Friday, September 1, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 27



ILIPOISHIA:
Nilipokuja kushtuka, nilijikuta nikiwa nimelala kitandani, mapigo yangu ya moyo yakinienda mbio kuliko kawaida, nikiwa nimeunganishwa mashine ya kunisaidia kupumua huku mwili wangu ukiwa umeunganishwa na vifaa vingi vya kitabibu, milio ya mashine mbalimbali ikisikika ndani ya chumba kile ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba ni wodini.
“Amefumbua macho! Dokta... amefumbua macho! Njooni haraka!”
SASA ENDELEA...
Harakaharaka madaktari wengi waliingia ndani ya kile chumba na kuzunguka kitanda changu, kwa mbali nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine, wote wakionekana kukiinamia kitanda changu. Macho yangu yalikuwa na ukungu, hali iliyonifanya nisiwe na uangavu wa kutosha machoni kuwaona ingawa bado nilikuwa na uwezo wa kutambua sura zao.
“Unaendeleaje Jamal?” nilisikia daktari mmoja akiniuliza. Kwa jinsi sauti yake ilivyokuwa ikisikika, ilikuwa mithili ya inayotoka kwenye redio mbovu. Nilijaribu kufumbua mdomo lakini nilishindwa kwani nilikuwa nimeunganishwa na mabomba mengi, mdomoni na puani, nikawa natingisha tu kichwa kuashiria kwamba najisikia vizuri.
Jopo la madaktari waliendelea kunizunguka pale, nikamuona mwingine akinipima kwa kutumia kifaa maalum kusikiliza mapigo ya moyo wangu, mwingine akaniweka ‘thermometer’ kwapani kwa lengo la kunipima joto huku mwingine akiwa bize kufuatilia maandishi yaliyokuwa yanaonekana kwenye mashine inayofanana na kompyuta, iliyokuwa ikipiga kelele kwa kutoa milio ya ‘kubipu’ kila mara.
“He is recovering! His heartbeats are stabilizing, blood sugar is coming to normal and the wound is healing!” alisema daktari mmoja wakati akiwaambia wenzake, kwa kuwa Kiingereza hakikuwa kikinipiga chenga, niliweza kuelewa vizuri kwamba alikuwa akiwaambia wenzake kwamba nimeanza kupata nafuu, mapigo yangu ya moyo yanaimarika, kiwango cha sukari kinarudi kwenye hali ya kawaida na jeraha langu linapona.

Niliwaona wote wakitabasamu na kunitazama usoni, kila mmoja akawa ananipongeza kwamba eti nimepigania vizuri maisha yangu kwa sababu nilikuwa na hali mbaya sana. Daktari mwingine ambaye kiumri alikuwa kijana mdogo, alinitania kwamba eti mimi ndiye binadamu wa kwanza niliyeweza kwenda kuzimu na kurudi, wenzake wote wakacheka.
Japokuwa mwenyewe alizungumza kama utani na wenzake nao wakacheka wakichukulia utani, kile alichokisema hakikuwa utani ingawa siwezi kusema kwamba kule nilikofika ndiyo kuzimu kwenyewe au la lakini ukweli ni kwamba nilikuwa nimefika mahali ambako sidhani kama kuna binadamu aliye hai amewahi kufika.
Kuna muda nilihisi huenda bado nipo kwenye ile hali ya kuuona mwili wangu wakati mwenyewe nikiwa pembeni lakini haikuwa hivyo, ni kweli nilikuwa nimerejewa na fahamu na kila kilichokuwa kinaendelea kilikuwa kikitokea kwenye ulimwengu halisi.
