Tuesday, July 25, 2017

Graves of The Innocents (Makaburi Yasiyo na Hatia)- 6


ILIPOISHIA:
Huku nikitetemeka, nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Nani!”
“Fungua!”
“Sifungui mpaka mjitambulishe na mueleze shida yenu.”
“Ni mimi mzee Sifuni, mwenyekiti wa kijiji.”
“Unaonekana hauko peke yako!”
“Ndiyo, nimeongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji, fungua tafadhali,” baada ya mwenyekiti huyo kusema hivyo, baba alinioneshea ishara kwa mkono kwamba niende ndani kwa sababu alishahisi wale watu wamekuja kwa shari. Nikatii nilichoambiwa na kwenda chumbani lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kinachoendelea.
Baba alipofungua tu mlango, nilisikia wakimuamrisha jambo:
“Upo chini ya ulinzi.”
“Kwa kosa gani?”
“Kwa kumshambulia mganga wa kienyeji aliyekuwa anatimiza majukumu yake hapa kijijini kwetu.”

“Hivi nyie mna wazimu nini? Mbona mnanifuatafuata sana? Sasa anayejiona mbabe aniguse,” nilimsikia baba akifoka kwa jazba. Yule mwenyekiti akawa anaawamrisha mgambo wamkamate baba lakini kila mmoja akawa anamtupia mpira mwenzake kwa hofu.
Nadhani lile tukio la ‘kumzimisha’ mganga ambaye kila mmoja alikuwa akimuona kama ni kiboko, liliwajaza hofu kubwa ndani ya mioyo yao. Baadaye niliwasikia wakiondoka huku wakitoa maneno ya kumtisha baba kwamba eti siku zake zinahesabika, wakaelekea ule upande tulikomtupia yule mganga ambaye bado alikuwa akiendelea kukoroma kama anayetaka kukata roho.
Wakamchukua na kuondoka naye ambapo taarifa tulizozipata kesho yake ni kwamba alisafirishwa usiku huohuo kuelekea nyumbani kwao, Malawi akiwa na hali mbaya sana. Siku zilizidi kusonga mbele, uhasama kati ya familia yetu na wanakijiji wengine ukazidi kushamiri pale kijijini, kila mtu akawa anatuchukia na kutusema vibaya.
Wiki kadhaa baadaye, siku hiyo nikiwa narejea kutoka shuleni, nilipata taarifa kwamba yule mganga kutoka Malawi amerejea tena na safari hii, amekuja na jeshi la waganga wengine kadhaa kwa lengo la kuja kumkomesha baba kwa alichomfanyia.
Taarifa hizo zilinishtua sana, ikabidi nimfikishie baba haraka lakini tofauti na nilivyotegemea, alizipokea kwa dharau na kuendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi bali mganga na yeyote atakayethubutu kumuingilia kwenye mambo yake, atamshikisha adabu.
Niliishiwa maneno, ikabidi nikae kimya kusubiri kuona mwisho wa hayo yote utakuwa nini. Taarifa za ujio wa waganga hao kutoka Malawi zilizidi kusambaa kwa kasi ya kimbunga, wanakijiji wengi wakawa wanaonesha kufurahia ujio wao.
Hatimaye siku moja usiku, tukiwa tumemaliza kupata chakula cha usiku, kundi la wanakijiji wengi liliwasili pale nyumbani kwetu, wakiongozwa na wale waganga ambao jumla yao walikuwa watano.
Wakaizunguka nyumba yetu huku watu wakipiga kelele kwa nguvu wakitaka eti baba akomeshwe. Siyo kwamba namtetea baba yangu lakini binafsi, mpaka muda huo nilikuwa sielewi kwa sababu gani watu wanamchukia kiasi hicho wakati hakuwa mchawi kama mwenyewe alivyokuwa anasema bali mganga.
Vifo vya wanakijiji wawili, Mwankuga na Mwashambwa havikuwa vigezo vya kumuita baba mchawi kwa sababu wao ndiyo walioanza kumchokoza na mimi nilikuwepo siku hiyo. Nikawa nahisi kwamba huenda ni chuki za watu ndizo zilizosababisha yote hayo.
“Anyolewe! Anyolewe!” ule umati uliokuwa nje ya nyumba yetu ulikuwa ukipiga kelele kushinikiza eti baba anyolewe uchawi. Baba akatutaka wote tutulie ndani na asiwepo wa kutoka nje hata mmoja, akaingia kwenye chumba chake cha uganga na muda mfupi baadaye, alitoka mpaka nje kulikokuwa na wale watu.
