Thursday, July 20, 2017

Makaburi ya Wasio na Hatia (The Graves of the Innocents)- 4


ILIPOISHIA:
“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?” alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha kwenye uso wangu.
SASA ENDELEA...
“Kwamba mwalimu wetu anaumwa. Nilisikia asubuhi nikawa siamini,” nilidanganya, nikamuona mwalimu Timbuka akishusha pumzi ndefu, wanafunzi wenzangu waliokuwa wakinitazama kwa shauku, nao walionesha kuridhika na majibu yangu.
Baada ya kutoa taarifa hizo, mwalimu Timbuka alitutaka tusipige kelele bali tuutumie muda huo kujisomea, akatoka na kutuacha wote tukiwa kimya. Moyoni mwangu niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Kwa hiyo mwalimu Mwashambwa naye atakufa?” nilijiuliza moyoni wakati nikiendelea kutafakari taarifa za ugonjwa wa mwalimu wetu. Nilijaribu kuunganisha matukio, hofu ikazidi kuongezeka ndani ya moyo wangu. Bado sikutaka kuamini kwamba baba alikuwa mchawi na alikuwa akihusika na kilichokuwa kinaendelea.
Muda ulizidi kusonga mbele, hatimaye ukawadia muda wa mapumziko. Kwa kawaida, ilikuwa ikifika muda wa mapumziko, kengele inagongwa mara mbili kuashiria wanafunzi wote tutoke madarasani lakini siku hiyo, kengele iligongwa tofauti. Iligongwa mfululizo huku walimu wakiwa wameshatoka na kusimama mstarini, kila mmoja akionekana kuwa ‘siriasi’.

