Thursday, August 31, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 34



ILIPOISHIA:
Alipofikisha tatu, nilifumba macho, nikashtukia ghafla tumehama pale tulipokuwa na kwenda upande wa pili, kule barabarani ambako watu wengi walikuwa wamesimama wakishangaa, tukajichanganya na wale watu.
“Hebu angalia wanachokishangaa,” alisema huku akinitaka nitazame pale tulipokuwa tumekaa awali. Macho yalinitoka nikiwa ni kama siamini.
SASA ENDELEA...
Watu wawili, mmoja akionesha kuwa mwanamke na mwingine mwanaume, wakiwa watupu kabisa huku miili yao iking’aa sana, walikuwa wamekaa kwenye msingi wa nyumba, wakiwa wanazungumza. Macho ya kila mmoja yalikuwa yaking’aa sana na nyuso zao zilikuwa na gizagiza fulani ambalo lilifanya iwe vigumu kwa watu kuwatambua sura zao.
“Hivi ndivyo tulivyokuwa tukionekana ndiyo maana unaona hawa watu wote wamekusanyika hapa,” alisema Isri huku akiniegamia.
Nilibaki nimepigwa na butwaa huku nikiwatazama wale watu ambao wala hawakuwa na taarifa kwamba tulikuwa tumeshajichanganya nao. Nilitamani kumuuliza Isri kwamba sasa iweje wale watu wawe wanaendelea kutuona wakati tulishahama na kujichanganya nao? Kabla hata sijamjibu, ni kama alizisoma hisia zangu, akaniambia kile walichokuwa wakiendelea kukiona, ilikuwa ni kiini macho.

Akaniambia kwamba watu wengi hawajui lakini hakuna jambo la hatari kama kusimama usiku na kuanza kutazama vitu usivyovijua au visivyo vya kawaida kwa sababu kama ni watu wenye nia ovu, unapowatazama tu wanajua kwamba unawatazama na wanao uwezo wa kubadilisha kile unachokiona wewe na kukuonesha kitu cha tofauti kabisa.
Akaniambia ndiyo maana baadhi ya watu hupata matatizo makubwa sana baada ya kuona majini usiku, wengine huona watu warefu wenye kwato, wengine huona miti ikibadilika au huona viumbe vya ajabu wakati kiukweli ni kwamba wanakuwa wamewaona wachawi wakiwa kwenye maumbo yao ya kawaida lakini kwa kuwa wachawi nao wanakuwa wameshagundua kwamba wanatazamwa, wanawafanyia kusudi.
“Sijaelewa, kwa hiyo unamaanisha hata mimi na wewe ni wachawi?”
“Sijamaanisha hivyo.”
“Kwani wewe ulijua kwamba wanatutazama?”
“Ndiyo nilijua,” alinijibu Isri na kunifanya nipigwe na mshangao mkubwa. Watu walikuwa wakizidi kuongezeka na wengi walikuwa ni walinzi wa maeneo ya jirani na pale, wengine wakiwa ni Wamasai na wengine wakiwa ni wafanyabiashara wanaodamka alfajiri na mapema kuwahi kuchukua bidhaa zao.
“Sasa mbona wanazidi kuongezeka, itakuwaje? Ina maana hapa hawatusikii wala hawatuoni?” nilimuuliza, akatingisha kichwa kuonesha kukubali, akaniambia ipo namna ya kuwatawanya. Aliposema hivyo tu, mara nilishangaa wale watu ambao watu wote walikuwa wakiwatazama, wakibadilika na kuwa mbwa wawili wakubwa, dume na jike.
Wakaanza kubweka kwa hasira na kuanza kutimua mbio kulifuata lile kundi la watu. Kiukweli kwa jinsi mbwa hao walivyokuwa wakubwa, wenye hasira huku meno yao makali yakiwa yametoka nje, hata mimi mwenyewe nilijikuta nikiogopa mno. Kufumba na kufumbua, kundi lote lilianza kutimua mbio, kila mmoja kivyake.
Na mimi nilitaka kukimbia lakini Isri alinikamata mkono kwa nguvu, wale mbwa wakawa wanazidi kuja kwa kasi, ikabidi nisimame nyuma yake. Watu walizidi kutimua mbio huku wakipiga kelele na ghafla tukasikia breki kali za gari zikifuatiwa na kishindo kikubwa.
“Tayari!” alisema Isri lakini sikumtilia maanani, akili zangu zote zikawa kwa wale mbwa. Cha ajabu, japokuwa sisi tulikuwa tumesimama, walitupita kwa kasi kubwa na kuendelea kuwatimua wale watu.
“Tayari huko,” alisema Isri kwa mara nyingine, ikabidi nimuulize tayari nini? Akaniambia twende tukajionee wenyewe. Yeye alitangulia, mimi nikawa namfuata, tukanyoosha na ile barabara ya lami mpaka mahali palipokuwa na njia panda, akanionesha kwa kidole nitazame mwenyewe.
Gari dogo aina ya Toyota Carina lilikuwa limeacha njia na kugonga kingo za daraja na kuingia mtaroni, huku barabarani kukiwa na mtu amelala huku damu nyingi zikimtoka akionekana amegongwa na gari lile.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko, akaniambia mtu huyo alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa pale wakitushangaa na wakati akiwakimbia wale mbwa ndipo akaingia barabarani bila kutazama, hali iliyosababisha agongwe na gari hilo kisha na lenyewe likapoteza mwelekeo na kugonga kingo za barabara.
