Monday, August 7, 2017

The Graves of The Innocent (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 13


ILIPOISHIA:
“YULE uliyekuwa umekaa naye kwenye basi ni nani?”
“Ni rafiki yangu.”
“Unamjua wewe? Na hicho alichokupa una uhakika gani kama ni simu? Ujinga wako utaiponza familia nzima,” alisema maneno ambayo yalinishangaza sana.
SASA ENDELEA…
“NI simu baba!”
“Sitaki kukuona naye tena na hiyo simu lete,” alisema huku akinipokonya ile simu. Nilizidi kumshangaa baba, nikaona kama anataka kunikosesha bahati ya bure. Kwa mara ya kwanza nilijikuta nikipandwa sana na hasira juu yake. Hata hivyo sikuwa na cha kufanya, tuliondoka Ubungo huku kila mmoja ndani ya gari tulilokuwa tumepanda, akiwa anashangaa mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Japokuwa tulikuwa tumebanana sana kwenye ile teksi kwa sababu ya wingi wetu, kila mmoja alikuwa akitamani yeye ndiyo akae dirishani. Tulikatiza mitaa mingi na hatimaye tukaiacha barabara ya lami na kuingia kwenye barabara ya vumbi. Baada ya muda, tulitokeza kwenye nyumba moja nzurinzuri, baba akawa wa kwanza kuteremka kwenye gari, na sisi wengine tukafuatia na kuanza kushusha mizigo.
Wakati tukiendelea kushusha mizigo, geti kubwa lilifunguliwa, mwanaume wa makamo aliyeonekana wanafahamiana vizuri na baba, alimuita kwa jina lake, baba akaacha kila alichokuwa anakifanya na kwenda kumkumbatia, wote wawili wakionyesha kuwa na furaha kubwa kwa kukutana.
“Hii ndiyo familia yangu, shemeji yako na watoto,” alisema baba huku akituonyeshea sisi, akatusogelea na kusalimiana na mama, kisha akaanza kutupa mikono, mmoja baada ya mwingine huku akituuliza majina.
“Naitwa Togolai,” nilimwambia aliponifikia, akanitazama usoni.
“Wewe ndiyo Togo?”
“Ndiyo,” nilisema huku na mimi nikiachia tabasamu hafifu kwa sababu na yeye alikuwa akitabasamu. Baada ya hapo, alitukaribisha ndani, wakati tunabeba mizigo kuingiza, walikuja watu wengine watatu, wasichana wawili na mwanaume mmoja ambao kwa kuwatazama tu, walionyesha dhahiri kwamba ni wanaye kwa jinsi walivyokuwa wamefanana na kupishana umri.
Mkubwa alikuwa wa kike, aliyemfuatia alikuwa wa kiume na mdogo kabisa naye alikuwa wa kike. Hawakupishana sana umri, yule mkubwa alikuwa akilinganalingana na dada yetu Sabina.
Tofauti yao na sisi, ilikuwa kubwa sana, kuanzia jinsi walivyokuwa wamevaa na mpaka muonekano wa miili yao. Walikuwa na mwonekano wa kimjini haswaa wakati sisi tulikuwa na mwonekano wa ‘bushi’, kuanzia sura zetu, mavazi yetu mpaka jinsi tulivyokuwa tukizungumza.
Walitukaribisha mpaka ndani, tukaenda kukaa kwenye sebule kubwa na ya kisasa. Japokuwa tulikuwa wengi, lakini wote tulitosha kwenye masofa ya kisasa. Ushamba wetu uliendelea kujidhihirisha mle ndani kwani tulikuwa tukishangaa kila kitu, kuanzia taa za umeme, feni, mapazia, kuta zilizokuwa zimenakshiwa kwa rangi nzuri na marumaru, kila kitu kilikuwa kigeni kwetu.
Tuliandaliwa chakula na mama wa familia ile ambaye alikuwa mchangamfu na anayependeza kimwonekano kuliko mama yetu. Kilikuwa ni chakula kizuri mno, ambacho ama kwa hakika tulikifurahia. Tukala mpaka kumaliza, mwenzetu mmoja akawa anataka kulamba bakuli la mboga, mama akamkata jicho la ukali na kumfanya aogope.
Baada ya chakula, tulianza kushangaa runinga maana kule hakukuwa kuangalia, ilikuwa ni mara yetu ya kwanza kuona runinga lakini achilia mbali runinga ya kawaida, ile iliyokuwa mle ndani ilikuwa kubwa sana, tena ya kisasa kabisa iliyounganishwa na spika ndogo za kisasa zilizokuwa zinatoa mdundo mzito.
Mpaka muda wa kulala unafika, hakuna aliyekuwa tayari kubanduka pale sebuleni, kila mmoja alikuwa anatamani kama akeshe palepale akitazama vipindi vizuri vilivyokuwa vinaonyeshwa. Ilibidi mama atumie ukali, kwani kwa muda huo baba ambaye ndiyo tunayemwogopa sana, alikuwa nje kwa mazungumzo na yule rafiki yake.
