Friday, December 26, 2014

KUTUBU KWANGU (MY REPENTANCE)- 3


ILIPOISHIA:
Kama hiyo haitoshi, nilimtumia ujumbe mfupi mzuri wa kumtakia usiku mwema, naye akanijibu ndani ya muda mfupi tu, nikalala na kuukumbatia mto wangu huku joto tamu likiendelea kuzunguka kwenye mwili wangu.
SASA ENDELEA...
Niseme tu wazi kwamba nilishampenda sana Ibrahim tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza tu, na sasa nilikuwa tayari kufanya chochote, hata ikibidi kujitongozesha ilimradi awe mpenzi wangu.
Naomba watu wasinielewe vibaya kwa sababu najua kwa mila za Kitanzania, ni vigumu sana mwanamke kueleza hisia zake za kimapenzi, tumezoea kwamba sisi ni watu wa kutongozwa tu.
Wapo wengi tu ambao walikuwa wakiwapenda watu fulani ila kwa sababu ya kukosa ujasiri, wakajikuta wakiolewa na watu ambao wala hawakuwahi kuwafikiria kwenye maisha yao.
Niliamua kujitoa mhanga mtoto wa kike, nikajiapiza kuwa lazima nimpate Ibrahim. Wala kilichonizuzua halikuwa gari lake au kusikia kwamba anafanya kazi benki, walaa! Ni mapenzi ya dhati ndiyo yaliyonisukuma mpaka kupata ujasiri wa namna ile.

Niliendelea kumfikiria Ibrahim mpaka usingizi uliponipitia, kesho yake asubuhi nikawahi kuamka kama kawaida yangu na kujiandaa kwa ajili ya kwenda chuo. Nilipomaliza kuvaa, niliwaaga baba na mama kama ilivyo kawaida yangu kila siku kisha nikatoka na kuanza kutembea kuelekea kituo cha daladala.
Siku hiyo hakukuwa na mvua kama jana yake ingawa kila kona kulikuwa na matope. Kumbukumbu juu ya Ibrahim zikanijia na kujikuta nikitabasamu mwenyewe. Nilitoa simu yangu kwenye mkoba na kutafuta namba yake, nikampigia.

