Monday, August 14, 2017

The Graves of The Innocent (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 20


ILIPOISHIA
“MUNGU wangu, hivi wewe mtoto una akili timamu kweli?” alisema baba huku akionyesha kushtuka mno, akageuka na kumuonyesha ishara baba yake Rahma kwamba aje, harakaharaka akaja mpaka pale tulipokuwa tumesimama.

SASA ENDELEA...
“UNASIKIA majanga ya huyu mtoto aliyoyazua tena?”
“Kuna nini?”
“Eti alikuwa kujitolea damu.”
“Mungu wangu, kwani hujawahi kumwambia ukweli?”
“Ukweli? Ukweli gani?” niliuliza kwa mshtuko.
“Wewe ni mpuuzi sana, yaani hili halijaisha unaanzisha jingine, kwa hiyo tutakuwa na kazi ya kurekebisha makosa yako tu muda wote,” baba alisema kwa kufoka, baba yake Rahma akawa anamtuliza na kumkumbusha kwamba kuna kazi hawajaimaliza.
“Huyu ndiyo ilitakiwa akaifanye hiyo kazi lakini ameshaharibu tena, unafikiri itakuwaje?”
“Twende tu tutajua hukohuko,” alisema baba Rahma huku akinishika mkono, akanipeleka mpaka kwenye gari aina ya Toyota Noah lililokuwa limepaki jirani na geti la kutokea. Kumbe tayari Rahma alishatolewa wodini na alikuwa ameshaingizwa ndani ya gari, mama na mama Rahma wakawa wamempakata.
Tulipoingia tu, gari liliwashwa na kuondoka, mama akageuka na kunitazama kwa uso wa huzuni kama anayeniuliza ‘ulikuwa wapi?’
Nilikaa na kutulia kimya, safari ikaendelea. Watu wote walikuwa kimya kabisa ndani ya gari, sauti pekee iliyokuwa inasikika, ilikuwa ni ya Rahma aliyekuwa anakoroma. Dereva aliendesha gari kwa kasi na baada ya takribani dakika thelathini, tayari tulikuwa tumefika nyumbani.
Siku hiyo hata sikuwa na hamu ya kulishangaa jiji, maghorofa yote ambayo awali nilikuwa na hamu ya kuyatazama jinsi yalivyo marefu na yenye kuvutia, hayakuwa na maana tena kwangu.
Baba na baba yake Rahma walisaidiana kumshusha mgonjwa na moja kwa moja wakampeleka chumbani kwake.
“Nenda bafuni kaoge, usitumie sabuni, utatumia hii badala ya sabuni,” alisema baba huku akinipa kitu kama jiwe laini lenye rangi nyekundu.
Nikageuka na kuanza kuelekea chumbani kwangu kwa lengo la kubadilisha nguo kwanza.
“Unaenda wapi tena? Nimekwambia kaoge, moja kwa moja bafuni nakuja hukohuko,” alisema baba kwa sauti iliyoonyesha kutokuwa na masihara hata chembe. Nilitii alichoniambia, kauli yake kwamba ‘dawa’ ya kumtibu Rahma nilikuwa nayo mimi, ikaanza kujirudia kichwani.
Nilipofika mlangoni, nilivua mabuti yangu, maana siwezi kuita viatu bali mabuti kutokana na jinsi muundo wake ulivyokuwa. Kule kwetu kijijini mabuti hayo yalikuwa yakivaliwa siku za sikukuu au kunapotokea safari kama hiyo tu lakini siku nyingine zote, mimi na wenzangu tulikuwa tukitembea pekupeku, si unajua maisha ya kijijini tena.
Basi niliyavua pale mlangoni na kuvaa ndala, nikaingia bafuni na kuvua nguo, nazo nikazitundika kwenye misumari maalum na kusogea kwenye bomba. Safari hii sikutaka kutumia bomba la mvua kwani tangu niliposhtukia nikioga damu badala ya maji, nilikuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
Nilichoamua ni kuoga kwa kutumia maji yaliyokuwa kwenye ndoo ya kuogea, nikajimwagia mwilini kwa kutumia kopo kisha nikaanza kujipaka ile dawa aliyonipa baba. Cha ajabu, nilipokuwa nikijipaka, ilikuwa ikitoa povu kama sabuni na ilikuwa na harufu fulani isiyo ya kawaida.
Yote tisa, kumi ni kwamba nilipojimwagia maji tena juu ya ile dawa, nilishangaa maji yaliyokuwa yakitoka mwilini mwangu yakiwa meusi kama maji yaliyochanganywa na mkaa au masizi. Mara ya kwanza nilihisi kama nipo ndotoni, nikakodoa macho lakini ndiyo ulikuwa ukweli.