Yaani kwa jinsi Isri alivyokuwa akizungumza kirahisirahisi, ungeweza kudhani anasimulia stori au anazungumza masihara, alikuwa anarahisisha sana mambo hali ambayo ilinifanya nigeuke na kumtazama usoni.
Nilishtuka sana nilipomtazama usoni, macho yake yalikuwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu sana na kung’aa huku kwenye kingo za mdomo wake kukiwa kama na michuruziko ya damu, meno makali kama ya wale mbwa yakiwa yametokea kila upande.
Mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki, nikahisi na mimi nipo kwenye mtego mbaya wa kifo, sikusubiri chochote, nilikurupuka na kuanza kutimua mbio kwa kasi kubwa nikiwa hata sielewi naelekea wapi.
“Togo! Togo rudi nakwambia, ohooo!” alisema kwa sauti kali ya kutisha lakini wala sikuvijali vitisho vyake. Jambo ambalo najisifia, ni uwezo mkubwa wa kutimua mbio. Unajua maisha ya kule kijijini tuliyokulia, ilikuwa ni lazima tu ujifunze kukimbia kwa kasi kubwa, kwani kinyume na hapo usingeweza kuambulia chochote mnapoenda kuwinda wanyama wa porini.
Nilikimbia kisawasawa, dakika chache baadaye nikawa nimeshafika mbali kabisa, nikatokezea kwenye barabara kubwa ya lami ambayo japokuwa ilikuwa ni usiku, yenyewe ilikuwa na magari mengi yakiendelea kupita, hasa makubwa ya mizigo.
Kiukweli nilikuwa mgeni kabisa na jiji lakini niliona ni bora nipotee kuliko kuendelea kukaa karibu na Isri. Japokuwa alikuwa amenieleza mambo mengi kuhusu yeye, yale mambo aliyoyafanya dakika za mwisho, ikiwemo kuwabadilisha wale watu kuwa mbwa, jinsi alivyokuwa akichekelea ile ajali iliyosababisha maafa makubwa na jinsi alivyobadilika na kuwa kama mnyama mkali wa porini, yalinifanya nimuogope mno.
Nikawa naendelea kukimbia pembezoni mwa barabara nikiwa hata sijui naelekea wapi. Kwa mbali kulianza kupambazuka, nikaanza kuona watu wachache wakifanya mazoezi ya kukimbia pembeni ya barabara.
Niliamini hao ndiyo wanaoweza kunisaidia uelekeo wa kufika nyumbani kabla hakujapambazuka kabisa.
Cha ajabu, kila nilipokuwa nikimkaribia mtu yeyote anayefanya mazoezi, alikuwa akitimua mbio za ajabu kunikwepa, mwingine almanusra agongwe na gari kwani alikuwa akija kwa mbele, na mimi nikawa nakimbia taratibu huku nikionesha dalili za kutaka kusimama ili nimuulize lakini ghafla aliponiona, alipiga kelele na kuvuka barabara kwa kasi kubwa mpaka upande wa pili bila hata kutazama, lori kubwa likapiga honi kali na dereva akakata kona kali kumkwepa.
Ilibidi nisimame na kujitazama mwilini kwa nini watu wananikimbia. Jambo la kwanza ambalo lilinishtua, kumbe kwa muda wote huo nilikuwa nikikimbia kwa kutumia mikono na miguu, hata sijui kwa nini muda wote huo sikujishtukia, harakaharaka nikainuka na kusimama kwa kutumia miguu.
Nilipojitazama mwilini, nilishtuka mno kugundua kwamba kumbe nilikuwa na manyoya mengi kama mnyama wa porini, nilipojitazama mikono, nilizidi kupagawa baada ya kugundua kuwa kumbe mikono yangu ilikuwa imebadilika na kuwa kama ya mbwa.
Mara nilishtukia jiwe kubwa likirushwa na kunikosakosa, kabla sijatulia nikashtukia jiwe lingine likinikosakosa, nikaona naweza kuuawa bure, nikaanza kutimua mbio lakini nilipojaribu kukimbia kwa miguu nilijikuta nikishindwa, ikabidi nijaribu kutumia na mikono, nikaweza na kasi ilikuwa kubwa zaidi. Nilikimbia sana huku nikilia nikiwa sielewi nini itakuwa hatma yangu.
Ni hapo nilipogundua kwamba kumbe Isri alikuwa amenigeuza umbo langu na kuwa kama mbwa mkubwa, nilimlaani sana moyoni mwangu na kujikuta nikiyakumbuka maneno ya baba ambaye mara kwa mara alikuwa akinionya kuhusu msichana huyo.
Nikiwa naendelea kukimbia, nilishtukia mtu mmoja akija kwa kasi kubwa nyuma yangu, nikazidi kuongeza kasi lakini kabla sijafika mbali nilishtukia kamba nene ilipita shingoni mwangu na kunifunga kitanzi, nikadondoka chini kama mzigo.
Nikiwa bado hata sijui nini cha kufanya, nilishtukia nikifungwa mikono na miguu, nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza kufanya chochote, ikabidi nitulie na kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia kitendo hicho na alikuwa na lengo gani kwangu maana niliona kifo changu kikiwa kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...