Friday, August 4, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 11


ILIPOISHIA:
Bado sikuwa na majibu na hakukuwa na mtu yeyote wa kunijibu zaidi ya baba mwenyewe. Jambo kubwa ambalo lilikuwa likijirudia ndani ya kichwa changu, lilikuwa ni je, kweli baba ni mchawi?
“Unasemaje?” nilisikia sauti ya baba akiniuliza kwa ukali, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo.
SASA ENDELEA...
“Sijaongea kitu,” nilijibu, nikasikia baba akiachia msonyo mrefu kisha ukimya ukatawala. Kumbe nilipotamka lile neno ‘sijaongea kitu’, niliongea kwa sauti kubwa kiasi cha kuwafanya abiria wengi ndani ya basi, wanisikie.
“Kaka, unaongea na nani?” sauti ya msichana aliyekuwa akicheka kwa sauti ilisikika, ikifuatiwa na abiria wengine, ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Nikashtuka na kukaa vizuri kwenye siti yangu.
“Anaogopa ajali huyo,” alipaza sauti abiria mwingine, watu karibu wote kwenye basi wakacheka. Nilimgeukia mama, nikamuona yeye yupo siriasi tofauti na abiria wengine, nikageuka na kukaa vizuri kwenye siti yangu.
Yule msichana aliyekuwa amekaa siti ya upande wa pili na pale nilipokuwa nimekaa, alivua ‘headphones’ zake, akawa anaendelea kunitazama huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Tangu tunaanza safari wala sikuwa najua kwamba kuna mtu kama yeye ndani ya gari, ni mpaka pale alianza kunicheka ndipo nilipoanza kumtilia maanani. Alikuwa ni msichana mdogo lakini wa kisasa, akiwa na simu ya kisasa mkononi, halafu akiwa amevalia mavazi kama wasichana wa mjini ambao nilizoea kuwaona kwenye TV.
Nilipoendelea kumtazama kwa macho ya kuibia, niligundua kwamba alikuwa na sura nzuri sana halafu akitabasamu kuna vishimo kwenye mashavu yake vinajitokeza, nikajikuta navutiwa kumtazama.

Safari iliendelea lakini mara kwa mara yule msichana alikuwa akinigeukia na kunitazama, tofauti na mara ya kwanza ambapo alikuwa kama anacheka kwa kunidharau, safari hii alikuwa akinitazama kwa makini.
Katika ujanja wangu wote niliokuwa nikiuonesha kijijini kwetu, makongorosi, Chunya, hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama kuzungumza au kujichanganya kwa namna yoyote na wasichana, hasa wa rika langu.
Tangu naanza kupevuka, mpaka namaliza shule ya msingi na hata baada ya kuanza maisha ya mtaani, sikuwahi kuwa na mazoea na msichana yeyote, zaidi ya dada zangu kwa hiyo kitendo cha msichana huyo kuwa ananitazama mara kwa mara, tena msichana mwenyewe mrembo kwelikweli, kilinikosesha mno utulivu.
Kuna wakati nilikuwa natamani hata nirudi kule kwenye siti yangu ya mwanzo, nilikokuwa nimekaa namama na ndugu zangu lakini nilipofikiria kuhusu kazi nzito niliyopewa na baba, ilibidi nijikaze kiume.
Nilipoona anazidi kunitazama, kuna wakati nilifumba macho na kujifanya nimelala lakini nikasikia ile sauti ya ajabu ya baba ikinijia, akaniambia sitakiwi kulala kwa sababu nina jukumu la kuhakikisha safari inakuwa salama.
Nikawa sina cha kufanya zaidi ya kujikaza kiume, safari hii na mimi niliamua kuwa namtazama. Kama kawaida yake, alinigeukia, akawa ananitazama kwa makini, ikabidi na mimi nimgeukie, tukawa tunatazamana. Cha ajabu, alipoona na mimi namtazama japo kwa uso uliojawa na aibu, aliachia tabasamu pana.
Nikajikuta na mimi nikitabasamu, haraka nikakwepesha macho yangu na kugeukia upande wa dirishani, nikawa natazama nje. Safari iliendelea huku nikiendelea kujishtukia, baadaye nilipomgeukia tena yule msichana, niligundua kwamba tayari alishalala huku headphones zake zikiwa masikioni.
Nikashusha pumzi ndefu kama mtu aliyetua mzigo mzito kichwani, nikakaa vizuri kwenye siti yangu na kuendelea nakazi niliyopewa na baba. Kwa bahati nzuri, safari hii hakukuwa na kipingamizi chochote, safari ikaendelea mpaka tulipofika sehemu maarufu iitwayo Chalinze Choma Nyama.
