Saturday, August 19, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 17


ILIPOISHIA:
Safari iliendelea mpaka tulipofika Magomeni ambako kulikuwa na foleni kubwa sana asubuhi hiyo, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
“Nimekwambia kwamba sijui kama tutafika salama, umewahi kuona asubuhi namna hii kunakuwa na foleni kama hii?” alisema Shenaiza huku akizidi kuonesha hofu kubwa ndani ya moyo wake, nikawa nazidi kumtuliza.
SASA ENDELEA…
Tulikaa kwenye foleni kwa zaidi ya dakika ishirini, magari yakiwa hayaendi mbele wala hayarudi nyuma. Nilitegemea kwamba muda mfupi baadaye askari wa usalama barabarani (trafiki) watafika na kusaidia kuondoa foleni hiyo lakini haikuwa hivyo.
Madereva wengine walipochoka, walianza kupiga honi kwa nguvu, huku wengine wakiteremka kwenye magari yao na kusogea upande wa mbele kujaribu kuangalia kilichokuwa kinasababisha foleni hiyo.
“Nasikia kuna ajali huko mbele, hapa hatuwezi kuondoka sasa hivi mpaka trafiki waje, wapime ajali yenyewe, wayatoe magari yaliyopata ajali unafikiri itakuwa sasa hivi?” kondakta wa daladala tuliyopanda, alisema na kutufanya abiria wote tuishiwe nguvu.
“Sasa tutafanyaje?”

