Saturday, September 2, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 28


ILIPOISHIA:
Niliendelea kumkumbatia msichana huyo huku marafiki na jamaa zangu wengine wakiwa pembeni wakitutazama, tukiwa kwenye hali hiyo, nilisikia mlango wa wodi ukifunguliwa na mtu akaingia mbiombio mpaka pale kitandani kwangu, nikashtuka na kumuachia Raya, Raya naye akainua uso wake, watu wote tukawa tunamtazama kwa mshangao mtu yule aliyeingia, tukiwa ni kama hatuamini.
SASA ENDELEA...
Hakuwa mwingine, bali Shenaiza ambaye alikuwa amevaamavazi ya hospitalini hapo kuonesha kwamba alikuwa amelazwa, mkononi akiwa na sindano iliyofungwa na plasta, nafikiri kwa ajili ya kumuingizia dawa au kumtundikia dripu, nikawa namtazama usoni, naye akawa ananitazama.
“Jama! Kumbe ni kweli hujafa?” alisema Shenaiza kwa sauti ya kukwamakwama, wote tukatazamana tena kisha nikageuka na kumtazama Shenaiza, alionesha kabisa kwamba hakuwa sawa, nikawa najiuliza maswali mengi kichwani ambayo sikuwa na majibu yake.
Nilikumbuka kwamba kuna muda mimi na Shenaiza tulikuwa tumnekaa siti moja kwenye treni la ajabu, tukielekea kusikojulikana, giza likiwa limetanda kila sehemu. Kama mimi nilikuwa kitandani, wodini, na Shenaiza naye alikuwa hospitalini hapo akiwa amelazwa, ina maana kwamba mimi na yeye tulikutana wapi?
Nilikumbuka pia kwamba yeye mwenyewe aliniambia kwamba ameamua kuyakatisha maisha yake kwa kujiovadozi dawa ya usingizi, na kwamba aliamua kufanya hivyo kama njia ya kupumzika na mateso aliyokuwa anayapata, sasa Shenaiza aliyejiua ni nani na huyo aliyekuwa amesimama mbele yangu ni nani?
Nilihisi kama kichwa kinapata moto kwa sababu ya utata wa kilichokuwa kinaendelea, hata hivyo nilipoemndelea kutuliza kichwa changu, nilianza kupata baadhi ya majibu.
“Kumbe kweli hukufa?” Shenaiza aliniuliza tena swali lile ambalo lilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.

