Wednesday, July 19, 2017

MAKABURI YA WASIO NA HATIA (GRAVES OF THE INNOCENTS)- 3


ILIPOISHIA:
Nikamuongoza baba mpaka kwenye kaburi la Alfred ambalo juu yake kulikuwa na msalaba ulioandikwa jina lake kamili, tarehe ya kuzaliwa na tarehe ya kufa kwake. Akaniambia niwe makini kwa kila atakachokuwa anakifanya, nikatingisha kichwa huku hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wangu kwani kiukweli nilikuwa nikiogopa sana makaburi na maiti.
SASA ENDELEA:
Baba alianza kufukuafukua ule upande wa kichwani kwenye lile kaburim akaingiza mkono mfukoni na kutoa kichupa kilichokuwa na ungaunga mweusi, akaumwaga kuanzia upande wa kichwani mpaka miguuni, kisha akaniambia tuanze kulizunguka lile kaburi kwa kuanzia kushoto kwenda kulia.
Alianza yeye, na mimi nikafuatia, tukawa tunazunguka lakini kwa kutembea kinyumenyume, baada ya kuzunguka raundi sana, nilianza kusikia kizunguzungu kikali, baba akaniambia nikae, yeye akarudi kusimama palepale alipokuwa amesimama.
“Hebu muite jina lake mara tatu kwa sauti kubwa,” alisema baba, nikawa simuelewi anamaanisha nini. Yaani mtu alishakufa siku nyingi zilizopita halafu ananiambia nimuite jina lake, tangu lini maiti ikaitika? Hata hivyo, ilibidi tu nitii kile alichoniambia, nikamuita.
Nililitaja jina lake kwa mara ya kwanza, baba akawa ananionesha ishara kwamba niongeze sauti, nikamuita kwa mara ya pili kisha kwa mara ya tatu. Cha ajabu kabisa, nilisikia akiitikia, tena niliweza kuthibitisha kabisa kwamba ni yeye kwa sababu nilikuwa naijua sauti yake na hata akizungumza neno moja tu, nakuwa nimeshamtambua.

Nilitetemeka kuliko kawaida, nikawa nageuka huku na kule kwa sababu alivyoitikia, ilionesha kwamba hayupo pale kwenye kaburi bali yupo umbali wa mita kadhaa pembeni. Nikiwa bado siamini, baba alinionesha kwa kidole, akaniambia nitazame chini ya mti mkubwa wa mjohoro uliokuwa pembeni kidogo ya makaburi.