Kabla ya kwenda kulala, ilibidi kwanza tuende kuoga mmojammoja kuondoa vumbi na uchafu tuliotoka nao kijijini. Mimi ndiye niliyekuwa wa mwisho kwenda kuoga ambapo nilipoingia kwenye bafu hilo la kisasa, nilishangazwa kwa jinsi lilivyokuwa safi. Yaani hata kama ningeambiwa nikae mle ndani kwa siku nzima na kuletewa chakula nilie humohumo ningekubali kwa sababu ya usafi wake.
Kule kijijini tulizoea kwenda kuoga mtoni, wakati mwingine kuogelea lakini mjini mambo yalikuwa tofauti. Nilivua nguo zangu na kuzikung’uta kwanza kwa sababu zilikuwa na vumbi jingi. Kwa bahati mbaya, wakati nikiikung’uta suruali niliyokuwa nimevaa, nilisahau kwamba ile dawa niliyopewa na baba nilikuwa nimeiweka kwenye mfuko, nilipokung’uta ikadondoka chini na kwa kuwa choo na bafu vilikuwa vimeungana, yaani upande mmoja kuna bafu na upande wa pili kuna choo, iliteleza mpaka kwenye sinki la choo.
Kutokana na umuhimu wa dawa hiyo, ilibidi niende kuiokota haraka lakini kabla sijafanya hivyo, niliitundika ile suruali kwenye bomba lililokuwa pembeni. Nikashtuka kuona maji yakianza kumwagika, yakaisomba ile dawa na kuipeleka kwenye shimo la choo, ikapotelea kwenye bomba la kutolea maji machafu.
Nilishangaa sana yale maji nani ameyafugulia lakini nilipotazama vizuri, niligundua kuwa kumbe pale nilipokuwa nimetundika suruali ile ilikuwa ni koki ya bomba ambayo kwa jinsi ilivyokuwa ya kisasa nilishindwa kuitambua.
“Ayaaa!” nilisema kwa sauti kubwa kwa sababu sikutegemea kabisa kile kilichotokea na hata sikujua nitamwambia nini baba kwa sababu wakati ananipa, alinisisitiza kuitunza sana dawa hiyo. Ilibidi nifunge maji kwanza, nikaegamia kwenye marumaru za bafuni, nikiwa na mawazo mengi juu ya nini cha kufanya.
Mwisho nilipiga moyo konde na kujiambia kwamba nitaenda kumweleza baba hali halisi na kwa sababu ananipenda na ananiamini. Nilimalizia kuvua nguo, nikawa nataka nioge maji kwa kutumia bomba linalomwaga maji kama mvua, kama nilivyokuwa nimeona kwenye runinga muda mfupi uliopita.
Kwa umakini mkubwa nilichunguza mahali ilipo koki yake, nilipoiona niliifungua, maji yakaanza kumwagika, harakaharaka nikaingia katikati yake na kuanza kujimwagia.
Ilibidi nifumbe macho wakati najipaka sabuni lakini taratibu nilianza kuona maji yanaanza kuwa ya uvuguvugu kidogo halafu yanakuwa kama mazito kidogo na yana chumvichumvi. Nikawa nikipaka sabuni haiishi mwilini, ikabidi nisogeze kichwa pembeni kidogo na kufumbua macho.
“Mungu wangu,” nilipiga kelele kwa nguvu baada ya kugundua kwamba kumbe kile nilichokuwa nikiamini kwamba ni maji, zilikuwa ni damu zikimwagika kama maji. Uda mfupi baadaye tayari nilikuwa kwenye mlango wa bafuni lakini cha ajabu, licha ya kutoa loki niliyoiweka wakati nikiingia, mlango uligoma kufunguka, nikawa nagongagonga kwa nguvu huku nikiendelea kupiga kelele.
Wa kwanza kufika alikuwa ni yule msichana ambaye alionyesha kuwa ndiyo mtoto mkubwa wa yule mzee, akasukuma mlango kwa nguvu kutokea nje. Nguvu alizotumia, ukichanganya na kwamba miguu yangu ilikuwa na majimaji, nilijikuta nikiteleza na kuanguka chini kama mzigo akaingia na kupigwa na butwaa kutokana na hali aliyonikuta nayo kwani sikuwa na nguo hata moja na bado nilikuwa nikipiga mayowe ya kuomba msaada.
Alichokifanya, haraka alivua khanga aliyokuwa amejifunga juu ya gauni lake na kunirushia ili nijisitiri kisha haraka akageuka na kutoka, nikamsikia akijifungia mlango wa chumbani kwake, nadhani alijisikia aibu sana kwa hali aliyonikuta nayo.
Cha ajabu sasa, wakati nageuka kutazama kule zile damu zilikokuwa zikimwagika, nilishangaa kuona kinachotoka si damu bali maji na wala hakuna dalili yoyote ya damu. Tayari kaka zangu walishafika na kunikuta nikihangaika kujifunga ile khanga niliyopewa, wakataka kujua nini kimetokea
Kelele hizo kumbe hata baba na yule mwenzake walizisikia, nao wakaja haraka kutaka kujua nini kimetokea.

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...