Saturday, June 25, 2016

PENZI LILILOKUFA (DEAD LOVE)- 1

Upepo wa bahari ulikuwa ukivuma kwa nguvu na kusababisha mawimbi makubwa ya maji yawe yanapiga kwa nguvu ufukweni, yakizoa mchanga na kuupeleka bahari kisha kurudi tena.
Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, ndivyo upepo ulivyokuwa ukizidi kuongezeka huku wingu jeusi likianza kutanda angani. Watu wote waliokuwa wakiufurahia upepo wa baharini, sasa walianza kuuona kuwa kero kwani ulikuwa ukiambatana na baridi kali huku kijua cha jioni kilichokuwa kikiwaka, kikimezwa na wingu zito jeusi.


Watu waliokuwa wamekaa ufukweni, waliendelea kupungua kwa kasi na muda mfupi baadaye, ufukwe ulikuwa kimya kabisa huku ngurumo za hapa na pale zikianza kusikika kuashiria mvua kubwa iliyokuwa ikitaka kunyesha.



Licha ya hali kubadilika na kuwa mbaya kiasi hicho, bado kuna mtu mmoja alionekana kuendelea kukaa juu ya gogo kubwa la mnazi, akionekana kuwa mbali kimawazo kiasi cha kushindwa kutambua mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokea ghafla.
Mhudumu wa kike wa ukumbi maarufu uliopo ufukweni mwa bahari, Kunduchi Beach Club aitwaye Winfrida ambaye alikuwa akikimbia huku na kule kukusanya chupa za vinywaji alivyowahudumia wateja wake kabla mvua haijaanza kunyesha, ndiye aliyegundua kwamba kuna mtu alikuwa amesalia ufukweni, akiwa hana dalili za kuondoka.
“We kaka! Kakaaa! Tunafunga geti kule, huoni mvua kubwa inayokuja? Ingia ndani,” alisema Winfrida huku akiendelea kukusanya chupa za bia na soda na kuziweka kwenye kreti, alipaza sauti lakini bado yule mtu aliendelea kujiinami, hali iliyomlazimu kumsogelea.
Tayari manyunyu ya mvua yalikuwa yameanza kudondoka, huku giza likiwa limetanda ghafla, ngurumo za radi zikisikika huku na kule na kuifanya hali kuzidi kuwa ya kutisha.
“Kaka, we kaka,” alisema Winfrida, safari hii akiwa amemgusa mtu huyo na kumtingisha, taratibu mtu huyo akainua uso wake na kumtazama Winfrida, ghafla na yeye akaonekana kushtuka kwani ilionekana hakuwa akijua kilichokuwa kikiendelea.
“Umepatwa na nini kaka? Huoni mvua inayokuja? Twende haraka unaona geti linafungwa kule,” alisema Winfrida huku akimshika mkono na kumuinua, akabeba kreti lake lililokuwa limejaa chupa tupu na kuanza kukimbia. Huku nyuma, yule mtu naye alisimama na kuanza kumfuata huku akiendelea kushangaa hali ya hewa kwani ilionesha imebadilika haraka mno.
Walipoingia kwenye geti tu, mlinzi aliyekuwa anawasubiri alifunga, wakakimbiampaka kwenye ukumbi mkubwa ambapo waliwakuta watu wengi wakiwa wamejistiri mvua, huku kila mmoja akionekana kumshangaa mtu huyo.
Muda mfupi tu baadaye, mvua kubwa ikaanza kunyesha, ikiwa imeambatanana upepo mkali sambamba na radi zilizofanya watu wote kuzidi kuingia ndani ya ukumbi huo na kujibanza kwenye kona.
“Inamaana ulikuwa umelala au? Nisingekushtua bado ungekuwa kulekule ufukweni,” Winfrida alimuuliza mtu huyo ambaye kwa kuwa sasa walikuwa kwenye mwanga wa taa, aliweza kumuona vizuri usoni na kubaini kwamba kumbe alikuwa analia. Akaweka kreti lake chini na kumsogelea.
“Inaonekana ahaupo sawa, nini kinachokusumbua?” aliuliza Winfrida lakini kauli yake ilionekana kama imeenda kutonesha donda ambalo bado halikuwa limepona kwenye mtima wa kijana huyo, aliyekuwa amevaa kitanashati.