Hata sijui nini kilitokea lakini muda mfupi baadaye tulisikia vishindo vya watu wakikimbia, huku wengine wakipiga kelele za kuombamsaada, muda mfupi baadaye tukamsikia baba akiiingia ndani na kufunga mlango, huku akitukana peke yake kuonesha jinsi alivyokuwa na hasira.
Muda mfupi baadaye alituita wanafamilia wote, akiwemo na mama, akaanza kutuambia kwamba pale kijijini hapafai tena sisi kuendelea kuishi kwa sababu tulikuwa na maadui wengi na kila mmoja alikuwa akijitahidi kadiri ya uwezo wake kutuangamiza.
Akasema anajiamini kwamba anaweza kuilinda vizuri familia yake kwa maana ya kujilinda yeye mwenyewe, sisi pamoja na mali zetu zote lakini akasema kuwa si vizuri kuishi mahali ulipozungukwa na maadui.
“Sasa tutafanya nini mume wangu?”
“Inabidi tuhamie mjini,” alisema baba, wote tukawa tunamtazama kwa macho ya shauku kubwa. Sisi tulizaliwa Makongorosi na maisha yetu kwa asilimia kubwa yalikua pale kijijini, hakuna aliyewahi kuishi nje ya pale, tukawa tunashangazwa na kauli ile ya baba ingawa kiukweli, mimi binafsi nilikuwa natamani sana kuishi mjini.
Alitwambia kwamba kuna rafiki yake wa siku nyingi waliyekuwa wakisoma pamoja, amewahi kumpa mwaliko wa kwenda kumtembelea jijini dar es Salaam na kuahidi kumpa hifadhi, akatuambia kwamba anadhani huo ndiyo muda muafaka wa sisi kuhamia Dar es Salaam.
Kiukweli, japokuwa nilikua nimeshinda nikiwa kama mgonjwa kutokana na hali halisi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea kututokea, habari kwamba tunahama kutoka Makongorosi, Chunya mpaka Dar es Salaam zilinifurahisha mno.
Baba alifunga kikao na kututaka wote tuanze kujiandaa kwa sababu muda wowote mambo yatakapokuwa tayari, tutasafiri lakini akatusisitiza kutomweleza yeyote kuhusu suala hilo, tukakubaliana naye. Usingizi ulikuwa mtamu sana siku hiyo, kila mmoja akawa anafikiria namna tutakavyoenda kuyaanza maisha mapya jijini Dar es Salaam.
Si mimi peke yangu ambaye nilikuwa nimechoshwa na kashfa za kuitwa mtoto wa mchawi, famili ayetu nzima ilikuwa imechoshwa. Basi siku hiyo ilipita, kesho yake tukaamka asubuhi lakini baba ndiye aliyekuwa wa kwanza, tukamkuta yupo nje, akatusisitiza kwamba sote hatutakiwi kutoka kabisa hapo nyumbani siku hiyo kwa sababu za kiusalama.
Alinisisitiza zaidi mimi kwa sababu mara zote ndiyo nilikuwa namtoroka na kwenda mitaani, nikamuahidi kwamba sitaondoka. Basi baadaye baba aliondoka, hatukujua ameenda wapi, tukaendelea na maandalizi ya safari huku kila mmoja wetu akionesha kuwa na furaha kubwa moyoni mwake.
Baada ya kama saa mbili hivi kupita, tulimuona baba akija akiwa ameongozana na wanaume wawili walioonesha kwamba siyo wakazi wa Chunya, akaja nao mpaka pale nyumbani, akatutambulisha kwamba ni wateja waliokuwa wanatafuta shamba la kununua. Baba akatuomba familia nzima tukubali kuuza shamba letu moja kwa ajili ya kupata fedha za safari.
Nilichokuwa nampendea baba ni hapo tu, alikuwa anapenda sana demokrasia linapokuja suala la mambo ya familia, tulikubali na kwa akaniita mimi niongozane naye mpaka kwenye shamba letu moja. Wakaanza kupimishiana na baada ya kukubaliana kila kitu, walihesabiana fedha, wakaandikishana kisha tukaondoka kurudi nyumbani.
Wale wageni waliaga na kuondoka, baba akatuita tena ndani na kuanza kuhesabu fedha zilizopatikana. Zilikuwa ni shilingi milioni mbili na laki tatu, akasema zingetosha kabisa kwa safari yetu. Tukakubaliana kwamba tumalizie maandalizi na asubuhi ya siku ya pili tuianze safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia? Safari ya Dar itawezekana? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...