Tuesday, August 8, 2017

The Graves of The Innocent (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 16


ILIPOISHIA:
“TOGO,” nilisikia sauti nzito ya baba ikiniita, harakaharaka nikamtoa Rahma, kila mmoja akawa anahaha kujiweza vizuri.
“Togooo,” alirudia kuniita, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio mno huku mdomo ukiwa mzito kufunguka.

SASA ENDELEA…
“NAAM!”
“Hebu sogea hapa dirishani,” alisema baba, harakaharaka nikavaa nguo zangu, Rahma naye akawa ameshavaa nguo zake na bila kujali atakutana na nani nje, alitoka kwa kasi.
“Wewe Togo, si nimekwambia sogea hapa?” alisema baba, safari hii akigonga kioo cha dirisha. Kwa kuwa tayari nilishavaa, nilisogea pale dirishani na kufunua pazia pamoja na dirisha moja, nikamuona baba amenikazia macho.
“Unafanya nini?”
“Nilikuwa nafanya mazoezi ya kupiga pushapu.”
“Kweli?”
“Kweli baba.”
“Hebu funua pazia lote,” alisema baba, kwa kuwa nilikuwa na uhakika Rahma ameshatoka, nilifunua pazia lote, akatazama huku na kule kisha akarudi kunitazama usoni.
“Mwanangu Togo, mbona tangu tumeanza safari umekuwa ni mtu wa kututia aibu kila sehemu? Una nini kwani wewe?”
“Mama sasa kwani mi nimefanya nini? Ina maana hata kufanya mazoezi ndani nako ni makosa?” nilimjibu mama ambaye kumbe alikuwa na baba kule nje, nikavaa uso wa huruma ili kuwafanya waniamini kile nilichokuwa nakisema.

“Hivi unatufanya sisi wote ni watoto wadogo kama wewe?” alisema baba huku akiwa amekazia macho suruali niliyokuwa nimevaa, ikabidi na mimi nijiangalie. Cha ajabu, suruali niliyokuwa nimevaa nilikuwa nimeigeuza nje ndani, aibu niliyoihisi ilikuwa kubwa mno, ikabidi niliachie pazia na kurudi kitandani huku nikikosa cha kujibu.