“Kuna nini kwani?” nilijiuliza wakati nikisimama na kutoka pamoja na wanafunzi wenzangu, tukaelekea mstarini huku kila mmoja akiwa na shauku kubwa ya kusikia kilichofanya tukusanyike muda huo, jambo ambalo siyo la kawaida.
Mwalimu mkuu wetu, Nyerema alisimama na kututaka wote kutulia na kumsikiliza alichokuwa anataka kutuambia.
“Ni siku mbaya kwetu, najua wote mnajua kwamba mwalimu wenu, Mwashambwa alikuwa anaumwa sana, taarifa mbaya ni kwamba hatunaye tena, tumepokea taarifa za kifo chake muda huu, nawaomba nyote mtulie na muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, taratibu nyingine mtatangaziwa baadaye,” alisema mwalimu Nyerema, vilio vikaanza kusikika kutoka kwa wanafunzi.
Siyo siri nilipatwa na mshtuko mkubwa sana, sikutaka kuamini kwamba mwalimu Mwashambwa ameondoka. Niliunganisha matukio na kile nilichoelezwa na baba, nikawa siamini.
“Ina maana baba ndiye anayehusika na kifo cha mwalimu wetu pia?” nilijiuliza moyoni nikiwa bado nimesimama palepale. Nikiwa katika hali ile, nilihisi kuna mtu ananitazama, nikageukia kule mtu huyo alipokuwepo. Hakuwa mwingine bali mwalimu Timbuka ambaye alikuwa akinitazama kwa makini. Kwa ilivyoonesha, alikuwa akinitazama kwa muda mrefu, nikabaki kubabaika kwa sababu sikuelewa kwa sababu gani ananitazama namna ile.
Ili kuvunga, nilijichanganya na wanafunzi wengine na kuondoka eneo hilo, nikarudi darasani ambako wanafunzi wengi walikuwa wakiendelea kulia kwa uchungu. Baadaye kengele iligongwa tena, tukatoka na kwenda mstarini ambapo tulipewa utaratibu wa namna ya kushiriki msiba wa mwalimu wetu.
Wakati wanafunzi wengine wakifunga safari kuelekea kwa mwalimu Mwashambwa, mimi nilichepuka na kukimbilia nyumbani, moyoni nikiwa na dukuduku kubwa.
“Amekufa kama ulivyosema.”
“Si nilikwambia? Umeamini sasa!”
“Kwa hiyo wewe ndiyo umemuua? Kwani baba wewe ni mchawi?” nilijikuta nikimuuliza baba swali ambalo hata yeye hakulitegemea, akanitazama kwa macho ya ukali.
“Nani aliyekwambia mimi ni mchawi?”
“Nimesikia watu wakisema, hata shuleni kwetu kote watu wananinyooshea vidole wakisema eti mimi na wewe tunashirikiana uchawi,” nilisema huku nikitetemeka, baba akanisogelea kisha akashusha pumzi ndefu.
“Mwanangu Togolai, lazima ujue kwamba hapa kijijini sisi tuna maadui wengi sana kwa sababu ya kazi ninayofanya baba yako. Watu wengi wananionea wivu kwa sababu hakuna mganga mwenye nguvu kama mimi ukanda wote huu. Sasa maadui zangu wameanza kunizushia na kunichafulia sifa nionekane mchawi lakini siyo kweli, mimi ni mganga wala siyo mchawi,” alisema baba kwa sauti iliyojaa busara na upole.
Licha ya maneno yote yaliyokuwa yanazungumzwa na watu, nilikuwa nikiamuamini sana baba. Niliyaamini maelezo yote aliyonipa kwa asilimia mia moja, na mimi nikashusha pumzi ndefu kisha tukawa tunatazamana na baba.
“Ikitokea mtu mwingine yeyote anakutania au anakuzodoa kuhusu uchawi, naomba uje unieleze moja kwa moja, wakati mwingine inabidi tuwe wakali ili kulinda heshima yetu,” alisema baba kisha akainuka na kuniacha nimekaa palepale, nikawa naendelea kuyatafakari maneno aliyoniambia.
Japokuwa nilikuwa nampenda sana mwlimu Mwashambwa, sikuweza kuhudhuria kwenye msiba wake nikihofia macho ya watu kwani tayari maneno yalikuwa yamesambaa sana kwamba baba alikuwa anahusika na vifo vya ghafla vya watu wawili, Mwankuga na Mwashambwa vilivyotokea mfululizo.
Hatimaye mazishi yalifanyika lakini manenomaneno yalizidi kuwa mengi kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele. Siku moja nikiwa shuleni, nilisikia wanafunzi wenzangu wakinitena kwamba mwisho wa ubabe wa familia yetu ulikuwa umefika kwa sababu wanakijiji walikaa kikao cha pamoja na kufikia maazimio ya kwenda kumleta mganga mashuhuri kutoka Chitipa, Malawi kwa ajili ya kuja ‘kuwanyoa’ uchawi watu wote waliokuwa wakihisiwa kuhusika na ushirkina pale kijijini kwetu, akiwemo baba.
“Baba nimesikia eti kuna mganga amefuatwa Malawi kuja kuwanyoa uchawi watu wote wanaotajwa kuhusika kusababisha viofo vya watu wasio na hatia hapa kijijini, ukiwemo wewe,” nilimwambia baba baada ya kurejea kutoka shuleni.
Tofauti na nilivyotegemea, baba hakuonesha kushtushwa na kitu chochote, akawa anaendelea kukatakata mizizi ya dawa nje ya nyumba yetu huku akisema kwamba wanajisumbua kwa sababu yeye siyo mchawi.
“Watanyoana wenyewe kwa wenyewe, mimi hakuna mtu anayeweza kunigusa,” alisema baba kwa kujiamini, nikakosa cha kuendelea kuzungumza. Maisha yaliendelea kusonga mbele, siku saba baadaye, mkutano wa wanakijiji ulitishwa kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Makongorosi ambapo wanakijiji wengi walikusanyika.
“Baba wewe huendi kwenye mkutano?”
“Siendi, kama unataka nenda kaniwakilishe, nina shughuli zangu muhimu siwezi kuziacha kwenda kusikiliza upumbavu wa watu wa kijiji hiki,” alisema baba kwa kujiamini.
Kwa kuwa siku hiyo sikuwa na kazi, ilibidi nifanye kama baba alivyoniambia, nikaenda kumuwakilisha ingawa nililazimika kukaa nyumanyuma, sikutaka watu wajue kwamba niko pale. Niweke wazi kwamba tuhuma zilizokuwa zinamkabili baba na familia yetu kwa jumla zilitufanya tuikose amani kabisa.
Kila tulipokuwa tukionekana, ilikuwa ni lazima tunyooshewe vidole, jambo ambalo binafsi liliniathiri sana kisaikolojia. Nikapoteza kabisa uwezo wa kujiamini, nikawa naishi kama digidigi, hali kadhalika kwa ndugu zangu wengine ingawa kwa baba yeye alionekana kutojali chochote.
“Tumechoshwa na uchawi hapa kijijini kwetu. Kwa pamoja tumefanikisha ujio wa mganga Mabwanji kutoka Malawi kwa lengo la kusafisha kijiji chetu. Wale wote waliokuwa wanaringia uchawi wao, kiboko yao amewasili, karibu uwasalimie wanakijiji,” alisema mzee wa kimila pale kijijini ambaye tulizoea kumuita Mwene.
Mwanaume mzee mwenye macho mekundu sana na midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi, kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu wote wakashangilia kwa nguvu.

“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo, akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...