Monday, August 21, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 27


ILIPOISHIA:
Sikutaka kumuamsha Rahma, nilimtoa kifuani kwangu taratibu kisha nikashusha miguu chini, nikawa nimekaa huku nikitazama huku na kule. Sikuweza kuona chochote kutokana na giza lililokuwa limetanda usiku huo. Mara nikasikia kishindo kizito kama cha kitu kilichodondoka kutoka darini mpaka sakafuni, mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio kuliko kawaida.
SASA ENDELEA...
Nilikaza macho kwenye giza kujaribu kuangalia ni kitu gani hicho kilichodondoka, kwa mbali nikaanza kuona kama mtu amepiga magoti kwenye kona ya chumba hicho, taratibu akaanza kuinuka, nikazidi kumkazia macho na kadiri muda ulivyokuwa ukizonga ndivyo nilivyozidi kuiona vizuri taswira yake.
Nilimtambua kwamba ni mwanamke kutokana na maumbile yake ingawa alionesha kuwa ni mzee kwani niliweza kuiona ngozi yake ilivyokuwa imekunjamana, nikamkazia macho usoni nikitaka niione sura yake. Hata hivyo eneo la usoni lilikuwa na giza sana, nikamuona akiinua mikono juu kama anayetoa ishara fulani, akageuka na kuanza kujisugua makalio yake ukutani.
Mara nilisikia kishindo kingine, hofu ikazidi kutanda ndani ya moyo wangu, kijasho chembamba kikawa kinanitoka huku nikiwa nimekodoa macho kwa nguvu zote.
 Nilitamani niamke nikawashe taa lakini ujasiri huo sikuwa nao, nilitamani niingie chini ya kitanda lakini mwili wote haukuwa na nguvu, nilitamani kupiga kelele kuwaamsha nyumba nzima lakini sikuwa na uwezo huo, nikawa natetemeka kuliko kawaida.
Nilipotazama kwa makini pale chini, nilimuona mtu mwingine kama yule wa kwanza naye akiinuka taratibu lakini tofauti yake, huyu alikuwa mwanaume kutokana na jinsi mwili wake ulivyokuwa na alionesha pia kuwa mzee zaidi maana mpaka mgongo wake ulikuwa umepinda.
Alipoinuka, naye alisogea ukutani na kuanza ‘kusonta’ ukutani kwa kutumia makalio yake kisha akasogea mbele na kushikama mikono na yule mwanamke wa kwanza, wakaiinua juu na kutoa ishara ambayo sikuielewa, mara nikasikia vishindo mfululizo.
Vilisikika vishindo kama sita hivi, ikimaanisha kwamba watu wengine sita walikuwa wameingia, uzalendo ukanishinda. Sijui nilipata wapi ujasiri, nikasimama wima kisha nikapaza sauti, ‘tokeni hapa washenzi nyie, hata mimi baba yangu ni mchawi vilevile’.
Kauli yangu ni kama iliwashtua watu wale wa ajabu ambao hata sielewi niwaelezeeje, wote wakashtuka na kunitazama, nikazidi kushtuka baada ya kuona wote macho yao yalikuwa yakiwaka kama mnyama mkali gizani.
Kwa wale ambao wameishi maeneo ya maporini watakuwa wananielewa kwamba mida ya usiku, wanyama kama simba, chui, mbwa mwitu au hata mbwa wa kawaida na paka, wakiwa kwenye giza totoro kisha wakakukodolea macho yao, huwa yanatoa mwanga fulani wa kutisha.
Kwa jinsi walivyonitazama, hofu ilinizidi maradufu lakini nikaona hakuna kingine cha kufanya zaidi ya kuendelea ‘kugangamala’. Sikuwa najua kama wakinigeukia nitafanya nini, sikuwa najua mbinu zozote za kupambana nao na eti nilijikuta nikijilaumu kwa nini baba hakunifundisha au hakunipa mbinu yoyote ya kukabiliana na wachawi.
Yule mwanamke aliyekuwa wa kwanza kuingia mle ndani, nilimuona akinisogelea huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya woga. Nilihisi haja ndogo ikitaka kunitoka lakini nilijikaza kiume na kusema liwalo na liwe, akanisogelea jirani kabisa huku akiendelea kunitazama kwa macho yake makali, cha ajabu, licha ya kunisogelea, sikuweza kabisa kuitambua sura yake.
Nimewahi kusikia kwamba wachawi wana kawaida ya kula nyama za watu, nikahisi na mimi usiku huo nakwenda kuliwa huku nikijiona. Niliujutia uamuzi wangu wa kusimama na kuwafokea watu hao, nikiwa bado natetemeka, nilisikia kofi moja zito likitua kwenye shavu langu la kushoto, maumivui niliyoyasikia yalikuwa hayaelezeki, nikapiga kelele kwa nguvu nikimuita baba.