“Nitasema wakati wa kuvaa nimevaa harakaharaka, bado nitaendelea kukataa kwamba sijafanya chochote,” nilijisemea huku nikiivua ile suruali na kuivaa vizuri. Kwa kuwa mwanzo Rahma alipokuja aliniambia kwamba chai ipo tayari, ili kuzidi kupoteza ushahidi, niliamua kupitia kwanza bafuni kabla sijaenda sebuleni.
Nikanawa uso harakaharaka na kutoka kuelekea sebuleni, bado wale mafundi walikuwa wakiendelea kutengeneza mlango na nahisi walikuwa wanajua kilichokuwa kinaendelea kati yangu na Rahma kwa sababu wakati natoka bafuni, wote waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kunitazama usoni, wakionyesha dhahiri kwamba walikuwa na shauku ya kunijua.
Sikuwasemesha kitu, hata salamu sikuwapa, nikapitiliza moja kwa moja mpaka sebuleni ambako niliwakuta karibu watu wote wakiwa wanakunywa chai isipokuwa wazazi wa pande zote mbili, kwa maana ya baba na mama yetu na baba na mama yao akina Rahma, kila mmoja akiwa na kikombe chake na vitafunwa vyake.
Kabla hata sijakaa, Rahma aliinuka na kunichukulia kikombe, akanimiminia chai na kunisogezea pale nilipokuwa nimekaa pamoja na vitafunwa. Watu wote walikuwa kimya kabisa, macho yakiwa kwenye runinga kubwa ya kisasa.
Wakati akinisogezea chai, Rahma alinitazama kwa macho ya kuibia, na mimi nikamtazama, macho yetu yakagongana ambapo nilimuona akiachia tabasamu pana huku aibu za kikekike zikiwa zimetawala kwenye uso wake.
Hakutaka kurudi kukaa pale alipokuwa amekaa awali, alichukua kikombe chake cha chai na kuja kukaa pembeni yangu, nikawaona ndugu zangu, akiwemo dada Sabina wakinitazama kwa macho ya chinichini.
Ukimya uliendelea kutawala, tukaendelea kunywa chai na baada ya kumaliza, Rahma na dada Sabina waliinuka na kuanza kutoa vyombo, tayari kwa ajili ya kwenda kuviosha lakini ghafla mama aliingia akiwa ameongozana na mama yake Rahma. Kwa kuwatazama tu sura zao, ilionyesha kuna jambo halikuwa sawa.
“Togo, njoo huku,” alisema mama, mama yake Rahma naye akamuita Rahma, ikabidi aache kutoa vyombo, wote tukaelekea kule nje ambako tulikuta wazazi wetu wakiwa wamekaa kwenye viti vilivyokuwa pale nje, wote wakionyesha kutokuwa na furaha kwenye nyuso zao.
“Hebu tumbieni, hivi Togo na Rahma mlikuwa mnafahamiana kabla?” aliuliza baba yake Rahma, muda mfupi tu baada ya sisi kufika.
“Hapana,” nilisema huku nikitingisha kichwa.
“Mbona ndani ya muda mfupi tu tangu mkutane mmekuwa na nyendo zinazotutia mashaka? Hivi mnajua kama nyie ni ndugu?” alisema baba yake Rahma na kunifanya nishtuke.
Alichokuwa ametuambia baba, ni kwamba baba yake Rahma alikuwa ni rafiki yake wa siku nyingi ambaye walishirikiana vitu vingi pamoja na ndiyo maana hata alipoona mambo hayaendi vizuri kule Chunya, majirani na wanakijiji wakiituhumu familia yetu kuwa inajihusisha na Imani za kishirikina aliamua kuondoka na sisi mpaka jijini Dar es Salaam.
“Sikuwa nimewafafanulia mwanzo lakini ukweli ni kwamba ukiacha urafiki wetu, sisi ni ndugu, mama yangu kwa maana ya bibi yenu na mama mzazi wa baba Rahma ni mtu na mdogo wake, kwa hiyo sisi ni ndugu na nyie ni ndugu, tena wa damu kabisa,” alisema baba, kauli ambayo ilinishtua mno.
“Msije mkatuletea aibu ya mwaka hapa maana naona mmeshaanza kuonyesha kupendana, nyie ni ndugu na kwa ukoo wetu sisi ndugu wakifanya dhambi kama hiyo, husababisha mabalaa makubwa sana kwenye ukoo mzima,” baba yake Rahma alizidi kupigilia msumari.
Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilijikuta kijasho chembamba kikinitoka, lilikuwa ni jambo ambalo sikulitegemea kabisa, nikageuka na kumtazama Rahma, nikamuona akiwa amejiinamia kwa aibu.
Sikuwahi kuwa na skendo yoyote ya mapenzi na hata wazazi wangu hawakuwahi kusikia jambo lolote baya kuhusu mimi lakini cha ajabu, ndani ya muda mfupi tu niliokutana na Rahma na kunionjesha ulimwengu wa kikubwa, tayari kila mtu alikuwa na wasiwasi na mimi. Nilijisikia aibu sana.
“Mmeelewa?” alihoji baba, nikajibu kwa kutingisha kichwa, wakatuambia tukaendelee na tulichokuwa tukikifanya, wakati tukiondoka tukawasikia wakipiga stori na kucheka, nadhani baba alizungumza kitu kuhusu mimi kilichowavunja mbavu wote.
Tulipoingia sebuleni, tulikuwa kama tumemwagiwa maji ya baridi, afadhali mimi kidogo niliweza kujikaza, Rahma alionyesha kuchoka mno, macho yakawa mekundu kama anayetaka kulia.
Hakuweza kuendelea kukaa pale sebuleni, nilimuona akiinuka kwa unyonge, akaelekea chumbani kwake ambapo tayari mafundi walikuwa wamemaliza kutengeneza mlango wa chumba chake, akaingia ndani na kujifungia.
Sikumuona tena akitoka mpaka muda wa chakula cha mchana, mimi na ndugu zangu tukawa tunaendelea kushangaa runinga na vitu vingine vya kisasa vilivyokuwa mle ndani.
Baada ya chakula cha mchana kuiva, mama yake Rahma alimtuma mdogo wake kwenda kumuita chumbani kwake wakati chakula kikipakuliwa. Muda mfupi baadaye, alikuja na majibu kwamba dada yake alikuwa amelala chumbani lakini alipojaribu kumuamsha, hakuamka.
“Unasema?” mama yake Rahma aliuliza kwa mshtuko, huku akiacha kila alichokuwa anakifanya. Haraka akakimbilia chumbani kwa mwanaye, huku akionyesha kuwa na wasiwasi mkubwa moyoni mwake, mama naye akamfuata, na mimi uzalendo ukanishinda, nikainuka na kuwafuata.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...