Wednesday, August 19, 2015

NILIMUUA NIMPENDAYE (I KILLED MY BELOVED ONE)- 1

Jina langu naitwa Eunice, mtoto wa tatu kati ya watano wa familia ya baba yetu, mzee Ansbelt. Nilizaliwa miaka 26 iliyopita katika Kijiji cha Mtae, Lushoto mkoani Tanga lakini nimekulia jijini Dar es Salaam kwani baba yangu aliyekuwa akifanya kazi ya uhandisi katika Kampuni ya Usambara Civil Engineering, alihamishiwa kikazi jijini na akafanikiwa kujenga nyumba Tabata.
Ni hapo ndipo mimi na ndugu zangu wa tumbo moja tulipokulia hadi tulipokuwa wakubwa. Kwa kweli kwa kipindi cha utotoni, tuliishi maisha mazuri sana kwani baba yetu alikuwa akijiweza kifedha hivyo alituhudumia vizuri kwa mavazi, chakula na elimu bora.
Nakumbuka sisi ndiyo tulikuwa wa kwanza kumiliki runinga mtaani kwetu na ndiyo tulikuwa wa kwanza kupelekwa shuleni na ‘school bus’, tukisoma katika shule iliyokuwa inafundisha masomo yote kwa Kiingereza (English Medium), iliyokuwa nje kidogo ya jiji.
Mama yetu hakuwa akifanya kazi, alikuwa akishinda nyumbani kuhakikisha sisi wanaye tunapata kila tulichokihitaji, ikiwemo malezi bora. Kutokana na aina ya malezi tuliyolelewa, tulikuwa tofauti sana na watoto wengine tuliokuwa tukiishi nao mtaani kwetu.
Mimi na ndugu zangu wengine wa kike hatukuwa sawa na wasichana wengine mtaani kwetu ambao walianza kujihusisha na mapenzi wakiwa na umri mdogo, wengi wakitoka na wanaume wenye umri mkubwa, sawa na baba zao.

Hata kaka zetu wawili, nao hawakuwa kama vijana wengi wa mtaani kwetu. Hawakuwa wakijichanganya na vijana wa kihuni waliokuwa wakitega kwenda shule na kushinda vijiweni kucheza kamari, kunywa pombe na kuvuta bangi.
Ratiba tuliyokuwa tunapangiwa na wazazi wetu, ilitubana kwani hakuna aliyekuwa anapata muda wa kufanya mambo hayo. Tulipotoka shule, hatukuruhusiwa kuzurura mitaani bali sote tulikuwa tukikaa kwenye chumba cha kusomea na kuendelea kufanya ‘home work’ baada ya kula na kupumzika kidogo. Kila mmoja mtaani kwetu alikuwa akituita watoto wa geti kali na wengine walituchukia kwa madai kwamba tulikuwa tunaringia fedha za baba yetu.
Hata hivyo, tuliendelea kuishi kwa misingi bora, tukiwaheshimu watu wote, wakubwa kwa wadogo. Siku zilizidi kusonga mbele, tukawa tunazidi kuwa wakubwa, wenye afya bora, wenye nidhamu na ndoto nyingi maishani.
Nakumbuka mimi kila siku nilikuwa nikiwaambia wenzangu kwamba nikiwa mkubwa nataka kuwa rubani. Ndoto hizo zilinifanya niyapende sana masomo ya Fizikia, Jografia na Hesabu pamoja na masomo mengine ya sayansi.
Niliamini hakuna kinachoweza kunirudisha nyuma kwenye ndoto zangu hizo kwani kila kitu kilikuwepo na wazazi wangu siku zote walikuwa wakiahidi kunisomesha mpaka nitakapotimiza malengo yangu.
Maisha yalianza kuingia doa siku moja wakati tukirudishwa kutoka shule, mimi na kaka yangu. Tulipokaribia kufika nyumbani, tulishtushwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yetu, wakionesha kuwa na nyuso za huzuni.
“Nyumbani kuna nini? Mbona watu wengi namna hii,” nilimuuliza kaka yangu, Gisla ambaye tulikuwa tukisoma naye shule moja. Naye hakuelewa chochote, tukabaki tukitazamana na kutazama upande wa nyumba yetu bila kupata majibu.
Baada ya kuteremka kwenye basi la shule, tulikuwa tukishauriana kama twende nyumbani au la kwani hali tuliyoiona ilitufanya tupatwe na woga wa ajabu. Tukiwa bado tumepigwa na bumbuwazi, tulimuona mama mmoja ambaye tulizoea kumuita mama Dotto akija mbiombio mpaka pale tulipokuwa tumesimama.
