Monday, August 21, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 18


ILIPOISHIA:
Nakumbuka neno la mwisho nililofanikiwa kulisema, ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa kutokana na midomo yangu kuwa mizito, ilikuwa ni: Mungu nisaidie! Nikafumba macho na giza totoro likatawala kila sehemu, sikuelewa tena kilichoendelea baada ya hapo!
SASA ENDELEA...
Katika hali ambayo sikuitegemea na ambayo mpaka leo huwa siwezi kuifafanua, muda mfupi baadaye nilijikuta nikizinduka lakini nikiwa kwenye hali ya tofauti kabisa. Nilizinduka nikiwa palepale nilipokuwa nimelala awali lakini katika hali ya ajabu, nilikuwa mwepesi sana.
Nikajikuta nikianza kupaa taratibu kuelekea juu. Nikiwa juu kidogo, niligeuka na kutazama pale nilipokuwa nimeangukia, nikashangaa kuona bado mwili wangu ulikuwa umelala palepale, damu nyingi zikiendelea kutoka kwenye jeraha la kifuani, tena safari hii zikitoka kwa mabongemabonge.
“Mungu wangu! Hiki ni kitu gani tena?” nilijikuta nikisema kwa sauti ya chini, ungeweza kudhani nilikuwa kwenye ndoto lakini haikuwa hivyo. Nilijiuliza kama mwili wangu bado ulikuwa pale chini, mimi niliyekuwa napaa nilikuwa ni nani? Sikupata majibu.
Niliendelea kupaa kuelekea juu mpaka nikafikia umbali wa mita kadhaa, ulioniwezesha kuona vizuri kila kitu kilichokuwa kinaendelea eneo la tukio. Niliwaona watu wakizidi kumiminika kwa wingi eneo la tukio, wengine wakishika vichwa vyao baada ya kuuona mwili wangu ukiwa kwenye hali ile.
Hali hiyo ya ajabu iliendelea kunitokea, nakumbuka niliendelea kushuhudia kila kitu kilichoendelea, jinsi mwili wangu ulivyochukuliwa kutoka eneo la tukio na kukimbizwa mpaka hospitali ambako nako niliona madaktari walivyokuwa wakichakarika kuokoa maisha yangu.
Niendelee kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea, katika ulimwengu wa kawaida sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa nimefumba macho na kulala pale kitandani kama maiti, nikiwa nimeunganishwa na mashine ya kunisaidia kupumua lakini katika ulimwengu mwingine ambao hata sijui niuiteje, nilikuwa nimesimama kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea.
Kazi ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari na manesi wakawa wanapishana huku na kule, huyu kabeba dawa, huyu kabeba chupa ya damu, huyu mikasi na sindano, ilimradi kila mmoja alikuwa bize.
Nilijisikia ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona watu ambao pengine hata hawakuwa wakinijua, wakipigana kuokoa maisha yangu. Niliendelea kuwatazama wanavyohangaika, kuna wakati machozi ya uchungu yalikuwa yakinitoka kwa sababu ya kilichotokea, nikawa naendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Narudia tena, mpaka leo huwa napata sana ugumu kuelezea hasa kile kilichotokea ni nini, yaani mimi niliyekuwa nashuhudia hayo yote nilikuwa nani na ule mwili ambao watu wote walikuwa wakiamini kwamba ni mimi, ulikuwa kitu gani?
Jambo pekee ninaloweza kusema, ni kwamba kila jambo linatokea maishani linatokea kwa sababu maalum na kuna mambo mengi sana yanayoendelea kutokea hapa duniani ambayo mimi na wewe hatuyajui. Huenda mimi nilitokewa na haya ili leo nije kutoa ushuhuda kwa watu ambao huwa ni wagumu kuamini kwamba kuna maisha mengine zaidi ya haya tunayoyajua.
Maisha haya ya kawaida ya binadamu tulio wengi, yamejawa na mambo mengi sana ambayo kwa akili za kawaida huwezi kuyaelewa na nilichojifunza ni kwamba mambo mengi humu duniani, hayapo kama ambavyo tumezoea kufikiria yapo. Kwamba hakuna jambo ambalo linatokea kwa bahati mbaya! Hata hizi ajali ambazo wengi huwa tunaona kwamba zimetokea kwa bahati mbaya, huwa hazitokei tu!
Waingereza wana msemo mmoja maarufu kwamba ‘everything is predestined’ wakimaanisha kila kinachotokea maishani tayari kilishapangwa! Nasisitiza hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya.