Sikumbuki kama nimewahi kutoa sauti kubwa kama hiyo maishani mwangu, mara mlango ukaanza kugongwa kwa nguvu nje, nikasikia kibao kingine kikitua kwenye shavu la upande wa pili, likafuatiwa na misonyo mingi kisha wale watu wakayeyuka wote na kupotea kama moshi upoteavyo angani.
“Togo! Nini kimetokea?” alisema baba baada ya kuwa amefanikiwa kufungua mlango na kuwasha taa. Jambo la aibu ni kwamba baada ya ule mchezo wa kikubwa niliocheza na Rahma, hakuna aliyekumbuka tena kuvaa nguo zake kwa hiyo nilikuwa kama nilivyozaliwa, baba akanitazama kwa mshangao.
Najua alishangazwa na mambo mengi kwa wakati mmoja, kwanza kwa nini nilikuwa chumbani kwa Rahma mpaka usiku huo wakati makubaliano yalikuwa ni kwamba kila mmoja atalala kwake, kwa maana kwamba baada ya c hakula ilitakiwa mimi nitoke na kwenda kwenye chumba nilichopangiwa lakini sikufanya hivyo. Yote tisa, kumi ni kwamba nilikuwa kama nilivyozaliwa, na Rahma naye ambaye bado alikuwa kwenye usingizi mzito, akikoroma bila kujua chochote kilichokuwa kinaendelea, hakuwa na chochote mwilini, nikamuona baba akishusha pumzi ndefu na kunipa ishara kwamba nivae kwanza nguo, akatoka na kuurudisha mlango.
Kumbe sekeseke hilo lilisababisha nitokwe na haja ndogo bila kujua, ikabidi nichukue tambara la kufanyia usafi na kufuta harakaharaka huku nikigeuka kumtazama Rahma asije kuwa ameamka na kuona nilichokifanya. Nilipomaliza kufuta, harakaharaka nilivaa nguo zangu huku nikitetemeka kuliko kawaida.
Baba alikuwa pale mlangoni akinisubiri, nilipomaliza aliingia na kunionesha ishara kwamba nisizungumze kwa sauti ya juu, akaniuliza nini kilichotokea.
“Wachawi baba, wachawi wengi wamekuja, angalia walivyonifanya,” nilisema huku nikimuonesha mashavu yangu ambayo nilikuwa nahisi kama yanawaka moto. Awali niliona baba hataki kuamini kama ambavyo imekuwa kawaida yake mara kwa mara ninapotokewa na mambo kama hayo lakini nashukuru safari hii kulikuwa na ushahidi wa moja kwa moja.
“Mungu wangu, umefanya nini?”
“Wamenipiga,” nilisema huku nikianza kutokwa na machozi.
“Hebu niambie ukweli, umefanya tena mapenzi na Rahma?”
“Ndiyo.”
“Lakini si tumeshawakataza nyie na kuwasisitiza kwamba msirudie ujinga wenu?” baba alizungumza kwa hasira lakini kwa sauti ya chini. Sikujua kwa nini alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini, akanishika mkono na kufungua mlango, akatazama huku na kule na alipojiridhisha, alinipeleka mpaka kwenye chumba ambacho ndicho nilichotakiwa kulala.
“Hutakiwi kumwambia yeyote kuhusu hiki kilichotokea, umenielewa?” baba aliniambia, nikatingisha kichwa lakini nilijiuliza, kama yeye ameweza kusikia zile kelele nilizopiga, si ina maana nyumba nzima wamesikia? Na kama wamesikia, kwa nini wengine wote hawakuamka isipokuwa yeye tu?
“Lakini kwa nini haya yanatokea?” utajua tu lakini unachoniudhi ni kwamba ukiambiwa jambo fulani usilifanye, wewe ndiyo unalifanya. Hukuwa na mambo ya wanawake kabisa lakini tangu tumefika hapa ndiyo umekuwa mchezo wako... utasababisha vifo vya wasio na hatia kwa nini unakuwa mgumu kuelewa?” baba alisema, safari hii siyo kwa ukali bali kwa hisia za ndano kabisa, kauli yake ikanishtua mno.
Yaani mimi ndiyo nisababishe vifo vya wasio na hatia? Kivipi? Halafu kulikuwa na uhusiano gani wa mimi kulala na Rahma na hayo yaliyokuwa yanatokea? Katika yote, jambo ambalo nilijiapiza, ni kwamba kamwe sitamuacha Rahma maana alikuwa amenionesha dunia ya tofauti mno.
Baba alitoa kichupa kilichokuwa na unga mweusi lakini kabla hajafanya chochote, aliniambia nikajitazame kwenye kioo kilichokuwa humo chumbani.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko usio wa kawaida.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...