Saturday, August 19, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia)- 25




ILIPOISHIA:
Nilianza kuwatazama mmoja baada ya mwingine, kuanzia mama ambaye uso wake ulikuwa na huzuni kubwa, baba ambaye alionesha kuwa katika tafakuri nzito na ndugu zangu wote ambao walikuwa wamenikodolea macho, kila mmoja akiwa na maswali mengi yasiyo na majibu. Mara mlango wa wodi ulifunguliwa, watu wote wakageuka kutazama ni nani aliyekuwa akiingia kwa kasi kiasi kile.
SASA ENDELEA...
“Shikamooni! Samahani naomba kuuliza eti hii ndiyo wodi aliyolazwa Togo?” alisema mtu huyo lakini kabla hajajibiwa, tayari alikuwa ameshasimama sehemu ambayo ilinifanya mimi na yeye tutazamane.
Moyo wangu ulinilipuka mno kugundua kuwa kumbe alikuwa ni yule msichana tuliyekutana naye kwenye basi na kujenga naye urafiki utafikiri tumejuana miaka kumi iliyopita.
Sikuelewa amejuaje kwamba nilikuwa hospitalini hapo kwa sababu mara ya mwisho alipokuja nyumbani na kunikuta nikiwa na Rahma, tukiondoka kuelekea ufukweni, nilimueleza kwamba tunaenda Coco lakini baadaye tukabadili uelekeo na kuelekea Msasani Beach kwa lengo la kumkwepa.
Kwa harakaharaka, isingewezekana mtu ambaye ametufuata Coco ajue kwamba kumbe tulienda Msasani na kama hiyo haitoshi, ajue kwamba kuna tatizo limetokea na kujua mpaka wodi niliyokuwa nimelazwa. Kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu.
“Ooh! Ahsante Mungu, Togo... umepatwa na nini baba?” alisema huku akinisogelea pale kitandani lakini baba alimzuia.
“Binti, sidhani kama nakujua. Wewe ni nani?”
“Togo alisema hawafahamiani ila walikaa siti moja kwenye basi tu, hata sijui amefuata nini,” alidakia Rahma na kuzungumza kwa chuki, moyoni nikajisikia vibaya sana kwa sababu kama mtu alikuwa amekuja kwa ajili ya kuniona, achilia mbali utata mkubwa uliokuwa nyuma ya tukio la yeye kujua mahali nilipo, hakupaswa kufanyiwa vile.

“Mruhusuni. Ni rafiki yangu!” nilitamka kwa sauti dhaifu ya kukwamakwama, yakiwa ndiyo maneno yangu ya kwanza kuyatamka tangu niliporejewa na fahamu. Baba akageuka na kunitazama kwa sekunde kadhaa, akageuka na kumtazama yule dada usoni, akageuka na kumtazama Rahma ambaye utulivu ulimuisha.
Akamruhusu anisogelee pale kitandani, huku uso wake ukilengwalengwa na machozi, aliniinamia pale chini kwa heshima.
“Pole baba, nimeona picha ya tukio la wewe kuokolewa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, nikajaribu kuulizia ndiyo nikaambiwa umelazwa hapa. Pole sana,” alisema huku safari hii machozi yakiwa yanamtoka. Nadhani kwa jinsi alivyoonesha kuguswa na hali yangu, hata baba alianza kumkubali kwani nilimsikia akishusha pumzi ndefu.
“Najua hakuna anayeweza kukuelewa ukieleza kilichotokea, nakuombea upone haraka,” alisema msichana huyo na kunifanya nikodoe macho kama fundi saa aliyepoteza nati. Alijuaje kwamba hakuna atakayenielewa nikieleza kilichotokea? Alijuaje kwamba maelezo ya Rahma yalikuwa tofauti kabisa na kile nilichoamini kwamba ndiyo ukweli? Nilijikuta nikichanganyikiwa.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, alinibusu kwenye mkono wangu uliokuwa na sindano ya dripu, akageuka na kuwashukuru watu wote kisha kwa heshima kubwa akaondoka zake. Japokuwa mavazi aliyokuwa amevaa yalimtafsiri katika picha nyingine tofauti kabisa, alionesha nidhamu ya hali ya juu mno.
“Huyu ni nani?” swali la baba lilinizindua kutoka kwenye dimbwi la mawazo, akanikazia macho akionesha kuwa na shauku ya kutaka kusikia nitamjibu nini.
