Thursday, September 21, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 38


ILIPOISHIA:
“Mara ya mwisho mlizungumza naye lini?”
“Kiukweli tangu aondoke hatujawahi kuzungumza naye, wanasema hospitalini hawaruhusu kutumia simu,” alijibu mwanaume huyo, nikashusha pumzi ndefu.
SASA ENDELEA...
Majibu ya watu hao wawili tu yalitosha kunifanya nielewe kilichokuwa kinaendelea lakini ili kupata ushahidi mkubwa zaidi, niliendelea kuwapigia simu wengine. Wachache hawakuwa wakipatikana hewani lakini karibu watu 16 wote walikuwa wakipatikana na majibu yao hayakuwa yakitofautiana.
Wapo waliosema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwenda kusoma nje ya nchi kwa msaada wa shirika hilo, wengine wakasema walipelekwa kwa matibabu lakini asilimia kubwa walisema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwa ahadi ya kwenda kutafutiwa kazi nchi za Uarabuni, India, Marekani na nchi za Ulaya.
“Kwani binti yako ana elimu kiasi gani mpaka uamini kwamba anaenda kutafutiwa kazi nzuri huko anakokwenda?”
“Kiukweli wala hajasoma, aliishia darasa la saba tu lakini tukaambiwa kule kuna watu wanatafutwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za ndani, na mshahara wake ni mkubwa kuliko hata mameneja wengi wa Tanzania, ndiyo maana tukamruhusu kwa shingo upande.
“Isitoshe kabla ya kuondoka, viongozi wa shirika hilo walitupa shilingi milioni moja kama shukrani tu na hapo ni nje ya mshahara wa binti yetu,” mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Akilimali, aliniambia wakati akizungumza nami kwenye simu.
“Uko bize sana na simu mpenzi wangu, kitaalamu simu huwa inatoa mionzi ambayo siyo mizuri kwa mtu kama wewe kwani inaweza kukuongezea matatizo mpenzi, au wewe hulioni hilo?” alisema Shamila baada ya kuingia wodini, ikiwa imepita takribani nusu saa tangu nilipomtaka yeye na Raya watoke na kunipisha.
Nilishindwa hata nimjibu nini, akanisogelea na kunibusu kwenye paji la uso wangu, akakiweka kitanda vizuri kisha akakaa pembeni yangu.
“Eti, unalijua shirika linaloitwa Black Heart?” nilimuuliza Shamila, akanitazama kwa macho ya mshangao kama anayejiuliza ‘umelijuaje?’.
“Jamal!” aliniita huku sauti yake ikionesha kuwa na hofu kubwa.
“Kumbe hicho ndicho ulichokuwa ukikihangaikia muda wote?”
“Ndiyo, kwani kuna tatizo?”
“Ni hatari mpenzi wangu, nakupenda sana na sitaki kuona ukipatwa na jambo lolote baya.”
“Kivipi? Mbona sikuelewi Shamila?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
“Kuna siku uliniuliza kuhusu yule mgonjwa anayeitwa Shenaiza, nikakueleza kwa kifupi kwamba baba yake siyo mtu mzuri hata kidogo.”
“Ndiyo nakumbuka, sasa kwani kuna uhusiano gani na hiki nilichokuuliza?” nilimtega Shamila kwani ilionesha kuna mambo mengi anayajua lakini anaogopa kuniambia.
“Usinifanye mimi mjinga Jamal, najua kila kitu kuhusu unachokifanya tangu mwanzo, najua kwamba unachimba kutaka kujua baba yake Shenaiza anashughulika na nini lakini nakuomba sana, achana na hicho unachokifanya.
“Watu wengi wameshapotea kwa sababu ya kumfuatilia huyo mzee! Jamal, mwenzio nakupenda na sitaki kuona ukipotea ndiyo maana nakwambia achana na hayo mambo.”
“Hapana, ni lazima niikamilishe hii kazi Shamila, nimerudi duniani kwa ajili ya kazi hii, sitaogopa chochote wala sitarudi nyuma,” nilimwambia kwa msisitizo, akanitazama tena machoni na kushusha pumzi ndefu kwa mara nyingine, akatazama huku na kule kuhakikisha hakuna mtu anayetusikiliza.
“Mhusika mkuu wa hiyo Black Heart ni baba yake Shenaiza.”