Yawezekana hata wewe usinielewe kwa sasa lakini napenda kukuhakikishia kwamba mambo mengi sana ambayo tunayajua na kuyaamini, hayapo vile ambavyo kwa miaka mingi tumekuwa tukiyaamini. Nikisema dunia nzima imejaa vitu vingi ambavyo havipo kama tulivyozoea kuviona, huenda ukawa hunielewi kwa urahisi lakini mimi nasimulia mambo ambayo yamenitokea mwenyewe.
Ukitaka kuamini, kuanzia sasa, anza kutazama kila kitu kwa jicho la tatu! Hata lile jambo ambalo ulikuwa unaamini kwamba unalijua au ulikuwa unaamini kwamba ni ukweli, hebu anza kulitazama kwa namna nyingine na jiulize maswali katika kila jambo, kuanzia kuhusu wewe mwenyewe, kwamba wewe ni nani, kwa nini upo duniani, umetoka wapi na unaelekea wapi na mambo yote yanayokuzunguka, utaanza kuelewa ninachokimaanisha.
Basi nikiwa nimesimama palepale kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea kwenye mwili wangu uliokuwa umelazwa pale kitandani ukiwa hauna fahamu hata kidogo, nilishtuka baada ya kuhisi upepo mkali ukianza kuvuma mle ndani ya wodi.
Sikuelewa ule upepo umetokea wapi kwa sababu milango na madirisha yote yalikuwa yamefungwa, baadhi ya vifaa vilivyokuwa mezani, vilianza kudodondoka, vikiwemo vichupa vya dawa na vifaa vingine vya kidaktari, manesi wakawa na kazi ya kuviokota na kuviweka sawa.
Ghafla nilihisi kama nashikwa na mtu mwenye nguvu sana, nikanyanyuliwa kutoka pale nilipokuwepo, kufumba na kufumbua, nikajikuta nipo kwenye mazingira mengine tofauti kabisa, mahali ambapo hata sijui nipaelezeeje. Kulikuwa na giza totoro kila upande, kiasi kwamba hata ukisogeza kidole jirani kabisa na jicho lako, usingeweza kuona kitu chochote.
Yule mtu ambaye alikuwa amenishika na kunitoa kule wodini, ambaye nasema ni mtu kwa sababu mikono yake ilikuwa ya kibinadamu kwa sababu na mimi nilimshika nikitaka kumjua ni nani lakini nikashindwa hata kumuona kwa sababu ya giza, aliniachia, nikajikuta nimesimama sehemu ambayo sikujua mbele ni wapi wala nyuma ni wapi, giza lilikuwa nene kikwelikweli.
“Jamal!” nilisikia sauti nzito, iliyokuwa ikisikika kama mwangwi, ikiliita jina langu. Umewahi kuingia kwenye sehemu ambayo ina uwazi mkubwa halafu ukatamka neno lolote na kusikia likijirudiarudia? Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, ile sauti nzito ilijirudiarudia mara kadhaa.
“Mungu wangu, hiki ni nini tena?” nilijisemea moyoni kwa hofu kubwa lakini tofauti na nilivyotegemea, wakati mimi nikiamini kwamba najisemea moyoni, niliisikia sauti yangu ikisikika utafikiri niliyatamka maneno yale mdomoni wakati ukweli ni kwamba niliyasemea moyoni.
Nikajikuta nikitetemeka kuliko kawaida, hofu kubwa ikiwa imeukumba moyo wangu ambao sasa ulikuwa ukidunda kwa nguvu kiasi cha mapigo yake kusikika vizuri kabisa hata kwa mtu aliyekuwa pembeni yangu.
“Jamal!” ile sauti ilisikika tena lakini tofauti na mwanzo, safari hii ilisikika ikionesha aliyeitoa alikuwa amesogea mbali kabisa na mimi, nikawa natamani kuitikia lakini nilishindwa kutokana na hofu kubwa iliyokuwa imenizingira.
“Jamal!” ile sauti ilisikika tena kwa mara ya tatu, safari hii ikionesha kwamba aliyekuwa akiniita alikuwa mbali zaidi. Katika hali ambayo siwezi kuielezea, nilijikuta nikianza kutembea kuelekea kule sauti ile ilikokuwa inazamia. Kwa mbali nikaanza kusikia sauti kama za watu wanaougulia maumivu makali, sauti za watoto wachanga waliokuwa wakilia na sauti za kutisha za wanyama ambazo nyingine hata sijawahi kuzisikia tangu nizaliwe.
Kuna wakati hofu ilinizidi na kutaka nigeuze nilikotoka lakini kitu ndani ya moyo wangu kikaniambia nizidi kusonga mbele. Kadiri nilivyokuwa nazidi kusonga mbele ndivyo zile sauti zilivyokuwa zinazidi kuongezeka, nikazidi kutetemeka kwa hofu huku nikiwa sijui nini itakuwa hatma yangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...