Thursday, August 17, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 16


ILIPOISHIA:
Nilimtazama Raya aliyekuwa bado amelala juu ya kifua changu, nikajiuliza mara mbilimbili kama nipokee au la. Mpaka simu inakata, sikuwa nimeamua nini cha kufanya, ikaanza tena kuita mfululizo ambapo nililazimika kuipokea, sauti ya Samantha ikasikika upande wa pili, ikinipa taarifa ambazo zilinishtua mno.
“Unasemaaa?” nilijikuta nikiuliza kwa sauti ya juu, iliyomzindua Raya usingizini.
SASA ENDELEA…
Wamekuja tena hapa hospitalini wanataka kuniua na wametishia kwamba wanahisi na wewe unahusika kwenye hiki kinachoendelea kwa hiyo wameapa kufanya kila kinachowezekana kuhakikisha wanatupoteza wote wawili.
“Lakini Shenaiza, hivi ingekuwa wewe ndiyo upo kwenye nafasi yangu ungejisikiaje? Yaani unajikuta tu upo katikati ya mambo ya hatari, maisha yako yanawindwa usiku kucha lakini hata huelewi chanzo ni nini, ungejisikiaje?”
“Ningejisikia vibaya Jamal lakini si nilishakwambia nitakueleza kila kitu? Wala huna haja ya kuwa na haraka wala kukasirika.”
“Utaniambia lini? Unajua kilichonitokea nilipoondoka hapo hospitalini? Bado kidogo ningekufa leo, kibaya ni kwamba sijui hasa kinachoendelea, sijui chochote kuhusu wewe wala matatizo yako ambayo sasa yameshakuwa yangu pia.”
“Huu sio muda wa kulaumiana Jamal, nakuomba kama ulivyofanya mara ya kwanza, njoo unitoroshe tena hospitali na nakuahidi safari hii tukitoka tu, nitakueleza ukweli wa kila kitu.”
“Hapana! Siwezi Shenaiza, tafuta mtu mwingine wa kuifanya kazi hiyo, sipo tayari.”
“Jamani Jamal, kwa hiyo upo tayari kuona nakufa wakati uwezo wa kunisaidia unao? Tena asubuhi hii ndiyo muda mzuri, watu wakija kuwaletea wagonjwa chai na sisi tunatumia muda huohuo kutoroka, nipo chini ya miguu yako,” alisema Shenaiza kwa sauti iliyoonesha alikuwa akilengwalengwa na machozi.

