Tuesday, July 8, 2014

HUJUI KUTONGOZA? FUATA MBINU HIZI

Ni wiki nyingine ambapo mwenyezi Mungu ametujaalia kukutana katika busati letu la mahaba ambapo tunajadiliana mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi. Leo nataka kuzungumza na wewe rafiki yangu ambaye umri wa kuingia kwenye ndoa umefika lakini bado hujabahatika kumpata mwenzi wako ambaye malengo yako ni kuingia naye kwenye ndoa.


Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku. Zamani ilikuwa kama kuna mwanamke au mwanaume unampenda, basi lazima uhangaike sana mpaka utakapopata nafasi ya kuzungumza naye,  na kama huna ujasiri wa kumtongoza ana kwa ana basi ndiyo umemkosa.


Siku hizi mambo yanamalizwa kidijitali. Kama umezidiwa na upweke, hata kama hujui kutongoza, zipo mbinu nyingi za kisasa zinazoweza kukurahishia, kuna simu za mikononi, kuna mitandao ya kijamii na njia chungu nzima hivyo huna haja ya kuendelea kuumia na upweke.
Ni matumaini yangu kuwa mada hii ambayo iyaegemea zaidi katika matumizi ya simu za mkononi itakusaidia wewe ambaye unampenda mtu fulani na lengo lako si kumchezea bali kuanzisha naye maisha ya kifamilia.
Kumbuka kuwa penzi bora ni lile ambalo wawili huanza kwa kuwa marafiki, ni makosa kukurupuka kumtongoza mtu kwenye simu au kwenye mitandao ya kijamii bila kumvuta kwanza karibu yako.
Hatua ya kwanza, ukishapata namba ya simu ya huyo umpendaye, tafuta muda ambao utakuwa umetulia kisha mpigie na jitambulishe. Mweleze kwamba umempigia simu kumjulia hali, kama akikuuliza mahali ulikoipata namba yake, unaweza kumjibu vyovyote lakini inashauriwa kuwa siyo vizuri kumtajia aliyekupa namba yake kwa sababu unaweza kuwagombanisha.
Usiwe na papara, mtakie siku njema na endelea na shughuli zako nyingine. Unaweza pia kuendelea kumtumia meseji za kawaida (siyo za mapenzi), ukimjulia hali, ukimuuliza kama ameshakula au amekula chakula gani, anafanya nini kwa muda huo na vitu anavyovipenda sambamba na vile asivyovipenda.
Endelea hivyo kwa muda, siri kubwa ambayo huijui ni kwamba watu wengi, hasa wanawake huwa wanapenda kujua kuwa mtu fulani anamjali kwa kumuuliza mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake ya kawaida. Jitahidi kuwa mcheshi lakini usizidishe masihara. Ukishafanikiwa kumvuta karibu yako na kumfanya aamini kwamba huwa unamfikiria mara kwa mara, sasa unaweza kupiga hatua moja mbele kwa kufanya yafuatayo:
MBINU ZA KUMTEKA
Tumia sauti ya utulivu yenye hisia ndani yake, utazidi kumvuta karibu yako. Usipende kuzungumza kwa sauti ya juu au kupayuka au kupiga simu ukiwa kwenye kelele. Akipokea tu simu yako, mjulie hali yake kisha msifie kidogo kuhusu sauti yake na namna anavyozungumza.
Msimulie kidogo kuhusu siku yako inavyokwenda, tumia maneno machache lakini yatakayomfanya asiboreke kukusikiliza. Ifanye stori yako iwe ya kuvutia kwa kutumia maneno matamu yatakayomfurahisha na kumfanya aache kila anachokifanya na kukusikiliza.
Badili mazungumzo, muulize kama anajua kwamba yeye ni mzuri sana na hujawahi kukutana na mtu anayevutia kama yeye. Kama wewe ni mwanaume na unayezungumza naye ni mwanamke, utakuwa katika nafasi nzuri ya ‘kum-win’ kwa sababu wanawake wengi wanapenda sana kusifiwa.
Akiwa amekolea na sifa unazomwagia, mweleze kwamba unavutiwa naye na unatamani kuwa na mpenzi anayefanana naye. Zungumza naye kwamba atakapokubali kuwa na wewe, utamtunza na kumlea kama malkia, mweleze malengo yako ya baadaye katika uhusiano wenu endapo atakukubalia.
Usimpe nafasi ya kukwambia kama amekubali au amekataa bali hitimisha mazungumzo yenu kwa kumtakia siku njema au kazi njema. Bila shaka utamuacha akiwa na shauku kubwa ya kuendelea kusikiliza ‘mistari’ yako.
Endelea kuwasiliana naye kwa mambo ya kawaida huku ukimpima kama yale uliyomwambia anayachukuliaje. Kama naye amekupenda, utaanza kuona mabadiliko kuanzia meseji atakazokuwa anakutumia, namna anavyopokea simu yako na uchangamfu anaokuonesha.
Kama bado haoneshi dalili zozote za kukuelewa, basi jua hajavutiwa na wewe na ukiendelea kuzungumzia mambo ya mapenzi, huenda ukaanza kumboa lakini kama ana dalili za kuingia kwenye kumi na nane zako, endeleza mawasiliano naye, omba kukutana naye sehemu tulivu kama ufukweni au popote ambapo mtakuwa wawili na hapo utakuwa na nafasi nzuri ya kueleza kwa kina juu ya hisia zako.



