Saturday, August 12, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 18




ILIPOISHIA:
“SIJUI itakuwaje sasa mume wangu, lazima balaa litokee tuombe tu Mungu Togo atuhakikishie kwamba hawajafanya mapenzi na ndugu yake,” mama Togo alimwambia mumewe.
Wakati wakizungumza hayo, mara wakawaona baba na mama Rahma wanakwenda walipokuwa wakitokea ofisini kwa daktari, wakaacha mazungumzo yao.

SASA ENDELEA...
“VIPI anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri, mtoto mjinga sana huyu.”
“Mh! Usimuite mjinga, huu siyo muda wake, uchungu wake naujua mimi, nimembeba kwenye tumbo langu kwa miezi tisa,” alisema mama yake Rahma akionyesha kutofurahishwa na kauli ya mumewe. Walitoka pamoja na kwenda kukaa kwenye benchi lililokuwa nje ya jengo hilo la hospitali, mimi nikaenda kukaa upande wa pili.
“Hivi, mnajua mimi bado sina majibu juu ya haya maswali niliyonayo.”
“Maswali gani yanayokusumbua?”
“Ni kwa sababu gani Rahma amechukua uamuzi wa kuyakatisha maisha yake?”
“Mh! Hawa watoto wetu wa siku hizi, mimi nahisi alikuwa anampenda Togo sasa kitendo cha kuwaambia kwamba ni ndugu ndiyo maana ameamua kufanya aliyoyafanya, tumshukuru Mungu bado yupo hai.”
“Unachokisema ni sawa lakini nahisi kuna kitu zaidi ya hicho, nahisi hawa watoto walikuwa wameshaanza kufanya mapenzi.”