Nilishindwa cha kumjibu, nikamuona Raya naye ambaye bado alionesha kuwa na usingizi, akijigeuza pale kitandani na kunikumbatia tena ikiwa ni ishara kwamba hakufurahishwa na kitendo cha mimi kuzungumza na Shenaiza alfajiri ile.
“Ok, basi sawa nitajua cha kufanya,” nilijibu harakaharaka kisha nikakata simu. Nililazimika kumkatisha kwa sababu sikutaka kuendelea kumkasirisha Raya.
“Good morning baby!” (Habari za asubuhi mpenzi) alisema Raya huku akijinyoosha mwili kwa uchovu, akanibusu mdomoni na kunikumbatia tena.
“Ulikuwa unaongea na nani kwenye simu?” aliniuliza swali ambalo nilijua kwamba majibu yake anayo ila anataka kunitega.
“Si huyu Shenaiza, asubuhi yote hii anaanza kuleta matatizo mengine!”
“Mh! Anasemaje tena?”
“Ananiambia kuwa wale watu wanaotaka kumuua, wameanza kunitafuta na mimi na wamemuapia kuwa ni lazima watufanye kitu kibaya, mimi na yeye.”
“Ooh! Mungu wangu, nakuomba Jamal uachane na huyo msichana, achana kabisa na mambo yake, kama ni matatizo ni yake wala wewe hayakuhusu, isitoshe mtu mwenyewe ndiyo kwanza mmejuana, achana naye nakuomba,” alisema Raya kwa hisia za hali ya juu.
Japokuwa alikuwa na hoja kwa alichokuwa anakizungumza, akili zangu zilikuwa ni kama zimezingirwa na ukungu, nikawa sielewi nataka nini maishani mwangu. Niliona kama matatizo yaliyokuwa yanamkabili Shenaiza, yalikuwa yananihusu sana na ni mimi pekee ndiye niliyekuwa na uwezo wa kumsaidia.
Japokuwa kuna wakati mwingine nilikuwa nikiona kama nabebeshwa mzigo nisioustahili, bado niliona ninayo nafasi ya kumsaidia. Ilibidi niamke na kuelekea bafuni, Raya naye akaamka na kunifuata, tukaoga pamoja huku Raya akionesha kufurahishwa mno na ukaribu wangu.
Tulirudi chumbani ambapo wakati mimi nikijiandaa, Raya alienda jikoni kuandaa kifungua kinywa. Nilipomaliza kujiandaa, tayari kifungua kinywa kilikuwa tayari, Raya akiwa ndani ya khanga moja tu, akanikaribisha mezani.
Mwenyewe alitamani asubuhi hiyo tuendelee kukaa kimahaba kama ilivyokuwa usiku lakini akili zangu zilikuwa zikienda mbio sana, nikapata kifungua kinywa harakaharaka kisha nikamuaga.
Haikuwa rahisi kwake kuniruhusu, ikabidi nimdanganye kwamba nitarudi muda mfupi baadaye na sitatoka tena siku hiyo mpaka usiku. Ilibidi aniruhusu kwa shingo upande lakini akanitaka kuwa makini sana kwa kila kitu nitakachokuwa nakifanya.
Tulikumbatiana, nikambusu kwenye paji la uso wake kisha nikatoka, hatua kadhaa mbele niligeuka na kumtazama, nikamuona machozi yakimlengalenga, sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea na safari yangu.
Nilitoka na kwenda moja kwa moja mpaka hospitalini alikokuwa amelazwa Shenaiza, bado ilikuwa ni mapema sana na ndugu, jamaa na marafiki wa wagonjwa wengi walikuwa wakiwapelekea vifungua kinywa.
Ilibidi na mimi niingie kwenye mgahawa mmoja ulikuwa nje ya hospitali na kuchukua kifungua kinywa kwa ajili ya Shenaiza. Nilifanya hivyo ili isiwe rahisi kwa walinzi na madaktari kunihisi vibaya. Saa kumi na mbili kamili nilikuwa nikiingia kwenye mlango wa wodi aliyokuwa amelazwa Shenaiza.
Niliingia kimyakimya bila kuonekana na mtu yeyote mpaka pembeni ya kitanda cha Shenaiza, nikamuinamia na kumsemesha kwa sauti ya chini.
“Shenaiza! Shenaiza!”
“Ooh! Jamal, ahsante kwa kuja mpenzi wangu,” alisema Shenaiza ambaye kwa ilivyoonesha, hakuwa amelala bali aligeukia ukutani tu, akanikumbatia na kunibusu kwa hisia nzito huku akionesha mwili wake kuwa kwenye maumivu makali.
“Ni wewe pekee ndiye unayeweza kunisaidia kwa sababu hata polisi nao naona wanasuasua tu, najua nakubebesha mzigo mzito lakini nakuhakikishia wema wako hautapita bure, usichoke kunisaidia,” alisema Shenaiza kwa sauti ya chini akijaribu kujikakamua na kuinuka pale kitandani.
Nilimsaidia kufanya hivyo, akakaa juu ya kitanda na kuanza kuangaza macho huku na kule.
“Huu ndiyo muda mzuri, inabidi tuondoke kabla hawa mashetani hawajafika,” alisema Shenaiza, nikawa naitika kila kitu alichokuwa ananiambia. Japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni kosa jingine kubwa, nilijikuta nikiwa sina cha kufanya zaidi ya kutii kile Shenaiza alichokuwa anakitaka.
Tukatoka mpaka nje ya hospitali hiyo bila kugunduliwa na mtu yeyote, sikutaka kufanya makosa kama yale niliyoyafanya siku ile nilipomtorosha Shenaiza kule Amana, tukaenda mpaka kwenye kituo cha daladala na kupanda iliyokuwa inaelekea Makumbusho.
Ili kuzidi kupoteza ushahidi, nilimwambia Shenaiza ajifunike khanga yake, na mimi nikavaa kofia kubwa ya pama, tukatulia kwenye siti ya watu wawili. Abiria wengine waliendelea kuingia na baada ya gari kujaa, safari ilianza huku moyoni nikisali kusitokee jambo lolote baya.
“Sidhani kama tutafika salama huko tunakokwenda, moyo wangu unasita sana,” alisema Shenaiza kwa sauti ya kutetemeka. Sijui alikumbwa na nini mpaka aanze kuzungumza maneno yake, nikawa nampa moyo kwamba asiogope chochote.
Safari iliendelea mpaka tuklipofika Magomeni ambako kulikuwa na foleni kubwa sana asubuhi hiyo, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
“Nimekwambia kwamba sijui kama tutafika salama, umewahi kuona asubuhi namna hii kunakuwa na foleni kama hii?” alisema Shenaiza huku akizidi kuonesha hofu kubwa ndani ya moyo wake, nikawa nazidi kumtuliza.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.




No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...