Ilibidi niendelee kujimwagia maji kwa wingi na kadiri nilivyokuwa nazidi kujimwagia, ndiyo ule weusi ulivyokuwa ukizidi kupungua. Nilijipaka kwa mara ya pili na kujimwagia maji, bado uchafu mweusi ukawa unanitoka kwa wingi, nikawa najimwagia maji kwa wingi mpaka ulipoisha kabisa.
“Ina maana mimi ndiyo nilikuwa mchafu kiasi hiki? Halafu huu ni uchafu gani unakuwa mweusi kiasi hiki?” nilijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu. Wakati naendelea kuoga, nilisikia mlango ukigongwa, ukafuatiwa na sauti ya baba.
Iweje baba anifuate bafuni? Alikuwa anataka kufanya nini? Nikiwa bado najiuliza maswali, nilisikia tena sauti ya baba akinilazimisha nifungue mlango. Ikabidi nifungue kidogo na kumchungulia.
“Umetumia hiyo dawa?”
“Ndiyo.”
“Umeona nini?”
“Maji meusi kama ya mkaa yalikuwa yananitoka.”
“Safi, sasa vaa hii,” alisema baba huku akinyoosha mkono na kupenyeza kitambaa cheupe kupitia ule upenyo mdogo niliouacha. Akanisisitiza kwamba nisiziguse kabisa nguo zangu, nijifunge na yeye ananisubiri nje.
Nilirudisha mlango na kuufunga vizuri, nikawa nakitazama kile kitambaa alichonipa. Japokuwa sikuwa mzoefu wa shughuli za mazishi kiasi hicho, niliweza kukitambua vizuri kitambaa hicho kwamba kilikuwa ni sanda. Ninavyofahamu mimi, sanda huvalishwa maiti, sasa baba alikuwa na maana gani kuniambia nivae sanda?
Sikupata majibu. Nikawa naendelea kuishangaa sanda hiyo huku mapigo ya moyo yakinienda mbio kuliko kawaida. Nikiwa bado katika hali ile, nilisikia baba akigonga tena mlango kwa nguvu, akaniambia ananisubiri.
Ilibidi niivae harakaharaka, kisha nikafungua mlango. Baba alinitazama kuanzia juu hadi chini, akanirekebisha sehemu ambazo sikuwa nimejifunga vizuri, akatoa kipande kingine na kunifunga kichwani, akanisogelea sikioni na kuniambia:
“Upumbavu uliofanya ndiyo uliotufikisha hapa tulipo. Lazima ufanye kila kinachowezekana kuokoa maisha ya Rahma. Kwa hiyo, utalazimika kufanya kile nitakachokwambia bila kuhoji chochote, ukikosea masharti Rahma atakufa na wewe ndiyo utakuwa umemuua, hutakiwi kuzungumza chochote mpaka tutakapomaliza hii kazi,” alisema baba kwa sauti isiyokuwa na masihara hata kidogo.
Nilizidi kutetemeka, yaani mimi ndiyo niwe nimemuua Rahma? Kwa lipi? Hata hivyo, kwa kuwa ndani ya moyo wangu, licha ya yote yaliyotokea nilishatokea kumpenda mno Rahma, nilichojiapiza ni kwamba nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha naokoa maisha yake.
“Nifuate,” alisema baba huku akigeuka, akawa anatembea kwa hatua ndefundefu, alipofika kwenye mlango wa chumba cha Rahma, aliniambia nigeuke na kuupa mlango mgongo.
“Utaingia kinyumenyume mpaka ndani,” alisema baba, bado kidogo nimuitikie ‘sawa’ lakini nikakumbuka alichoniambia kwamba sitakiwi kuzungumza chochote. Alitangulia, akafungua mlango, nikamfuata kinyumenyume kama alivyonielekeza.
“Chumba kizima kilikuwa kimefukizwa ubani wenye harufu kali, alinipa ishara kwamba niendelee kutembea kinyumenyume mpaka aliponipa ishara kwamba nisimame, nikageuka na kutazama pale kitandani. Rahma alikuwa amelala, damu nyingi zikiendelea kumtoka na kulowanisha kitanda kizima.
Hakuwa na nguo yoyote mwilini zaidi ya kipande cha sanda alichokuwa amefunikwa kuanzia juu kidogo ya mapaja mpaka kifuani ambacho nacho kilikuwa na damudamu.
Baba akanitazama usoni, na mimi nikamtazama nikiwa na shauku kubwa ya kusikia kile atakachoniambia. Nilikuwa tayari kwa chochote ilimradi Rahma apone.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...