“Mh! Ninavyomjua Togo huwa hana kawaida ya kuwa karibu na wasichana kabisa, ni muoga sana wa wasichana, sidhani kama hilo linawezekana.”
“Hata Rahma naye si mcharuko kiasi hicho, sijawahi hata kumuona akiwa na mwanaume kichochoroni, kama mambo hayo anayafanya basi anafanya kwa siri sana, kwa ufupi anajiheshimu.”
“Sasa kama tatizo siyo hilo, mnafikiri nini kinaweza kuwa chanzo?”
“Mh! Mimi nakuunga mkono rafiki yangu, kuna kitu nimekihisi na kwa kuunganisha matukio, inawezekana ni kweli wakawa wameshaanza kukutana kimwili,” alisema baba na kusimama, akageuka huku na kule, nilishajua ananitafuta mimi na hakuwa akijua kwamba kumbe nilikuwa palepale jirani yao, nikisilikiza kila kilichokuwa kinaendelea.
“Hebu njoo hapa,” alisema huku uso wake ukiwa na jazba, nikasogea huku uso wangu nikiwa nimeuinamisha chini.
Pale kulikuwa na makundi mawili, baba yake Rahma na baba, wao walikuwa waking’ang’ania kwamba lazima mimi na Rahma tayari tumeshavunja amri ya sita wakati mama na mama yake Rahma, wao walikuwa wakitutetea, kila mmoja na mwanaye.
“Ule mzigo niliokupa safarini uko wapi?” nilishangaa baba akiniuliza swali tofauti kabisa na nililolitegemea. Nikaanza kuvuta kumbukumbu anazungumzia mzigo gani, kwa kutumia tafsida akanifafanulia mpaka nikaelewa kwamba kumbe alikuwa akimaanisha ile dawa aliyonipa pale Mlima Nyoka, Mbeya baada ya kunusurika kwenye ajali mbaya ya gari.
“Ipo nyumbani,” nilimdanganya lakini ukweli ni kwamba licha ya kunisisitiza sana niitunze dawa hiyo, ilikuwa imeniponyoka na kutumbukia kwenye shimo la choo, nyumbani kwa akina Rahma wakati nikioga.
“Una uhakika?”
“Ndi... ndi...yo,” nilibabaika. Baba alikuwa akinijua vizuri, nadhani kwa kubabaika huko, alielewa kwamba dawa hiyo haipo salama, akasimama na kunishika mkono, akanivuta kwa nguvu pembeni.
“Nakuuliza kwa mara ya mwisho, dawa yangu iko wapi?”
“Baba nisamehe, ilitumbukia chooni.”
“Unasemajee?” baba alishtuka kuliko kawaida. Mshtuko aliouonyesha ulinifanya nielewe kwamba kumbe dawa ile kutumbukia chooni halikuwa jambo la kawaida.
“Kwa nini umeniangusha mwanangu? Kwa nini umewapa ushindi?” alisema baba huku akiwa anatingisha kichwa chake kwa masikitiko, nikawa sielewi anamaanisha nini.
“Halafu kwa nini usiniambie mapema ili tujue nini cha kufanya?”
“Nisamehe baba.”
“Nataka uniambie ukweli, wewe umeshafanya mapenzi na Rahma, kweli si kweli?” baba alinihoji, safari hii akiwa amenikazia macho usoni, nikawa nashindwa kama nikubali au nikatae.
“Unaona upumbavu wako? Yaani hili halijaisha umeanzisha jingine, hivi una nini wewe?” alisema baba, akiwa tayari ameshajipa majibu kuhusu swali alilouliza. Nilishindwa cha kusema, nikajiinamia chini kwa aibu, masikitiko na huzuni vyote kwa wakati mmoja.
“Upumbavu ulioufanya utasababisha matatizo makubwa sana kwa watu wasio na hatia, hata sijui itakuwaje,” alisema baba huku akionyesha kuchanganyikiwa kabisa, akaondoka na kuniacha palepale nikiwa nimesimama, na mimi nikiwa nimechanganyikiwa.
Alienda pale alipokuwa amemuacha mama na wazazi wa Rahma, wakawa wanazungumza kitu kisha nikaona wote wamegeuka na kunitazama, hata sijui walikuwa wakizungumza nini.
“Wakiwa bado wananitazama, nesi mmoja alifungua mlango wa wodi aliyokuwemo Rahma na kutoka mbiombio mpaka kwenye ofisi ya madaktari iliyokuwa hapohapo jirani, muda mfupi baadaye akatoka tena mbiombio lakini safari hii alikuwa ameongozana na madaktari wawili ambao nao walikuwa wakikimbia.
Niliwaona akina baba wakikatisha mazungumzo yao na kusimama, huku macho yao yakiwa kwenye ule mlango wa wodi. Mle wodini kulikuwa na wagonjwa kadhaa ila sijui kwa nini akili yangu ilinituma kuamini kwamba walikuwa wakimkimbilia Rahma. Hata akina baba nao nadhani walishajua kwamba mwenye tatizo ni Rahma.
Sikutaka kuandikia mate wakati wino upo, nilitimua mbio kutoka pale nilipokuwa na kukimbilia kwenye mlango wa ile wodi, nikaupiga kikumbo mlango na kuingia mpaka ndani, macho yakiwa pale kwenye kitanda alichokuwa amelazwa Rahma.
Madaktari na manesi walikuwa wamemzunguka, nikasogea kutaka kujionea amepatwa na nini? Nilichokiona sikukiamini. Rahma alikuwa akitapatapa kama anayetaka kukata roho, kibaya zaidi damu nyingi zilikuwa zikimtoka mdomoni na puani, kiasi cha kusababisha mashuka meupe aliyokuwa amelalia yalowe damu.
“Aisee, huruhusiwi kuingia humu, muda wa kuona wagonjwa haujafika,” mlinzi ambaye mkononi alikuwa na rungu kubwa, aliniambia huku akilitingisha lile rungu, akanionyesha ishara kwamba nitoke nje vinginevyo ataniadhibu.
Ilibidi nitoke tu kwani sikutaka matatizo zaidi, ukizingatia na hali niliyomuona nayo Rahma ndiyo nilizidi kuchanganyikiwa.
“Vipi kuna nini?” baba aliniuliza nilipotoka tu, ikabidi nimueleze hali halisi, nikamuona na yeye akishusha pumzi ndefu na kushika kiuno.
“Haya yote ni kwa sababu yako na hawezi kupona kwa kutibiwa hospitali, dawa yake unayo wewe,” alisema baba huku akinitazama kwa macho ya ukali.
“Mimi? Dawa gani?”
“Inabidi ufute makosa ya upumbavu wako wote ulioufanya, hiyo ndiyo itakuwa ponapona yake, mtoto mshenzi sana wewe, wala sikukutegemea,” alisema baba huku akinisogelea mwilini, nikahisi lazima atanizabua  makofi kwa sababu anapokasirika sana huwa hawezi kudhibiti hasira zake.
“Itabidi tuwaombe tuondoke naye mpaka nyumbani, nitaenda kukuelekeza nini cha kufanya kumsaidia,” alisema kwa sauti ya kunong’ona, nikahisi kama amechanganyikiwa akili. Yaani kwa hali aliyokuwa nayo, halafu eti akawaombe madaktari tuondoke naye kurudi nyumbani? Niliona ni kitu kisichowezekana.
Baba aligeuka na kuondoka, akasogea pembeni na kuanza kuzungumza na baba yake Rahma. Akina mama wao niliwaona wameshaanza kuchanganyikiwa, mama yake Rahma akawa analia. Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu, hasa kwa jinsi baba alivyokuwa ananishutumu kwamba mimi ndiyo chanzo cha yote yale.
Mara mlango wa wodi ulifunguliwa, daktari mmoja akachungulia nje na kuwaonyesha ishara ya kuwaita baba na baba yake Rahma, mapigo ya moyo wangu yakalipuka mno, sikujua anaenda kuwaambia nini, akilini nikawa nahisi kabisa kwamba mambo yameshaharibika.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...