“Ni rafiki yangu.”
“Huyu ndiyo mliyekuwa naye kwenye basi?”
“Ndiyo.”
“Na ndiyo aliyekupa simu si ndiyo?”
“Ndiyo.”
“Amejuaje kama umelazwa hapa?”
“Anasema kuwa ameniona kwenye mitandao.”
“Mitandao? Wewe umefikaje kwenye mitandao?” baba alinihoji, huku na yeye akionesha kutokuwa na uelewa wa mambo ya teknolojia kama mimi. Nilimuona baba yake Rahma naye akisogea na kuja kuungana na baba pale pembeni ya kitanda changu.
“Eti anasema amemuona kwenye mitandao,” alisema baba huku akimgeukia baba yake Rahma.
“Inawezekana, unajua hawa vijana wa siku hizi ni wepesi sana wa kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp na Instagram kwa hiyo tukio lisilo la kawaida likitokea tu, haraka wanapiga picha kwa kutumia simu zao na kuliweka mtandaoni kwa hiyo habari zinasambaa kwa kasi,” alisema baba yake Rahma.
Na mimi nikawa nimepata elimu kidogo maana kiukweli sikuwa najua chochote kuhusu hayo mambo maana kule ‘bush’ kwetu tulichokuwa tunakijua ni redio tu. Muda mfupi baadaye, madaktari waliingia na kuwataka watu wote wawapishe ili waweze kuendelea kunipa huduma.
Madaktari walifurahi kuniona nikiwa na hali ile, wakaanza kuniuliza jinsi nilivyokuwa najisikia. Niliwaambia kwamba nahisi mwili wote umekuwa mzito, kila kiungo hakina nguvu. Waliniambia ni kwa sababu ya kiwango kikubwa cha chumvi nilichokuwa nimekula na mwili kukosa hewa safi kwa muda.
Hata hivyo, waliniambia kwamba hali hiyo ni ya muda tu, mwili utapata nguvu hasa baada ya kumaliza kiwango cha dripu walichonipangia, ambazo zilikuwa zikiendelea kutiririka kwa kasi kuingia mishipani mwangu.
“Kwa hiyo leo naweza kuruhusiwa kutoka?”
“Leoleo utatoka wala usiwe na wasiwasi.”
“Kwani saizi ni saa ngapi?”
“Ni saa moja za jioni,” alisema daktari huku akinipima mapigo ya moyo kwa kutumia kifaa maalum, akarekebisha kasi ya dripu kuingia mwilini mwangu kisha akawa anaandika jambo kwenye faili huku akijadilianana wenzake.
“Kwani wewe hujui kuogelea.”
“Najua vizuri tu.”
“Sasa mbona maji yalikuzidi nguvu? Si vizuri kucheza na maji kama hujui kuogelea vizuri, sawa kijana?” alisema daktari huku akinitazama. Niliamua kukaa kimya maana hata ningeeleza kilichotokea, hakuna ambaye angenielewa. Kwa kifupi ni kwamba ilionesha eti mimi nilikuwa nachezea maji ya baharini ndiyo maana nikazama na kutaka kupoteza maisha.
Hicho ndicho walichokuwa wakikiamini watu wote lakini ukweli nilikuwa nao moyoni mwangu, nikaona njia nzuri ni kunyamaza tu kwa sababu sikuwa napenda kukaa hospitalini, isitoshe hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kulazwa. Kule kijijini kwetu, mtu ukiumwa ilikuwa hakuna kwenda hospitali, baba anamaliza kila kitu yeye mwenyewe.
Kwenye majira ya kama saa tatu za usiku, nilimuona baba na baba yake Rahma wakiingia wodini wakiwa wameongozana na wale madaktari waliokuwa wakinitibu, wakapewa baadhi ya maelekezo kisha wakaja pale kitandani kwangu, daktari mmoja akanichomoa dripu na kuniambia nijaribu kusimama.
Nilifanya hivyo, japokuwa kwa mbali nilikuwa nasikia kizunguzungu, niliweza kusimama vizuri. Wakaniambia nijaribu kutembea hatua chache, nilifanya hivyo na wote waliridhishwa na maendeleo yangu. Yule daktari akawaelekeza akina baba sehemu ya kwenda kulipia, baba yake Rahma akanishika mkono na kuanza kuniongoza kuelekea nje.