“Inabidi tushuke tutembee kwa miguu, kule hospitali wakishtukia kwamba nimetoroka wanaweza kuanza kutufuatilia na huenda wakatukamata hapahapa, tuondoke,” alisema Shenaiza huku akisimama kwenye siti aliyokuwa amekaa, na mimi nikasimama, tukamlipa kondakta nauli yake kisha tukashuka.
“Inabidi tutembee mpaka upande wa pili tukachukue Bajaj au bodaboda,” alisema Shenaiza huku akizidi kujitanda ushungi wake ili isiwe rahisi kwa mtu yeyote kumtambua, na mimi nilishusha kofia yangu ya pama, tukawa tunatembea kuelekea kule kwenye Bajaj.
Tukiwa tunatembea katikati ya tuta la barabara lililokuwa linatenganisha barabara mbili za lami, ghafla tulishtushwa na muungurumo mkali wa pikipiki kubwa mbili zilizokuwa zinakuja upande wetu, tukiwa hata hatujui zimetokea wapi.
“Tulijua lazima tutakupata tu, wewe ndiyo unajifanya kimbelembele kuingilia ishu za watu si ndiyo?” alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya kukwaruza, wote wakiwa wamesimamisha pikipiki zao kubwa huku na kule na kutufanya mimi na Shenaiza tubaki katikati, hofu kubwa ikanitanda ndani ya moyo wangu.
Cha ajabu zaidi, wakati wakiwa wametuzunguka pale barabarani, foleni ilianza kutembea, magari yakaanza kuondoka huku abiria waliokuwa wameshuka, nao wakiingia kwenye magari na kuendelea na safari.
“Leave him alone, what wrong has he done? (Mwacheni, kwani kuna jambo gani baya amefanya?) Kama mnanitaka mimi nichukueni lakini siyo huyu kijana wa watu,” alisema Shenaiza lakini hakuna aliyemsikiliza, ukichanganya na kelele za magari na vyombo vingine vya usafiri vilivyokuwa vikiondoka baada ya foleni kuanza kutembea, hakuna mtu aliyejua kilichokuwa kinaendelea.
“Siku nyingine hutakiwi kuingilia mambo yasiyokuhusu,” alisema mwanaume mmoja huku akinisogelea, nikawa nazidi kutetemeka kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, wangeweza kunifanya chochote wanachokitaka bila mtu yeyote kujua kilichokuwa kinaendelea.
“Nimesema muacheni?” alisema Shenaiza lakini kabla hata hajamalizia, mmoja kati ya wale wanaume wanne, alimtwanga ngumi nzito ya usoni, akapepesuka na kutaka kudondoka lakini mwingine alimdaka na kumsimamisha.
Hofu niliyoipata ilikuwa haielezeki, kama Shenaiza, mwanamke mrembo kiasi kile alipigwa ngumi nzito kiasi kile, mimi je? Nilijiuliza huku nikizidi kutetemeka, tayari nilishaanza kusikia harufu ya mauti.
Ghafla iliibuka pikipiki nyingine ambayo tofauti na zile nyingine, yenyewe ilikuwa na mtu mmoja tu, tena mwanaume aliyeonesha kuwa na umri mkubwa kuliko wale wengine, akafunua kioo cha kofia ngumu (helmet) aliyokuwa ameivaa, akanitazama kwa ukali, macho yangu yakagongana na yake.
Nilichokigundua, hakuwa Mtanzania na kwa kiasi kikubwa, alikuwa na sura inayofanana na Shenaiza kwa mbali, jambo lililonifanya niamini kwamba lazima atakuwa na uhusiano wa kindugu na msichana huyo, aliendelea kunitazama bila kuzungumza kitu chochote.
Nikiwa bado naendelea kutetemeka, magari yaliyokuwa kwenye foleni yakiwa yamepungua kabisa na eneo lote kurejewa na hali yake ya utulivu, nilimuona yule mwanaume akiwapa ishara fulani wale watu waliooonesha kuwa ni wafuasi wake, Shenaiza ambaye sasa alikuwa akivuja damu nyingi puani, akabebwa juujuu na kupakizwa kwenye pikipki ya yule mwanaume kisha akaondoka kwa kasi kubwa na kutokomea.
“Hili litakuwa funzo kwako na kwa watu wengine wenye tabia kama yako, usipende kuwasogelea wanawake usiowajua,” alisema mmoja kati ya wale wanaume, nikashtukia nikipigwa na kitu kizito kichwani, nikadondoka mzimamzima kama gunia. Sikuweza hata kupiga kelele za kuomba msaada.
Nikiwa pale chini, kwa taabu nilimuona mwanaume mmoja akichomoa kisu kikubwa na kunikalia, akakinyanyua na kukishindilia upande wa kushoto wa kifua changu bila huruma. Siwezi kuyaelezea maumivu ambayo niliyasikia, nikafumbua mdomo ili kupiga kelele za kuomba msaada lakini sauti haikutoka, nikasikia wale watu wakipongezana kisha wakapanda kwenye pikipiki zao na kuondoka kwa kasi.
Damu nyingi zilikuwa zinanitoka upande wa kushoto wa kifua changu kiasi cha kunifanya nilowe chapachapa. Nilijitahidi kuinuka pale nilipokuwa nimelala huku damu nyingi zikiendelea kunitoka lakini maumivu makali yalinirudisha chini.
Kwa kutumia mikono yangu miwili, nilijaribu kuminya pale kwenye jeraha kubwa ili kuzuia damu isiendelee kunimwagika lakini nilijikuta mikono ikikosa nguvu, kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo nilivyokuwa nazidi kuishiwa nguvu.
Watu wengi walianza kukimbilia pale nilipokuwa nimeanguka na kunizunguka, niliwasikia wengine wakishindwa kuficha hisia zao na kuanza kuangua vilio. Nadhani hali waliyoniona nayo iliwafanya waamini kwamba siwezi kabisa kupona kutokana na damu zilivyokuwa zinaendelea kunimwagika mithili ya bomba lililopasuka.
Nikiwa kwenye maumivu makali, nilijigeuza na kuanza kutazama angani, upeo wa macho yangu ukagota kwenye mawingu meupe na ya bluu yaliyokuwa yakilipendezesha anga, nikabaki nimetulia nikiwa kwenye hali hiyo.
Kelele za watu wengi waliokuwa wanazidi kuongezeka eneo la tukio kunishangaa, zilianza kupungua taratibu masikioni mwangu, zikazidi kupungua na baadaye nikawa nasikia kama watu wananong’ona. Kwa mbali nilisikia mlio wa ving’ora ambavyo hata hivyo sikujua ni vya nini.
Nikiwa naendelea kutazama angani, taswira ndani ya mboni za macho yangu ilianza kufifia taratibu na kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo nayo ilivyozidi kufifia, japokuwa ilikuwa ni asubuhi, kigiza kikaanza kutanda kwenye macho yangu.
Nakumbuka neno la mwisho nililofanikiwa kulisema, ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa kutokana na midomo yangu kuwa mizito, ilikuwa ni: Mungu nisaidie! Nikafumba macho na giza totoro likatawala kila sehemu, sikuelewa tena kilichoendelea baada ya hapo!

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...