Tulipomtazama usoni, macho yake yalikuwa mekundu sana kuonesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu.
“Twendeni huku wanangu,” alisema mama Dotto na kutushika mikono, mmoja kushoto na mwingine kulia, akatupeleka mpaka nyumbani kwake, tukaingia sebuleni kisha akafunga mlango, akatusogelea na kutushika mabegani.
“Wanangu kuna matatizo nyumbani. Nawaomba mjikaze kwani kazi ya Mola haina makosa,” alisema mama Dotto huku akijifuta machozi, tulitazamana tukiwa bado hatujapata majibu ya alichokuwa anakimaanisha. Ilibidi nivunje ukimya na kumuuliza tena alikuwa anamaanisha nini.
“Baba yenu amepata ajali mbaya akiwa kazini, hivi tunavyozungumza hatunaye tena duniani,” alisema mama Dotto, kauli iliyoamsha vilio vya nguvu kutoka kwangu na kwa kaka Gisla.
Awali hatukuamini alichokuwa anakizungumza, tukawa tunahisi labda tupo ndotoni. Tulitoka mbiombio ndani kwa mama Dotto, tukawa tunakimbilia nyumbani kwetu huku tukipiga mayowe ya nguvu.
Tuliwapita watu wengi waliokuwa nje ya nyumba yetu ambao walijitahidi kutuzuia bila mafanikio, tukaingia mpaka sebuleni ambapo tulishangaa kukuta vitu vyote vimetolewa na kutandikwa mazulia ambayo yalikuwa yamekaliwa na watu waliokuwa wanaomboleza.
Tulipoangalia kwenye kona moja, tulimuona mama akiwa ameshikiliwa na wanawake wenzake wengi, akiwa analia kwa uchungu huku akilitaja jina la baba. Nilishindwa kujizuia, nilijaribu kumkimbilia mama pale alipokuwa ameshikiliwa lakini mwili uliniisha nguvu, miguu ikanilegea kisha nikaanza kuhisi kizunguzungu kikali, nikaanguka chini kama mzigo, puuh!
Mwili uliniisha nguvu, miguu ikanilegea kisha nikaanza kuhisi kizunguzungu kikali, nikaanguka chini kama mzigo, puuh! Nilikuja kushtuka saa kadhaa baadaye, nikajikuta nimelala nje ya nyumba yetu huku nikipepelewa kwa vitenge na wanawake ambao niliwatambua kwamba ni majirani zetu.
Niliporejewa na fahamu tu, nilikumbuka kilichonifanya nikawa katika hali hiyo, nikaendelea kuomboleza msiba wa baba huku nikiwa na hamu kubwa ya kujua nini kilichotokea. Nililia sana huku nikiwa bado siamini kama ni kweli baba ametangulia mbele ya haki.
Nikawa naendelea kuomboleza, huku wanawake wengi ambao ni majirani na marafiki wa familia yetu wakitumbembeleza. Kati ya waombolezaji wote, mimi na mama ndiyo tulikuwa na hali mbaya zaidi. Niliumizwa sana na kifo cha ghafla cha baba kwani nilishaona ambacho kingetokea mbele yetu. Mama hakuwa na kazi yoyote na kwa kipindi chote tangu nikiwa mdogo, sikuwahi kumuona akijishughulisha na shughuli yoyote ya kutuingizia kipato.
Hakuwa kama wanawake wengine mtaani kwetu ambao walikuwa wakifanya biashara mbalimbali ambazo ziliwaongezea kipato zikiwemo ufugaji wa kuku wa nyama na mayai, kukopesha vitu kama vyombo vya nyumbani, mashuka au nguo, ufundi cherehani na shughuli nyingine za kiujasiriamali.
Sitaki sana kumlaumu mama lakini nadhani maisha aliyozoeshwa na baba ndiyo yaliyomfanya awe hivyo. Wakati nikiendelea kulia kwa uchungu, nilikuwa nikifikiria nini hatima yetu mimi na ndugu zangu kwani hakuna hata mmoja kati yetu aliyekuwa amefikia hatua ya kujitegemea. Sote bado tulikuwa tukitegemea malezi ya baba na mama.
Wakati tukiendelea kuomboleza, nilimuona mfanyakazi mmoja aliyekuwa akifanya kazi na baba akifika nyumbani kwetu, akiwa ameongozana na wanaume watatu huku mmoja akiwa na bunduki mkononi. Bila hata kuuliza, nilijua kuwa lazima amekuja na polisi. Sikuelewa sababu iliyomfanya aje na polisi msibani, nikahisi lazima kuna tatizo kubwa.