“Hebu naomba mtupishe kidogo nizungumze na Shenaiza,” niliwaambia watu wote waliokuwa wamenizunguka pale wodini lakini Raya alikataakatakata.
“jamal! Are you out of your mind?” (Jamal umechanganyikiwa) alisema raya kwa sauti ya juu. Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza ndiye aliyekuwa chanzo cha mimi kutaka kupoteza maisha, iweje leo nimuone yeye ndiyo wa maana kiasi c ha kuwataka watu wote watoke nje?
“Kama amekuja kwa lengo la kukumalizia je? Mimi siendi popote, nitakaa hapahapa kukulinda,” alisema Raya huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara, nikashindwa cha kufanya.
Wale watu wengine wote walitoka lakini kama Raya alivyosema, hakutaka kuinuka pale pembeni ya kitanda changu alipokuwa amekaa na mimi sikuona sababu yoyote ya kumlazimisha.
Bado tulikuwa tukiendelea kutazamana na Shenaiza, kadiri nilivyokuwa nazidi kumtazama ndivyo nilivyokuwa naendelea kukumbuka mambo mengi yaliyotokea kwenye ulimwengu usio wa kawaida na kwenye ulimwengu wa kawaida.
“Haya sema shida yako iliyokuleta,” Raya alivunja ukimya, Shenaiza akashusha pumzi ndefu na kusogea kwenye kitanda nilichokuwa nimelazwa.
‘Samahani dada wala mimi sijaja hapa kwa nia mbaya, kwanza nimejikaza tu kwani bado naumwa sana, nimetoroka tu wodini baada ya kusikia Jamal yupo hapa,” alisema Shenaiza kwa sauti ya chini, nikamuona Raya naye akishusha pumzi kwani alishajiandaa kwa shari lakini msichana huyo akaonesha kwamba hakuwa amekuja kisharishari.
“Nilisikia kwamba umekufa na mimi nilithibitisha hilo,” alisema Shenaiza kwa upole, nikamuliza amesikia wapi na amethibitishaje hilo?
“Niliambiwa na daktari mmoja kati ya wale waliokuwa wanakutibu, akaniambiakwamba ulishakata roho lakini walikuwa wamekuunganisha kwenye mashineya kusaidia moyo wako uendelee kudunda, akanihakikishia kwamba saa chache baadaye watakutoa kwenye mashine hiyo.
“Mh! Sikuelewi! Raya wewe unamuelewa anachokisema huyu?”
“Mimi namuelewa, ni kweli hata mimi daktari aliniambia kwamba huwezi kupona,” alisema Raya na kunifanya nikose cha kujibu, nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine usoni kwa zamu. Unajua miongoni mwa mambo ambayo sikuwa nataka kuyasikia, ni kwamba eti watu wote walikuwa wanajua kwamba nimekufa.
“Halafu kuna mambo yananichanganya sana kichwa changu, sijui ni ndoto, maruweruwe au uchawi hata sielewi. Mbona nakumbuka kama mimina wewe kuna sehemu tulikutana halafu tukaongea mambo mengi tu? Na kubwa zaidi mbona nakumbuka kama na mimi nilikufa?”
Swali hilo la Shenaiza liliunga kabisa na kile nilichokuwa nakifiria kichwani mwangu muda wote. Ni kweli hata mimi nilikuwa najua kwamba kuna sehemu mimina Shenaiza kuna sehemu tulikuwa pamoja na tukazungumza mambo mengi tu pamoja, tena tukiwa tumekaa kwenye siti moja kwenye treni la ajabu.
“Utakuwa ulikuwa unaota, ulikutana wapi na Jamal wakati tangu siku ile ulipomsababishia atake kufa hajainuka kitandani na leo ndiyo amefumbua macho?” Raya aliingilia mazungumzo yale, sote tukawa tunamtazama kwa sababu hakuwa akijua chochote.
“Mh! Inawezekana kweli nilikuwa naota, kwa sababu katika maisha yangu sijawahi kupanda treni hata siku moja lakini nakumbuka eti tulikuwa tumekaa kwenye siti mojaya treni,” alisema Shenaiza na kuzidi kunihakikishia kwamba kumbe kile kilichotokea kilikuwa ni jambo halisi, Raya akazidi kubisha.
“Sasa mtu yupo kitandani anaumwa hoi hajitambui atapandaje treni? Dada ulikuwa unaota na sidhani kama Jamal anahitaji kusikia ndoto zako, kama hicho ndicho kilichokuleta naomba uondoke, mgonjwa anahitaji kupumzika,” alisema Raya kwa msisitizo.
“Basi tuachane na hayo, Jamal nimekuja kukuomba msamaha!”
“Msamaha wa nini Shenaiza?”
“Kwa yote niliyokufanyia. Haikuwa kusudioa langu kukuingiza kwenye matatizo, najua wewe na watu wako wote wa karibu mnanichukia sana.”
“Msamaha wako una maana gani leo? Kama angekuwa amekufa ungemuomba nani msamaha? Dada hebu nakuomba uondoke,” Raya alijibu kwa ukali, nikamuona Shenaiza akijiinamia na kuanza kuangua kilio.
“Wewe! Kwa nini unatusumbua kukutafuta? Kwa nini unatoka wodini bila taarifa wakati unajua hali yako siyo nzuri? Unatusababishia matatizo kwa ndugu zako,” manesi wawili waliingia mbiombio mle wodini, akawamshika Shenaiza huku an kule na kumtoa msobemsobe huku mwenyewe akiendelea kuangua kilio. Mimi na Raya tukatazamana!
“Inaonesha mnafahamiana kuliko hata mimi ninavyojua, huyu si mmekutana juzijuzi tu hapo, mbona inaonesha kama kuna kinachoendelea nyuma ya pazia?” Raya aliniuliza, akionesha dhahiri kuwa na wivu mkali ndani ya moyo wake, nikashindwa cha kumjibu.
“Jamal, nakupenda sana mpenzi wangu, nakuomba uamini ninachokisema. Sijawahi kumpenda mtu yeyote katika maisha yangu na wewe mweyewe ni shahidi kwamba umenikuta nikiwa simjui mwanaume yeyote.
“Niliamua kukupa zawadi ya kuwa mtu wa kwanza kunijua na nataka uwe wa mwisho kwangu, nataka unioe tuishi pamoja milele Jamal,” alisema Raya huku machozi yakimlengalenga.
Kiukweli na mimi nilikuwa nimetokea kumpenda Raya baada ya kuwa nimeutezsa moyo wake kwa kipindi kirefu na kweli nilishaanza kuweka mnalengo ya maisha yangu ya baadaye nikiwa naye lakini niliona kama huo siyo muda muafaka wa kuzungumzia mapenzi.
Ndiyo kwanza nilikuwa nimerejea kwenye ulimwengu wa kawaida, bado kuna maswali mengi ambayo sikuwa nimeyapatia majibu, kuhusu mimi mwenyewe na pia kumhusu Shenaiza na familia yake.
Hata hivyo, sikutaka Raya ajisikie vibaya kwa namna yoyote, mwenyewe nilishajiwekea nadhiri moyoni kwamba nitakuwa sehemu ya furaha ya raya, hasa baada ya kugundua ni kwa kiasi gani alikuwa akinipenda.
Nikamkumbatia na kubusu kwenye paji lake la uso, nikamwambia hakuna chochote kinachoendelea kati yangu na Shenaiza isipokuwa ilikuwa ni lazima niendelee kuwa naye karibu kwa sababu kuna mambo muhimu ilikuwa ni lazima niyajue, hasa kuhusu baba yake Shenaiza.
“Kuna kazi nimepewa ya kuhakikisha namzuia baba yake Shenaiza hicho anachokifanya, na ni lazima nitimize.”
“Kazi? Nani aliyekupa hiyo kazi? Halafu umzuie kwani anafanya nini na wewe umejuaje?” Raya alinibana kwa maswali, nikawa nashindwa hata namna ya kumjibu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.

       

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...