Dereva alipunguza mwendo na kusimamisha basi, akatutangazia abiria kwamba anatoa dakika kumi tukachimbe tena dawa na kujinyoosha. Bila kupoteza muda, abiria walianza kuteremka, mimi nikageuka na kutazama pale mama na wale ndugu zangu walipokuwa wamekaa, nikawaona nao wakiinuka.
Ilibidi nisubiri abiria wengine wapite, ndugu zangu walipokaribia, niliinuka na kuungana nao, tukawa tunataniana na kaka na dada zangu kama kawaida yetu tunapokutana. Cha ajabu, eti nao walikuwa wakinicheka kwamba woga wa kupata ajali ulisbabisha niwatie aibu kwa kupayuka kwenye basi.
Wakawa wananicheka na kunisukumasukuma, jambo ambalo sikupendezewa nalo. Tuliposhuka chini, waliendelea kunitania lakini kwa kuwa sikuwa naupenda utani wao, niliamua kujitenga nao, nikazunguka mpaka nyuma ya gari, nikasimama nikiegamia basi huku nikitazama kule tulikotokea, uso wangu ukiwa umekosa amani.
“Hawa washenzi wangejua mimi na baba ndiyo tuliowalinda wasipate ajali wasingekuwa wananicheka hivi,” nilisema huku nikikumbuka pia vicheko vya abiria wengine ndani ya basi, muda ule nilipopayuka kwa nguvu ndani ya basi.
Mawazo yangu yalizama kwenye hisia chungu, nikawa naendelea kuwaza mambo mengi ndani ya kichwa changu. Ghafla nilishtushwa na sauti ya kike pembeni yangu.
“Mambo!”
“Safi tu,” nilijibu huku nikianza kujichekesha, aibu zikiwa zimenijaa baada ya kugundua kuwa ni yule msichana wa kwenye basi aliyekuwa akinitazama sana.
“Mbona umekaa peke yako huku halafu unaonekana kama una mawazo sana?”
“Ahh! Kawaida tu, nahisi uchovu wa safari,” nilimjibu, huku lafudhi ya kijijini ikishindwa kujificha kwenye mazungumzo yangu. Aliendelea kunipigisha stori za hapa na pale, akionesha kuchangamka mno utafikiri tunafahamiana.
“Nisindikize kule upande wa pili nikanunue soda za kopo, naona huku hakuna,” alisema msichana huyo ambaye manukato yake mazuri aliyojipulizia, yalizifurahisha mno pua zangu.
Tulisimama pembeni ya barabara, akageuka huku na kule kuangalia kama hakuna gari linalokuja, na mimi nikawa namfuatisha kwa sababu sikuwa mzoefu sana wa barabara ya lami na sikuwa najua vizuri namna ya kuvuka barabara. Alipohakikisha kwamba hakuna gari, alinishika mkono, nadhani aliniona jinsi nilivyokuwa na hofu moyoni, tukaanza kuvuka.
Mikono yake ilikuwa laini mno kiasi kwamba nilifurahia jinsialivyonishika. Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nikaanza kuhisi hali isiyo ya kawaida. Tulivuka mpaka ng’ambo ya pili, akafungua pochi yake ndogo na kutoa noti ya shilingi elfu kumi, akampa muuzaji wa vinywaji aliyekuwa na kibanda chake pembeni ya barabara.
“Unakunywa soda gani?” aliniuliza huku yeye akichukua soda yake, nikakosa cha kujibu zaidi ya kuanza kuchekacheka tu.
“Nakuchagulia, nataka unywe ninayokunywa mimi,” alisema huku akinigeukia, akanipa soda ya Sprite ya kopo, akafungua ya kwake na kuingiza mrija, mimi nikawa nashangaashangaa kwa sababu sikuwahi kunywa soda ya kopo hata mara moja wala sikuwahi kutumia mrija.
Akiwa ameshapiga funda moja, alichukua lile kopo la soda mikononimwangu, anaipa ile ambayo alishaifungua na kunywa kidogo, nikawa namshangaa kwani hayo yalikuwa mambo mageni kabisa kwangu, nilizoea kuyaona kwenye video.
Alifungua na ile nyingine, nayo akapiga funda moja, nikawa sina cha kufanya zaidi ya kuendelea kunywa, akawa ananitazama kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito.
“Unaitwa nani?”
“Togo,” nilimjibu kwa kifupi, akageuka kama anayetazama upande wa pili wa barabara, nikapata fursa ya kulisanifu vizuri umbo lake. Alikuwa ni msichana mzuri sana, upande wa nyuma alikuwa amejazia huku kiuno chake kikiwa kimegawanyika, kama nyigu ambao kule kijijini tulikuwa tukiwaogopa kutokana na sumu yao wanapokung’ata.
Suruali ya jeans aliyovaa, ililifanya umbo lake lijichonge vizuri, ghafla akageuka, akanibamba nikiwa namtazama kwa nyuma, nikazidi kujisikia aibu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...