Machozi yakaanza kumtoka kwa wingi na kutiririka mpaka chini ya kidevu chake, yakapotelea kwenye ndevu zake alizokuwa amezinyoa vizuri. Ghafla umeme ulikatika baada ya radi moja kupiga kwa nguvu, giza likatawala eneo lote la ukumbi huo.
Harakaharaka Winfrida alimshika mkono kijana huyo na kumuongoza kutembea mpaka upande kulipokuwa na kaunta, akavuta viti viwili , kimoja akampa kijana huyo ambaye bado hakuwa anaelewa nini kilichokuwa kinamsumbua, akakaa huku akiendelea kulia.
Kama isingekuwa umeme kukatika ghafla, huenda watu wengi wangemuona jinsi alivyokuwa anamwaga machozi kama chemchemi ya maji, akajiinamia kwenye meza ambapo aliendelea kulia kwa kwikwi kwa muda mrefu, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha.
“Pole sana lakini kulia pekee hakuwezi kukusaidia chochote, tafadhali niambie unaitwa nani, unatokea wapi na nini kilichokusibu mpaka ukawa kwenye hali kama hii,” alisema Winfrida kwa sauti ya upole, mtu huyo akashusha pumzi ndefu na kutoa kitambaa mfukoni mwake, akajifuta machozi na kamasi na kumtazama Winfrida.
“Ahsante kwa kunishtua kule ufukweni, ahsante sana,” alisema kijana huyo huku akiendelea kujifuta machozi, Winfrida akatingisha kichwa kama ishara ya kupokea shukrani hizo.
“Naitwa Abdallah au Dulla kama wengi wanavyopenda kuniita,” alijibu kijana huyo, Winfrida akamkazia macho usoni ambapo kwa msaada wa mshumaa uliokuwa umewaswa kaunta, aliweza kumuona vizuri, akendelea kumtazama akiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia kilichomfanya awe kwenye hali kama hiyo.
“Ni mambo ya kawaida ya dunia ndiyo yaliyonifanya niwe kwenye hali kama hii, wala usijali ila nashukuru sana kwa msaada wako,” alisema Dullah huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu tano.
“Naomba unisaidie maji ya kunywa ya Kilimanjaro,” alisema huku akimkabidhi Winfrida fedha hiyo. Alipoinuka na kueleka kaunta, Dullah alitoa simu yake mfukoni na kuibonyeza, akashangaa kugundua kuwa kumbe tayari ilikuwa imefika saa moja kasoro za jioni.
Akajishangaa kukaa ufukweni muda mrefu kiasi hicho kwani kumbukumbu zake zilimuonesha kuwa wakati anafika ufukweni hapo, ilikuwa ni saa tano za asubuhi. Akageuka upande mwingine na kugundua kuwa kulikuwa na watu wengi eneo hilo, wote wakiwa wamejificha mvua iliyokuwa ikiendelea kumwagika kwa wingi, ikiambatana na upepo na radi nyingi.
Muda mfupi baadaye, Winfrida alirudi na kumletea maji kama alivyoagiza, akamfungulia na kumkabidhi chenji, akakaa palepale alipokuwa amekaa awali. Dullah alimimina maji kwenye glasi na kuyanywa yote, alipoishusha glasi, ilikuwa tupu.
Akashusha pumzi ndefu na kumuangalia Winfrida ambaye bado alikuwa ametulia, akisubiri kusikia chochote kutoka kwa Dullah.
Kabla hajazungumza chochote, simu ya mkononi ya Dullah ilianza kuita mfululizo, akaiangaalia namba ya mpigaji lakini badala ya kupokea, alijiinamia tena na kuanza kulia, safari hii kwa uchungu zaidi kuliko mwanzo, jambo lililomfanya Winfrida abaki njia panda.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue hapahapa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...