Nilitazama lakini sikuona kitu, nikamgeukia baba, akaniambia niendelee kutazama bila kupepesa macho. Katika hali ambayo sikuitegemea, nilimuona Alfred akiwa amesimama chini ya mti, nywele zake zikiwa zimekuwa ndefu na chafu sana, rangi ya ngozi yake ikiwa imebadilika na kuwa utafikiri amejipaka unga wa mkaa usoni. Akiwa ni kama na yeye amegundua kwamba nimemuona, Alfred aligeuka na kuanza kutimua mbio, muda mfupi baadaye akapotelea kwenye msitu mkubwa uliokuwa pemebi ya makaburi hayo.
Nilibaki nimepigwa na butwaa, nikiwa siamini kabisa nilichokiona, baba akanigeukia na kunitazama usoni.
“Unaona sasa? Mambo mengine usiwe unakuwa mbishi tu,” alisema, nikawa bado nimepigwa na butwaa, nikihisi kama nipo kwenye ndoto za kutisha ambazo sikuwa najua mwisho wake utakuwa nini.
Ilibidi baba anishike mkono na kuanza kunivuta, akili zangu zikarudi sawa, nikawa bado nageukageuka kutazama kule Alfred alikokuwa amepotelea. Nitakuja kueleza zaidi juu ya mazingira ya kifo cha Alfrted ambapo sasa na mimi nilianza kuamini kwamba hakikuwa kifo cha kawaida. Baba ni kama alikuwa amenifumbua macho.
Tulirudi mpaka nyumbani, tukakuta bado watu wanazidi kuongezeka pale kwenye msiba wa Mwankuga.
Tulienda mpaka nyumbani lakini kwa kuwa bado nilikuwa na maswali mengi kuhusu kifo cha mzee huyo, ilibidi nimtoroke tena baba na kwenda pale msibani. Safari hii watu walikuwa tayariw ameshakaa pale nje kwa kujipanga, kila mmoja akiwa na uso wa huzuni.
Kitendo cha mimi kuonekana tu eneo hilo, nilishangaa watu wakiacha kila walichokuwa wanakifanya na kunikodolea macho. Hata wale waliokuwa wanalia, wote walinyamaza, wakawa wananitazama. Sikuelewa kwa sababu gani hali hiyo imetokea, hofu kubwa ikatanda ndani ya moyo wangu.
Kwa mbali nikaanza kusikia minong’ono huku watu wakiendelea kunitazama. Mzee mmoja ambaye naye siku za nyuma nimewahi kusikia kwamba ana tabia ya kuwaibia watu fedha kwa uchawi wa ‘chuma ulete’, alisimama na kuongea kwa jazba.
“Baba yako alichokifanya ameona hakitoshi ameamua kukutuma na wewe uje kuendeleza uchawi wenu hapa. Mwaka huu mtaisoma namba, kamwambie anajikaanga kwa mafuta yake mwenyewe, mwisho wake umekaribia,” alisema mzee huyo na kusababisha watu karibu wote pale msibani wamuunge mkono, zogo kubwa likatokea huku wengine wakiinuka na kutaka kuja kunishushia kipigo.
Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini watu walikuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini nilipofika msibani hapo. Kumbe walikuwa wanahisi baba amenituma mwenda kufanya uchawi! Maskini, nilibaki natetemeka kwa hofu kubwa kwa sababu sikuwa najua chochote kuhusu uchawi wala kuroga.
Ili kuokoa maisha yangu, ilibidi nitimue mbio, wakaendelea kunisindikiza kwa maneno makali wakimtuhumu baba na sisi familia nzima kwamba tunahusika na mambo ya kishirikina na kwamba eti sisi ndiyo tumemuua mzee Mwankuga kutokana na ugomvi wetu wa kugombea mpaka wa shamba.
Nilirudi nyumbani nikiwa natweta, mtu wa kwanza kuniona alikuwa ni baba ambaye alikuwa amekaa nje ya nyumba yetu, kwenye gogo kubwa la mti wa mvule akiandaa dawa zake, akashangaa kuniona naingia mbiombio huku nikilia. Alinisimamisha lakini sikusimama kwa hofu kwamba wale watu watakuwa wananifuatilia, nikapitiliza mpaka ndani na kwenda kujifungia chumbani kwetu.
Nilijuta kwa kutosikiliza kile alichokuwa ameniambia, nikawa natetemeka kwa hofu kubwa ndani ya moyo wangu. Niliendelea kujifungia chumbani kutwa nzima, nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Kwa mujibu wa maelezo ya baba, kama Mwankuga alikuwa amekufa, mwalimu Mwashambwa ambaye naye alikuwa naye kwenye lile tukio la kule porini, naye angekufa, jambo ambalo kidogo lilikuwa gumu kwangu kuliamini.
Kilichotokea siku hiyo, kuanzia kule porini tulikokuwa tumeenda kuchimba dawa na baba, kifo cha Mwankuga, kilichotokea kule makaburini na kelele za watu waliokuwa wakiituhumu familia yetu kuwa ya kichawi, vilinifanya nianze kumtazama baba kwa jicho la tofauti.
Basi siku hiyo ilipita nikiwa na mawazo mengi sana kuhusu yale matukio yaliyotokea, kila nilipokuwa nikifikiria, nilikosa majibu. Gumzo kubwa liliendelea kutawala kijijini kwetu kuhusu uchawi wa baba, kuna ambao walidiriki hadi kuja jirani na nyumba yetu na kuanza kutoa vitisho kwamba dawa yetu inachemka.
Nilifedheheka sana moyoni mwangu. Siku tatu baadaye, Mwankuga alizikwa kwenye makaburi ya kijiji huku msiba wake ukitawaliwa na vituko vya kishirikina vya hapa na pale ambavyo bado watu wengi waliendelea kuamini kwamba familia yetu inahusika.
Hatimaye Mwankuga alizikwa na kidogo zile kelele tulizokuwa tunapigiwa zikaanza kupungua. Hata hivyo, siku ya kwenda shule ilipofika (kipindi hicho bado nilikuwa nasoma Shule ya Msingi Makongorosi, Chunya) nilikumbana na unyanyapaa mkubwa sana shuleni.
Wanafunzi wenzangu walikuwa wakinitenga na kuniita mchawi, wakawa wanaituhumu familia yetu kwamba inahusika na vifo vya watu wengi waliokuwa wanakufa katika mazingira ya kutatanisha pale kijijini kwetu. Hata hivyo, kama baba alivyotufundisha wanafamilia wote, hatukutakiwa kujibizana na mtu yeyote, nikawa nasikiliza tuhuma zote bila kujibu chochote.
Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kutaka kumuona mwalimu Mwashambwa kwa sababu kwa mujibu wa baba, na yeye alikuwa pamoja na marehemu Mwankuga siku waliyokuwa wanapigana kichawi na baba kule porini. Nilikuwa na shauku kubwa ya kumuona mwalimu huyo kwa sababu nilitaka kujifunza kitu juu ya uchawi na wachawi.
Niliamini kwa kumtazama tu, naweza kugundua kitu kilichokuwa kimejificha nyuma ya maisha yake. Hata hivyo, baadaye ulipowadia muda wa kipindi cha hesabu, mwalimu wa darasa alikuja na kutuambia kwamba mwalimu Mwashambwa alikuwa anaumwa sana hivyo asingeweza kuja shuleni wala kuingia darasani mpaka atakapopona.
“Kumbe ni kweli!” nilijikuta nimeropoka kwa sauti kubwa, kauli iliyosababisha wanafunzi wote pamoja na mwalimu wanigeukie pale nilipokuwa nimekaa, nikasikia miguno ya chinichini ikitawala darasa zima.
“Ni kweli nini?” mwalimu wetu wa darasa, Madam Timbuka alihoji huku akinifuata pale nilipokuwa nimekaa. Nilijisikia aibu kubwa iliyochanganyikana na hofu, sikujua nimjibu nini mwalimu huyo kwani ndani ya akili yangu, nilikuwa nimezipokea taarifa hizo za ugonjwa wa mwalimu Mwashambwa na kile alichoniambia baba kwamba mwalimu huyo alikuwa mchawi na walikuwa wakishirikiana na marehemu Mwankuga.
“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?” alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha kwenye uso wangu.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Championi Jumatatu.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...