Thursday, September 7, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 32


ILIPOISHIA:
Nilipomtazama usoni, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho yake yakatua kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
SASA ENDELEA...
“Umebadilisha nguo saa ngapi? Na hiyo fulana umeipata wapi mbona inanukia pafyumu ya kike?” alinihoji Raya uso akiwa ameukunja, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, huku nikiuvaa ujasiri wa kiume.
“Yaani hiyo ndiyo salamu? Ama kweli mapenzi yamepungua, kwa hiyo hata nikifa huwezi kujali tena?” ilibidi nimgeuzie kibao Raya. Moyoni nilikuwa najua kwamba nakosea lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili kutuliza hali ya mambo.
“Wewe ndiyo wa kunitamkia mimi maneno hayo? Nikupende vipi Jamal, kwa nini unautesa moyo wangu?” alisema Raya na kuanza kuangua kilio. Kauli yangu ni kama ilikuwa imeenda kutonesha donda ndani ya nafsi yake.
Nilijisikia vibaya lakini ikabidi niendelee ‘kumkazia’, nikamwambia wakati anaondoka kwa kususa, nilikuwa nikimfuata lakini kwa bahati mbaya nikaanguka na kusababisha jeraha langu lifumuke na kuanza kumwaga damu.
“Huoni kwamba nimefungwa plasta na bandeji upya? Kama huamini muulize yule nesi, amenisaidia sana, huenda sasa hivi ungekuja na kukuta stori nyingine,” nilimwambia Raya, kauli ambayo ilionesha kumshtua mno.

“Mungu wangu, kwani ilikuwaje?” alisema Raya huku akikaa pembeni ya kitanda changu, akawa anajifuta machozi huku akionesha kushtushwa mno na nilichomweleza, nikamwambia shati langu lilikuwa halitamaniki kwa damu na kwamba hiyo fulana nilikuwa nimesaidiwa tu na msamaria mwema.
Maskini Raya! Alianza kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake, ule moto aliokuja nao ukazimika, akaanza kunipa pole na kuniomba msamaha kama ameniudhi! Yaani japokuwa mimi ndiyo nilikuwa na makosa, yeye ndiyo alikuwa akiniomba msamaha!
Nilimkubalia na kumuomba apunguze wivu kwa sababu nampenda yeye peke yake na ukaribu wangu na Shenaiza ulikuwa ni kwa sababu maalum tu. Hakutaka tena kuendelea kulizungumzia suala hilo, akili yake yote akaielekeza kwangu kuhakikisha nakula vizuri chakula alichokuwa ameniandalia.
Nilikifurahia chakula alichokuwa ameniandalia, nikala vizuri na kumfanya na yeye afurahi, nikamshukuru kisha akatoa vyombo na kuvirudisha kwenye kikapu chake, akasafisha kila kitu pale kitandani kwangu kisha akakaa tena pembeni yangu, mkono wake mmoja ukiwa kwenye mwili wangu, mara kwa mara akawa ananibusu kwa mahaba mazito.
“Niambie kama kweli unanipenda Jamal!”
“Nakupenda sana Raya na kwangu wewe si tu mpenzi, bali mke mtarajiwa, namshukuru Mungu kwa kukuleta karibu yangu,” nilimwambia, nikamuona akitabasamu.
Maneno yangu matamu yalienda kumaliza kila kitu, nikaendelea kumpamba, akawa anacheka kwa furaha utafikiri siyo yule aliyeingia macho yakiwa yamemvimba na kuwa mekundu kwa kulia. Nikawa nimefanikiwa kabisa kumsahaulisha mabaya yote.
Mpaka muda wa kuondoka unafika, Raya alikuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, akaniaga kwa kunimwagia mvua ya mabusu na kuniambia kwamba anatamani angelala na mimi wodini lakini kwa kuwa sheria haziruhusu, tutaonana asubuhi ya siku inayofuatia, akaondoka zake.
“Huyo ndiyo Raya?”
“Ndiyo! Vipi kwani mbona umeniuliza hivyo?”
“Aah, nilitaka tu kumjua vizuri,” nesi Shamila aliongea huku akionesha kabisa kuwa na kinyongo ndani ya moyo wake. Kumbe muda wote wakati nikizungumza na Raya, alikuwa kwenye ofisi ya manesi akitusikiliza kila kitu kwa mbali, akajikausha kama hayupo mpaka Raya alipoondoka.
“Kumbe hanizidi kwa uzuri, tena isitoshe mimi tayari nina kazi, naishi kwangu na kuendesha maisha yangu bila tatizo lolote. Mwanaume atakayenioa atafaidi sana,” Shamila alijipigia debe, nikawa nimeshamuelewa kwa nini anasema vile, nikakosa hata cha kumjibu.