Endapo atakubali kukutana na wewe, basi hiyo ni hatua nzuri sana kuonesha kwamba unaelekea kufanikiwa. Jambo la msingi ni kuanza kujiandaa kwa ajili ya kukutana naye kwa sababu mwonekano wako wa kwanza mbele ya macho yake ndiyo utakaompa sababu ya kukuchagua au kukukataa. Kwanza anza kwa kufanya kitu ambacho huwa kinakufurahisha na kukuweka kwenye mudi nzuri kama kuimba, kucheza muziki, kufanya mazoezi au chochote unachokipenda sana.
Baada ya hapo, hakikisha nguo zako ni safi, jipulizie manukato mazuri, piga mswaki, jitengeneze nywele zako vizuri na hakikisha kila kitu mwilini mwako ni kisafi. Pangilia mazungumzo kati yako na umpendaye kabla hata hamjakutana, hii itakuongezea kujiamini.
Hakikisha sehemu mnayoenda kukutania kwa mara ya kwanza unaifahamu vizuri na imetulia vya kutosha. Baada ya hapo, muandalie zawadi ndogo mfano chokleti, mkufu au ua zuri. Usihangaike kutafuta zawadi kubwa kwa sababu siyo muhimu mnapokutana kwa mara ya kwanza.
Muda utakapowadia, wahi kufika eneo mlilopanga kabla ya mwenzako, hii itamfanya akuheshimu zaidi kwa sababu atajua hubahatishi mambo. Msalimie kwa uchangamfu kisha mkaribishe sehemu ya kukaa. Jitahidi kupunguza maneno mengi badala yake zungumza kwa staha na muda mwingi msikilize yeye. Muulize kinywaji au chakula anachokipenda kishe muagizie.
Kama wewe ni mwanaume, mkishamaliza kunywa au kula, lipa bili hata kama yeye anao uwezo wa kulipa. Ukweli ambao wengi hawaujui, wanawake wanapenda zaidi kuhudumiwa hata kama wana utajiri mkubwa kiasi gani.
Mkishamaliza, uwanja ni wako sasa wa kueleza hisia za ndani ya moyo wako. Zungumza kwa busara na kwa utulivu, huna haja ya kupaniki kwa sababu mpaka amekubali kukutana na wewe, tayari una asilimia kubwa ya kumpata hivyo punguza woga. Jitahidi kumtazama kwenye macho yake unapozungumza naye, hii itakuongezea ujasiri.
Naam! Baada ya hapo naamini utakuwa umeutua mzigo mzito uliokuwa nao, usimlazimishe kukupa majibu hapohapo endapo ataomba umpe muda. Baada ya hapo, tayari utakuwa umefanikiwa kumvuta kwako kwa asilimia tisini, ongeza ukaribu zaidi na utaona matokeo yake kwa sababu hataweza kukataa ombi lako na mwisho mtatimiza lengo lenu la kufunga ndoa na kuishi pamoja siku za mbele.




3 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...