukiwa mume wangu mtarajiwa, kwa hiyo usijali,” alisema Raya huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akakusanya vitu vyake, akaja kunibusu kisha akaniaga.
Akatoka na kufunga mlango, mara Shamila naye akaingia, ni kama alikuwa amekaa sehemu anasubiri aondoke tu ili na yeye aingie. Akaja uso akiwa ameukunja, nilishaelewa ni kwa sababu gani yupo kwenye hali hiyo.
“Vipi?”
“Mbona unapenda kunitesa Jamal, kwani huyo mwanamke wako huwezi kumkataza kukubusu mbele yangu?”
“Siyo hivyo mpenzi wangu, naomba kaa kwanza tuzungumze.”
“Sitaki, na kwa sababu yeye ameanza basi mimi namaliza,” alisema Shamila na kwenda kufunga mlango kwa funguo, akashusha na mapazia yote, nikawa sielewi alichokuwa anataka kukifanya.
“Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilishtuka kumuona akianza kufungua vifungo vya gauni lake la kazini, mara akalivua na kubaki na sidiria na nguo ya ndani tu, ukichanganya na jinsi alivyokuwa amegawanyika na kujaa sehemu za katikati, nilijikuta nikikosa cha kufanya.
“Una..ta..ka kufa...nya ni...ni,” sikumalizia kauli yangu, akawa tayari ameshafikapale kitandani, tukagusanisha ndimi zetu huku Shamila akionesha kweli kudhamiria kile alichokitaka. Hakuogopa kabisa kwamba pale ni wodini.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

2 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...