“Si naongea na wewe mbona hunijibu?”
“Sasa nitakujibu nini Shamila? Ndiyo maana nimebaki kimya,” nilimwambia kwa upole. Sikutaka kumuudhi kwa sababu naye alikuwa na umuhimu mkubwa kwenye maisha yangu, katika kipindi hicho nilichokuwa hospitalini hapo chini ya uangalizi wake.
Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale, mara kwa mara akimtoa kasoro Raya na kujisifia, nikawa namuunga mkono kwa sababu kama nilivyosema sikutaka kumuudhi na kubwa zaidi, nilikuwa nataka kumtumia kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu baba yake Shenaiza.
“Hivi ukiniangalia unahisi nitaruhusiwa lini kutoka?”
“Mh! Yaani wewe unafikiria kutoka? Unajiona umeshapona siyo? Unajua wewe unashangaza sana!”
“Nashangaza kivipi?”
“Hivi unajua tangu ulipoletwa hapa hospitalini na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, ulikaa siku ngapi bila kurudiwa na fahamu zako?” Shamila aliniuliza.
“Sasa kwani kuna uhusiano gani kati ya nilichokuuliza na hayo unayoyasema?”
“Nakuona una mambo mengi sana. Ndiyo kwanza umerudiwa na fahamu zako lakini hutulii, mara uinuke kitandani, mara umkimbilie huyo Raya wako, mara uende wodini kwa Shenaiza na sasa hivi unaulizia siku ya kutoka,” alisema Shamila, nikaona ni kama alikuwa amenipania.
Nilijua nini kilichokuwa kikimsumbua ndani ya moyo wake. Ni kweli sikuwa na muda mrefu tangu nirejewe na fahamu lakini kwa kuwa mwili wangu ulikuwa na nguvu, sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda, hasa ukizingatia kwamba kuna kazi kubwa ilikuwa inanisubiri.
“Hata madaktari wenyewe nikiwaeleza hizo hekaheka ulizonazo, watashauri uwe unachomwa sindano za usingizi muda wote ili uendelee kupumzika, sijawahi kuona mgonjwa msumbufu kama wewe,” Shamila alizidi kunishukia.
Nisingeweza kuendelea kusubiri wodini hapo eti mpaka niruhusiwe na madaktari, kitu pekee nilichoona ni kikwazo kwangu kufanya kazi niliyotumwa, niliona ni lile jeraha la kifuani tu ambalo nilikuwa nimelitonesha.
Hayo mambo ya kupoteza fahamu hayakuniingia akilini kwa sababu kwanza siyo kweli kwamba nilipoteza fahamu na kulala tu kitandani nikiwa sielewi kinachoendelea bali kilichokuwa kimetokea ilikuwa ni kama tu kuhama kutoka ulimwengu mmoja mpaka mwingine.
Jambo ambalo kwa mtu mwenye akili alipaswa kujiuliza, hivi inawezekana vipi mtu aliyekuwa amepoteza fahamu, awe na pilikapilika nyingi muda mfupi baada ya kurejewa fahamu hizo kama mimi?
Yaani mtu umetolewa leo kwenye mashine ya kukusaidia kupumua ukiwa mahututi halafu saa chache baadaye unaweza kusimama na kutembea mwenyewe kutoka wodi moja hadi nyingine? Kulikuwa na siri kubwa iliyojificha ndani ya moyo wangu.
Kwa jinsi Shamila alivyoanza kunibadilikia kwa sababu ya wivu wake wa kimapenzi, niliona njia nyepesi ya mimi kupata kile nilichokuwa nakitaka, ni kumuingiza kwenye mtego wa mapenzi, kwamba nijifanye nampenda sana yeye kuliko Raya, nimuaminishe kwamba atakuwa mpenzi wangu ili nimtumie vizuri kupata kile nilichokuwa nakitaka.
Ilikuwa ni lazima kesho yake niende kule nilikoelekezwa na Shenaiza kukutana na mdogo wake anipe hiyo bahasha yenye maelezo yote kuhusu kilichokuwa kinafanywa na baba yake lakini hilo lingewezekana tu kama ningekula njama na Shamila, ikabidi nianze kucheza na akili yake.
“Lakini Shamila, kwa nini unaongea na mimi kwa ukali kiasi hicho? Au nimekosea kukuonesha hisia zangu kwamba nakupenda?” nilimwambia, nikamuona akishtuka kuliko kawaida, akanitazama kwa macho yake mazuri.
“Kwani umewahi kuwa na hisia za kunipenda Jamal?” alinihoji, safari hii kwa sauti ya chini na ya upole, akawa ananisogelea pale kitandani huku akinitazama kwa macho yaliyobeba hisia nzito.
“Nakuapia kama ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu na si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu, akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu la kifuani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...