“Ni shirika la nini?”
“Kwa nje linajitambulisha kama shirika la kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali, kuwasafirisha wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, kuwalipia gharama za masomo watoto na vijana kutoka kwenye familia maskini pamoja na kuwatafutia kazi nzuri wananchi nje ya nchi.”
“Umesema kwa nje, vipi kwa ndani?”
“Jamal, unajua mpaka nafikia hatua ya kuufungua mdomo wangu kukwambia masuala haya ninayahatarisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa kwa sababu ikija kufahamika kwamba mimi ndiyo niliyekwambia nitauawa mwenzako,” alisema Shamila kwa hofu kubwa. Sikuelewa hasa hofu yake ilikuwa ikisababishwa na nini. Nikamtoa wasiwasi kwamba nitamlinda, akaniambia kuwa sina uwezo wa kumlinda kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa nahitaji kulindwa ndiyo maana nilishindwa kujitetea siku nilipovamiwa na kutaka kuuawa.
Ni kweli alizungumza pointi lakini nilijivisha roho ya kiume, nikaendelea kumtoa wasiwasi na kujitutumua kwamba siku hiyo walinibahatisha tu, akakubali kunieleza kwa upana.
Aliniambia kwamba licha ya shirika hilo kujinadi kwa sura hiyo ya nje, likijifanya linasaidia jamii ya watu maskini, ukweli ni kwamba lilikuwa likifanya biashara haramu ya viungo vya binadamu. Akaendelea kuniambia kwamba shirika lilikuwa na mtandao mpana, likiwagusa viongozi kadhaa wa ngazi za juu serikalini pamoja na watu wengine wenye taaluma mbalimbali, wakiwemo madaktari.
Aliniambia kwamba watu wote waliokuwa wakisafirishwa kwenda nje ya nchi na shirika hilo, walikuwa wakienda kutolewa viungo vyao muhimu, kama moyo, mapafu, figo na vingine vingi, vikitolewa na kupandikizwa kwa watu waliokuwa wakivihitaji.
Akaniambia kwamba kwenye nchi zilizoendelea, kuna watu wengi wanaojiweza kifedha lakini wanakuwa na matatizo mbalimbali ya kiafya kiasi kwamba fedha zao haziwasaidii kupona kwa kutumia madawa mbalimbali ya hospitalini. Ni hao ndiyo waliokuwa wateja wakubwa wa viungo hivyo vya binadamu.
Akanifafanulia kwamba; kwa mfano kama kuna tajiri ana matatizo ya figo au ini na ameshatumia madawa yote bila kupata nafuu, njia nyepesi ya kumrudishia afya bora ilikuwa ni kupandikizwa viungo vingine kutoka kwa mtu asiye na matatizo.
Akasema kwa kuwa uhitaji ni mkubwa siku hizi kutokana na mtindo wa maisha, hasa kwa nchi zilizoendelea, njia nyepesi iliyokuwa inatumiwa na baba yake Shenaiza na wenzake, ilikuwa ni kuwasafirisha watu kutoka nchi za kimaskini na kwenda kuwauza kwa bei ghali kwa ajili ya kutolewa viungo vyote muhimu ambavyo huwekewa watu wanaojiweza kiuchumi.
Maelezo yake yalinishangaza na kunishtua sana, akanihakikishia kwamba tangu shirika hilo lianze kufanya kazi miaka kadhaa iliyopita, hakukuwa na hata mtu mmoja ambaye aliondoka na kurejea nyumbani salama, wengi walikuwa wakirejeshwa wakiwa maiti na wengine hawakuwa wakirejeshwa kabisa.
Ndugu zao wanapowaulizia, hutulizwa kwa kupewa fedha na kuambiwa wapo salama na ipo siku watarejea nchini.
“Ina maana serikali kupitia kwa vyombo vya usalama hawajui kuhusu hiki kinachoendelea?”
“Watu wanajua sana, lakini nimeshakwambia huu ni mradi wa vigogo wakubwa serikalini, hakuna anayeweza kufumbua mdomo wake na ukijaribu tu, basi ujue kifo kinakuita.”
Japokuwa mle wodini mlikuwa na kipupwe, nilijikuta nikitokwa na kijasho chembamba, mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini Shamila alikuwa akinikataza kujihusisha na mambo yale.
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...