Unajua namna nyepesi ya kujigundua kwamba unaishi kwenye ulimwengu wa kawaida unapoona upo kwenye mazingira ambayo huelewielewi kama upo ndotoni au la, ni kujaribu kupepesa macho, kukunja vidole vya mikono au kuigusa ngozi ya mwili wako kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Ukiona umeweza kupepesa macho, kukunja vidole au umesikia maumivu baada ya kujifinya au kujichoma na kitu chenye ncha kali, basi ujue kwamba haupo ndotoni au kwenye ulimwengu wa tofauti bali upo kwenye ulimwengu halisi. Hicho ndicho nilichokifanya mimi na kweli majibu yalionesha kwamba nilikuwa nimerejea kwenye ulimwengu wa kawaida.
Madaktari waliendelea kujadiliana na mwisho walifikia muafaka wa kuamua kunipunguza baadhi ya vifaa mwilini mwangu, ikiwemo mirija ya kunisaidia kula pamoja na ile ya kutolea haja ndogo kwani kwa kipindi chote nilichokuwa sina fahamu, kila kitu kilikuwa kikifanyika kwa msaada wa mirija.
Hilo lilifanyika, kitu pekee kilichoachwa mwilini mwangu ilikuwa ni mashine ya kunisaidia kupumua ambayo nayo walikubaliana kwamba niendelee kuitumia kwa muda lakini nitakapofikia hatua ya kuweza kupumua mwenyewe vizuri, wataitoa.
Niliwaona madaktari wote wakiwa na nyuso za furaha sana mle ndani ya wodi yangu, tofauti kabisa na kipindi nilipokuwa nikiwatazama kutokea pembeni kabla sijarejewa na fahamu ambapo kila mmoja alikuwa akionesha sura ya kukata tamaa.
“Vipi Jamal, unajisikiaje?” nesi mmoja wa kike aliniuliza kwa sauti ya upole wakati akinisafisha mwili wangu kwa kutumia kitambaa laini kilichokuwa kimewekwa kwenye kopo lenye maji ya uvuguvugu.
Nikamjibu kwa sauti ya chini kwamba nilikuwa najisikia vizuri, akaendelea kunifutafuta uso wangu, hasa kwenye yale maeneo niliyokuwa nimebandikwa bandeji za kushikilia ile mirija iliyotolewa. Yule nesi aliendelea kunipigisha stori za hapa na pale, huku mara kwa mara akiingizia utani ambao nilielewa kwamba ulikuwa ni kwa lengo la kunichangamsha.
Unajua jambo ambalo watu wengi hawalijui, madaktari, manesi na wauguzi, huwa wanafundishwa saikolojia ya namna ya kucheza na akili za mgonjwa na kumfanya ajisikie amani ndani ya moyo wake na kuamsha upya matumaini ya kupona, hata kama alikuwa mahututi.
Ndiyo maana ni nadra sana kumuona daktari aliyesomea vizuri kazi yake na kuhitimu, akimfokea mgonjwa au kuzungumza naye kwa lugha isiyo rafiki. Fuatilia kwa makini, madaktari karibu wote, wa hospitali za binafsi na za serikali, huwa wanakuwa wapole sana wanapozungumza na wagonjwa wao, hata kama una tatizo kubwa, atakupa maneno laini ya kishujaa yatakayokufanya uamini kwamba lazima utapona.
Hata manesi wale waliofundishwa vizuri na kuelewa, huwa wapole sana kwa wagonjwa kwa sababu wamefundishwa hivyo. Ukiona nesi anawabwatukia wagonjwa wake, anawatolea lugha chafu na za matusi, wengi wanakuwa ni wale ambao wameingia kwenye fani hiyo kwa njia za kiujanjaujanja, pengine wamefoji vyeti au vyuoni walifeli lakini wameingizwa kwa migongo ya ndugu zao au kwa kutoa rushwa.
Basi yule nesi aliendelea kunipa maneno matamu, eti akawa ananisifia kwamba japokuwa nilikuwa nimepoteza fahamu kwa muda mrefu, eti bado nilikuwa naonekana ‘handsome’, nikashindwa kujizuia na kuachia tabasamu hafifu.