Nguo nilizokuwa nimevaa hazikuwa zile nilizovaa wakati nilipotokewa na tukio lile, hata sikukumbuka nani alinibadilisha na alinibadilisha saa ngapi. Nilipotoka nje, niliwakuta ndugu zangu wote wakiwa wamekusanyika, wote wakainuka baada ya kuniona nikitembea kwa kujivuta, wakaja na kunizunguka.
“Unaendeleaje mwanangu,” alisema mama huku akija na kunikumbatia, nikamwambia naendelea vizuri, akaja mama yake Rahma ambaye naye alinikumbatia, akaja dada Sabina, Rahma na wengine wote, kila mtu akawa ananikumbatia na kunipa pole kwa kilichotokea.
Wote wakageuka na kuanza kuniongoza kwenye gari aina ya Toyota Noah lililokuwa eneo la mapokezi, mimi nikasaidiwa kukaa siti ya mbele, pembeni ya dereva, ndugu zangu wengine wote wakakaa nyuma. Kwa sababu ya wingi wao, hawakutosha, ikabidi mama na mama Rahma pamoja na baba zetu wao wapande kwenye teksi iliyokuwa imepaki mbele ya ile Noah tuliyopanda.
Muda mfupi baadaye, dereva aliingia, akanisabahi na kunisaidia kufunga mkanda, kabla hajaondoka nilimuona yule msichana akitokea upande wa pili, akamuonesha dereva ishara kwamba asiondoe kwanza gari, akaja pale kwenye dirisha la siti niliyokuwa nimekaa.
“Togo, vipi unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri, namshukuru Mungu.”
“Pole sana mpenzi wangu,” alisema, nikiwa bado nashangaa kwa nini ameniita hivyo, alinivuta na kugusanisha mdomo wake na wangu, nikabaki nimeganda kama nimepigwa na shoti ya umeme. Aliponiachia, harakaharaka niligeuka kuangalia kama Rahma hakuwa ameona kitendo hicho, kwa bahati nzuri alikuwa akipiga stori na dada Sabina, kiufupi hakuna aliyeona zaidi ya dereva ambaye naye alizuga kama hajaona kitu.
“Hii ni zawadi maalum kutoka kwako,” alisema huku anikipa bahasha kubwa ya rangi ya pinki, akanibusu kwenye paji la uso kisha akaniachia na kunipungia mkono, akampa ishara dereva kwamba aondoke. Wakati hayo yakiendelea, kumbe baba aliyekuwa amekaa siti ya mbele ya ile teksi iliyokuwa imeshaanza kutoka pale eneo la maegesho, alikuwa akishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea.
Nilipomtazama, macho yangu na yake yaligongana, akanikazia macho, ikabidi nikwepeshe macho yangu, safari ya kurudi nyumbani ikaanza huku mara kwa mara baba akichomoza kichwa na kunitazama, jambo ambalo sikulifurahia.
Bado nilikuwa na maswali mengi kuhusu huyu msichana, sikuwa najua ndani ya ile bahasha kuna nini na kwa sababu gani anaonekana kunijali kiasi hicho. Baada ya dakika kadhaa, tukawa tumeshawasili nyumbani.
Magari yaliposimama tu, baba alishuka haraka na kunifuata, kabla hata dereva hajanisaidia kufungua mkanda, baba alifika na kunitazama kwa macho ya ukali, safari hii nikaona kama ananionea, na mimi nikamkazia macho, tukawa tunatazamana kama majogoo yanayotaka kupigana, huku nikiificha ile bahasha asiione maana angeweza kunipokonya kama alivyofanya kwenye simu.
“Kwa nini unakuwa huelewi unapoonywa jambo? Unataka mpaka nini kitokee ndiyo ujue kwamba yule msichana ni mtu hatari kwako na kwetu sisi sote?”
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Championi Ijumaa.

Magari yaliposimama tu, baba alishuka haraka na kunifuata, kabla hata dereva hajanisaidia kufungua mkanda, baba alifika na kunitazama kwa macho ya ukali, safari hii nikaona kama ananionea, na mimi nikamkazia macho, tukawa tunatazamana kama majogoo yanayotaka kupigana, huku nikiificha ile bahasha asiione maana angeweza kunipokonya kama alivyofanya kwenye simu.
“Kwa nini unakuwa huelewi unapoonywa jambo? Unataka mpaka nini kitokee ndiyo ujue kwamba yule msichana ni mtu hatari kwako na kwetu sisi sote?”
Itaendelea next issue.



No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...