Muda mfupi baadaye alipokea, nikamsalimia kwa adabu na kumuuliza kama ameamka salama. Alinijibu kwamba yupo poa na kwa muda huo anajiandaa kwenda kazini.
“Mi mwenyewe naelekea Morocco kupanda daladala.”
“Ahaa! Sasa kwa nini usinisubiri nikupe lifti?”
“Hutachelewa sana,” nilijibaraguza ili asinione najirahisisha sana kwake, akaniambia kuwa wala hatachelewa, baada ya dakika kumi tu atakuwa ameshafika. Tuliagana, nikakata simu huku nikiwa na furaha ya ajabu ndani ya moyo wangu.
Nilitembea harakaharaka mpaka kituoni, nikatafuta sehemu tulivu na kukaa huku macho yote yakiwa upande ule Ibrahim alikotokea jana yake. Nilitoa kioo changu kidogo ninachotembea nacho kwenye mkoba na kujikagua usoni, nikajiweka sawa na kuendelea kumsubiri.
Kweli dakika kumi baadaye, gari la Ibrahim lilifika pale kituoni, akapunguza mwendo na kusimama huku akishusha kioo. Kwa kuwa tayari nilishamuona, niliinuka harakaharaka na kumfuata, akanifungulia mlango wa mbele, nikaingia na kukaa.
“Mambo!” Ibrahim alinisabahi huku tabasamu pana likiwa limeupamba uso wake. Kiukweli Ibrahim alikuwa na mvuto wa kipekee machoni pa mtu yeyote. Nikajihisi mkondo kama wa umeme ukipita mwilini mwangu na kusambaa kwenye kila kiungo.
Nilimjibu huku na mimi nikiachia tabasamu pana, akaondoa gari na safari ya kuelekea Posta ikaanza. Mazungumzo ya kawaida yaliendelea huku mara kwa mara nikigeuka na kumtazama Ibrahim usoni.
Kila macho yetu yalipogongana, moyo wangu ulikuwa ukinilipuka mno mpaka nikawa najishtukia. Kwa kuwa siku hiyo hakukuwa na foleni kubwa, baada ya dakika kadhaa tayari tulikuwa Posta. Akanipeleka mpaka jirani na chuoni kwetu, tukaagana kisha akaondoa gari kwenda kazini kwake.
Nilimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yangu, nikatembea harakaharaka kuingia chuoni huku moyo wangu ukiwa na furaha ya ajabu. Siku hiyo hata akili zangu hazikuwepo kwenye masomo kabisa, nilikuwa nikiwaza jinsi ya kumuingiza Ibrahim kwenye kumi na nane zangu! Moyo wangu ulishampenda.
Muda wa lanchi ulipofika, nilimtumia meseji Ibrahim na kumwambia kama ana nafasi aje tule wote mi nitamlipia, akanijibu kwamba alikuwa na kazi nyingi hivyo isingekuwa rahisi kuonana.
“Kwani kazini unatoka saa ngapi?”
“Saa kumi na moja.”
“Kuna mahali nataka unisindikize, utakuwa na nafasi?”
“Yaa, nikitoka kazini huwa naenda nyumbani moja kwa moja kwa hiyo usijali nitakusindikiza,” alisema Ibrahim bila hata kuhoji ni wapi nilipokuwa nataka anisindikize. Wala sikuwa na safari yoyote, nilitaka tu ukaribu wake.
Kichwani nikapata akili kwamba nitamwambia anisindikize ufukweni kuchukua mchanga kidogo wa bahari kwa ajili ya kumpelekea mama. Nilipanga kwamba tukifika ufukweni, nitamfanyia vituko mpaka mwenyewe achanganyikiwe na mimi. Muda wa lanchi ulipopita, nilirudi darasani, nikawa naona kama saa haziendi haraka.
Hatimaye muda wa kutoka ulifika, nikakusanya kila kitu changu na kutoka, nikampigia simu Ibrahim kwamba atanikuta namsubiri palepale aliponishusha asubuhi. Kwa kuwa mimi niliwahi kidogo kutoka chuo, ilinibidi nimsubiri Ibrahim kwa zaidi ya dakika arobaini.
Kwangu hiyo wala haikuwa kazi kubwa, hatimaye nikaliona gari lake likija taratibu pale nilipokuwa nimekaa, akashusha kioo na macho yetu yakagongana, wote tukatabasamu. Harakaharaka niliingia kwenye gari na kukaa pembeni ya Ibrahim, nikamgeukia, na yeye akanigeukia, tukawa tunatazamana.
“Mambo!” alivunja ukimya, nikamjibu huku nikiachia tabasamu pana, na yeye akatabasamu na kuyafanya meno yake meupe yaonekane vizuri. Siyo siri nilijikuta nikizidi kumpenda Ibrahim.
Nilimwambia kuwa nataka anisindikize baharini nikachukue mchanga mama kaniagiza, wala hakuwa na kipingamizi chochote. Akawasha gari na kuanza kuendesha taratibu, tukawa tunaelekea baharini, upande wa Hospitali ya Ocean Road. Njiani tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale, akawa ananiuliza kuhusu masomo yangu na kunisisitiza kuwa nikazane kwani elimu ndiyo ukombozi wetu.
Tulifika baharini, akatafuta sehemu nzuri na kupaki gari, pembeni ya barabara kisha tukashuka. Nikaona huo ndiyo muda muafaka wa kufanya nilichokuwa nakitaka.
“Samahani, nikitaka kuogelea kidogo utanisubiri?”
“Wala usiwe na wasiwasi, kwani huwa unapenda kuogelea?”
“Napenda sana,” nilisema huku moyoni nikifurahi kwani nilichokuwa nakitaka kilikaribia kutimia. Ibrahim alinisindikiza, tukashuka kwenye ngazi za ukingo wa bahari mpaka chini ambako haikuwa rahisi kwa wapita njia kutuona.
“Geukia kule nibadilishe nguo,” nilisema huku nikijichekeshachekesha, kweli Ibrahim akageuka na kunipa mgongo, nikavua suruali niliyokuwa nimevaa na kubaki na taiti, juu nikavua blauzi na kubaki na sidiria tu kisha nikachukua mtandio mwepesi na kujifunga juu kidogo ya kifua.
Nilifanya vile kwa makusudi kwani nilijua nitakapoingia kwenye maji na ule mtandio, utanichora mwilini na kulifanya umbo langu zuri la kuvutia lionekane vizuri. Nikaanza kutembea taratibu kumfuata Ibrahim ambaye bado alikuwa amenipa mgongo.
“Tayari,” nilisema huku nikimgusa begani, akageuka na kunitazama. Mshtuko alioupata haukuweza kujificha, alinitazama kuanzia juu mpaka chini kama ndiyo kwanza anakutana na mimi kwa mara ya kwanza, nikajua ameshaingia kwenye mtego.
“Vipi mbona umeduwaa,” nilimuuliza lakini hakuwa na jibu zaidi ya kutabasamu. Nikageuka na kuanza kutembea kwa maringo kuelekea kwenye maji, huku nikijitingisha kwa makusudi. Ibrahim akazidi kupagawa.
Nilipoingia kwenye maji, nilianza kuogelea kihasarahasara huku nikimuita Ibrahim naye aje tuogelee naye lakini alikataa, bado akawa anaendelea kunitazama kwa macho yaliyokuwa yamebeba ujumbe mzito.
Sikuogelea sana, nikachukua mchanga kidogo na kuuweka kwenye mfuko kama geresha tu kisha nikatoka kwenye maji. Kwa kuwa nilikua nimevaa taiti na sidiria tu huku juu nikiwa nimejifunga mtandio mwepesi, umbo langu lilionekana vizuri kabisa, uzalendo ukamshinda Ibrahim, akanitamkia:
“Kumbe umeumbika hivi? Loh, mpenzi wako anafaidi.” Nikacheka sana kwa furaha kwani nilichokuwa nakitaka, kilikuwa kimetimia. Tayari Ibrahim alishaanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue. Unaweza pia kuisoma Facebook kwa ku-like page ya Simulizi za Majonzi.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...