Akaniambia eti kama angekuwa hana aibu za kikekike, angenitongoza ili nimuoe, nikazidi kuachia tabasamu pana kwani sijawahi kusikia eti mwanamke anamtongoza mwanaume amuoe, japokuwa anaweza tu kumrahisishia mazingira ya kumpata, nikajikuta nikivutiwa naye kwani ukiachilia mbali masihara yake, pia alikuwa na sura nzuri ya kuvutia na umbile lililokaa kikekike haswaa!
“Yaani sikomi tu, tamaa za wasichana warembo na huruma zangu ndiyo iliyonifanya niingie kwenye mtego wa Shenaiza, hata kupona vizuri bado nimeanza kumzimikia nesi,” nilijisemea mwenyewe moyoni na kuzidi kutabasamu.
Alizidi kunipigisha stori mpaka nikaona ile mashine ya kunisaidia kupumua kama inaninyima uhuru, nikamuomba aitoe ili nijaribu kupumua mwenyewe, akafanya hivyo na kwa bahati nzuri, tayari nilikuwa na uwezo wa kupumua mwenyewe vizuri, madaktari wakazidi kufurahi na kushauri kwamba kwa kuwa nilikuwa na hali nzuri, nihamishiwe kwenye wodi za kawaida kwa sababu kwa muda wote huo, bado nilikuwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
Mipango ilianza kuandaliwa na hatimaye nilihamishiwa kwenye wodi ya wanaume ambapo nilipoingizwa tu, ndugu, jamaa na marafiki walianza kufurika kwa wingi kuja kuniona kwani fursa hiyo waliikosa nilipokuwa ICU kwa sababu kule huwa ndugu hawaruhusiwi kumuona mgonjwa ambaye yupo kwenye hali mbaya kama niliyokuwa nayo mimi, labda kama kuna sababu maalum.
Miongoni mwa watu wa mwanzomwanzo kabisa kuja kuniona, alikuwa ni Raya ambaye hakuamini kabisa aliponiona nikiwa nimefumbua macho, akanikumbatia kwa nguvu pale kitandani bila kujali dripu niliyokuwa nimeunganishwa, akawa ananibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu huku akiangua kilio kwa nguvu.
“Nilijua nimekupoteza mpenzi wangu, ooh ahsante Mungu! Ahsante Mungu,” alisema Raya, ikabidi niinue ule mkono ambao haukuwa na dripu nikaupitisha mgongoni kwake na kumkumbatia, nikambusu shavuni, kitendo ambacho kwa kiasi kikubwa kilimfariji sana.
Japokuwa mwili wangu haukuwa na nguvu, ilikuwa ni lazima nifanye hivyo kwa sababu kusema ukweli, tangu nipatwe na matatizo, Raya alionekana kuguswa pengine kuliko mtu mwingine yeyote.
Niliamini uchungu ambao alikuwa nao msichana huyo, ungekuwa sawa na wa mama yangu endapo angefahamu kilichokuwa kimenitokea mwanaye lakini kwa kuwa wazazi wangu hawakuwa wakijua chochote kutokana na mazingira ambayo mimi mwenyewe ndiye niliyeyatengeneza (nitafafanua kuhusu hili baadaye), Raya ndiye aliyesimama kwenye nafasi ya mama yangu.
Kingine nilichojifunza, ni kuacha kuhukumu watu wote kwambe eti siku hizi duniani hakuna tena mapenzi ya kweli! Siyo sahihi kabisa, kuna watu wana mapenzi mpaka shetani mwenyewe anayaogopa, mmoja wapo akiwa ni Raya.
Niliendelea kumkumbatia msichana huyo huku marafiki na jamaa zangu wengine wakiwa pembeni wakitutazama, tukiwa kwenye hali hiyo, nilisikia mlango wa wodi ukifunguliwa na mtu akaingia mbiombio mpaka pale kitandani kwangu, nikashtuka na kumuachia Raya, Raya naye akainua uso wake, watu wote tukawa tunamtazama kwa mshangao mtu yule aliyeingia, tukiwa ni kama hatuamini.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...