Sikutaka kupitwa na jambo, nikajifanya nainuka ili niende chooni, nikasogea mpaka upande waliokuwa wamesimama huku nikiwa nimetega masikio kwa makini.
“Mkewe ni yupi kati ya hawa,” aliuliza mmoja kati ya wale askari, yule mfanyakazi mwenzake baba ambaye tulizoea kumuita baba Sufiani, akaongea nao jambo kwa sauti ya chini kisha nikaona wote wamenigeukia mimi.
Nikawa natetemeka kwani sikuwa najua kilichokuwa kinaendelea. Wakanisogelea mpaka pale nilipokuwa nimesimama, wakanipa mikono ya pole kisha baba Sufiani akanitambulisha. Akawatajia wale askari jina langu kisha akawaeleza kuwa mimi ndiyo mtoto wa kike mkubwa wa marehemu Ansbelt.
Ikumbukwe kwamba tulizaliwa watano kwenye familia yetu, wavulana wawili na wasichana watatu, mimi nikiwa ndiyo mkubwa kwa upande wa wasichana na nikiwa ndiyo wa pili kuzaliwa baada ya kaka yangu Gisla.
Baada ya hapo, aliwatambulisha watu hao kwangu na kunieleza kuwa ni polisi kutoka Kituo Kikuu ambao walikuwa wakifuatilia tukio la mauaji ya baba. Aliposema ‘mauaji ya baba’ nilishtuka kidogo kwani awali nilisikia kwamba baba amepata ajali akiwa kazini. Sasa kama amekufa kwa ajali, kwa nini wanazungumzia mauaji? Nilijiuliza bila kupata majibu.
Wale askari walisema wanahitaji kuzungumza na mimi kwa ufupi kabla hawajazungumza na mama. Tulisogea pembeni ambapo jambo la kwanza waliniuliza jinsi tulivyokuwa tukiishi na marehemu baba. Niliwaeleza kuwa siku zote tulikuwa tukiishi kwa amani na upendo, huku akituonesha mapenzi makubwa.
“Umewahi kusikia kama baba yako ana ugomvi na mtu yeyote?” aliniuliza yule askari aliyekuwa ameshika bunduki, nikawa natazama juu kwa lengo la kuvuta kumbukumbu. Kiukweli sikuwahi kusikia kama baba ana ugomvi na mtu yeyote, siyo kazini kwake wala nyumbani. Alikuwa akiishi vizuri na majirani na kila mmoja alimpenda kutokana na ucheshi wake.
Niliwajibu kwamba sijawahi kusikia baba akikorofishana au kuwa na ugomvi na mtu yeyote. Wakaniuliza kabla halijatokea tukio hilo, baba yangu alikuwa katika hali gani? Nilivuta kumbukumbu na kujaribu kuzitazama siku kadhaa nyuma, nikagundua kuwa baba hakuwa na tofauti yoyote na siku zote. Nikawajibu kwamba alikuwa kawaida tu.
Mmoja kati yao alikuwa akiyaandika majibu yote kwenye kitabu cheusi alichokuwa nacho kisha baada ya hapo, waliomba kwenda kuongea na mama. Kabla hawajaondoka, niliwauliza nini kilichotokea mpaka baba yangu akafa. Mmoja kati yao akaniambia kwamba baba alikuwa amepigwa na kitu kizito kichwani na kusababisha apasuke sehemu ya nyuma ya kichwa chake, hali iliyosababisha kifo chake.
Nilishtuka mno kusikia hivyo, kwa mara nyingine nikajikuta nikiishiwa nguvu, miguu ikanilegea na mwili wote ukanyong’onyea, nikaanguka tena. Kwa bahati nzuri, baba Sufiani aliniwahi kabla sijajibamiza chini, akanidaka na kusaidiana na wale askari wengine kunipeleka kwenye kundi la wanawake waliokuwa wanaendelea kuomboleza.
Wakaanza upya kunipepelea mpaka nilipozinduka.
Niliporejewa na fahamu, nilijikuta nikiwa pembeni ya mama ambaye bado alikuwa akiendelea kulia kwa uchungu. Wale askari waliokuwa wamekuja na baba Sufiani hawakuwepo tena.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue. Kitabu cha mkasa huu tayari kipo mitaani. Piga 0719401968 kwa maelezo zaidi.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...